Haiwezekani kujiandaa kwa majanga makubwa kiasi hiki, rais wa Uturuki asema
Idadi ya waliofariki kutokana na tetemeko kubwa la ardhi kusini mwa Uturuki na Syria iliongezeka hadi zaidi ya watu 11,200 siku ya Jumanne huku waokoaji wakifanya kazi dhidi ya wakati katika hali mbaya ya msimu wa baridi
Moja kwa moja
Christian Atsu: Mchezaji wa Ghana hajulikani alipo, asema ajenti wake

Ajenti wa Christian Atsu anasema mwanasoka huyo hajulikani aliko,siku moja baada ya kuripotiwakuwa alitolewa kwenye vifusi vya jengo "akiwa na majeraha" baada ya tetemeko la ardhi la Uturuki.
Zaidi ya watu 11,000 kusini mwa Uturuki na kaskazini mwa Syria sasa wamefariki katika mkasa huo
Fowadi wa Ghana Atsu anachezea Hatayspor na makamu wa rais wa klabu hiyo Mustafa Özat alisema mchezaji huyo aliokolewa.
"Tunafanya kila tuwezalo kumpata Christian," alisema Nana Sechere.
"Kama unavyoweza kufikiria, huu unaendelea kuwa wakati mbaya kwa familia yake."
Katika chapisho la mtandao wa kijamii,wakala huyo aliongeza: "Kufuatia taarifa za jana kutoka kwa klabu kwamba Christian alitolewa akiwa hai, bado hatujathibitisha aliko Christian."
Meneja wa Hatayspor Volkan Demirel aliiambia tovuti ya michezo ya Uturuki ya Spor Arena hakukuwa na "habari bado" kuhusu Atsu au mkurugenzi wa michezo Taner Savut, ambaye aliripotiwa kutoweka Jumatatu pamoja na mchezaji huyo.
"Kama wangekuwa hospitalini, huoni ningetoa taarifa? Tafadhali usiwe na uhakika kwamba alinusurika. Hili lisiandikwe kwa vile alinusurika," alisema.
MH17: Putin 'alituma' kombora lililoangusha ndege - wachunguzi

Chanzo cha picha, Reuters
Kuna dalili kubwa kwamba Rais wa Urusi Vladimir Putin aliamua kutuma kombora lililoangusha ndege ya MH17 mnamo 2014, wachunguzi wa kimataifa wanasema.
Ndege hiyo ilipigwa na kombora lililotengenezwa na Urusi kwa ajili ya Ukraine na kuua karibu watu 300.
Waendesha mashitaka walisema kuna ushahidi kwamba Bw Putin aliamua kutuma kombora kwa watu wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Moscow.
Hakuna maelezo yanayoainisha kwamba Bw Putin aliamuru ndege hiyo iangushwe.
Mnamo Novemba, mahakama ya Uholanzi iliwakuta na hatia ya mauaji wanaume watatu - Warusi wawili na mmoja kutoka Ukraine ingawa hawakuepo wakati MH17 inaangushwa.
Urusi, ambayo imekanusha kuhusika na kuangushwa kwa ndege hiyo, ilipuuzilia mbali maamuzi haya na kusema kuwa ni " kashfa tu" na ina uchochezi wa kisiasa.
Waendesha mashtaka walisema Jumatano kwamba walikuwa wamemaliza miongozo yote na hawakuweza kuendelea na kesi nyingine za uhalifu.
Ndege hiyo aina ya Boeing 777 ilikuwa ikiruka kutoka mji mkuu wa Uholanzi kuelekea Kuala Lumpur ilipopigwa na kombora lililotengenezwa kutoka Urusi hadi angani Julai 2014 wakati wa mzozo kati ya waasi wanaoiunga mkono Urusi na wanajeshi wa Ukraine katika eneo la Donbas nchini Ukraine.
Kulikuwa na abiria 298 na wafanyakazi 196 huku abiria wengi wakiwa wanatoka Uholanzi na wengine wakiwa wanatoka Malaysia, Australia, Uingereza, Ubelgiji na nchi zingine.
Katika taarifa yake, Timu ya Pamoja ya Upelelezi ilisema mahakama iliamua kwamba Urusi ilikuwa na "udhibiti wa jumla" juu ya Jamhuri ya Watu wa Donetsk, ambayo ilidhibiti eneo hilo mnamo Julai 2014.
Ilitaja katika mazungumzo ya simu yaliyorekodiwa ambapo maafisa wa Urusi walisema kwamba uamuzi wa kutoa msaada wa kijeshi "uko kwa Rais".
"Kuna habari kamili kwamba ombi la wanaotaka kujitenga liliwasilishwa kwa rais, na kwamba ombi hili lilikubaliwa," ilisema.
Lakini taarifa hiyo inaongeza kuwa haijulikani ikiwa ombi hilo "linataja wazi" mfumo uliotumika kuangusha MH17.
"Ingawa tunazungumza juu ya dalili kubwa, kiwango cha juu cha ushahidi kamili na wa mwisho haujafikiwa," wachunguzi walisema.
Soma zaidi:
- "Sio hatari sana." Kauli mpya za Putin kuhusu vita vya Ukraine
- Putin anafikiria nini na anapanga nini?
Mamluki maarufu wa Urusi Igor Mangushev auawa nchini Ukraine

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Mke wa Mangushev alilalamika kwamba hakuna mtu anayechunguza mauaji yake. Mamluki maarufu wa Urusi Igor Mangushev amefariki dunia hospitalini, siku chache baada ya kupigwa risasi ya kichwa akiwa karibu na eneo la Ukraine, marafiki zake wamesema.
Mke wa Mangushev Tatyana alielezea kifo chake kama mauaji.
Aliongoza kitengo cha kuzuia ndege zisizo na rubani huko Luhansk inayokaliwa, lakini pia alikuwa mmoja wa waanzilishi wa kikundi cha mamluki kilichopigana na vikosi vya Ukraine mnamo 2014.
Alipanda jukwaani msimu uliopita wa kiangazi akiwa ameshikilia fuvu la kichwa cha mtu.
Katika video iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii mwezi Agosti, Mangushev alirekodiwa akisema fuvu hilo lilikuwa la mpiganaji wa Ukraine aliyeuawa akitetea kiwanda cha chuma cha Azovstal katika bandari ya kusini ya Mariupol.
Mzalendo huyo mwenye itikadi kali alisema Urusi hapigani na watu, bali anakabiliana na wazo la Ukraine kama "taifa linalopinga Urusi", na haijalishi ni raia wangapi wa Ukraine watakufa.
Ufyatuaji risasi huo uliosababisha kujeruhiwa na hatimaye kifo cha Mangushev umezua uvumi mkubwa kuhusu ni nani aliyetekeleza shambulizi hilo katika kituo cha ukaguzi katika mji wa Kadiivka unaokaliwa na Urusi nchini Ukraine.
Mamlaka ya Urusi inachunguza mauaji hayo na hadi sasa haijasema lolote kuhusiana na kisa hicho.
Soma:
Msako wa wizi makaburini waanza Afrika Kusini baada ya maiti kuibiwa

Chanzo cha picha, South African Police Service
Polisi wa nchini Afrika Kusini wameanza kufanya uchunguzi na kutaka mashahidi kufuatia wizi wa maiti katika kaburi lililokuwa jimbo la kaskazini la Limpopo.
Ndugu yake mmoja aligundua hilo siku ya Jumapili alipokwenda makaburini kusafisha eneo hilo kwa ajili ya maandalizi ya shughuli ya kumbukumbu ya marehemu huyo.
Kwa mshtuko mkubwa alikuta shimo karibu na kaburi na mwili wa Modike Philemon Masedi ukiwa haupo. Washukiwa hao waliingia kwenye kaburi hilo kwa kukata uzio kisha kuchimba shimo karibu na kaburi ili kupata jeneza na kuiba maiti, polisi walisema.
Iliripotiwa kuwa Bw Masedi alifariki Januari 15 na akazikwa siku saba baadaye.
"Kilichosababisha tukio hili hakijajulikani kwa sasa," Brigedia Motlafela Mojapelo, msemaji wa polisi, alisema.
Mkuu wa polisi wa mkoa huo Thembi Hadebe amewataka watu katika eneo hilo "kuacha kunyoosheana vidole" ili kuepuka aina yoyote ya watu kujichukulia sheria mkononi.
Rais Zelensky azuru Uingereza kwa mara ya kwanza tangu Ukraine ivamiwe

Chanzo cha picha, REX/SHUTTERSTOCK
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky atawasili nchini Uingereza leo, ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwaka jana.
Serikali ya Uingereza ilisema kuwa itakutana na Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak na kutoa hotuba katika Bunge.
Pia imetangaza kuwa mafunzo ya Uingereza kwa vikosi vya Ukraine yataongezeka ili kuwafikia marubani wa ndege za kivita na wanamaji.
Inatarajiwa pia Uingereza itatangaza vikwazo vipya vinavyolenga Urusi kwa baadaye.
Mipango imetangazwa kuwafundisha marubani wa Ukraine kurusha ndege za kivita za kiwango cha Nato katika siku zijazo, ombi kuu kutoka Ukraine.
Nchi za Magharibi zimekuwa zikifikiria jinsi ya kuimarisha uungaji mkono kwa Ukraine, huku nchi hiyo ikijiandaa kwa mashambulizi mapya ya Urusi baadaye mwezi huu.
Kuongezwa kwa mpango wa mafunzo kutoka Uingereza kunaashiria mabadiliko, baada ya Uingereza kusema "haina maana" kutuma ndege zake Ukraine.
Wiki iliyopita, msemaji wa Bw. Sunak aliwaambia waandishi wa habari kwamba ndege za kijeshi za Uingereza "zilikuwa za kisasa sana na huchukua miezi kujifunza jinsi ya kuzitumia".
Uingereza tayari imetangaza mipango ya kutuma vifaru vya Challenger 2 nchini Ukraine, huku wanajeshi wa Ukraine wakipokea mafunzo ya jinsi ya kuziendesha.
Alisema Bw Sunak atatoa fursa ya kuipatia Ukraine "uwezo wa masafa marefu zaidi" ili kuvuruga uwezo wa Urusi kulenga miundombinu muhimu ya kitaifa ya Ukraine.
Iliongeza kuwa mafunzo ya Uingereza yataongezwa mwaka huu, na wanajeshi 20,000 zaidi wa Ukraine watapewa mafunzo.
Soma zaidi:
- Vita vya Ukraine: Rais Zelensky alifikaje Washington?
- Mizinga kutoka Ujerumani, Marekani na Uingereza inavyoweza kubadili vita vya Ukraine
Tetemeko la ardhi Uturuki:Erdogan ‘anafaa kuwajibikia hili' kiongozi wa upinzani asema

Chanzo cha picha, Getty Images
Hasira inaongezeka nchini Uturuki kutokana na serikali kushindwa kujiandaa baada ya maelfu ya watu kufariki katika matetemeko mawili makubwa ya ardhi siku ya Jumatatu.
Idadi ya vifo nchini Uturuki imeongezeka hadi 6,957, kulingana na shirika la maafa nchini humo.
Takwimu hizo zimekuja wakati Rais Recep Tayyip Erdogan akiwasili katika mojawapo ya maeneo yaliyoathirika zaidi.
Lakini kuna kuongezeka hasira kisiasa na chini kwa chini kwa majibu na maandalizi ya serikali yake.
Wengi katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi wamepinga kile walichosema ni hatua za polepole kutoka kwa Mamlaka ya Kudhibiti Maafa na Dharura ya Uturuki (AFAD).
Katika bandari ya kusini mwa Uturuki ya Iskenderun siku ya Jumanne Arzu Dedeoglu alisema wapwa zake wawili walinaswa chini ya vifusi. Familia yake ilikuwa imekodisha tinga tinga kuchimba vifusi kutumia na rasilimali zao ili kuwaokoa watu lakini alisema maafisa hawakuwaruhusu kufanya hivyo.
"Tulingoja hadi jioni, lakini hakuna mtu aliyekuja," Bi Dedeoglu alisema. "Tulileta tinga tinga kwa njia zetu wenyewe, lakini hawakutaka tuitumie - walituzuia. Tuna watoto wawili chini ya vifusi: binti za dada yangu, Ayşegül na İlayda.
"Wamekwenda sasa, wamekwenda."

Chanzo cha picha, EPA
Huduma za dharura zilipowasili hatimaye, Bi Dedeoglu alipiga kelele kwamba "wamechelewa sana". Wafanyakazi wa uokoaji walisimama kwa muda, lakini familia ya wasichana hao iliwasihi wasiache.
"Tafadhali msiondoke - labda watoto wangu bado wako hai," mama yao alisema.
Wakati wengi wakishutumu serikali kwa kujibu polepole sana tetemeko hilo, wengine wanasema serikali haikujiandaa vya kutosha mapema.
"Ikiwa kuna mtu mmoja anayehusika na hili, ni Erdogan," alisema Kemal Kilicdaroglu, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Uturuki.
Bw Erdogan ametangaza hali ya hatari ya miezi mitatu katika mikoa 10 iliyoathiriwa zaidi na tetemeko la ardhi. Itakamilika kabla ya uchaguzi wa Mei 14, wakati kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 68 atajaribu kusalia madarakani baada ya miaka 20.
Soma zaidi:
- Waokoaji wampa mtoto maji kwa kifuniko cha chupa akiwa chini ya kifusi
- 'Mmechelewa... Kwanini hamkuja mapema?'
Mgogoro wa naira wa Nigeria: Mahakama ya Juu yasitisha tarehe ya mwisho kubadilisha noti

Chanzo cha picha, Getty Images
Mahakama ya Juu Zaidi nchini Nigeria imesitisha kwa muda makataa ya Ijumaa ya kuacha kutumia noti za zamani, jambo ambalo lilikuwa limesababisha mzozo wa fedha nchini humo.
Benki nyingi hazijapata noti mpya za naira za kutosha, na kusababisha matukio ya kukata tamaa na machafuko huku watu wakijaribu kuzipata.
Video zilitolewa za watu wakivua nguo kwenye benki katika maandamano na mapigano kwenye ATM.
Machafuko hayo yalisababisha wasiwasi kuwa huenda yakaathiri uchaguzi wa mwezi huu, kwani Wanigeria wengi hawana akaunti za benki.
Benki Kuu ilitangaza sarafu iliyobuniwa upya katika jaribio la kudhibiti mfumuko wa bei, ambao kwa sasa unaendelea kwa 20%.
Kesi hiyo iliyoletwa na majimbo ya kaskazini ya Kaduna, Kogi na Zamfara imeahirishwa hadi Februari 15.
Soma zaidi:
- Benki kuu Nigeria yatoa fedha kupambana na Boko Haram
LeBron James avunja rekodi ya ufungaji wa muda wote katika NBA

Chanzo cha picha, Getty Images
LeBron James amekuwa mfungaji bora wa muda wote wa NBA, akipita rekodi ya Kareem Abdul-Jabbar ya miaka 39.
Nyota huyo wa Los Angeles Lakers James, 38, alifikisha pointi 38 katika kushindwa 133-130 na Oklahoma City Thunder na kuvuka alama ya Abdul-Jabbar ya 38,387.
Awali Abdul-Jabbar alivunja rekodi ya kufunga mabao Aprili 1984, miezi minane kabla ya James kuzaliwa.
"Kuweza kuwa mbele ya gwiji na mtu stadi kama Kareem, ina maana kubwa kwangu," alisema James.
James mwenye hisia aliinua mikono yote miwili kusherehekea huku Abdul-Jabbar mwenye umri wa miaka 75, ambaye alikuwa kwenye mechi katika uwanja wa nyumbani wa Lakers, alisimama na kupiga makofi.
Kulikuwa na mapumziko mafupi kwa ajili ya sherehe ya kuashiria mafanikio, huku James akichukua kipaza sauti ili kutoa hotuba fupi.
Soma zaidi:
- LeBron James: Mabadiliko ya nyota wa NBA aliyeanza kama kijana wa shule mwenye kipaji
- Fainali NBA: Los Angeles Lakers washinda Miami Heat
DR Congo imezisimamisha chaneli za Runinga za Rwanda
Mamlaka ya udhibiti wa vyombo vya habari katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameiagiza ofisi ya ndani ya watoa satelaiti za televisheni la Canal+ kuondoa chaneli za Rwanda ambazo zinaonekana nchini humo.
Kusimamishwa kwa chaneli hizo kutaendelea kwa muda wa siku 90 na kunaweza kufanywa upya kulingana na hali itakavyoendelea, mdhibiti, CSAC RDC, alisema katika taarifa.
Kinshasa inashutumu kuwa chaneli za Rwanda zinachochea uasi wa raia, miongoni mwa madai mengi, tovuti ya Chronicles inaripoti.
Canal+ ina takriban chaneli 10 za Runinga za Rwanda, ikiwa ni pamoja na shirika la utangazaji la serikali ya Rwanda RBA, ambazo hupeperusha vipindi vya habari na maoni kuhusu vita vinavyoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, tovuti ya habari imeongeza.
DR Congo, Marekani na wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanaishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi la waasi la M23 katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.
Rwanda imekanusha hilo na kuilaumu serikali ya Kongo kwa machafuko katika eneo lenye utajiri wa madini mashariki mwa DR Congo.
Soma zaidi:
- Ipi nafasi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutatua mvutano wa Congo na Rwanda?
- Tunachokifahamu kuhusu kinachoendelea mashariki mwa DRC
Video: Umati wa watu wajawa na furaha huku familia ikiokolewa katika vifusi nchini Syria
Video ya kusisimua imeibuka wakati familia ya watu sita ilipotolewa wakiwa hai kutoka kwa vifusi huko Idlib, Syria.
Umati wa watu ulilipuka kwa furaha huku watu wazima wawili na watoto wanne wakiokolewa na kuingizwa kwenye ambulensi zilizokuwa zikisubiri.
Maelezo ya video, Umati wapiga kelele za 'Mungu ni mkubwa' wakati familia moja ilipookolewa katika vifusi Syria Vyanzo vya Marekani vyasisitiza puto ya China lilikuwa la kijeshi

Chanzo cha picha, US FLEET FORCES COMMAND
Vyanzo vya kijasusi vya Marekani vimesisitiza kuwa puto lililodunguliwa siku ya Jumamosi lilitumiwa na jeshi la China kwa ajili ya ujasusi.
Maafisa ambao hawakutajwa majina waliliambia gazeti la Washington Post wanaamini kwamba puto kama hizo zilitumika kukusanya taarifa za kijasusi kwenye maeneo yanayohusika kimkakati. Wao ni pamoja na Japan, India, Taiwan na Ufilipino.
Maafisa wa China tayari wamekanusha kutumia puto hizo kwa uchunguzi. Afisa mmoja aliliambia gazeti la Washington Post kwamba jumuiya ya kijasusi ya Marekani inaamini kuwa baadhi ya puto hizo zilikuwa zikisafirishwa kutoka Hainan, kisiwa cha kusini mwa China ambacho kina kambi ya jeshi la wanamaji.
Ikimnukuu afisa mkuu wa utawala wa Biden ambaye hakutajwa jina, Habari za CBS zilithibitisha kwamba jumuiya ya kijasusi ya Marekani inaamini kuwa puto hiyo ilikuwa sehemu ya "mpango wa uchunguzi wa angani unaoendeshwa na Jeshi la Ukombozi la Watu kutoka Hainan".
Siku ya Jumatatu, Marekani ilitoa taarifa kwa nchi washirika 40 kuhusu madai ya ujasusi, afisa mkuu wa utawala wa Biden alithibitisha kwa CBS News.
Katika muhtasari huo, Naibu Katibu wa Jimbo Wendy Sherman pia alifichua puto moja ilizunguka sayari mnamo 2019, ikisafiri juu ya Hawaii na Florida. Kulingana na afisa wa utawala wa Biden, kundi la viongozi wa Bunge la Congress la Marekani wanaohusika na kusimamia masuala ya kijasusi ya kitaifa, wanaojulikana kama Genge la Wanane, watafahamishwa kuhusu maendeleo siku ya Jumatano, na Congress itasasishwa siku ya Alhamisi.
Wiki iliyopita, Pentagon ilisema puto la pili la kijasusi la China limeonekana juu ya Costa Rica na Venezuela.
Kupatikana kwa puto zinazodaiwa kuwa za kijasusi kumesababisha mzozo wa kidiplomasia kati ya Marekani na China.
Tazama: Picha kabla na baada ya tetemeko la ardhi nchini Uturuki zinaonyesha kiwango cha uharibifu
Matetemeko mawili ya ardhi yenye ukubwa mkubwa ambayo yalitikisa Uturuki siku ya Jumatatu yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 8,000 huku wengine wakiendelea kutolewa kwenye vifusi
Majengo kadhaa yaliporomoka, tazama majengo haya kabla na baada ya tetemeko la Ardhi kukumbuka maeneo hayo.




Habari za hivi punde, Tetemeko la ardhi Uturuki na Syria: Idadi ya vifo ni zaidi ya 9,000
Zaidi ya watu 9,000 wanajulikana kuuawa nchini Uturuki na Syria kufuatia tetemeko la ardhi la Jumatatu. Idadi ya watu waliouawa nchini Uturuki imeongezeka hadi 6,957, kulingana na shirika la maafa nchini humo.
Ni vigumu kuthibitisha idadi hiyo nchini Syria, lakini vyombo vya habari vya serikali na kundi la uokoaji vinasema takriban watu 2,500 wamefariki..
Msafara wa vikosi vya Umoja wa mataifa washambuliwa tena na umati wa watu DRC watatu wafariki
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Samba Cyuzuzo
- Nafasi, BBC Great Lakes

Chanzo cha picha, Getty Images
Watu watatu wamefariki dunia, na malori manne yaliteketezwa kwa moto katika shambulio lililofanywa na umati wa watu dhidi ya msafara wa vikosi vya Umoja wa Mataifa Jumanne jioni huko Minigi takriban kilomita 7 kaskazini mwa Goma, mashariki mwa DR Congo.
Vikosi vya Umoja wa Mataifa nchini DRC, Monusco, vimesema msafara huo ulikuwa unaelekea Goma wakati "watu waliokuwa wakiandamana" walifunga barabara "kwa mawe makubwa" kabla ya kuanza "kushambulia".
"Kwa bahati mbaya, watu watatu (raia) walikufa katika mzozo huo" wakati vikosi "vilikuwa vikijaribu kulinda msafara", taarifa ya kikosi hicho ilisema.
Maandamano mapya yametikisa Goma tangu Jumatatu, huku waasi wa M23 wakiukaribia mji huo kutoka magharibi.
Waandamanaji wanatoa wito kwa Vikosi vya Kanda ya Afrika Mashariki, na vikosi vya Umoja wa Mataifa kupambana na waasi.
Waasi wa M23 wamemshutumu Rais Felix Tshisekedi kwa "kuchochea machafuko" kwa kuunga mkono maandamano "badala ya kuhimiza amani" kwa njia ya mazungumzo.
Mamlaka ya DRC inaishutumu jirani yake Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23, jambo ambalo Kigali imekuwa ikikanusha.

Chanzo cha picha, BBC Monitoring
Tetemeko la ardhi Uturuki: Mbwa aliyeokoa makumi ya watu katika tetemeko la mwaka 2017 Mexico apelekwa Uturuki
Maelezo kuhusu taarifa - Author, By Vanessa Buschschlüter
- Nafasi, BBC News Online Latin America editor

Chanzo cha picha, TWITTER/M_EBRARD
Mexico inatuma baadhi ya mbwa wake maarufu wa utafutaji na uokoaji nchini Uturuki kusaidia kutafuta watu waliofukiwa chini ya vifusi kufuatia tetemeko la ardhi la Jumatatu.
Ndege iliyokuwa na mbwa 16 ilipaa kutoka mji wa Mexico City mapema Jumanne.
Mexico, ambayo inakabiliwa na matetemeko ya ardhi, ina timu maalum za kiraia na kijeshi ambazo mara nyingi hutumwa kusaidia wakati majanga yanapotokea.
Mbwa hao walivutia mioyo ya watu wa Mexico wakati wa tetemeko la ardhi la 2017 nchini humo, walipookoa maisha ya watu kadhaa.
Mbwa anayeitwa Frida alipata umaarufu kimataifa alipoonekana akiwatafuta manusura katika Jiji la Mexico akiwa amevalia miwani na buti za kujikinga.

Chanzo cha picha, Getty Images
Jeshi la wanamaji lilimsifu Frida kwa kuokoa maisha ya watu 12 na kupata miili 40 katika operesheni katika nchi za Mexico, Haiti, Guatemala na Ecuador.
Wakati Frida alikufa kutokana na uzee mwaka jana, angalau mmoja wa mbwa wenzake waliokuweko katika tetemeko la Mexico la mwaka 2017 atakuwa sehemu ya timu ya Navy ya Mexico inayosafiri kwenda Uturuki.
Ecko, mbwa mwenye asili ya Ubelgiji, Malinois, alionekana kwenye uwanja wa ndege wa Mexico City akiwa na mhudumu wake wa jeshi la wanamaji.

Chanzo cha picha, TWITTER/M_EBRARD
Lakini mbwa hao hawapelekwi kijeshi tu. Kikundi cha utafutaji na uokoaji cha kiraia kinachoitwa Los Topos de Tlatelolco (The Moles of Tlatelolco) pia kiko njiani.
Kikundi cha wafanyakazi hao wa kujitolea wenye uzoefu mkubwa walikuwa wamemtumia ujumbe Waziri wa Mambo ya Nje wa Mexico Marcelo Ebrard kutaka kushiriki kutoa msaada wao.
Ndani ya saa chache, Bw Ebrard alijibu kwamba usafiri ulikuwa umepangwa kwa ajili yao kwa usaidizi wa ubalozi wa Uturuki katika Jiji la Mexico.

Chanzo cha picha, TWITTER/M_EBRARD
Mexico sio nchi pekee inayotuma mbwa kusaidia katika juhudi za uokoaji nchini Uturuki na Syria. Croatia, Jamhuri ya Czech, Ujerumani, Ugiriki, Libya, Poland, Uswizi, Uingereza na Marekani pia zinapeleka mbwa na wakiwa na waongozaji wao.
Rwanda imemtoza mshatakiwa faini ya dola 900 kwa kosa la kifo cha mwandishi wa habari

Chanzo cha picha, John Williams Ntwali/Facebook
Mahakama nchini Rwanda imemtoza faini ya $900 (£746) mwanamume mmoja baada ya kukiri kosa la kuua bila kukusudia kutokana na kifo cha mwandishi wa habari aliyekuwa akiikosoa serikali.
John Williams Ntwali aliuawa mwezi uliopita baada ya gari la mwendo kasi kugonga pikipikiki ya abiria aliyokuwa amepanda.
Mamlaka ilisema ilikuwa ajali ya barabarani. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yaliitisha uchunguzi huru, yakielezea kifo chake kuwa cha kutiliwa shaka.
Human Rights Watch ilisema Bw Ntwali amekuwa akitishwa mara kwa mara na kushambuliwa katika vyombo vya habari vinavyounga mkono serikali kutokana na ripoti yake ya uchunguzi.
Kesi hiyo haikuwa wazi kwa umma lakini baadhi ya waandishi wa habari walialikwa kushuhudia kusomwa kwa hukumu hiyo.
Tetemeko la ardhi Uturuki: Kipa wa Malatyaspor Ahmet Turkaslan afariki dunia

Chanzo cha picha, Yeni Malatyaspor
Mlinda mlango wa Uturuki Ahmet Eyup Turkaslan amefariki dunia kufuatia tetemeko la ardhi lililotokea Jumatatu nchini kwao, klabu yake ya Yeni Malatyaspor imethibitisha.
Zaidi ya watu 5,000 wamepoteza maisha nchini Uturuki na Syria kufuatia tetemeko hilo la ardhi.
"Kipa wetu, Ahmet Eyup Turkaslan, alipoteza maisha yake baada ya kukumbwa na tetemeko la ardhi. Pumzika kwa amani," klabu hiyo ilisema kwenye mtandao wake wa Twitter na kuongeza "Hatutakusahau, ni mtu mzuri".
Turkaslan, 28, alichezea klabu ya daraja la pili ya Uturuki Yeni Malatyaspor mara sita baada ya kujiunga nayo mwaka 2021.
Winga wa zamani wa Crystal Palace na Everton, Yannick Bolasie, ambaye kwa sasa anachezea timu ya daraja la pili ya Uturuki, Caykur Rizespor,nae aliandika kwenye mtandao wake wa Twitter: "RIP kaka Eyup Ahmet Turkaslan.
"Unamuoa mtu kwenye benchi la akiba sasa, baadaye unaambiwa ametutoka." Bolasie aliongeza: "Salamu zangu za rambirambi kwa familia yake yote na wachezaji wenzake wa Yeni Malatyaspor. Inasikitisha."
Tetemeko la ardhi Uturuki na Syria: Waokoaji waendelea kuchimba vifusi huku idadi ya waliofariki ni zaidi ya 7,800

Chanzo cha picha, Reuters
Idadi ya waliofariki kutokana na tetemeko kubwa la ardhi kusini mwa Uturuki na Syria iliongezeka hadi zaidi ya watu 7,800 siku ya Jumanne huku waokoaji wakifanya kazi dhidi ya wakati katika hali mbaya ya msimu wa baridi kuchimba ili kuokoa manusura kutoka kwenye vifusi vya majengo yaliyoporomoka.
Kadiri ukubwa wa maafa ulivyozidi kudhihirika zaidi, idadi ya waliofariki ilionekana uwezekano wa kuongezeka kwa kiasi kikubwa. Afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa alisema huenda maelfu ya watoto wamefariki.
Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan alitangaza hali ya hatari katika majimbo 10. Lakini wakaazi katika miji kadhaa iliyoharibiwa ya Uturuki walionyesha hasira na kukata tamaa kwa kile walichosema ni jibu la polepole na lisilotosha kutoka kwa mamlaka juu ya tetemeko baya zaidi kuwahi kuikumba Uturuki tangu 1999.
Erdogan alitangaza majimbo 10 ya Uturuki kuwa eneo la maafa na akaweka hali ya hatari kwa miezi mitatu ambayo itairuhusu serikali kupita bunge katika kutunga sheria mpya na kuweka kikomo au kusimamisha haki na uhuru.
Serikali itafungua hoteli katika kitovu cha utalii cha Antalya ili kuwahifadhi kwa muda watu walioathiriwa na tetemeko hilo, alisema Erdogan, ambaye anakabiliwa na uchaguzi wa kitaifa katika muda wa miezi mitatu.
Idadi ya vifo nchini Uturuki iliongezeka hadi 5,894, Makamu wa Rais Fuat Oktay alisema. Zaidi ya 34,000 walijeruhiwa. Nchini Syria, idadi ya waliouawa ilikuwa angalau 1,932, kulingana na serikali na huduma ya uokoaji katika eneo linaloshikiliwa na waasi kaskazini magharibi.
Hujambo, na karibu katika taarifa zetu za moja kwa moja, kufahamu yaliyojiri kote ulimwenguni.
