Vita vya Ukraine: Marekani haikuhimiza wala kuiwezesha Ukraine kushambulia ndani ya Urusi - Blinken

Washington "haijahimiza wala kuwezesha" Ukraine kufanya mashambulizi ndani ya Urusi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema.

Moja kwa moja

  1. Mwanamuziki D'Banj akamatwa kwa kashfa ya ufisadi Nigeria

    w

    Chanzo cha picha, D'BANJ/INSTAGRAM

    Tume Huru ya Ufisadi na Makosa Mengine nchini Nigeria (ICPC) imethibitisha kwa BBC idhaa ya Pidgin kumshikilia mwanamuziki wa Nigeria Daniel Oyebanjo maarufu kama D'Banj.

    Taarifa ya ICPC ilisema inamshikilia mwimbaji kwa uchunguzi wa ulaghai unaohusishwa na Mpango wa N-Power, mabilioni ya pesa ya kuwezesha vijana Nigeria.

    N-Power ni mpango ambao Rais Muhammadu Buhari alianzisha tarehe 8 Juni, 2016, kushughulikia masuala ya ukosefu wa ajira kwa vijana na uwezeshaji, na kusaidia kuongeza maendeleo ya kijamii.

    Katika taarifa ilitolewa na kaminshna wa ICPC, Azuka Ogugua, tume ilieleza chanzo cha kuzuiliwa kwa D'banj.

    "Takriban watu 10 wamealikwa na ICPC katika miezi michache iliyopita kuhusiana na ulaghai wa N-Power, na wamepewa dhamana ya kiutawala baada ya kuzuiliwa kwao. Mialiko kadhaa kwa Bw Oladipo Daniel Oyebanjo, kufika mbele ya timu ya wachunguzi ilipuuzwa na kutoheshimiwa.

    “Bw Oyebanjo (D'banj) alijisalimisha na kuzuiliwa katika Makao Makuu ya ICPC mnamo Jumanne, 6 Desemba 2022, na kwa sasa anasaidia wapelelezi kubaini mazingira ya madai ya ulaghai ya walalamishi.

  2. Vita vya Ukraine: Marekani haikuhimiza wala kuiwezesha Ukraine kushambulia ndani ya Urusi - Blinken

    w

    Chanzo cha picha, MAXAR TECHNOLOGIES/HANDOUT VIA REUTERS

    Washington "haijahimiza wala kuwezesha" Ukraine kufanya mashambbulio ndani ya Urusi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema.

    Alikuwa akizungumza muda mfupi baada ya Moscow kuishutumu Kyiv kwa kufanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kwenye viwanja vitatu vya ndege vya Urusi, viwili vikiwa mamia ya maili kutoka Ukraine.

    Ukraine haijatoa maoni yoyote kuhusu suala hilo.

    Rais wa Urusi Vladimir Putin ameonya mara kwa mara Marekani na washirika wake kutovuka "mstari mwekundu" kwa kusambaza silaha za masafa marefu kwa Ukraine.

    Muungano wa kijeshi wa Nato unaoongozwa na Marekani umekataa kutoa silaha kama hizo kwa Kyiv, huku kukiwa na wasiwasi kwamba hii inaweza kusababisha kuongezeka kwa Urusi yenye silaha za nyuklia ambayo iliivamia Ukraine mnamo 24 Februari.

    Milipuko miwili ya uwanja wa ndege wa Urusi iliripotiwa Jumatatu, katika mikoa ya Ryazan na Saratov.

    Maeneo hayo yana washambuliaji wa kimkakati wanaotumiwa kufanya mashambulizi ya mara kwa mara ya makombora kwenye miundombinu muhimu ya nishati ya Ukraine.

    Urusi ilisema kulikuwa na shambulio jingine siku ya Jumanne, katika eneo la Kursk linalopakana na Ukraine.

    Shambulizi la hivi punde la kombora la Urusi dhidi ya Ukraine lilitokea siku ya Jumatatu, wakati makombora 70 yaliporushwa kwenye shabaha kote nchini.

    Watu wanne waliuawa, maafisa wa eneo hilo walisema.

    Mamilioni ya watu kote nchini sasa hawana umeme na maji ya bomba, na hivyo kuzua hofu kwamba watu wanaweza kufa kutokana na baridi kali.

    Blinken Alisema "Hatujawahimiza wala kuwawezesha Waukraine kushambulia ndani ya Urusi, lakini jambo muhimu ni kuelewa watu wa Ukraine wanaishi kila siku kutokana na uvamizi unaoendelea wa Urusi dhidi ya nchi yao." Alisema alikuwa amedhamiria kwamba Waukraine wana "vifaa ambavyo wanahitaji kujilinda, kutetea eneo lao, kutetea uhuru wao."

    Akizungumza pamoja naye, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin alisisitiza kuwa Marekani haitaizuia Ukraine kuendeleza uwezo wake wa kufanya mashambulizi ya masafa marefu. "Jibu fupi ni hapana. Hatufanyi hivyo kabisa," Bw Austin alisema, akiongeza kuwa Washington tayari ilikuwa imeipa Ukraine zaidi ya $19bn (£16bn) katika usaidizi wa usalama.

  3. Aliyemuua shujaa wa ukombozi Afrika kusini aachiliwa huru

    w

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Janusz Walus amesema watu weusi na weupe wanapaswa kuishi tofauti

    Wizara ya sheria ya Afrika Kusini imethibitisha kuwa mtu aliyemuua shujaa wa kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini Chris Hani ameachiliwa huru kwa msamaha.

    Uamuzi wa mwezi uliopita wa mahakama ya kikatiba kumwachilia Janusz Walus ulizua ukosoaji mkubwa nchini Afrika Kusini.

    Mjane wa Bw Hani alieleza kuwa ni jambo la kishetani.

    Mwanachama huyo mkuu maarufu wa mrengo wa kijeshi wa ANC aliuawa kwa kupigwa risasi mwaka 1993.

    Mauaji hayo yalikuwa jaribio lililofeli la kuzuia nchi kubadilika kutoka utawala wa wazungu wachache hadi utawala wa kidemokrasia.

    Wiki jana Bw Walus alipata matibabu katika hospitali ya gereza baada ya kudungwa kisu na mfungwa mwenzake.

  4. Mtoto wa rais wa zamani wa Msumbiji ahukumiwa miaka 12 jela

    Mahakama ya Msumbiji imemhukumu mtoto wa kiume wa rais wa zamani na watu wengine kifungo kwa kuhusika katika kashfa ya rushwa ya "tuna bond".

    Mwana wa Rais wa zamani Armando Guebuza, Ndambi Guebuza, na wakuu wawili wa zamani wa ujasusi, Gregorio Leao na Antonio do Rosario, kila mmoja alifungwa miaka 12 jela.

    Washtakiwa wenzake nane walitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha kati ya miaka 10 na 12.

    “Uhalifu uliofanywa umeleta matokeo ambayo madhara yake yatadumu kwa vizazi,” Jaji Efigenio Baptista alisema wakati akitoa hukumu hizo.

    Jumla ya watu 19 walikuwa wamefunguliwa mashtaka ya ulaghai, ubadhirifu na utakatishaji fedha kwa madai ya majukumu yao katika kashfa kubwa ya kifedha ya Msumbiji.

    Wanane wameachiliwa kwa kukosa ushahidi.

    Kashfa hiyo ilihusisha nchi hiyo kukopa zaidi ya $2bn ($1.6bn) kutoka kwa benki za kimataifa, nyingi bila kujua au kuidhinishwa na bunge la nchi hiyo, na kusababisha mzozo wa kiuchumi.

    Kashfa ilitokeaje?

    Kati ya 2013-2014, kampuni tatu mpya zilizoanzishwa zilichukua $ 2.2bn (£ 1.5bn) ya deni, nyingi bila ujuzi au idhini ya bunge la nchi.

    Pamoja na hayo, serikali ya Msumbiji ilisimama kama mdhamini wa mikopo hiyo, ikimaanisha kuwa serikali ingelipa pesa hizo ikiwa mambo yataenda vibaya.

    Pesa hizo zilidaiwa kutumika kununua kiwanda kikubwa cha samaki aina ya jodari na meli ya usalama wa baharini, na pia kufadhili mikataba mingine inayohusisha kampuni ambazo jimbo hilo linamiliki hisa.

    Mnamo 2016, serikali ilibadilisha baadhi ya deni kwa bondi ya kawaida, iliyotolewa na serikali.

    Muda mfupi baadaye, ilikubali kiwango kamili cha ukopaji, na kusababisha mgogoro wa kiuchumi nchini Msumbiji.

    Sarafu ya nchi ilipoteza theluthi moja ya thamani yake, mfumuko wa bei uliongezeka na wafadhili wa kigeni wakajiondoa.

    Wakaguzi pia waliripotiwa kugundua $500m ya pesa hizo hazikuwepo.

    Mikopo hiyo ilitolewa na Credit Suisse na benki ya Urusi VTB, huku mabenki watatu ya zamani ya Credit Suisse wakikiri mashtaka ya Marekani ya utakatishaji fedha juu ya kesi hiyo.

    Mwishoni mwa mwaka jana mamlaka ya Uingereza iliitoza benki ya uwekezaji faini ya $178m kutokana na kashfa ya ufisadi wa samaki aina ya jodari.

    Benki hiyo pia iliamriwa kufuta deni la $200m "lililochafuliwa na ufisadi" ambalo lilikuwa linadaiwa na Msumbiji.

    Faini hiyo ilikuwa sehemu ya maafikiano ya $475m na wadhibiti wa Uingereza, Uswisi na Marekani.

  5. Kenya kupiga marufuku shule za bweni kwa wanafunzi chini ya darasa la tisa

    w

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kenya inapanga kukomesha shule za bweni mwaka ujao kwa wanafunzi wa hadi darasa la tisa (kama miaka 14-15), ambazo zinajumuisha shule za msingi na za upili.

    Katibu Mkuu wa Elimu Belio Kipsang aliambia kongamano la walimu wakuu kwamba wazazi watalazimika kuwapeleka watoto wao shule za kutwa.

    Alisema serikali imefanya uamuzi wa kuruhusu watoto kuwa chini ya uangalizi wa wazazi au walezi wao.

    Watoto kutoka jamii za wafugaji wa kuhamahama hata hivyo hawatashirikishwa kwenye sheria sheria hizo.

    Kenya ina takriban 28% ya watoto wake wa shule za msingi katika vituo vya bweni, alisema, akibainisha kuwa idadi hiyo ilikuwa kubwa ikilinganishwa na nchi nyingine.

    Alisema ni jukumu la wazazi kutunza watoto wao, kama waelimishaji wa kwanza, akisema "hatuwezi kutoa malezi kwa walimu".

    "Tunahitaji kuanza kujumuika kwamba tunahitaji kuwa na watoto wetu, na njia pekee ya kuwa na watoto hawa ni wao kuwa katika mazingira ya shule ya kutwa," alisema.

  6. Wanawake waishtaki Apple baada ya wapenzi wao kuwachunguza kwa vifaa vyake

    AirTags

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Apple inashitakiwa na wanawake wawili wanaodai kuwa AirTags zilitumika kuwafuatilia.Vifaa wadogo wameundwa kuwekwa kwenye pochi au funguo, ili kuwazuia kupotea. Hata hivyo mapema mwaka huu BBC iliripoti kuwa wanawake kadhaa walizibaini AirTags zikiwafuatilia.

    Apple bado haijajibu ombi la BBC la kuomba maoni yao. Hapo awali kampuni hiyo ilisema kwamba AirTags zake zina hatua kadhaa zinazozuia ufuatiliaji usiohitajika.

    Kesi hiyo iliwasilishwa katika mahakama ya San Francisco. Wanawake hao wawili wanasema AirTags zilitumiwa na wapenzi wao wa zamani kuwafuatilia. Pia wamesema kwamba AirTags zimehusishwa na mauaji ya wanawake mwaka huu huko Akron, Ohio na Indianapolis.

    Apple imekuwa ikifahamu kwa muda mrefu, kabla ya kutoa AirTags, kwamba zinaweza kutumika kwa shughuli za uhalifu. Wakati wa kuzitoa, Apple ilisema kwamba "AirTags zimeundwa kufuatilia vitu sio watu".

    Vifaa hutumia mawimbi ya bluetooth ambayo yanaweza kutambuliwa na Apple's Find My Network. Kampuni hiyo inasema imeunda safu kadhaa za ulinzi ambazo hulinda watu dhidi ya kufuatiliwa.

    AirTags hupiga kelele kubwa zinapotenganishwa na mmiliki kwa muda. Iwapo AirTag itapatikana kwa mtu ambaye AirTag haijasajiliwa naye, ujumbe unapaswa kuonekana kwenye simu yake ukimjulisha.

    Hapo awali BBC ilizungumza na wanawake kadhaa ambapo mmoja alisema aliipata AirTag ikiwa imefungwa kwenye koti lake. "Ikiwa utaunda bidhaa ambayo ni muhimu kwa kufuatilia vitu vilivyoibiwa, basi utakuwa umeunda zana nzuri ya kuvizia," Eva Galperin, Mkurugenzi wa Usalama wa Mtandao katika Wakfu wa Electronic Frontier, aliiambia BBC mapema mwaka huu.

  7. Habari za hivi punde, Ujerumani yawakamata washukiwa 25 kwa kupanga njama ya mapinduzi

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Zaidi ya polisi 3,000 walishiriki katika uvamizi wa nyumba 130 kote Ujerumani (picha ya maktaba)

    Watu 21 wamekamatwa katika uvamizi uliofanyika kote nchini Ujerumani wakishukiwa kupanga njama ya kuipindia serikali.

    Ripoti za Ujerumani ziasea kwua kundi la mrengo wa kulia zaidi na wanajeshi wa zamani walipanga kuvamia jengo la bunge.

    Mwanaume mmoja Mjerumani aliyetambuliwa kama mwanamfalme Heinrich XIII, 71, anadaiwa kuwa kiongozi wa mpango huo wa mapinduzi.

    Kulingana na waendesha mashitaka wa shirikisho, ni mmoja wa watu wawili wanaodaiwa kuwa viongozi wa wale ambao wamekamatwa katika majimbo yote 11 ya Ujerumani.

    Wapangaji wa njama hiyo pia wanasemekana kuwa ni pamoja na wajumbe wa vuguvugu lenye itikadi kali la Reichsbürger [Raia wa Reich] , ambalo kwa muda mrefu limekuwa likikabiliana na polisi kwa mashambulio ya ghasia na kueneza nadharia za njama za ubaguzi. Pia wamekataa kutambua taifa la kisasa la Ujerumani.

  8. Kenya kuzindua kampeni ya chanjo surua huku ikikabiliwa na mlipuko

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wizara ya afya nchini Kenya itazindua kampeni ya wiki mbili dhidi ya ugonjwa surau ikiwalenga watoto milioni 1.2 m wenye umri wa miezi tisa handi miaka mitano.

    Hii inafuatia mlipuko wa ujongwa huo kuzikumba kaunti 7 ambapo 90% ya watoto wenye chini ya umri wa miaka mitano walikosa dozi mbili za chanjo hiyo.

    Ukame unaoendelea katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo umeifanya shughuli ya utoaji wa chanjo hiyo kuwa ngumu kwa wahudumu wa afya kutoa chanjo hiyo muhimu kwa maisha ya watoto, kutokana na watu kuhama kutoka sehemu moja kuelekea sehemu nyinginekusaka chakula na maji.

    Wizara ya afya bado haijafichua ni visa au vifo vingapi viliripotiwa , lakini inawataka wazazi na walezi kuhakikisha kuwa watoto wanapata chanjo ili kudhibiti mlipuko wa maradhi hayo.

    Surua ni ugonjwa unaoambukiza haraka na husababisha mgonjwa kuwa vipimo vya juu vya joto na upele. Utoaji wa chanjo umepungua kote duniani tangu lilipotokea janga la Covid – 19.

    Kampeni inatarajiwa kuanza Ijumaa na kumalizika tarehe 18 Disemba.

  9. China inalegeza vikwazo vya Covid baada ya maandamano

    Uchina inalegeza vikwazo vya Covid baada ya maandamano dhidi ya sera yake ya sifuri-Covid

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Uchina inalegeza vikwazo vya Covid baada ya maandamano dhidi ya sera yake ya zero-Covid

    China inasema watu walio na dalili ya Corona isiyo kali sasa wataweza kutengwa nyumbani badala ya katika vituo vya serikali katika hatua ya kurahisisha sera yake ya Zero-Covid.

    Watu hao sasa wataweza kujitenga nyumbani na kutuma ripoti ya matokeo ya vipimo.

    Nchi pia imefuta mahitaji ya watu kufanyiwa vipimo vya PCR katika maeneo mengi ya umma isipokuwa hospitalini na shuleni.

    Hatua hiyo inajiri wiki moja baada ya maandamano ya raia dhidi ya udhibiti wa janga la corona kuzuka kote nchini.

    Masharti ya kuwaweka walio na virusi katika karantini za serikali ulikosolewa vikali sehemu kubwa ya watu wakilalamikia jinsi familia zilivyotenganishwa na wapendwa wao.

    Baadhi ya watu waliokaidi amri hiyo walipelekwa karantini kwa lazima.

    Video za mwaka mzima zimeonyesha walinzi wakiwatoa watu nje ya nyumba zao, ikiwa ni pamoja na picha za video kutoka Hangzhou wiki iliyopita ambazo zilionyesha mtu akipigana na maafisa.

    Mabadiliko hayo ni ishara wazi kwamba China inaelekea kuachana na sera yake ya Zero Covid.

    Nchi hiyo inakabiliwa na wimbi kubwa la maambukizi ya coro - zaidi ya 30,000 kila siku.

  10. Wamorocco wafurika mijini kushangilia ushindi wa kihistoria wa Kombe la Dunia

    Morocco

    Chanzo cha picha, EPA

    Mashabiki wenye furaha walimiminika katika mitaa ya miji mikubwa ya Morocco baada ya nchi hiyo kutinga robo fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.

    Simba ya Atlas iliifunga Uhispania kwa mabao 3-0 katika mikwaju ya penalti baada ya kutoka sare tasa.

    Watamenyana na Ureno Jumamosi (15:00 GMT).

    "Haiwezekani sio Morocco," ndivyo Shirikisho la Soka la Morocco lilivyoelezea ushindi huo.

    Fataki zilipigwa na bendera kupeperushwa katika mitaa ya mji mkuu, Rabat, huku watu wakishangilia kwa kuimba na kupiga ngoma hadi usiku wa manane.

    Ruka X ujumbe, 1
    Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

    Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

    Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

    Mwisho wa X ujumbe, 1

    Mfalme wa Morocco Mohammed VI pia alijumuika katika sherehe za barabarani huku akipeperusha bendera huku akipeperushwa barabarani

    Ruka X ujumbe, 2
    Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

    Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

    Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

    Mwisho wa X ujumbe, 2

    Taifa hilo linakuwa timu ya nne ya Afrika kutinga robo fainali ya Kombe la Dunia kwa wanaume baada ya Cameroon (1990), Senegal (2002) na Ghana (2010).

  11. Shirika la Trump lapatikana na hatia ya uhalifu unaohusu kodi baada ya kesi ya New York

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, waendesha mashitaka wanaishutumu kampuni kwa kuwa na "utamaduni wa hongo na ulaghai" wakati wa kesi mjini Manhattan

    Kampuni ya makazi ya rais wa zamani wa Marekani Donald Trump imepatikana na hatia ya uhalifu wa kodi.

    Shirika la Trump limepatikana na hatia kwa makosa yote Jumanne baada ya jopo la mahakama kufanyia uchunguzi kesi yake kwa siku mbili na kutoa tathmini yake mjini New York.

    Biashara hiyo ya makazi inahusishwa na rais huyo wa zamani wa marekani, iwe Bw Trump au watu wa familia yake hakuna aliyekuwepo mahakamani binafsi katika kesi hiyo.

    Akiapa kukata rufaa juu ya kesi hiyo, Bw Trump alisema kuwa ame "katishwa tamaa" na akaielezea tena kesi hiyo kama ya "hila".

    Kampuni hiyo ilipatikana a hatia ya kuwatajirisha wakuu wake kwa faida ambazo hazikusajiriwakwa zaidi ya muongo.

    Vitu ambavyo havikulipiwa kodi ni pamoja na magari ya kifahari na ada za shule za kibinafsi, ambapo waendesha mashitaka walisema, walidanganya kulipwa mishahara ya chini na hivyo kupunguza kiwango cha kodi ambayo biashara hiyo ilitakiwa kulipa.

    Kampuni hiyo inatarajiwa kukabiliwa na faini ya karibu dola milioni 1.6(£1.3m) na pia huenda ikakabiliwa na ugumu katika upataji wa mikopo na fedha siku zijazo.

  12. Iran: Rais wa zamani asema watawala lazima wazingatie matakwa ya waandamanaji

    Mwandamanaji

    Chanzo cha picha, @VAHID/TWITTER

    Rais wa zamani wa Iran ametoa hadharani maoni nadra akiwasifu waandamanaji wanaoipinga serikali na kuwataka wenye mamlaka kuzingatia matakwa yao "kabla hawajachelewa".

    Mohammad Khatami, mwenye umri wa miaka 79, alisema "kauli mbiu nzuri" ya "mwanamke, maisha, uhuru" inaonyesha jamii ya Iraniinaelekea kwenye mustakabali bora.

    Pia alikosoa kukamatwa kwa wanafunzi katika msako wa vikosi vya usalama.

    Maoni hayo yalikuja katika taarifa ya kuadhimisha Siku ya Wanafunzi Jumatano.

    Wanafunzi wamekuwa mstari wa mbele katika machafuko yaliyoanza katikati ya mwezi wa Septemba kufuatia kifo cha Mahsa Amini, mwanamke mwenye umri wa miaka 22 ambaye alizuiliwa na polisi wa maadili kwa madai ya kukiuka sheria ya vazi la hijabu.

    Maandamano hayo yanayoongozwa na wanawake yameenea katika miji zaidi ya 150 na vyuo vikuu 140 katika majimbo yote 31 ya nchi hiyo na yanaonekana kuwa moja ya changamoto kubwa zaidi kwa Jamhuri ya Kiislamu tangu mapinduzi ya 1979.

    Uongozi wa Iran, akiwemo Rais mwenye misimamo mikali Ebrahim Raisi, umezitaja kuwa ni "machafuko" yanayochochewa na maadui wa kigeni wa nchi hiyo na kuviamuru vikosi vya usalama "kukabiliana nao kwa uthabiti".

    Kufikia sasa, waandamanaji wasiopungua 473 wameuawa na 18,215 wamezuiliwa, wakiwemo wanafunzi 586, kulingana na Shirika la Habari la Wanaharakati wa Haki za Kibinadamu (HRANA). Pia imeripoti vifo vya maafisa 61wa usalama.

    Soma:

  13. Waasi wa M23 waunga mkono harakati za kuleta amani DR Congo

    M23

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waasi wa M23, moja ya makundi makuu yanayopigana mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wamesema wako tayari kujiondoa katika maeneo ambayo wanayashikilia katika eneo hilo, kwa kuzingatia maazimio ya mkutano wa kilele wa mwezi uliopita uliofanyika mji mkuu wa Angola, Luanda

    Kundi hilo la waasi limechukua maeneo mengi ya Rutshuru na Nyiragongo katika miezi ya hivi karibuni na kusababisha maelfu ya watu kulazimika kuyahama makazi yao.

    Kundi la M23 pia limeomba kukutana na Jeshi la Kanda ya Afrika Mashariki pamoja na wasuluhishi wa mchakato wa amani unaoongozwa na viongozi wa kanda hiyo.

    Taarifa kutoka kwa msemaji wa kisiasa wa M23 Lawrence Kanyuka, inaongeza kuwa kundi hilo linaunga mkono juhudi za kikanda kuelekea na suluhu ya kudumu la kuleta utulivu mashariki mwa DR Congo.

    Haya yanajiri wakati ambapo mazungumzo ya amani ya wiki nzima yalihitimishwa Jumanne katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

    M23 hawakuwa sehemu ya mkutano huo, ambao uliwaleta pamoja wawakilishi kutoka kwa makundi 50 yenye silaha yanayofanya kazi katika eneo hilo lenye utajiri wa madini.

    Wajumbe walikubaliana juu ya kupokonywa silaha na mpango wa kuleta utulivu kwa waasi wa zamani.

    Unaweza pia kusoma:

    • Kwa nini jeshi la Kenya linajiunga na mzozo wa DRC
    • DR Congo: Je taifa hili limelaaniwa na utajiri wake?
    • Jumuiya ya Afrika Mashariki, majeshi na mustakabali wa amani DRC
    • Mzozo wa DRC: Je inawezekana kuyamaliza makundi ya wapiganaji Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo
    • Hujambo na karibu.