Makamu wa Rais wa Malawi Saulos Chilima akamatwa kwa tuhuma za rushwa
Ofisi ya kupambana na rushwa nchini humo inasema kuwa kati ya Machi na Oktoba mwaka jana, alipokea zaidi ya dola 280,000 na vitu vingine kama malipo baada ya kusaidia kampuni mbili kupewa kandarasi za serikali.
Moja kwa moja
Makamu wa Rais wa Malawi Saulos Chilima akamatwa kwa tuhuma za rushwa
Chanzo cha picha, AFP
Makamu wa Rais wa Malawi Saulos Chilima amekamatwa kwa tuhuma za rushwa.
Ofisi ya kupambana na rushwa nchini humo inasema kuwa kati ya Machi na Oktoba mwaka jana, alipokea zaidi ya dola 280,000 na vitu vingine kama malipo baada ya kusaidia kampuni mbili kupewa kandarasi za serikali.
Taarifa kutoka kwa ofisi hiyo inasema Bw Chilima atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka kadhaa yakiwemo makosa matatu ya ufisadi.
Hapo awali alihojiwa na wachunguzi kutoka ofisi hiyo lakini hajazungumzia madai hayo.
Chilima aligombea kiti cha urais mwaka 2019 lakini akashika nafasi ya tatu katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali.
Baadaye aliungana na Rais wa sasa Lazarus Chakwera katika kama mgombea mwenza.
Lakini uhusiano wa hivi karibunu kati ya Makamu wa Rais na Bw Chakwera umezorota kutokana na shutuma za ufisadi na upendeleo serikalini.
Bw.Chilima amewahi kufanya kampeni katika jukwaa la kupinga ufisadi akiahidi kumaliza miongo kadhaa ya ulafi serikalini na kumaliza umaskini katika mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani.
Mahakama ya Sudan yafuta uamuzi wa kumpiga mwanamke kwa mawe hadi kufa
Chanzo cha picha, AFP
Mahakama ya rufaa kusini mwa jimbo la White Nile nchini Sudan imebatilisha uamuzi wa mahakama kwamba mwanamke aliyepatikana na hatia ya uzinzi apigwe mawe hadi kufa, wakili wake alisema.
Mwezi Juni, mahakama katika mji wa Kosti ilimpata Maryam Tiraab na hatia chini ya sheria ya Sudan ambayo inasema kwamba mtu aliyeolewa au kuoa, atapigwa mawe hadi kufa ikiwa atafanya uzinzi.
Intisaar Abdullah, wakili wake wa utetezi, aliiambia tovuti ya habari ya Sudan Tribune, siku ya Alhamisi kwamba mahakama ya rufaa "ilibatilisha uamuzi wa mahakama kuhusu Tiraab''.
Bi Abdullah alisema kuwa mahakama ya rufaa iliamua kurudisha kesi hiyo kwa mahakama ya mwanzo, na kuiamuru ichunguze upya uamuzi huo, ikisema kuwa "haijazingatia miongozo ya kesi ya haki".
Alisema kuwa mahakama ya rufaa pia iliamuru mahakama ya mwanzo kuanza upya mchakato wa shauri upya, kwa mujibu wa "maagizo iliyokuwa imetoa", bila kutoa maelezo zaidi.
Mawakili wa utetezi wa Bi Tiraab walisema uamuzi wa awali ulikuwa "haramu" kwa kuwa mteja wao hakuwa na "uwakilishi wa kisheria".
Bi Tiraab, 20, ambaye alitengana na mumewe mnamo 2020, alishtakiwa kwa uzinzi na mumewe mwaka mmoja baadaye.
Uamuzi wa mahakama hiyo uliwakasirisha mawakili wengi wa Sudan, ambao walimuunga mkono Bi Tiraab, na kuapa kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Mtoto wa miaka mitano aumwa na kuburutwa na nyoka Australia
Chanzo cha picha, 3AW/BEN BLAKE
Mtoto wa miaka mitano wa Australia amenusurika kuumwa, kubanwa na kuburutwa ndani ya bwawa la kuogelea na chatu karibu mara tatu ya ukubwa wake.
Beau Blake alikuwa akifurahia kuogelea nyumbani wakati mnyama huyo mwenye urefu wa mita 3 (futi 10) alipompiga, baba yake alikiambia kituo cha redio cha eneo hilo.
Wawili hao walivutwa kutoka kwenye bwawa na babu wa Beau na mvulana huyo alivutwa kwa nguvu kutoka kwa mnyama na baba yake Ben.
Lakini Beau yuko katika hali nzuri na amepata majeraha madogo tu.
"Mara tuliposafisha damu na kumwambia kwamba hatakufa kwa sababu hakuwa nyoka mwenye sumu ... alikuwa mzuri sana," baba yake Ben alikiambia kituo cha redio cha Melbourne 3AW siku ya Ijumaa kuhusu tukio hilo. "Yeye ni askari kamili," Ben aliongeza, akisema familia - ambayo wanaishi katika mji wa pwani wa Byron Bay huko New South Wales, watafuatilia majeraha ya kuumwa kuona kama kuna dalili za maambukizi.
"[Beau] alikuwa akitembea tu ukingoni [mwa bwawa]... na ninaamini chatu alikuwa ameketi pale akingoja mwathiriwa aje... na Beau alikuwa hivyo."
"Niliona kivuli kikubwa cheusi kikitoka kwenye kichaka na kabla hawajashambulia, tayari alikuwa amefungwa kwenye mguu wake."
Babu wa Beau mwenye umri wa miaka 76 Allan aliruka kwenye bwawa na kumrusha mvulana na nyoka kwa Ben.
"Mimi sio kijana mdogo... [hivyo] nilimfanya aachiliwe ndani ya sekunde 15-20," Ben alisema.
Ben alikiambia kituo cha redio kwamba chatu ilikuwa kawaida kwa maisha katika eneo hilo.
Kanye West kugombea urais 2024, amtaka Trump kuwa mgombea mwenza
Chanzo cha picha, Reuters
Rapa Kanye West amesema ana nia ya kugombea urais wa Marekani mwaka 2024, licha ya kukabiliwa na kashfa kadhaa kutokana na tabia yake ya hivi karibuni.
Nyota huyo ambaye amebadilisha jina lake kihalali na kuwa Ye, alituma video ya nembo yake ya kampeni kwenye mitandao ya kijamii, sambamba na nukuu ya Ye 24.
Pia alidai kuwa alimwomba Donald Trump kuwa mgombea mwenza wake.
Hapo awali West aliwania urais mwaka 2020, lakini kampeni hiyo haikufua dafu, na kupata kura 70,000.
Madai yake ya hivi karibuni yalikuja katika video iliyochapishwa baada ya West kuonekana katika kilabu cha gofu cha Trump cha Mar-A-Lago mapema wiki hii, akiandamana na Nick Fuentes, mzalendo mashuhuri wa kizungu.
West alisema ombi lake la mgombea mwenza lilimwacha rais huyo wa zamani, ambaye hivi majuzi alizindua kampeni yake ya kuchaguliwa tena, "likiwa na wasiwasi zaidi".
Katika video iliyopewa jina la Mar-A-Lago Debrief, West alidai: "Trump kimsingi alianza kunizomea mezani, akiniambia nitashindwa.
Wakati West akiwania urais mwaka 2020, alitangaza kampeni yake akiwa amechelewa sana kujitokeza kwenye kura katika takribani majimbo sita.
Alifanya mkutano mmoja tu, ambapo aliangua kilio alipokuwa akizungumzia utoaji wa mimba, na kufadhili matangazo mawili ya televisheni.
Mwishowe, aliorodheshwa tu kama mgombea katika majimbo 12.
Kwa ombi lake la 2024, mwanamuziki huyo alisema kuwa amemsajili mchambuzi wa mrengo wa kulia Milo Yiannopoulos kama meneja wake wa kampeni.
Rais wa zamani wa visiwa vya Comoro aombewa hukumu ya kifungo cha maisha jela
Chanzo cha picha, AFP
Waendesha mashitaka katika katika visiwa vya Comoros wameitaka mahakama imuhukumu rais wa zamani wa nchi hiyo Ahmed Abdallah Sambi kifungo cha maisha jela kwa madai ya kufanya uhaini wa hali ya juu..
Sambi, 64, alikuwa rais kati ya mwaka 2006 na 2011 na amekuwa mahabusu tangu mwaka 2018.
Anakabiliwa na mashitaka yanayohusiana na madai ya kuuza hati za uraia wa nchi hiyo kwa watu wasio na utaifa wanaoishi katika mataifa ya Ghuba.
Alishitakiwa bila kuwepo mahakamani baada ya kukataa kufika mahakamani, kulingana na wavuti binafsi wa visiwa vya Comoros- Infos website.
Amepangiwa kuhukumiwa tarehe 28 Novemba.
Vita vya Vita vya Ukraine: Merkel asema hana uwezo tena wa kumshawishi Putin
Chanzo cha picha, get
Kansela wa zamani wa Ujerumani Angela Merkel ametetea sera yake dhidi ya Urusi kabla ya uvamizi wa Februari nchini Ukraine, akisema alikuwa ameishiwa madaraka ya kumshawishi Vladimir Putin.
Alisema alijaribu kuitisha mazungumzo ya Ulaya na rais wa Urusi na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron katika msimu wa joto wa 2021.
"Lakini sikuwa na uwezo wa kupata njia yangu," aliambia idara yahabari ya Spiegel.
"Kweli kila mtu alijua: katika vuli atakuwa amekwenda," alisema.
Baada ya mihula minne kama kansela Bi Merkel aliondoka madarakani mwezi Desemba. Alitembelea Moscow mnamo Agosti 2021, na aliambia jarida la habari la Ujerumani kwamba "hisia ilikuwa wazi sana: 'Kwa upande wa siasa za madaraka umekamilika'."
Aliongeza kuwa "kwa Putin, mamlaka pekee ndiyo yenye thamani".
Ilikuwa muhimu kwamba, kwa mkutano wao wa mwisho, Bw Putin alimleta Waziri wa Mambo ya Nje Sergei Lavrov akutane naye badala ya yeye mwenyewe, alisema.
Hapo awali walikutana moja kwa moja, alibainisha.
Kwa kuzingatia uvamizi wa Rais Putin - uliotanguliwa na wiki za ujenzi mkubwa wa kijeshi kwenye mipaka ya Ukraine - wengi wamehoji kuwa Bibi Merkel na viongozi wengine wa Umoja wa Ulaya walipaswa kuwa na mtazamo mkali zaidi kwa Kremlin.
Mtaalamu wa sera za kigeni katika chama chake cha Christian Democrat (CDU), Mbunge Roderich Kiesewetter, ni miongoni mwa wale wanaosema alijua kwamba Bw Putin anajaribu kugawanyisha na kudhoofisha Ulaya, lakini aliamini "nguvu laini" ndiyo njia sahihi.
Alidai kabla ya uvamizi kwamba Ujerumani ilikuwa tegemezi sana kwa gesi ya Urusi.
Katika mahojiano ya Spiegel, Bi Merkel alisema msimamo wake kuhusu Ukraine katika mazungumzo ya amani ya Minsk umeinunulia Kyiv muda wa kujilinda vyema dhidi ya jeshi la Urusi.
Makubaliano ya kusitisha mapigano yaliafikiwa mjini Minsk baada ya Urusi kutwaa rasi ya Crimea ya Ukraine mwaka 2014 na wakati wa vita vyake vya uwakilishi katika eneo la Donbas.
Lakini mambo muhimu, ikiwa ni pamoja na kupokonya silaha na usimamizi wa kimataifa, hayakutekelezwa.
Bi Merkel alisema hajutii kuondoka madarakani mwezi Disemba, kwa sababu anahisi serikali yake inashindwa kupata maendeleo sio tu kuhusu mzozo wa Ukraine, bali pia migogoro ya Moldova, Georgia, Syria na Libya, ambayo yote yalihusisha Urusi.
Yeye na Bw Putin wote walikuwa na uzoefu wa moja kwa moja wa maisha katika Ujerumani Mashariki ya kikomunisti - alikulia huko na alihudumu huko kama afisa wa KGB wa Soviet, akifanya kazi ya siri ya kijasusi.
Bw Putin anazungumza Kijerumani vizuri na Bi Merkel anazungumza Kirusi kiasi fulani.
Zaidi ya wanawake watano huuawa kila saa na mwanafamilia- UN
Maelezo kuhusu taarifa
Author, Grace Kuria
Nafasi, BBC News
Chanzo cha picha, Getty Images
Karibu wanawake na wasichana 45,000 duniani waliuawa na wapenzi wa karibu au wanafamilia mwaka 2021 kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa.
Hii ina maana kwamba zaidi ya wanawake au wasichana watano wanauawa kila saa na mtu katika familia zao.
Ingawa idadi hii ni ya kushangaza, ripoti iliyotolewa kwa pamoja na ofisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu madawa ya kulevya na uhalifu (UNODC) na wanawake wa Umoja wa Mataifa, ilifichua kwamba kiwango cha kweli cha mauaji ya wanawake kinaweza kuwa kikubwa zaidi.
Afrika ni eneo la pili baada ya Asia, kurekodi visa vya mauaji ya wenzi wa karibu wa kike/familia, vikiwa 17,200.
Hata hivyo, bara hilo linachukuliwa kuwa eneo lenye kiwango cha juu cha unyanyasaji, ikilinganishwa na ukubwa wa idadi ya wanawake.
"Wanawake na wasichana wa Afrika wako katika hatari kubwa ya kuuawa na wapenzi wao wa karibu au wanafamilia wengine."
Upungufu wa data umeonekana kuwa changamoto, kwani kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, kati ya mauaji ya wanawake 81,000 yanayokadiriwa mwaka 2021, wanne kati ya kumi, hawana ‘taarifa za muktadha’ kuruhusu kutambuliwa na kuchukuliwa kuwa mauaji yanayohusiana na jinsia.
"Takwimu kuhusu mauaji yanayohusiana na jinsia yanayofanywa katika nyanja ya umma ni chache sana, na hivyo kufanya kuwa vigumu kujulisha sera za kuzuia mauaji ya aina hii."
Umoja wa Mataifa unatoa wito wa kuimarishwa kwa mifumo ya ulinzi kwa wanawake watetezi wa haki za binadamu na wanaharakati wa haki za wanawake.
"Natoa wito kwa serikali na washirika kote duniani kuongeza ufadhili wa muda mrefu na msaada kwa mashirika ya haki za wanawake."
Mkurugenzi mtendaji wa UN Women Sima Bahous alisema.
Haya yanajiri huku maadhimisho ya kimataifa ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yakianza Ijumaa, chini ya kaulimbiu, ‘Ungana! Harakati za kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.’
Mvulana wa miaka mitano anusurika siku kadhaa baada ya tetemeko la ardhi Indonesia
Maelezo ya video, Mvulana wa miaka mitano anusurika siku kadhaa baada ya tetemeko la ardhi Indonesia
Wahudumu wa uokozi wamemvuta mtoto mvulana mwenye umri wa miaka mitano kutoka kwenye vifusi siku tatu baada ya tetemeko kubwa lililokumba Indonesia.
Katika video ya uokozi iliyoshirikishwa mtandaoni na idara ya zima moto ya eneo, mvulana huyo kwa jina Azka alionekana akiwa mwenye ufahamu na mtulivu alipokuwa akinyenyuliwa kutoka kwenye vifusi vya jengo na kupelekwa mahali salama.
Alitibiwa na madaktari katika eneo la Cianjur la West Java kabla ya kuungana na familia yake.
Hofu ya Ebola yafanya Uganda kufunga shule mapema kwa likizo ya Krismasi
Chanzo cha picha, Getty Images
Krismasi huenda inakuja mapema kwa wanafunzi nchini Uganda hukumamilioni yao wakirejea nyumbani mapema kwa likizo ya shule siku ya Ijumaa.
Hata hivyo uamuzi wa kufungwa kwa shule kote nchini wiki mbili kabla ya mwisho wa muhula umechukuliwa ili kuzuia kuenea kwa Ebola, huku nchi hiyo ikiendelea kupambana na moja ya milipuko yake mbaya zaidi.
Pia inakinzana na msimamo rasmi wa serikali kwamba hali imedhibitiwa.
Katika miezi miwili iliyopita watu 55 wamekufa na virusi hivyo - na kuna uwezekano wa vifo 22 vya Ebola kabla ya mlipuko huo kutangazwa rasmi mnamo 20 Septemba.
Baadhi ya wataalam wameelezea kutoridhishwa kwao na hatua ya kufungwa kwa shule, wakisema kuwa kuwaweka wanafunzi ndani kwa wiki nyingine mbili itakuwa njia bora ya kukomesha kuenea kwa ugonjwa huo hatari.
Ebola ni maambukizi ya virusi ambayo husambazwa kupitia maji maji ya mwili wa mgonjwa.
ICC yataka kuanzisha kesi dhidi ya kiongozi wa waasi wa LRA Joseph Kony
Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Joseph Kony alijielezea kama "mpigania uhuru"
Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Jinai (ICC) anasema anataka kuanzisha kesi dhidi ya kiongozi wa waasi wa Uganda Joseph Kony.
Hii ni mara ya kwanza kwa ofisi ya mwendesha mashtaka inataka kusikizwa ili kuthibitisha mashtaka, bila mshukiwa kuwepo.
Hati ya kukamatwa kwa Kony ilitolewa kwa kiongozi wa Lord's Resistance Army miaka 17 iliyopita kwa makosa 33 ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Kundi la LRA lilianzisha uasi nchini Uganda katika miaka ya 1990, na kuua, kuwakata viungo na kuwateka nyara watu hasa watoto.
Bw Kony haijulikani aliko lakini LRA imekuwa ikifanya kazi nchini Sudan na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Ghana kupambana mechi zinazofuata baada ya kufungwa na Ureno
Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo amesifu "uchezaji wa kishindo" wa timu ya taifa katika mchezo wao wa kwanza wa Kombe la Dunia dhidi ya Ureno ambao uliisha kwa mabao 3-2.
Black Stars imekuwa timu ya kwanza ya Kiafrika kufunga bao katika michuano ya mwaka huu, lakini iko mkiani mwa Kundi H.
Itacheza na Korea Kusini tena Novemba 28.
Katika ujumbe wake wa Twitter, Rais Addo alisema "anajivunia timu nzima" licha ya kupoteza dhidi ya Ureno.
Aliongeza: "Wana nafasi ya kupigana tena siku nyingine na wameonyesha wanachohitaji kufanya ili kukabiliana na timu yoyote kwenye mashindano."
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje
Mwisho wa X ujumbe
Waasi wa M23 wasema hawatarudi nyuma DRC
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, wanajeshi wa Kenyan ni sehemu ya kikosi cha kikanda kilichopelekwa DRC kupambana na waasi wa M23
Waasi wa M23 wanaoendesha harakati zao mashariki mwa Jamuhuri
ya Kidemokrasi ya Congo wamesema kuwa
usitishwaji wa mapigano uliotarajiwa kuanza leo Ijumaa jioni "haulihusu "
kundi hilo.
Wametoa wito kwa serikali ya Congo kufanya nao mazungumzo ya moja kwa moja.
Msemaji wa M23, Lawrence Kanyuka, amesema kuwa kwa kuwa hawakuwa na
wawakilishi katika mkutano mdogo wa Jumatano uliofanyika mjini Angola,
hawakujumuishwa katika mkataba.
“SisiM23 sio Warundi, sio Wanyarwanda, sio Wakenya,
na wala sio Waangola. Sisi ni Wacongo ,
na tuko nyumbani, wanatuambia tuondoke wapi ? Tunaondoka nyumbani kuelekea wapi
?” Bw Munyarugerero anasema.
Waliotia Saini mkataba huo - kutoka Rwanda, DRC, Angola na Burundi – walisema
chini ya usitishwaji wa mapigano, iwapo waasi hawataondoka katika eneo hilo kikosi cha kanda ya Afrika Mshariki
kitayashambulia maeneo yao.
Serikali ya Kinshasa imekataa kufanya mazungumzo na M23, ikiwaita magaidi.
Januhuri ya kidemokrasi ya Congo, inaishutumu Rwanda kuwaunga mkono waazi,
ambao wameteka eneo kubwa la jimbo la Kivu Kaskazini, mashariki mwa nchi hiyo.
Rwanda inakana kuhusika katika mzozo huo wa Congo.
Unaweza pia kusoma:
Kwa nini jeshi la Kenya linajiunga na mzozo wa DRC
DR Congo: Je taifa hili limelaaniwa na utajiri wake?
Jumuiya ya Afrika Mashariki, majeshi na mustakabali wa amani DRC
Mzozo wa DRC: Je inawezekana kuyamaliza makundi ya wapiganaji Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo
Trump ashtakiwa kwa tuhuma ya ubakaji New York
Chanzo cha picha, Getty Images
Mwandishi E Jean Carroll amemshtaki Donald Trump katika jimbo la New York Marekani kwa madai ya kumbaka katika miaka ya 1990.
Bi Carroll ni miongoni mwa wa kwanza kushtaki chini ya Sheria ya Watu Wazima Walionusurika, ambayo ilianza kutekelezwa siku ya Alhamisi.
Sheria ya serikali inaruhusu muda wa mwaka mmoja kwa waathiriwa kuwasilisha kesi za unyanyasaji wa kijinsia huko New York kwa madai ambayo yangevuka mipaka ya sheria.
Rais huyo wa zamani amekanusha madai dhidi yake.
Bi Carroll anadai kuwa shambulio hilo lilitokea katika chumba cha kuvaa cha duka la kifahari la New York miaka 27 iliyopita.
Sheria ya Waathirika wa Watu Wazima inaruhusu waathiriwa kujitokeza ikiwa unyanyasaji wa kijinsia ulitokea walipokuwa na umri wa zaidi ya miaka 18.
Bi Carroll pia amemshtaki Rais wa zamani Trump kwa kumharibia jina baada ya kumshutumu kwa kusema uwongo alipotangaza hadharani madai yake kwa mara ya kwanza mwaka wa 2019. Bw Trump ameyataja madai ya Bi Carroll kuwa "ya kubuni".
Kesi ya madai ya kesi hiyo imepangwa kusikizwa tarehe 6 Februari.
Katika taarifa, wakili wa Bi Carroll, Roberta Kaplan, alisema kesi mpya iliyowasilishwa Alhamisi inanuiwa kumwajibisha Bw Trump kwa madai ya kushambuliwa.
Urusi yafikisha 'jibu kwa Blinken' kuhusu sheria ya propaganda ya wapenzi wa jinsia moja
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Sheria itapanuliwa zaidi kwa ajili ya kuwatia hatiani watu wazima pamoja na watoto
Bunge la chini la Urusi limepiga kura kwa kauli moja kuongeza muda wa marufuku yake dhidi ya kile
kinachoitwa "propaganda ya wapenzi
wa jinsia moja".
Chini ya toleo la sasa, uenezaji wowote wa mapenzi ya jinsia
moja – ikiwa ni pamoja na kwa njia ya vitabu, filamu na mtandao – ni kinyume cha
sheria na adhabu kali itatolewa kwa yeyote atakayepatikana na hatia hiyo.
Sheria hiyo ilipawe jina bandia la "Jibu kwa sheria ya Blinken", baada ya Waziri wa mambo ya
nje wa Marekani Antony Blinken kuikosoa
kama "pigo kwa uhuru wa kujieleza".
Wanaharakati wanasema ni jaribio zaidi la Urusi la kuwakandamiza wapenzi wa jinsia moja (LGBT)
wa Urusi.
Mswada wa sheria hiyo uliidhinishwa
kwa kura 397 za wabunge wote wa bunge la Urusi - Duma - bila kukosa mbunge
yoyote.
Mswada huo utahitaji kupitishwa na bunge la juu la Urusi kabla
ya kusianiwa na Rais Vladimir Putin, lakini hili wengi wanaliona kama hatua ya
kiutawala.
Toleo la awali la sheria tata ya " propaganda ya mapenzi ya jinsia moja"
iliidhinishwa mwaka 2013, na kupiga
marufuku "propaganda za uhusiano wa
mapenzi yasiyo ya kawaida" – ikimaanisha mahusiano ya kingono ya watu wa
jinsia moja – miongoni mwa watoto.
Atlético Madrid: Mganga mkuu klabu ya soka ya Uhispania kumtibu Papa Francis
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Papa Francis ana ratiba yenye shughuli nyingi licha ya tatizo lake la kutembea.
Mkuu wa timu ya madaktari wa Atlético Madrid ameitwa Vatican kusaidia kumtibu Papa Francis, ambaye anakabiliwa na tatizo la goti.
Papa mwenye umri wa miaka 85 amesitisha shughuli mbalimbali katika miezi ya hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na safari ya Afrika, kwa sababu ya matatizo ya kutembea.
José María Villalón alisema Papa alikuwa "mzuri sana" lakini pia "mkaidi sana" kwani alikataa kufanyiwa upasuaji.
Papa ni shabiki mkubwa wa klabu ya Argentina ya San Lorenzo - si klabu ya Madrid.
Msingi wa soka wa San Lorenzo ni Buenos Aires, ambapo papa - Jorge Mario Bergoglio - alizaliwa.
Tangu Mei Papa - kiongozi wa zaidi ya Wakatoliki bilioni moja duniani - ametembea kwa msaada wa fimbo, au kutumia kiti cha magurudumu.
Katika mahojiano na kituo cha redio cha Uhispania Cope, Dk Villalón alisema "Nina matumaini kwamba Papa anaweza kusaidiwa", lakini alikiri kwamba ratiba ya Papa ilifanya matibabu kuwa magumu zaidi.
Pia alikiri kwamba, katika mkutano wake wa kwanza na papa, alikuwa na "woga sana" kwa sababu ya jukumu la changamoto hii mpya.
Mke wa rais wa Ukraine Olena Zelenska: Tutavumilia
Mke wa Rais wa Ukraine Olena Zelenska ameiambia BBC kwamba Ukraine
itavumilia kipindi hiki kijacho cha majira ya baridi kali licha ya ukosefu wa umeme
uliosababishwa na makombora ya Urusi , na wataendelea kupigana na kile
alichokielezea kama vita vya mitazamo ya dunia, kwa sababu"bila
ushindi hakutakuwa na amani ".
Alikutana na mwandishi wa BBC katika mji wa kihistoria ambako kunashuhudiwa baridi kali.
Mitaa ambayo kwa
kawaida huwa ina mwanagaza wa taa sasa ni giza, kutokana na ukosefu wa umeme huku Warusi wakiendelea kushambulia
mitambo ya umeme ya Ukraine.
Watu wa Ukraine wameshinda majivuno kwa kusimama imara dhidi ya
mashambulio ya Urusi. Lakini hili ni jaribio lingine la ujasiri.
"Tuko tayari kuvumilia hili," Olena Zelenska anasema
wakati wa mahojiano akiwa katika eneo lenye ulinzi mkali ndani ya jengo lililozingirwa na mifuko ya mchanga
iliyowekwa kwa ajili ya kuzuia makombora mjini Kyiv.
"Tulikuwa na changamoto nyingi sana, kuona waathiriwa wengi,
kuvurugwa kwa mambo mengi, kiasi kwamba tunaona ukosefu wa umeme sio kitu
kibaya zaidi kutokea kwetu." Alitoa mfano wa kura ya maoni ya hivi karibuni - 90 % ya
Waukraine walisema wako tayari kuishi na ukosefu wa umeme kwa vmiaka miwili
hadi mitatu iwapo wangeona matarajio ya kujiunga na Muungano wa Ulaya.
Waukraine wote watakuwa imara kwasababu ya vita
hivi, alibashiri Mke wa rais wa Ukraine.
Urusi na Ukraine: Mengi zaidi
YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
Hujambo na karibu kwa matangazo yetu mubashara leo Ijumaa tarehe 25.11.2022