Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Mzozo wa Ukraine: Urusi yakamilisha zoezi la kuondoa vikosi vyake Kherson

Wizara ya ulinzi huko Moscow, iliyotajwa na shirika la habari la Tass, imethibitisha kwamba wanajeshi wote wa Urusi kwenye ukingo wa magharibi wamevuka upande mwingine.

Moja kwa moja

Dinah Gahamanyi

  1. Na hapa ndio tunafikia mwisho wa taarifa zetu za moja kwa moja kwa leo, hadi kesho majaaliwa.

  2. Mshauri wa kijeshi wa Ukraine asema wataikomboa Crimea

    Ukraine imeapa kurudisha ardhi yote iliyotwaliwa na Urusi, ikiwemo Crimea kusini.

    Peninsula ya kusini ilitwaliwa na Urusi mwaka 2014 na nchi hizo mbili zimekuwa zikipigania uhuru wake tangu wakati huo.

    Mshauri wa ulinzi Yuriy Sak anaiambia BBC "Tutaikomboa ardhi yetu na tutarejesha eneo la Ukraine ndani ya maeneo yanayotambulika kimataifa ambayo ni pamoja na Crimea."

    "Nina hakika kwamba mipango yetu ya kijeshi bado itakuwa ya kiwango kizuri kama vile tulivyofanya huko Kyiv, Chernihiv, Kharkiv na sasa Kherson," anaongeza.

    Wakati huo huo kumekua na ripoti kuwa vikosi vya Ukraine vimeanza kurejea Kherson wakati vile vy Urusi vimeondoka.

    Video mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii za bendera za Ukraine zikipepea juu ya majengo ya utawala. Sasa wizara ya ulinzi ya Ukraine inasema Kherson inarejea katika udhibiti wa Ukraine na vitengo vya jeshi vinaingia mjini humo.

  3. Watu sita wauawa katika shambulio la kombora huko Mykolayiv Ukraine

    katika mji wa karibu wa Mykolayiv - karibu kilomita 95 kaskazini magharibi mwa Kherson - watu wasiopungua sita wameuawa baada ya kombora kugonga jengo la ghorofa.

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amelitaja shambulio hilo la kombora kuwa la kijinga. Zelensky aliandika kwenye Telegram, kwa Kiukreni na Kiingereza: "Mykolayiv. Ilikuwa ni jibu la kijinga la serikali ya kigaidi kwa mafanikio yetu ya mstari wa mbele. "Jengo la makazi la ghorofa tano lilipigwa. Ghorofa zote tano ziliharibiwa. "Kwa bahati mbaya, watu waliuawa na kujeruhiwa.

    Operesheni ya kutafuta majeruhi na kuokoa inaendelea.

    "Urusi inaendelea na mbinu zake za kutisha. Lakini tunaendelea na mapambano yetu. Wavamizi watachukuliwa hatua kwa kila uhalifu dhidi ya Ukraine na Ukraine '' anasema Zelesky.

  4. Kikosi kutathmini urejeshwaji wa Zimbabwe katika Jumuiya ya Madola

    Timu kutoka Jumuiya ya Madola inatarajiwa kuwasili nchini Zimbabwe mwishoni mwa juma hili kutathmini ikiwa nchi hiyo inafaa kurudishwa tena katika jumuiya hiyo.

    Harare ilijiondoa kwa hiari katika baraza hilo mnamo mwaka 2003 baada ya kusimamishwa uwanachama kufuatia ukiukwaji wa haki za binadamu chini ya utawala wa kiongozi wa zamani Rober Mugabe.

    Ziara hiyo inajiri huku upinzani nchini Zimbabwe ukisema kuwa kuna ukandamizaji umerejea upya dhidi ya wafuasi wake.

    Ujumbe huo unaokwenda kwa wiki nzima unaongozwa na naibu katibu mkuu Luis Franceschi na utakagua hatua zilizopigwa katika kutekeleza mageuzi ya kisiasa na kiuchumi.

    Ni ziara ya tatu tangu Zimbabwe ilipowasilisha ombi la kujumuishwa upya katika juymuiya hiyo ya madola mnamo 2018 – ikiwa ni sehemu ya mpango wa rais Emmerson Mnangagwa ya kujihusisha upya baada ya kutengwa kwa miaka kadhaa kutoka magharibi.

    Lakini tuhuma zinaongezeka za uovu wa kisiasa. Hapo jana Alhamisi mbunge wa upinzani Godfrey Sithole aliachiliwa kwa dhamana baada ya kufungwa kwa miezi mitano gerezani kwa tuhuma za kuchochea ghasia.

    Mbunge mwingine ambaye pia anashutumiwa Job Sikhala bado anasalia gerezani kwa mashtaka ambayo makundi ya kutetea haki za binaadamu yanasema ni uzushi.

    Zimbabwe sio nchi pekee ilioomba kurudishwa upya katika jumuiya hiyo ya madola, inayojumuisha mataifa yakiwemo yale yaliokuwa chini ya ukoloni wa Uingereza. Miongoni mwa nchi zilizorudi upya katika Jumuiya hiyo baada ya hapo awali kujiondoa ni Afrika kusini, Pakistan, Fiji, na Gambia. Afrika kusini ilitangaza kujitoa katika jumuiya hiyo mnamo Mei mwaka 1961 baada ya kupitisha sheria ilioifanya nchi hiyo kuwa Jamhuri na kusitisha utawala wa malkia. Ilijunga upya miaka 33 baadaye mnamo 1994 baada ya kumalizika kwa ubaguzi wa rangi nchini.

    Mnamo 2008 Jumuiya ya madola ilikubali kuirudisha Pakistan mwaka mmoja baada ya kuusitisha uwanachama wake kufuatia hatua ya kiongozi aliyekuwepo Pervez Musharaf kuidhinisha hali ya hatari na kuwazuia maelfu ya wanaharakati wa upinzani. Gambia ilijiunga na jumuiya ya madola kwa mara ya kwanza mnamo 1965, muda mfupi tu baada ya kupata uhuru kutoka kwa Uingereza. Ilijiondoa mnamo Octoba 2013 chini ya rais wa zamani Yahya Jammeh aliyeishutumu jumuiya hiyo kwa kuwa anachokitaja "taasisi ya ukoloni mambo leo".

    Takriban miaka mitano baadaye, mwaka 2018, Gambia ilijiunga upya na jumuiya hiyo. Hii ni baada ya rais mpya wakati huo Adama Barrow kuomba nafasi taifa lake kurudi kuwa mwanachama Februari 2017, na mwezi Desemba mwaka huo huo bunge nchini liliidhinisha ombi hilo la kurudi. Kwa sasa kuna mataifa 54 katika jumuiya ya madola.

  5. Kombe la Dunia 2022: Sadio Mane kushikiriki licha ya kuwa na majeraha

    Sadio Mane amejumuishwa kwenye kikosi cha Senegal kitakachoshiriki Kombe la Dunia nchini Qatar licha ya kusumbuliwa na majeraha siku ya Jumanne.

    Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 30 alilazimika kutoka nje katika kipindi cha kwanza cha ushindi wa 6-1 wa Bayern Munich dhidi ya Werder Bremen.

    Mabingwa hao wa Ujerumani walisema alipata jeraha "katika eneo la goti" na ataukosa mchezo wa Jumamosi dhidi ya Schalke.

    Senegal itaanza mashindano ya Kundi A dhidi ya Uholanzi tarehe 21 Novemba.

    "Tunafuatilia hali ilivyo na tumemtuma mmoja wa madaktari wetu kumpima," kocha wa Senegal Alioy Cisse alisema katika mkutano na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Senegal Dakar siku ya Ijumaa.

    "Siku ya Alhamisi, Sadio alikaa siku nzima mjini Munich kabla ya kusafiri kwenda Austria kwa vipimo zaidi. Habari njema ni kwamba hahitaji kufanyiwa upasuaji. "Tunataka hali kubadilika katika wiki mbili-tatu. Sitaki kumtenga."

    Akiwa mfungaji bora wa mabao nchini mwake, akiwa na mabao 34 katika mechi 93, utimamu wa Mane ndio ufunguo wa nafasi za Senegal na Cisse atatoa jasho kwa upatikanaji wake kabla ya mechi yao ya kwanza dhidi ya Uholanzi, mechi dhidi ya wenyeji Qatar (Novemba 25) na Ecuador (Novemba 29). )

  6. Urusi: Kuondoa vikosi Kherson haimainishi kutakua na mabadiliko, bado ni eneo la Urusi

    Kremlin bado inachukulia eneo la Kherson kuwa sehemu ya Urusi. Na haioni chochote cha kufedhehesha kutokana na kitendo cha kuondoa vikosi vyake kutoka eneo la Kherson.

    Msemaji wa rais wa Urusi Dmitry Peskov alisema kuwa kuondolewa kwa wanajeshi wa Urusi kutoka Kherson hadi benki ya kushoto ya Dnieper hakutabadilisha hali ya eneo la Kherson lililoshikiliwa na Urusi.

    "Hili ni somo la Shirikisho la Urusi, hali hii inafafanuliwa kisheria na kulindwa. Hakuna na hawezi kuwa na mabadiliko yoyote hapa," aliwaambia waandishi wa habari.

    Peskov alikataa kujibu swali kutoka kwa waandishi wa habari kuhusu jinsi Vladimir Putin alichukua ripoti ya Jenerali Sergei Surovikin kuhusu hali ya Kherson na uamuzi wa Waziri wa Ulinzi Sergei Shoigu kuondoa kikundi cha kijeshi cha Urusi kutoka kwa jiji hilo.

    "Kulikuwa na [uamuzi] wa Waziri wa Ulinzi, kwa hivyo nakuomba uwasiliane na Wizara ya Ulinzi, sina la kusema juu ya mada hii," Peskov alisema.

    Akijibu swali kutoka kwa BBC, Peskov alisema kuwa Kremlin haioni kuwa ni fedheha kuondoka kutoka Kherson.

  7. Habari za hivi punde, Kujiondoa kwa Urusi kutoka mji wa Kherson 'kumekamilika'

    Habari za hivi punde ni kuwa Urusi imeonda vikosi vyote kutoka mji wa Kherson. Asubuhi nzima, picha zimeonekana kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha sehemu kadhaa zilizoharibiwa kwenye daraja pekee la barabara nje ya Kherson.

    Hilo liliwafanya wanablogu wanaofuatilia kwa karibu vita hivyo kusema kujiondoa kwa Urusi kutoka ukingo wa magharibi wa mto Dnipro kumekwisha. Sasa wizara ya ulinzi huko Moscow, iliyotajwa na shirika la habari la Tass, imethibitisha kwamba wanajeshi wote wa Urusi kwenye ukingo wa magharibi wamevuka upande mwingine.

    Ilikuwa siku ya Jumatano ambapo wakuu wa jeshi la Urusi walitangaza kuwa wanaondoka kutoka upande huo wa mto.

    Uamuzi wa kurudi nyuma ni pigo kubwa kwa jeshi la Urusi katika kukabiliana na shambulio la Ukraine.

    Rais Vladimir Putin hakushiriki katika tangazo hilo la televisheni. Wizara hiyo ilisema Ijumaa kwamba hakukuwa na hasara ya wafanyikazi, silaha au vifaa vya kijeshi na kwamba hakuna vifaa vilivyoachwa nyuma.

  8. 50 Cent kuandaa tamthilia ya TV kumhusu Tapeli wa Nigeria Hushpuppi

    Msanii maarifu wa muziki wa rap wa Marekani 50 Cent ametangaza kuwa anatengeneza msururu wa vipindi vya televisheni kuhusu maisha ya mfungwa -tapeli sugu Mnigeria na mshawishi wa mtandao wa Instagram, Hushpuppi.

    Tangazo hilo la 50 Cent limezua mjadala mtandaoni huku baadhi wakiunga mkono wazo hilo, huku wengine wakisema utawafanya Wanigeria waonekana vibaya.

    Akituma ujumbe huo kwenye ukurasa wa Instagram, 50 Cent ambaye jina lake halisi ni Curtis Jackson, alisema kuwa ilimbidi afanye hivyo: "Kwa jaili ya walaghai wangu ni lazima nifanye hili, Msururu wa Hushpuppy unakuja karibuni! (Hushpuppy series coming soon !)"

    Msanii huyo wa muziki wa rap ana historia ya kuandaa vipindi vya TV, ikiwa ni pamoja na msururu wa maigizo wa Power, ambao kwa mara ya kwanza ulianza kutangazwa mwaka 2014.

    Hushpuppi, ambaye jina lake halisi ni Ramon Abbas, kwa sasa anatumikia kifungo cha miaka 11 jela kwa mchango wake katika mtandao wa kimataifa wa utapeli.

    Huspuppi alikuwa maarufu kwenye mtandao wa Instagram ambao aliutumia kuonyesha utajiri wake mkubwa kwa wafuasi wake milioni 2.8 ,hadi alipokamatwa mjini Dubai mwaka 2020, na akaunti yake kufungwa.

    Kwenye mtandao wa Twitter baadhi ya watu wanaonyesha furaha yao juu ya mpango wa 50 Cent: "Nasubiri kwa hamu kuona ni nini 50 Cent atatupatia kuhusu hili !"mtu mmoja alisema.

    Mwingine anasema50 Cent anapaswa "Kuipiku Nollywood kwa hili".

    Hatahivyo,Wengine wameelezea kutofufahishwa kwaona hili, huku mmoja wao akituma ujumbe akisema : "kwanini usitazame karibu yako na kuandaa msururu wa kitu ambacho kinaongelea jambo chanya kuhusu Wanigeria, kwani kuna mengi yanayokuzingira na kote duniani"

    Tazama:

    Unaweza pia kusoma:

    • Wanaijeria 'matapeli' walionadi utajiri wao mtandaoni walivyonaswa Dubai
    • Wakili wa mmoja wa ‘matapeli’ Wanaigeria waliokamatwa baada ya kujinadi Instagram adai alitekwa nyara na FBI
  9. Idadi ya watu wanaoumwa na nyoka Nigeria yaongezeka kutokana na mafuriko

    Maafisa nchini Nigeria wanaendelea kuwatahadharisha watu kuhusu tatizo ambalo limekuwa likitokea mara kwa mara, baada ya mafuriko makubwa yaliyoshuhudiuwa katika maeneo mbali mbali ya nchi.

    Wanasema kuwa hivi karibunikumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya watu wanaoumwa na nyoka katika baadhi ya maeneo yaliyofurika maji baada ya mvua kubwa kunyesha.

    Katibu mkuu wa wizara ya masuala ya kibinadamu nchini Nigeria Dkt. Nasir Sani Gwarzo, ameiambia BBC kwamba watu wanakimbia kutafuta kukwepa mafuriko, pamoja na Wanyama, wadudu na vitu vingine.

    Amesema kuwa nyoka pia wanatafuta mahala pa kujificha, kila mara mafuriko yanapotokea, lazima kuwe na ongezeko la watu wanaoumwa na nyoka, hususan kama mji una nyoka wengi.

  10. Uwasilishaji wa misaada Tigray kuanza 'mwisho wa wiki'

    Misaada ya kibinadamu itaanza kuwafikia watu wanaokabiliwa na njaa na magonjwa katika eneo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia mwishoni mwa juma, kulingana na mshauri wa usalama wa taifa wa waziri mkuu wa Ethiopia.

    Mamilioni ya watu katika eneo hilo wanahitaji chakula, dawa na vifaa vingine vya kimsingi.

    Bw Redwan Hussien amenukuliwa akisema na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwamba "msafara wa msaada utapita bila kuzuiwa" kama ilivyokubaliwa katika mazungumzo ya amani.

    Duru ya mwisho ya mazungumzo kati ya wawakilishi wa Tigray na serikali mjini Addis Ababa yanatarajiwa kumalizika Ijumaa nchini Kenya.

    Pande zote mbili zimekuwa zikikutana kujadili utekelezaji wa mkataba wa amani uliotiwa saini wiki iliyopita nchini Afrika Kusini.

    Serikali ya Ethiopia na chama cha Tigray People's Liberation Front wamejitolea kumaliza miaka miwili ya mapigano.

    Mpango huo unatoa wito kwa uwasilishaji wa misaada kuanza upya huko Tigray na huduma muhimu kurejeshwa.

    Mamilioni ya watu huko Tigray wanahitaji chakula na dawa haraka.

    Soma:

  11. Kombe la Dunia Qatar 2022: Ukweli kuhusu Sadio Mané

    Sadio Mane mwenye umri wa miaka 30, ni mmoja wa wachezaji bora zaidi wa soka duniani kwa sasa. Huku akijiandaa kuiwakilisha nchi yake Senegal katika Kombe la Dunia la Qatar 2022, huu ndio ukweli kumhusu.

    • Mané mwenye alizaliwa katika kijiji cha Bambali, Sédhiou, nchini Senegal
    • Tangu akiwa na umri mdogo alitamani kuwa mchezaji soka
    • Baba yake yake ambaye alikuwa Iman alimzuia kucheza soka alipokuwa mtoto
    • Lakini akiwa na umri wa miaka saba, baba yake alifariki na alipotimiza umri wa miaka 15, alitoroka kijijini kwao kwenda katika mji mkuu Dakar kutekeleza azma yake ya kuwa mwanasoka.
    • Mwaka 2009, wakati alipokuwa akichezea timu ya M’Bour ligunduliwa na maskauti na baadaye alitambuliwa na Génération Foot,
    • Mwaka 2011 alijiunga na klabu ya Metz, ambayo ilikuwa na ushirika na Génération Foot
    • Alijiunga na klabu ya Austria ya Salzburg tarehe 31 Agosti 2012
    • Baadaye alijiunga na klabu ya Southampton na kuichezea katika msimu wa mwaka 2014- 2015
    • Mwaka 2016 hadi 2022 aliichezea klabu ya Liverpool lakini tarehe 22 June, 2022 alijiunga na klabu ya Ligi ya ujerumani Bundesliga, Buyern Munich.

    Unaweza pia kusoma:

    • Sadio Mane: Nyota wa Senegal anayetarajiwa kufanikiwa Bayern Munich
    • Ballon d'Or 2022: Kwa nini Sadio Mane atakumbukwa zaidi kuliko Benzema na tuzo ya Ballon d'Or?
    • Fahamu mambo sita usiyoyajua kuhusu Sadio Mane wa Senegal na Liverpool
  12. Chuo kikuu Uganda chasitisha hatua 'tata' ya kuwapima ujauzito wanafunzi wa kike

    Tangazo la kuwataka wanafunzi wa kike wanaosoma katika Chuo kikuu cha kimataifa cha Kampala Uganda kupima ujauzito la sivyo wazuiwe kufanya mtihani limeibua mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii.

    Tangazo hilo ambalo lilisambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii, lakini baadaye kufutwa, liliwataka wanafunzi wa kike wanaosoma masomo ya ukunga na uuguzi - kupima ujauzito, la sivyo watazuiwa kufanya mtihani.

    Mkuu wa kituo cha utafiti -African Population na Health Research, na mwanaharakati wa masuala ya jinsia, Catherine Kyobutungi, alishirikisha ujumbe huo kwenye ukurasa wake wa Twitter.

  13. Simba wanaozurura wazua wasiwasi na uharibifu mkubwa katika vijiji vya Msumbiji

    Simba, ambao wanadhaniwa kuwa walitoroka kutoka katika shamba moja nchini Msumbiji, wamesababisha wasi wasi na mkanganyiko katika vijiji vya Moamba vilivyopo katika jimbo la Maputo nchini Msumbiji.

    Simba hao wamewauwa mifugo ya wanavijiji –jambo ambalo limekuwa likifanywa pia na fisi tangu mwanzoni mwa mwaka huu ambao waliwaua mbuzi na kondoo nyakati za usiku.

    Katika kipindi cha siku 15 pekee, zaidi ya mifugo 20 wameuawa na kuliwa na simba.

    Wanavijiji wanalalamika kwamba mamlaka hazifanyi lolote kuhusu suala hili, na simba wanaweza kuanza kuwashambulia binadamu.

  14. Vita vya Ukraine: Ukraine yadai kupata mafanikio makubwa huku Urusi ikiondoka Kherson

    Jeshi la Ukraine linasema limepata mafanikio makubwa katika siku ya mwisho karibu na Kherson, baada ya Urusi kusema kuwa inajiondoa katika mji huo wa kusini.

    Wanajeshi wa Ukraine wanasema wameukomboa mji muhimu wa Snihurivka, kilomita 50 (maili 30) kaskazini mwa Kherson.

    Kyiv pia imedai shinikizo kubwa kwa pande mbili karibu na Kherson, pamoja na kupiga hatua kilomita 7 katika baadhi ya maeneo.

    Urusi inasema imeanza kuondoka katika jiji hilo - lakini mchakato huo unaweza kuchukua wiki.

    Tangazo la Jumatano lilitazamwa kama kikwazo kikubwa katika juhudi za vita vya Moscow, ijapokuwa maafisa wa Ukraine walikuwa na mashaka - wakionya kwamba ujanja huo unaweza kuwa mtego.

    Hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja wa kujiondoa kwa Warusi kwa kiwango kikubwa kutoka Kherson.

    Kamanda mkuu wa Ukraine Valeriy Zaluzhny alisema siku ya Alhamisi kwamba hawezi kuthibitisha au kupinga kujiondoa kwa Urusi - lakini akasema majeshi yake yamepiga hatua muhimu.

    Vita vya Ukraine: Mengi zaidi

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  15. Kijiji kinachouzwa kwa bei ya rahisi Ulaya

    Kijiji cha Salto de Castro kilichopo nchini Uhispania kinauzwa kwa pauni 259,000.

    Kijiji hiki kilichopo katika eneo hili la jimbo la Zamora lililopo kwenye mpaka na nchi ya Ureno, kina majumba maarufu ya watu wa Uhispania.

    Miongoni mwa nyumba za kijiji zipatazo 44, kuna hoteli, nyumba za kuishi, kanisa, shule na dimbwi la kuogelea pamoja na kambi ya kijeshi.

    Hatahivyo, tatizo la kijiji hiki ni kwamba hakuna mtu anayeishi huko na kimetelekezwa kwani watu walikihama zaidi ya miaka 30 iliyopita.

    Mmiliki wa kijiji hicho alikinunua mwanzoni mwa karne hii na alitaka kukifanya kiwe eneo la utalii, lakini mzozo wa eneo la ulaya ulizuia mpango huo.

    Watu wengi wameelezea haja ya kukinunua kutokana na bei yake ya chee.

    Ronnie Rodríguez, ambaye ni mwakilishi wa mmiliki wa kijiji hiki, amesema kuwa watu 300 wameelezea nia ya kununua kijiji hicho. Watu hao wanatoka mataifa ya Urusi, Ufaransa, Ubelgiji, na Uingereza. Baadhi hata wamelipa malipo ya awali ili kisichukuliwe na wanunuzi wengine, kulingana na Rodríguez.

  16. Marekani na Uhispania kuipatia Ukraine mifumo mipya na ya kisasa ya ulinzi wa anga

    Marekani na Uhispania zimetangaza kwamba zitatuma mifumo na makombora yake.

    Mshauri wa kitaifa wa masuala ya usalama nchini Marekani Jake Sullivan alitangaza kwamba Marekani Ukraine itaipatia Ukraine mifumo ya Avenger - silaha za kukabiliana na mashambulizi ya anga.

    Avenger ni bunduki zinazofyatua makombora ya aina ya Stinger, ikiwa ni mifumo ya ulinzi ya masafa mafupi.

    Idadi ya mifumo hii mipya itakayopelekwa Ukraine bado haijaelezwa.

    Kulingana naSullivan, Marekani pia itatuma makombora kwa Ukraine kwa ajili ya mifumo yaulinzi ya Hawk.

    Uhispania iliahiti kutoa msaada wa aina hizo mpya za mifumo ya ulinzi zaidi ya mifumo mingine miwili ambayo tayari iliikabidhi Ukraine.

    Kulingana na Shirika la habari la Ukriform lililonukuu vyombo vya habari vya Ukraine msaada wa Uhispania ulitangazwa na Waziri wa nchi hiyo wa ulinzi Bi Margarita Robles katika mkutano na wanajeshi wa Ukraine ambao wanapewa mafunzo nchini Uhispania..

    Hawk ni mfumo wa masafa ya kati wa kudhibiti mashambulio ya ndege: makombora yake hupiga maeneo yaliyo katika umbali wa kilomota 50 na katika kimo cha kilomita 20 kwenda juu.

    Kulingana na Bi Robles zaidi ya mifumo hiyo ya kukabiliana na mashambulio ya ndege, Uhispania itaipatia Ukraine betri za howitzers, mtambo wa jenereta wa nishati na tayari iimesafirisha sare za kijeshi (magwanda) 77,000 ya majira ya baridi kwa ajili ya wanajeshi wa Ukraine.

    Vita vya Ukraine: Mengi zaidi

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  17. Hujambo na karibu tena kwa matangazo yetu mubashara ya leo tarehe 11.11.2022