Vita vya Ukraine: Iran yakiri kupatia Urusi ndege zisizo na rubani
Urusi imekuwa ikikanusha matumizi ya ndege zisizo na rubani za Iran nchini Ukraine.
Moja kwa moja
Iran yakiri kupatia Urusi ndege zisizo na rubani kwa mara ya kwanza

Chanzo cha picha, Ofisi ya Rais Ukraine
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir Abdollahian amekiri kwamba nchi hiyo ilitoa ndege zisizo na rubani kwa Urusi.
Tehran ilithibitisha rasmi hatua hiyo kwa mara ya kwanza katika mkutano na waandishi.
Kulingana na Bw Abdollahian utoaji huo ulifanywa hata kabla ya kuanza kwa uvamizi wa Urusi wa Ukraine.
"Tulikabidhi Urusi idadi ndogo ya ndege zisizo na rubani miezi michache kabla ya vita vya Ukraine," waziri huyo alisema.
Abdollahian alipinga madai kwamba Tehran inasambaza makombora na ndege zisizo na rubani kwa Urusi kwa ajili ya operesheni za kijeshi nchini Ukraine, na kuongeza kuwa Iran inaunga mkono kukomeshwa kwa vita nchini Ukraine.
Kauli hiyo ya Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imekuja wakati kumekuwa na majadiliano kuhusu Urusi kutumia ndege zisizo na rubani za Iran nchini Ukraine, ikiwa ni pamoja na mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati na makazi ya kiraia.
Katika wiki za hivi karibuni, Ukraine imeripoti ongezeko la mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kwenye miundombinu ya kiraia, hususan matumizi ya ndege aina ya Shahed-136 zilizotengenezwa na Iran.
Urusi inakanusha matumizi ya ndege zisizo na rubani za Iran nchini Ukraine.
Vita vya Ukraine: Putin aidhinisha wakazi wa Kherson kuhamishwa

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Urusi Vladimir Putin ameidhinisha hadharani kuhamishwa kwa raia kutoka sehemu za Kherson zinazokaliwa na Urusi kusini mwa Ukraine.
Vikosi vya Kyiv vimekuwa vikisonga mbele kwa kasi katika mji huo wa kimkakati wa bandari.
Bw Putin alisema watu wanaoishi katika maeneo hatari wanapaswa kuondoka kwani "raia hawapaswi kuteseka".
Takriban watu 70,000 wameripotiwa kuhamishwa tayari kutoka Kherson - jiji kuu pekee lililopatikana na Moscow tangu wanajeshi wake walipovamia mwezi Februari.
Raia walio katika hatari ya kushambuliwa kwa makombora wanapaswa "kuondolewa", Bw Putin alisema, wakati wa likizo ya Siku ya Umoja katika Red Square ya Moscow.
Kyiv inaishutumu Urusi kwa kuwaondoa kwa nguvu raia wa Ukraine - hatua ambayo inachukuliwa kuwa uhalifu wa kivita - ingawa Moscow inakanusha hilo.
Mashambulizi makali ya kombora na ndege zisizo na rubani za Urusi kwenye miundombinu ya raia kote Ukraine yamesababisha hasara kubwa, na kufanya Kyiv kukatikiwa na umeme mara kwa mara.
Hatua ya Putin ilifuatia ripoti za siku ya Alhamisi kwamba wanajeshi wa Urusi pia walikuwa wakiondoka Kherson - jambo ambalo lingeashiria kujiondoa kwa kiasi kikubwa.
Kherson alitekwa mara tu baada ya Urusi kushambulia jirani yake tarehe 24 Februari, lakini hivi majuzi vikosi vya Ukraine vimefanikiwa kutkomboa eneo la viunga mwa mji huo.
Kenya Airways kusitisha safari 40 za ndege kufuatia mgomo wa marubani
Zaidi ya abiria 9,000 wamekwama katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyata Kenya (JKIA) jijini Nairobi na katika viwanja vingine vya ndege vya kimataifa duniani kufuatia mgomo wa marubani wa shirika la ndege la Kenya Airways.
Shirika la ndege la Kenya Airways limesema hadi safari 40 za ndege zinaweza kusitishwa katika siku ya kwanza ya mgomo wa marubani.
Mamia ya abiria wamehamishiwa katika mashirika mengine ya ndege, na wengine kupewa malazi katika hoteli jijini Nairobi wakisubiri mipango mipya ya usafiri.
Shirika hilo la ndege hata hivyo linasema linaendesha safari za ndege chache za kimataifa kwa kutumia marubani ambao sio wanachama wa chama cha marubani na ambao hawashiriki mgomo huo.
Foleni ndefu zimeshuhudiwa siku nzima ya Jumamosi huku wasafiri wenye wasiwasi wakisubiri kwa saa kadhaa kujua hali ya safari zao.
"Nilikuwa nikisafiri kwenda Mumbai kwa sababu za matibabu, na sasa ni lazima nighairi safari za ndege na uhifadhi wa hoteli, ni ghali sana," abiria mmoja aliambia BBC kwenye uwanja wa ndege.
Afrika Kusini yakosolewa kwa kufanya mazoezi ya kijeshi na Urusi

Chanzo cha picha, Getty Images
Chama kikuu cha upinzani cha DA nchini Afrika Kusini kimeilaani serikali kwa kufanya mazoezi ya pamoja ya jeshi la wanamaji na Urusi, na kuyataja kuwa "kiziwi wa sauti" na "kosa kubwa la uamuzi".
Urusi imewekewa vikwazo na mataifa kadhaa yenye nguvu duniani kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine lakini inaonekana kuwa imepata washirika miongoni mwa mataifa ya Afrika, baadhi yao yalijiepusha na azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linalolaani uvamizi huo au kuwa na mikataba ya kijeshi na nchi hiyo.
Zoezi la kwanza la kijeshi kati ya Afrika Kusini na Urusi liliripotiwa mnamo Novemba 2019.
Zoezi la wiki hii lilifanyika katika kambi ya wanamaji karibu na Durban na lilijumuisha jeshi la wanamaji la China pia.
Wiki iliyopita, serikali ya Afrika Kusini ilikuwa katika maji ya moto kwa kuruhusu oligarch ya Kirusi kuweka meli yake kubwa mjini Cape Town kinyume na matakwa ya meya wa jiji hilo.
Kwa picha: Hali JKIA baada ya marubani wa Kenya Airways kutangaza mgomo

Abiria wamekuwa wakipanga foleni katika kituo cha wasafiri wa kimataifa katika uwanja wa JKIA ili kujua hali ya safari zao. Baadhi ya safari zimeahirishwa na wateja wengine kuhamishiwa ndege zingine, lakini wengine wao wamesubiri hadi saa 6 kuhudumiwa.



Marubani wa Kenya Airways kuendelea na mgomo

Chanzo cha picha, KQ
Chama cha marubani nchini Kenya KALPA,kimetoa wito kwa wanachama wake kususia kazi kuanzia leo Jumamosi Novemba 5.
Taarifa iliyotiwa saini leo na katibu mkuu wa chama hicho Captain Murithi Nyaga, ilisema wanachama wa chama hicho hawataendesha ndege yoyote kutoka uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta kuanzia saa kumi na mbili kesho asubuhi.
“Tarehe 19 mwezi Oktoba mwaka 2022, kama hiki kilitoa ilani ya siku 14 kwa usimamizi wa shirika la Kenya Airways, ikiwa hatua ya mwisho katika juhudi za kutafuta mazingira bora ya utendakazi, na kuhakikisha shirika la Kenya Airways linasimamiwa vyema.
Muda wa Ilani hiyo ya mgomo umekamilika na sasa tuko na haki ya kuweka vifaa vyetu chini ya sehemu ya 41, sura ya nne ya katiba,” alisema mwenyekiti wa chama cha Marubani nchini Kenya Murithi Nyaga.
Wachimba migodi wananusurika kwa siku tisa chini ya ardhi kwa kunywa kahawa tu

Chanzo cha picha, NEWS1
Wachimba migodi wawili ambao walitumia siku tisa wamenasa katika mgodi wa zinki ulioporomoka wa Korea Kusini wakiishi kwa kutumia unga wa kahawa wa papo hapo wameokolewa.
Wanaume hao, wenye umri wa miaka 62 na 56, wanaaminika kuwasha moto na kujenga hema kwa plastiki. Inasemekana wako katika hali dhabiti.
Haya yanajiri wakati wa maombolezo ya kitaifa kwa Korea Kusini yakiendelea baada ya zaidi ya watu 150 kuuawa katika mkasa katika mji mkuu Seoul wiki iliyopita.
Wachimbaji hao wawili walikwama karibu mita 200 (futi 650) chini ya ardhi baada ya sehemu ya mgodi wa zinki waliokuwa wakifanya kazi kuporomoka tarehe 26 Oktoba huko Bonghwa, mashariki mwa nchi.
Hatimaye waliokolewa usiku wa tarehe 4 Novemba - zaidi ya siku tisa baada ya masaibu yao kuanza.
Wote wawili waliweza kutoka nje ya mgodi na kupelekwa katika hospitali ya mtaa. Daktari wao alisema wanapaswa kupona kabisa hivi karibuni.
Rais Yoon Suk-yeol aliita uokoaji wao "wa ajabu kweli". “Asante na asante tena kwa kurejea salama kutoka kwenye njia panda za maisha na kifo,” aliandika kwenye Facebook.
Mamlaka ilisema wachimbaji hao walinusurika kwa kunywa maji ambayo yalianguka kutoka kwenye dari na kutumia unga wa kuchanganya kahawa kama mlo.
Shughuli ya uokoaji ilianza siku ya Alhamisi wakati wafanyakazi wa dharura walipotoboa shimo na kuingiza kamera ndogo katika juhudi za kuwatafuta wachimba migodi hao, kulingana na shirika la habari la Yonhap la Korea Kusini.
Hatimaye waligunduliwa wakiwa wamekaa bega kwa bega ili kupata joto, katika chumba kikubwa ambapo mashimo kadhaa ya migodi hukutana.
Vita vya Ukraine: Putin aruhusu wafungwa wa zamani kujumuishwa jeshini

Chanzo cha picha, AFP
Wauaji waliopatikana na hatia na wauzaji dawa za kulevya ambao wametoka gerezani hivi majuzi nchini Urusi wanakabiliwa na kuandikishwa kupigana nchini Ukraine chini ya mabadiliko ya sheria.
Rais Vladimir Putin aliifanyia marekebisho sheria ya kuwaita askari wa akiba na kuwajumuisha wanaume waliopatikana na hatia ya uhalifu mkubwa ambao walitoka gerezani hivi majuzi.
Wafungwa wa zamani waliopatikana na hatia ya uhalifu wa ngono dhidi ya watoto au ugaidi bado hawajajumuishwa katika mpango huo.
Wanajeshi wa Urusi wameshutumiwa kwa uhalifu wakati wa uvamizi wa Ukraine.
Tume Huru ya Kimataifa ya Uchunguzi kuhusu Ukraine, iliyoundwa na Umoja wa Mataifa mwezi Septemba iliripoti kwamba uhalifu wa kivita ulifanywa na vikosi vya Urusi ikiwa ni pamoja na mauaji ya raia na vitendo vya "unyanyasaji wa kijinsia" uliotekelezwa na "baadhi" ya askari .
Urusi inakanusha kushambulia raia kimakusudi na inashutumu vikosi vya Ukraine kwa kushambulia kwa mizinga raia katika maeneo yanayoshikiliwa na watu wanaotaka kujitenga nchini humo, jambo ambalo Ukraine inakanusha.
Tume ya Umoja wa Mataifa ilisema imegundua "matukio mawili ya mabya yaliyotendwa na wanajeshi wa Urusi na wanajeshi wa Ukraine" lakini idadi ya tuhuma za uhalifu wa kivita dhidi ya Urusi "ni kubwa zaidi".
Musk atetea uamuzi wa kufuta wafanyakazi wa Twitter

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Bw Musk amekuwa akitafuta njia za kupunguza gharama na kupata pesa kwa njia tofauti kutoka kwa jukwaa hilo. Mmiliki mpya wa Twitter Elon Musk ametetea kufutwa kazi kwa takriban nusu ya wafanyikazi wa kampuni hiyo, akisema "hakuwa na budi" kwani Twitter ilikuwa ikipoteza zaidi ya dola milioni nne kwa siku.
Ujumbe kutoka kwa Yoel Roth, mkuu wa usalama na uadilifu wa Twitter, iliashiria "takriban asilimia 50 ya wafanyakaziwa kampuni yote imeathiriwa".Lakini Bw Musk alisema kujitolea kwa gwiji huyo wa mitandao ya kijamii katika kudhibiti maudhui "hakujabadilika kabisa".
Bw Musk, mtu tajiri zaidi duniani, alinunua Twitter kwa mkataba wa dola bilioni 44.
Bilionea huyo alisisitiza katika ukurasa wake wa twitter kwamba wote waliopoteza kazi walipewa malipo ya miezi mitatu ya kuachishwa kazi, "ambayo ni 50% zaidi ya inavyotakiwa kisheria".
Huku ripoti zikiibuka Ijumaa kwamba maelfu ya wafanyikazi wa Twitter kote duniani walikuwa katika hatari ya kupoteza kazi, maswali yakibuliwa juu ya mustakabali wa wafanyikazi waliohusika kuondoa maudhui hatari.
Vikundi vya usalama mtandaoni na wanaharakati wamependekeza Bw Musk anaweza kulegeza sera za udhibiti, na kufanya Twitter isifanye kazi vizuri katika kuondoa matamshi ya chuki na habari potofu kwenye jukwaa hilo.
Marufuku ya kudumu ya Twitter yaliyotolewa kwa watu wenye utata - ikiwa ni pamoja na rais wa zamani Donald Trump - pia inaweza kuondolewa.
Hujambo na karibu.
