Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Waziri Mkuu wa zamani wa Italia atetea Urusi kuivamia Ukraine

Silvio Berlusconi ametetea uvamizi wa Vladimir Putin nchini Ukraine, akisema kiongozi wa Urusi "alisukumwa" katika mzozo huo.

Moja kwa moja

  1. Kufikia hapo tunakamilisha matangazo haya ya moja kwa moja. Kwaheri.

  2. Idadi ya waliofariki kutokana na Ebola nchini Uganda yaongezeka

    Idadi ya watu waliothibitishwa kufariki kutokana na Ebola nchini Uganda imeongezeka na kufikia wanne.

    Wizara ya afya ya nchi hiyo ilisema katika taarifa yake Ijumaa kwamba watu wengine watatu sasa wamethibitishwakufariki. Wa kwanza alikuwa mwanamume mwenye umri wa miaka 24 aliyefariki siku ya Jumatatu.

    Wagonjwa wanne zaidi pia wamethibitishwa kuwa na virusi, na kufikisha 11 jumla ya watu walioambukizwa

    Uganda ilitangaza mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika wilaya ya kati ya Mubende mapema wiki hii.

    Hii ni mara ya tatu kwa ugonjwa wa Ebola ya Sudan kuzuka nchini humo. Chanjo zinazopatikana kwa sasa hazifanyi kazi dhidi ya aina hii.

    Lakini wataalam wanasema kuwa Ebola ya Sudan ina historia ya chini ya maambukizi na vifo.

  3. Waziri Mkuu wa zamani wa Italia atetea Urusi kuivamia Ukraine

    Waziri Mkuu wa zamani wa Italia Silvio Berlusconi ametetea uvamizi wa Vladimir Putin nchini Ukraine, akisema kiongozi wa Urusi "alisukumwa" katika mzozo huo.

    Berlusconi mwenye miaka 85 alisema vikosi vya Urusi vilikusudiwa kuwapa "watu serikali wanayostahili" kisha kuondoka.

    Waziri Mkuu huyo aliyeshika nafasi hiyo mara tatu ni mshirika wa muda mrefu wa rais wa Urusi. Wikiendi hii chama chake kinatarajiwa kutwaa mamlaka ikiwa ni sehemu ya muungano wa mrengo wa kulia katika uchaguzi mkuu nchini Italia.

    Simulizi inayodai kuwa serikali ya Ukraine ilikuwa ikiwachinja wazungumzaji wa Kirusi mashariki mwa nchi hiyo iliundwa na vyombo vya habari mjini Moscow, Bw Berlusconi aliiambia TV ya Italia.

    Alisema taarifa hiyo, iliyochochewa na vikosi vya wanaotaka kujitenga na wanasiasa wanaopenda utaifa katika serikali ya Urusi, ilimuacha Putin bila chaguo ila kuanzisha uvamizi mdogo.

    "Putin alisukumwa na wakazi wa Urusi na chama chake na mawaziri wake kubuni operesheni hii maalum," alisema.

    "Wanajeshi walipaswa kuingia, kufika Kyiv ndani ya wiki moja,na kuchukua nafasi ya serikali ya Zelensky na watu wake watulivu na wiki moja baadaye kurudi," Bw Berlusconi aliongeza.

  4. Vita vya Ukraine: Urusi yatangaza watu ambao hawatajumuishwa jeshini huku wanaume wakitoroka nchi

    Wizara ya ulinzi ya Urusi imefichua idadi kubwa ya kazi ambazo wawafanyakazi wake hawataruhusiwa kujiunga na jeshi kwa lengo la kuongeza juhudi zake za kivita nchini Ukraine.

    Wafanyakazi wa teknolojia ya mawasiliano, benki na waandishi wa habari wanaofanya kazi kwa vyombo vya habari vya serikali wataepuka "agizo kujumuishwa jeshini" liliotangazwa na Rais Vladimir Putin Jumatano.

    Takriban raia 300,000 wanakabiliwa na uwezekano wa kuijumuishwa jesheni kama sehemu ya harakati hiyo.

    Hatua hiyo imesababisha baadhi ya wanaome kukimbilia mipakani huku vijana wakijaribu kutoroka ili kukwepa mpango huo.

    kitangaza misamaha hiyo siku ya Ijumaa, wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema waajiri lazima waandae orodha ya wafanyikazi wanaokidhi vigezo na kuiwasilisha kwa ofisi zake.

    Lakini ilikubali baadhi ya sekta zilipaswa kutengwa ili "kuhakikisha kazi ya viwanda maalum vya teknolojia ya juu, pamoja na mfumo wa kifedha wa Urusi" haukuathiriwa na uhamasishaji huo mkubwa kijeshi wa kwanza wa nchi tangu Vita vya Pili vya Dunia.

  5. Ujerumani iko tayari kuwasaidia Warusi wanaotoroka kusajiliwa kama wanajeshi wa akiba

    Inadaiwa kuwa Ujerumani iko tayari kuwasaidia Warusi wanaotoroka kusajiliwa kama wanajeshi wa akiba, amesema Mwandishi wa BBC News Damien McGuinness kutoka Berlin.

    ‘’Warusi wanaokataa vita hivi vya ufashisti wanapaswa kupewa hifadhi katika Ulaya huru,’’ alisema mmoja wa wanasiasa wakuu wa chama tawala cha Social Democratic Party cha Ujerumani.

    Kwa wengi katika serikali ya Ujerumani, hawa ni Warusi ambao wanaondoka nchini ili kuepuka kuitwa vitani nchini Ukraine.

    Bado haijawa wazi jinsi hii itafanya kazi: kama watapewa hifadhi au kupewa visa vya kibinadamu.

    Kwa vyovyote vile, inaonekana kuna makubaliano ya jumla nchini Ujerumani kwamba kulaumu Warusi wote hakutakuwa jambo la tija na kwamba ‘’wapinzani wa Kirusi’’ wanapaswa kusaidiwa.

    Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz pia anapinga mapendekezo ya hivi karibuni ya baadhi ya nchi za Ulaya Mashariki kufunga mipaka ya Umoja wa Ulaya kwa raia wa Urusi.

    Mara kwa mara aliita uvamizi huo ‘’Vita vya Putin’’ na kusema kwamba Warusi wanaopinga Kremlin wanapaswa kuungwa mkono.

    Soma zaidi:

  6. EU inaandaa vikwazo vipya dhidi ya Urusi

    Wazungu wameanza kujadili vikwazo vipya dhidi ya Urusi kujibu uamuzi wa Vladimir Putin wa kusajili wanajeshi wa akiba, vitisho vyake vya siri vya nyuklia dhidi ya Magharibi, na ahadi yake ya wazi ya kunyakua maeneo mengine kadhaa ya Urusi.

    Vikwazo vipya vya Ulaya vinaweza kuwa ishara na kutangaza kitu.

    Wakati wa miezi sita ya vita, Ulaya ilikata uhusiano wake sana tu wa kibiashara na kifedha na Urusi.

    Baada ya mara sita na nusu ya vikwazo, EU ina kadi mbiu mbili zilizosalia: bei ya juu ya mafuta na kuweka ukomo kwa bei ya gesi ya Urusi.

    Ya kwanza inapingwa na wachache, wakati ya pili inapingwa na wengi katika EU, kwa kuwa hatua hizi ni ngumu kutekeleza na zinachangia kizuizi cha mafuta na gesi na Urusi katika majira ya baridi ijayo.

    Majadiliano ya vikwazo yalianza Ijumaa na yanapaswa kukamilishwa na mkutano wa kilele wa viongozi wa EU-27 huko Prague mnamo Oktoba 6-7.

    Msingi wa vikwazo vipya unaweza kuwa upanuzi wa orodha ya vikwazo kwa watu binafsi na makampuni, pamoja na ukomo wa bei ya mafuta ya kutoka Urusi.

    Itaanza kutekelezwa kuanzia Desemba, lakini sio kwa usafirishaji wa kupitia mabomba.

    Ulaya imepiga marufuku bima, ufadhili na usafirishaji wa mafuta kutoka Urusi.

    Marekani iliogopa kwamba vikwazo vya Ulaya vitasababisha kuongezeka kwa bei za dunia na kutoa njia mbadala – ukomo wa bei kwamafuta ya kutoka Urusi.

    Akijibu hatua hiyo, Putin alisema kwamba basi hatasafirisha chochote: si mafuta wala gesi, wala bidhaa za mafuta.

    Bado haijabainika nini kitatokea kwa vikwazo hivyo ikiwa EU itaamua kuweka ukomo kwa bei ya mafuta yaliyonunuliwa kutoka Urusi kama sehemu ya vikwazo vipya.

    Na pia, si ukweli kwamba nchi zote 27 zitakubaliana na hili.

    Mara ya mwisho, Hungary ilipinga vikali, na matokeo yake idhini ya vikwazo vya mafuta ilichelewa, na vikwazo wenyewe viligeuka kutekelezwa nusu na kuchelewa kwa miezi sita.

    Soma zaidi:

  7. China: Mwanamume aliyeshambilia wanawake waliokuwa wanakula chakula afungwa miaka 24 jela

    Mwanamume aliyeongoza shambulizi baya dhidi ya wanawake wanne waliokuwa wanakula katika mgahawa mmoja nchini China amehukumiwa kifungo cha miaka 24 jela.

    Chen Jizhi alipatikana na hatia ya shambulio katika mji wa kaskazini-mashariki wa Tangshan mwezi Juni ambalo lilianza wakati mmoja wa wanawake hao alikataa alichokuwa anataka mwanamume huyo.

    Wanaume wengine 27 walihukumiwa kutokana na vurugu hizo ambapo walitumia chupa, viti na ngumi kuwapiga wanawake hao.

    Video ya uchunguzi ilisambaa, na kuzua mjadala kuhusu unyanyasaji wa kijinsia nchini Uchina.

    Baada ya shambulio hilo, wanawake wawili kati ya hao walikaa katika chumba cha wagonjwa mahututi kwa muda, huku wanawake wengine wawili wakionekana kwenye picha wakiwa wamezungukwa na damu kila mahali, ingawa majeraha yao awali yalichukuliwa na polisi kama ‘’madogo’’.

    Chen alitozwa faini ya yuan 320,000 (£40,000, $45,000) pamoja na kifungo chake cha miaka 24 jela.

    Washtakiwa wengine walihukumiwa kifungo cha kati ya miezi sita na miaka 11 jela.

    Mahakama iliamuru Chen na washtakiwa watano kufidia gharama za matibabu ya waathiriwa wanne na hasara nyinginezo, gazeti la Global Times linaripoti.

    Wanaharakati wa haki za wanawake wanasema unyanyasaji wa majumbani bado umeenea na hauripotiwi sana nchini China.

    Ripoti iliyotolewa punde tu baada ya shambulio hilo ilibaini kuwa ushughulikiaji wa kesi hiyo na naibu mkurugenzi wa polisi wa wilaya na maafisa wengine ulikuwa ‘’wa polepole na kwa njia isiofaa.’’

    Mamlaka ya Uchina ilikagua mjadala wa mtandaoni kuhusu mashambulizi dhidi ya wanawake, na kujaribu kuliweka shambulizi hilo kama uhalifu wa magenge, waandishi wa habari wanasema.

    Uovu katika shambulizi hilo ulizua hasira na mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii, na kuwa moja ya mada iliyojadiliwa zaidi kwenye mtandao maarufu wa kijamii wa Weibo nchini China.

  8. Wakenya 22 waokolewa kutoka kwa walanguzi Asia

    Wakenya 22 wameokolewa kutoka kwa mashirika ya ulanguzi wa binadamu huko Laos Kusini Mashariki mwa Asia.

    Raia wa Uganda na Burundi pia waliokolewa wakati wa operesheni hiyo iliyoratibiwa na Serikali za Kenya, Laos, na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji.

    Haya yanajiri wiki chache tu baada ya kundi jingine la Wakenya waliokuwa wakishikiliwa na walanguzi wa binadamu katika nchi jirani ya Myanmar kuokolewa.

    Ubalozi wa Kenya nchini Thailand hivi majuzi uliwatahadharisha raia wake kuwa waangalifu na kazi za ualimu, mauzo na huduma kwa wateja zinazotangazwa na makampuni ya biashara yenye kujihusisha na Afrika Mashariki.

    Maafisa waliwashauri waombaji kuthibitisha uhakika wa wanachojihusisha nacho kabla ya kuondoka nchini.

    Serikali inasema imepokea simu za masikitiko kutoka kwa Wakenya waliokwama katika mataifa mengi Kusini-mashariki mwa Asia baada ya kuangukia kwenye ulaghai wa kazi.

    Wakenya wengi ambao hawajashughulikiwa wamenaswa na matangazo ya kazi za kiwandani ambayo yanageuka kuwa madanguro, uhalifu wa mtandaoni na ulanguzi wa dawa za kulevya.

    Ukosefu wa matarajio ya kazi umewasukuma vijana wengi kutoka makwao na kuwaweka katika hatari ya ulanguzi wa binadamu.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Vurugu yashuhudiwa wakati lori lililokuwa limebeba unga lilipopinduka Kenya

    Video zinasambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha raia wakikimbilia kuchukua mabandali ya unga wa mahindi kwenye lori lililopinduka kwenye barabara kuu katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

    Umati wa waporaji ni pamoja na madereva, waendesha teksi, waendesha pikipiki na watembea kwa miguu.

    Chanzo cha ajali hiyo hakijafahamika na hakukuwa na maafisa wa polisi walioonekana, kulingana na video inayosambazwa.

    Mwandishi wa habari wa ndani ni miongoni mwa wale ambao wameweka picha kwenye Twitter kutoka eneo la tukio

    Bei za bidhaa za kimsingi za vyakula kama vile unga wa mahindi na unga wa ngano, viazi, mboga mboga na matunda zimekuwa zikipanda nchini - kutokana na mchanganyiko wa mambo ya nje na ya ndani.

    Wiki iliyopita serikali ilifutilia mbali ruzuku ya petroli ambayo imeongeza bei ya reja reja hadi juu kabisa.

  10. Oleksandr Usyk ataka 'mapambano matatu zaidi' kabla ya kustaafu, likiwemo na Tyson Fury

    Oleksandr Usyk wa Ukraine anasema anataka ‘’mapambano matatu zaidi’’ kabla ya kustaafu, likiwemo pambano la uzani wa juu na Muingereza Tyson Fury.

    Usyk, 35, alihifadhi mataji yake ya WBA (Super), WBO na IBF dhidi ya Anthony Joshua mwezi uliopita huku Fury akiwa na mkanda wa WBC.

    Pia anataka pambano zuri la ‘’kituko’’ na bingwa wa uzani wa wasuper-middleSaul ‘Canelo Alvarez’ kabla ya kumalizia taaluma yake kwenye Uwanja wa Olimpiyskiy huko Kyiv.

    ‘’Nahitaji tu kumpiga Fury halafu utakuwa wakati wa kustaafu kwangu,’’ alisema.

    Usyk alimpigia simu Fury baada ya kumpiga Joshua kwa mara ya pili kabla ya promota wa Fury Frank Warren kusema pambano hilo ‘’litafanyika’’.

    Lakini mapema mwezi huu Fury, 34, alimpa Joshua nafasi ya kupigania taji lake baadaye mwaka huu na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 sasa ‘’amekubali masharti yote’’ kwa pambano la Waingereza 3 Disemba.

    ‘’Kuunganishwa kwa mikanda yote ni muhimu zaidi kuliko pambano au kutetea taji lolote,’’ Usyk alisema katika mahojiano kwenye ukurasa wake wa YouTube.

    ‘’Nataka kumshinda Fury na sitaki kufanya kazi nyingi hivyo kwa ajili ya kutetea tena taji lingne’’. Kuna mengi zaidi ya hayo na ninaweza kuyafanikisha.’’

    ‘Canelo Alvarez’ alishinda kwa pointi nyingi zaidi dhidi ya Gennady Golovkin wikendi iliyopita ili kusuluhisha shindano lao la tatu kwa ushindi wa pili kwa raia huyo wa Mexico, 32, baada ya sare ya kutatanisha katika pambano lake la kwanza na Wakazakh.

    ‘’Ninaweza kuwa na mapigano matatu zaidi,’’ Usyk aliongeza.

    ‘’Ni jambo la kweli kabisa kuwa katika kiwango changu cha juu. Nikiwa na Fury, Canelo na pambano la kumuaga huko Olimpiyskiy.

    ‘’Akiwa na Canelo alisema alitaka kupigana nami. Itakuwa pambano lisilo la kawaida kwa ajili ya kupata pesa tu.’’

    Pia unaweza kujikumbusha:

  11. Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu yaongeza idadi ya wafanyakazi wake nchini Ukraine

    Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), Karim Khan, alitangaza kuwa atapeleka wafanyakazi wa ziada nchini Ukraine kuchunguza kesi za kijeshi.

    Wanachama wa timu yake watasafiri hadi Ukraine wiki ijayo kuchunguza madai ya uwezekano wa uhalifu wa kivita mashariki mwa nchi hiyo, Khan alisema katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York siku ya Alhamisi.

    Mnamo mwezi Mei, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ilifanya operesheni kubwa zaidi katika historia yake nchini Ukraine.

    Tangu wakati huo, wataalam wa mahakama wanakuwepo kila wakati nchini humo.

    ‘’Sasa tuko katika hatua ya uchunguzi, kukiwa na lengo na bila upendeleo, wakati mwingine kunakuwa na kazi ya kuchosha sana kubaini ukweli na kutenganisha ukweli na uwongo,’’ alisema.

    Kulingana na mwendesha mashitaka mkuu, kile ambacho tayari amekiona nchini Ukraine kinasababisha wasiwasi mkubwa.

    ‘’Baada ya kuzuru Ukraine mara tatu, nimeona uharibifu mwingi na mateso jambo ambalo linaimarisha azimio langu na dhana yangu ya hapo awali kwamba kuna sababu za msingi za kuamini kwamba uhalifu umetendwa,’’ Khan alisema.

    ICC inachunguza uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu, mauaji ya halaiki na vitendo vya uchokozi.

    Khan alisema kuwa vipaumbele vya uchunguzi wa mahakama ni kulengwa kwa makusudi vitu vya kiraia na kulazimishwa kwa watu kuondoka Ukraine, wakiwemo Watoto.

    Soma zaidi:

  12. Jumuiya ya Afrika Magharibi imewekea vikwazo kwa serikali ya Guinea

    Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (Ecowas) imeamua kuwawekea vikwazo watu binafsi katika serikali ya kijeshi ya Guinea ili kukabiliana na mapinduzi ya mwaka jana mjini Conakry.

    Viongozi hao kutoka umoja huo walikutana mjini New York walikokuwa wakihudhuria Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

    Walikubaliana juu ya ‘’vikwazo vya taratibu’’ kwenye orodha ya watu wanaohusishwa na serikali ya Guinea ambao watatambuliwa ‘’hivi karibuni,’’ shirika la habari la AFP linaripoti.

    Viongozi wa Guinea wanasema wanahitaji miaka mitatu kuirejesha nchi hiyo katika demokrasia na hawajafurahishwa na matakwa ya Ecowas ya kutaka mabadiliko ya haraka katika kipindi cha mpito.

    Katika taarifa yake, waziri mkuu wa mpito wa Guinea, Bernard Gomou, awali alimuelezea mkuu wa Ecowas na rais wa nchi jirani ya Guinea-Bissau, Umaro Sissoco Embalo, kama ‘’kibaraka’’ na mtu ‘’aliyefurahi kupita kiasi’’ ambaye ‘’alilazimisha kuingia’’ kuongoza shirika la kikanda.

    Guinea ilisimamishwa kuwa miongoni mwa nchi za Ecowas kufuatia mapinduzi ya Septemba mwaka jana.

    Soma zaidi:

  13. Mtoto wa Desmond Tutu azuiwa kuendesha ibada ya mazishi kutokana na ndoa yake ya jinsia moja

    Mtoto wa marehemu Desmond Tutu amezuiwa na Kanisa la Uingereza kuongoza mazishi kwa sababu ameolewa na mwanamke.

    Mpho Tutu van Furth ni kasisi wa Kianglikana katika Dayosisi ya Washington na alikuwa ameombwa kuongoza mazishi ya marehemu baba yake wa imani, Martin Kenyon, huko Shropshire siku ya Alhamisi.

    Bi Tutu van Furth aliambia BBC kwamba "Hatua hiyo ni mbaya na imemuumiza’’.

    Kanisa la Anglikana haliruhusu makasisi wake kuwa katika ndoa ya watu wa jinsia moja kwa sababu fundisho lake rasmi ni kwamba ndoa ni kati ya mwanamume mmoja na mwanamke mmoja.

    Hata hivyo kanisa dada la Anglikana nchini Marekani, The Episcopal Church, wanaruhusu makasisi kuingia katika ndoa za jinsia moja.

    "Ushauri ulitolewa kulingana na mwongozo wa sasa wa Baraza la Maaskofu kuhusu ndoa za jinsia moja," taarifa kutoka Dayosisi ya Hereford ilisema.

    Askofu wa zamani wa Liverpool, Mchungaji Paul Bayes, ambaye ni mwanaharakati wa kanisa kubadili msimamo wake , alisema "tunahitaji mabadiliko".

    "Tunahitaji kwa haraka kutengeneza nafasi kwa ajili ya dhamiri, nafasi kwa ajili ya uchungaji, na nafasi ya upendo," alisema.Baada ya familia ya Bw Kenyon kuambiwa uamuzi wa Kanisa, walihamisha ibada ya mazishi kutoka St Michael and All Angels huko Wentnor, karibu na Bishops Castle, hadi kwenye jumba la kasri la karibu ili Bi Tutu van Furth aweze kuongoza na kuhubiri.

    "Inasikitisha sana," Bi Tutu aliambia BBC . "Inahisi kama jibu la ukiritimba na labda ukosefu wa huruma.

    Baba yake Desmond Tutu, aliyefariki Desemba 2021, alishinda tuzo ya amani ya Nobel mwaka 1984 kwa mapambano yake dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini. Pia alifanya kampeni kuunga mkono haki za wapenzi wa jinsia moja na kuunga mkono ndoa zao.

  14. Ukraine yadaiwa kupokea mfumo wa kuzuia ndege zisizo na rubani kutoka Israel

    Gazeti la Israel la Zman Yisrael linaripoti kwamba Ukraine inadaiwa kupokea mifumo ya kuzuia ndege zisizo na rubani ya Israel.

    Chanzo cha uchapishaji wa habari hizi kilisema kuwa mauzo hayo yalifanywa kupitia Poland ili kukwepa marufuku ya Israeli ya kuuza silaha hizo za hali ya juu kwa Ukraine.

    IDF hutumia mifumo hii ya kuzuia ndege zisizo na rubani kutoka Gaza, Lebanon na Syria.

    Serikali inaonekana kufumbia macho uuzaji huo, ikiwa imedhamiria kutoruhusu mpango wa kusambaza teknolojia za hali ya juu za ulinzi kwenda Kiev, vyombo vya habari vya Israeli viliandika ..

    Kulingana na uchapishaji huo, kampuni iliyosafirisha mifumo hii iliiambia Wizara ya Ulinzi kwamba uuzaji huo ulifanywa kupitia Poland, na inaonekana kwamba haikujua kuwa Warsaw ilitumika kuhamisha silaha kwa Kyiv kwa matumizi ya kuzikabili ndege zisizo na rubani za Urusi.

    Israel ni moja wa viongozi wa ulimwengu katika kubuni na kutengeneza mifumo ya kuzuia ndege zisizo na rubani na ina angalau kampuni sita zinazohusika katika hili: IAI, Elbit Systems, MCTECH, Avnon Group na Spear.

    Soma zaidi:

  15. CNN yaghairi mahojiano na rais wa Iran baada ya kumlazimisha mtangazaji avae hijab

    Mwandishi wa habari mkongwe wa CNN Christiane Amanpour alighairi mahojiano na Rais wa Iran Ebrahim Raisi baada ya kumtaka avae hijabu kwenye mkutano wao mjini New York.

    Amanpour alidokeza kuwa hakuna marais waliotangulia walioomba hili alipowahoji nje ya Iran.Anasema msaidizi wa Raisi alimwambia ni kwa sababu ya "hali nchini Iran".

    Mahojiano hayo yangekuwa ya kwanza kwa Bw Raisi katika ardhi ya Marekani, wakati wa ziara yake katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.Amanpour alisema alikuwa tayari kuiendesha wakati mmoja wa wasaidizi wa rais aliposisitiza kwamba alifunika nywele zake kwa ombi la Bw Raisi.

    "Tuko New York, ambapo hakuna sheria au mila kuhusu hijabu," alisema baadaye kwenye ukurasa wake wa Twitter.

    Amanpour alisema msaidizi wa Bw Raisi aliweka wazi mahojiano hayatafanyika ikiwa hatavaa hijabu, akisema ni "suala la heshima".

    Timu yake iliondoka kwenye mahojiano ikikataa kile alichokiita "hali isiyokuwa ya kawaida na isiyotarajiwa".Mtangazaji huyo wa Marekani baadaye alichapisha picha yake akiwa hana hijabu mbele ya kiti kilichokuwa tupu ambapo Bw Raisi angeketi kwa mahojiano yao.

    Kifo cha mwanamke raia wa Iran kwa madai ya kuvunja sheria za hijabu kimezua machafuko makubwa nchini huko.Mahsa Amini, 22, alizirai wiki iliyopita, saa chache baada ya polisi wa maadili kumkamata.

    Maafisa waliripotiwa kumpiga Bi Amini kichwani kwa fimbo na kugonga kichwa chake kwenye mojawapo ya magari yao. Polisi wamesema hakuna ushahidi wa kutendewa vibaya na kwamba alipata "kushindwa mshtuko wa ghafla".

    Maandamano hayo ambayo sasa ni siku ya saba yamefikia miji na miji mingine 80 ya Jamhuri ya Kiislamu. Takriban watu 17 wameuawa.

    Soma zaidi:

  16. Marekani imesema inachukulia kwa uzito vitisho vya Urusi kutumia Nyuklia dhidi ya Ukraine

    Marekani imesema inachukua "kwa uzito" vitisho vilivyofichwa vya Vladimir Putin vya kutumia silaha za nyuklia kutetea maeneo ya Ukraine, afisa wa ngazi ya juu wa Ikulu ya White House aliambia BBC.

    John Kirby alisema Marekani haibadilishi "mkao wake wa kimkakati wa kuzuia", lakini kwamba Bw Putin alizungumza bila kuwajibika.

    Siku ya Jumatano kiongozi wa Urusi alionya nchi yake itatumia njia zote ili kulinda eneo lake.

    Ilikuja wakati mikoa minne ya Ukraine ambayo sehemu yake inamilikiwa na vikosi vya Urusi inakaribia kuandaa kura za haraka za kujiunga na Urusi.

    Ukraine na washirika wake wanaziita kura hizi kuwa ni zoezi la udanganyifu, lililoundwa ili kutoa uhalali wa uongo wa unyakuzi haramu.

    "Ni mfano hatari kwa Bw Putin kutumia matamshi ya aina hii katika muktadha wa vita ambavyo ni dhahiri kwamba anashindwa ndani ya Ukraine," msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa Bw Kirby aliambia BBC.

    Mwenendo wa Urusi nchini Ukraine ulilaaniwa vikali katika mkutano maalum wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York siku ya Alhamisi.

    "Wiki hii, Rais Putin alisema Urusi haitasita kutumia 'mifumo yote ya silaha inayopatikana' katika kukabiliana na tishio kwa uadilifu wa eneo lake - tishio la kutisha zaidi kutokana na nia ya Urusi ya kunyakua maeneo makubwa ya Ukraine katika siku zijazo. .." alisema Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony Blinken.

    Soma zaidi: