Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Ukraine ilimuua binti wa mshirika wa Putin, Urusi yasema

Urusi imewashutumu maafisa wa ujasusi wa Ukraine kwa kuhusika na mauaji ya Darya Dugina, binti wa mmoja wa wafuasi wakuu wa Rais Vladimir Putin.

Moja kwa moja

  1. Tunakomea hapo kwa leo hadi kesho kwaheri.

  2. Ryan Giggs: Ni muda wake wa kulipia gharama, uendesha mashitaka walieleza jopo la mahakama

    Ryan Giggs amekabiliwa na ukweli halisi na ni mara ya kwanza kwake"kulipia gharama", jopo limeambiwa

    Nyota wa zamani wa Manchester United , 48, amekana tabia ya udhibiti, pamoja na kumshambulia mpenzi wake wa zamani wa kike Kate Greville, 38, mwezi Novemba 2020.

    Pia amekana kumshambulia dada yake Emma, mwenye umri wa miaka 26.

    Mwendesha mashitaka Peter Wright QC alisema kuwa jumbe zilizotumwa na Bw Giggs zilieleza taarifa ya "umiliki wa hisia, kutumia nguvu za mwili kupindukia, na kudhibiti na kulazimisha".

    Katika hotuba yake katika mahakamaya Manchester Crown, Bw Mr Wright alirejelea maelezo yake kwamba kulikuwa na ‘’ Ryan Giggs wawili tofauti kabisa ".

    Yule ambaye anaonekana hadharani na Ryan Giggs ambaye hujitokeza katika nyakati fulani ndani ya nyumba," aliongeza

    Wright alisema Giggs "alidhani kuwa angefanya lolote analotaka kufanya" kwa Bi Greville na kwamba "asingefanywa lolote".

    Bw Wright alilikumbusha jopo la mahakama simu za dharura zilizopigwa katika nambari 999 na Bi Greville dada yake Emma kufuatia mashambulizi ya Giggs dhidi yake.

    Ameelezea simu hizo -ambapo Bw Giggs alisikika akimfokea kwa maneno makali Bi Greville.

  3. Matokeo ya uchaguzi Kenya 2022: Je pingamizi la uchaguzi la Bw Odinga linahusu nini?

    Sehemu muhimu ya kesi ya Raila Odinga kuhusuuchaguzi wa Kenya ni juu ya nafasi ya Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi na mipaka (IEBC), Wafula Chebukati.

    Bw Odinga anasema kuwa asingepaswa kumtangaza William Ruto kama mshindi bila makubaliano na wengi wa makamishna wa tume , na hivyo “kutovuka ” majukumu yao ya kikazi.

    Tunafahmu kuwa makamishna wanne kati ya saba hawakuunga mkono tangazo la matokeo ya uchaguzi wa urais.

    Lakini kuna ufafanuzi tofauti wa mamlaka aliyonayo Bw Chebukati. Baadhi ya wataalamu wanaamini kuwa chini ya tatiba ya Kenya, yeye pekee ndiye anayepewa mamlaka ya kutangaza matokeo ya uchaguzi wa urais, akifanya kazi kama msimamizi wa kura ya urais.

    Pia wanaelezea ukweli kwamba anawajibika kisheria ya kufanya hivyo katika kipindi cha siku saba kuanzia tarehe ulipofanyika uchaguzi.

    Hatahivyo, maoni mengine ya kisheria yanadai chini ya sheria ya IEBC ya2011 IEBC, BwChebukati anaweza tu kutangaza kile ambacho kamishna “amejumlisha na kuthibitisha.”

    Hiki ndicho Mahakama ya juu zaidi ya Kenya itatakiwa kutatua.

    Unaweza pia kusoma:

    • Raila Vs Ruto: Mawakili katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais Kenya
    • Wafahamu majaji wa Mahakama ya Juu zaidi Kenya
    • Kinachofuata ni kipi?Macho yote sasa katika mahakama ya Juu zaidi baada ya Odinga kukataa matokeo
  4. Ukraine ilimuua binti wa mshirika wa Putin, Urusi yasema

    Urusi imewashutumu maafisa wa ujasusi wa Ukraine kwa kuhusika na mauaji ya Darya Dugina, binti wa mmoja wa wafuasi wakuu wa Rais Vladimir Putin.

    FSB, kitengo cha usalama wa ndani cha Urusi, kinasema kuwa raia wa Ukraine aliyewasili nchini humo mwezi Julai ndiye aliyehusika na shambulio hilo la Jumamosi usiku.

    Maafisa walisema kuwa mshukiwa huyo aliondoka Urusi na kuelekea Estonia baada ya Dugina kuuawa kwenye gari lililotegwa bomu kwenye barabara moja viungani mwa mji wa Moscow.

    BBC haikuwezi kuthibitisha madai hayo.

    Ukraine imekanusha kuhusika na shambulizi hilo na Ilya Ponomarev, mbunge wa zamani wa Urusi, alisema jana kwamba makundi ya ndani yanayopinga utawala wa Putin ndiyo yalihusika na mauaji hayo.

    Darya Dugina ni nani

    Darya Dugina, 29, alikuwa mwandishi wa habari, mchambuzi wa kisiasa na mfuasi mkubwa wa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

    Alionekana mara kwa mara kwenye runinga ya Urusi na mnamo Mei aliita vita vya Ukraine "mgongano wa ustaarabu".

    Mapema mwaka huu aliidhinishwa na mamlaka za Marekani na Uingereza, ambazo zilimshutumu kwa kuchangia "taarifa potofu" mtandaoni kuhusu uvamizi wa Urusi.

    Dugina aliuawa Jumamosi jioni wakati bomu lilipolipuka kwenye gari alilokuwa akiendesha karibu na Moscow.

    Kumekuwa na uvumi mkubwa kwamba bomu hilo linaweza kuwa lilikusudiwa babake, mwana itikadi kali wa Urusi Alexander Dugin.

    Soma zaidi:

  5. Uchaguzi Kenya 2022: Odinga awasilisha lori lililojaa makaratasi ya ushahidi

    Mwanasiasa mkongwe wa Kenya Raila Odinga amefika mahakamani na lori lililojaa karatasi za ushahidi alipokuwa akiwasilisha kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais.

    Gazeti moja nchini limeshirikisha kwenye ukurasa wa Twitter picha ya lori hilo likiwasili katika jengo la mahakama:

    Bw Odinga, mgombea mwenza wake, Martha Karua na mawakili watakaowawakilisha tayari wamewasilisha kesi hiyo katika Mahakama ya Juu.

    Mahakama hiyo ina wiki mbili za kuchunguza kesi hiyo na kutoa uamuzi.

    Mmoja wa mawakili wa Bw Odinga ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter walipokuwa wakiwasilisha kesi mahakamani:

  6. Waziri Mkuu wa Somalia aapa kuchukua hatua baada ya shambulio dhidi ya hoteli

    Waziri Mkuu wa Somalia Hamsa Abdi Barre ameahidi kuwawajibisha maafisa walioshindwa kuzuia shambulio baya la al-Shabab kwenye hoteli ya Hayat mjini Mogadishu.

    Bw Barre alisema hayo kwenye televisheni ya Taifa ya Somalia inayomilikiwa na serikali baada ya vikosi vya usalama kukomesha uvamizi huo uliyodumu saa 35 katika hoteli hiyo maarufu.

    "Hatuwezi kuvumilia kurudiwa kwa kile kilichotokea," alisema na kuapa kwamba "wale ambao walipuuza majukumu yao watawajibishwa".

    Waziri wa Afya Ali Hajji Aden alisema kuwa watu 21 waliuawa na 117 kujeruhiwa katika mapigano kati ya vikosi vya usalama na wanamgambo wa al-Shabab katika hoteli hiyo.

    Bw Barre aliwatembelea waliojeruhiwa na kusema waliojeruhiwa vibaya watapelekwa nje ya nchi kwa matibabu maalum.

    Serikali ya Somalia ilikosolewa vikali kwa kushindwa kukomesha haraka kuzingirwa kwa hoteli.

    Wanasiasa walielezea wasiwasi wao juu ya uwepo wa vitengo tofauti vya vikosi vya usalama bila amri kuu huko Mogadishu, ambayo walisema yenyewe ni "tishio la usalama.

    Maelezo zaidi:

    • Uvamizi wa hoteli Somalia: Zaidi ya 20 wafariki katika shambulio la al-Shabab
    • Mashambulio ya mabomu ya 1998: Al shabaab iliwezaje kushambulia maeneo ya ndani ya afrika mashariki?
    • Je wapiganaji wa al-Shabab kutoka Somalia wana malengo gani?
  7. Wanaharakati wa mazingira wa nchini DRC wakabiliwa na vitisho

    Mashirika manane ya mazingira yenye makao yake makuu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yanasema kuwa yanakabiliwa na vitisho kwa sababu ya kampeni yao dhidi ya upigaji mnada wa vitalu vya mafuta na gesi.

    Mashirika ambayo ni pamoja na Greenpeace Africa yanasema wanakampeni wamepokea vitisho vya moja kwa moja ambavyo ni pamoja na tuhuma za uhaini, vitisho vya kuuawa na kupigiwa simu na watu wasiojulikana.

    Serikali nchini DR Congo ilizindua mnada wa haki za leseni na kuahidi kuwa mazingira yatalindwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

    Tisa kati ya vitalu vya mafuta viko katika msitu mkubwa wa "bonde la kati" na eneo la peatlands magharibi mwa nchi na mipango ya kuchimba visima katika eneo hilo imekuwa na utata.

    Ombi la kusitisha maendeleo ya mafuta na gesi nchini lililozinduliwa na mashirika yasiyo ya kiserikali kabla ya mnada huo limevutia zaidi ya watia saini 100,000.

    Rais Felix Tshisekedi anasema uzalishaji wa mafuta na gesi utaruhusu nchi hiyo kupunguza utegemezi wake katika uchimbaji madini.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Watu zaidi ya kumi wafariki nchini Uganda kutokana na tuhuma za pombe yenye sumu

    Polisi kaskazini-magharibi mwa Uganda wanachunguza vifo vya watu zaidi ya kumi, wanaoshukiwa kufariki baada ya kunywa pombe iliyotengenezwa nchini humo inayodaiwa kuwa na sumu.

    Vifo hivyo vinasemekana kusajiliwa kati ya Jumamosi na Jumapili.

    Wengine kadhaa, akiwemo mfanyabiashara mmoja aliyekuwa akiuza pombe hiyo inayojulikana kwa jina la City 5 Pineapple Flavored Gin, wamelazwa hospitalini kwa tuhuma kuwa ilitiwa sumu.

    Haijulikani ni viambato gani katika kinywaji hicho vimetumika, lakini ‘maji yasiyo na madini’’, pombe ya ziada na ladha ya mananasi’’ yameorodheshwa kwenye chupa.

    Msemaji wa jeshi la polisi mkoani humo amesema kuwa sampuli za pombe hiyo zimekusanywa na zitawasilishwa kwa mkemia wa serikali kufanya vipimo.

    Washukiwa wanne wametiwa mbaroni, na kiwanda ambapo pombe hiyo ilikuwa ikitengenezwa kimefungwa, huku uchunguzi ukiendelea.

    Vifo kutokana na pombe hiyo inayosemekana kuwa jambo la kawaida sana nchini Uganda. Mwaka 2010, takriban watu 80 walikufa kusini-magharibi mwa Uganda baada ya kunywa pombe iliyotiwa methanol, kulingana na mamlaka.

  9. Kenya: Tume ya IEBC yatangaza tarehe mpya ya uchaguzi katika maeneo ulioahirishwa

    Tume Huru ya uchaguzi na Mipaka (IEBC) nchini Kenya imetangaza Agosti 29 kuwa siku ambayo itaendesha uchaguzi mdogo katika maeneo ambayo upigaji kura uliahirishwa katika Uchaguzi Mkuu uliokamilika.

    Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alisema tume hiyo imejiandaa kikamilifu kuandaa uchaguzi siku ya Jumatatu baada ya kuahirisha zoezi hilo mara mbili.

    ‘’Tutafanya uchaguzi Jumatatu labda kuwe na mapendekezo mengine kutoka kwenu,’’ Chebukati aliwaambia wagombeaji walioshiriki uchaguzi huo wakati wa mkutano nao katika eneo la Bomas of Kenya, Nairobi.

    Makamishna wote saba wa IEBC wamehudhuria mkutano huo wakiwemo wanne, makamu mwenyekiti Juliana Cherera na makamishna Francis Wanderi, Justus Nyangaya, na Irene Masit, waliokataa kujihusisha na matokeo ya uchaguzi wa urais yaliyotangazwa na mwenyekiti Wafula Chebukati.

    Uchaguzi huo uliokuwa ufanyike wakati wa uchaguzi mkuu mnamo Agosti 9 ulisogezwa mbele hadi Agosti 23 baada ya tume hiyo kugundua makosa ya mchanganyiko wa karatasi za kupigia kura zilizochapishwa.

    IEBC ilisimamisha mara mbili uchaguzi wa ugavana wa Mombasa na Kakamega na viti vinne vya maeneo bunge - Pokot Kusini, Kitui Vijijini, Rongai, na Kacheliba.

    Soma zaidi:

  10. Mzozo wa Ukraine: Urusi inakabiliwa na uhaba wa wanajeshi - Uingereza

    Ripoti ya mapema ya wizara ya ulinzi nchini Uingereza , iliokusanywa na kitengo cha ujasusi wa nchi hiyo inasema kwamba Urusi inakabiliwa na uhaba wa wanajeshi kuendeleza kampeni yao ya mashambulizi katika eneo la Donbass.

    Mapema tarehe 15 mwezi Agosti , kanda moja ya video iliokuwa ikisambazwa katika mitandao ya kijamii ya Ukraine , ilidai kwamba wanajeshi wa kitengo kimoja cha Urusi walikataa kuendelea na vita.

    Kitengo hicho kilisema kwamba kimetimiza wajibu wake wa kudhibiti jimbo la Luhanskna kwamba hakingetaka kujihusisha katika vita vya jimbo Jirani la Donetsk licha ya vitisho na unyanyasaji kutoka kwa makamanda wake.

    Urusi inadaiwa kuendelea kutafuta wanajeshi wa ziada ili kuwapa motisha wanajeshi wake waliopo Donbas.

    Makomando huenda wakaanza kuwapatia fedha wanajeshi waliosalia ili kuwapa motisha, ilisema ripoti hiyo.

  11. Mwendesha mashtaka wa mahakama ya kimataifa (ICC) arejea Sudan juu ya Darfur

    Mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa kivita (ICC) yuko nchini Sudan kwa ziara ya tatu ya aina hiyo tangu 2019.

    Wakati wa nyuma ilikuwa mwaka mmoja uliopita, wakati mmiliki wa ofisi hiyo Karim Khan alipozungumza kuhusu hati za kukamatwa kwa uhalifu uliofanywa wakati wa vita huko Darfur mwaka 2003.

    Mmoja wa wanaosakwa ni Rais wa zamani Omar al-Bashir, ambaye aliondolewa madarakani miaka mitatu iliyopita na anazuiliwa Khartoum.

    Anatafutwa kwa mauaji ya halaiki, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

    Sudan imekuwa ikikabiliwa na machafuko makubwa baada ya mapinduzi ya kijeshi mwaka jana.

  12. Mtoto wa rais wa Uganda yuko kwa ziara rasmi nchini Ethiopia

    Jenerali Muhoozi Kainerugaba (Kulia) alikutana na Rais wa Rwanda Paul Kagame hivi majuzi

    Mtoto wa rais wa Uganda yuko nchini Ethiopia kwa ziara ya kikazi, wizara ya mambo ya nje ya Uganda imethibitisha.

    Jenerali Muhoozi Kainerugaba siku za nyuma aliwahi kutuma ujumbe kwenye Twitter akiunga mkono waasi wa Tigray, lakini jeshi la Uganda liliiambia BBC mwezi Julai kuwa ni maoni yake binafsi na si msimamo wa jeshi.

    Ripoti za vyombo vya habari vya ndani zinasema anatarajiwa kukutana na Waziri Mkuu Abiy Ahmed.

    Jenerali Kainerugaba katika miezi ya hivi karibuni ametumwa na Rais Yoweri Museveni nchini Rwanda kusaidia kutatua mivutano ya muda mrefu kati ya nchi hizo mbili ambayo ilisababisha kufungwa kwa mpaka wa pamoja kwa miaka mitatu.

    Pia alitumwa mwezi Juni mwaka huu kukutana na Rais anayeondoka wa Kenya Uhuru Kenyatta ili kutoa ujumbe maalum.

    Kuongezeka kwa ushirikiano wa kidiplomasia kwa Jenerali Kainerugaba kunatazamwa na baadhi ya watu kama jaribio la Rais Museveni wa muda mrefu kumuandaa mwanawe kuchukua wadhifa wa urais.

    Sheria ya UPDF

  13. Imran Khan: Polisi wa Pakistan wamshtaki Waziri Mkuu wa zamani kwa ugaidi

    Polisi wa Pakistan wamemfungulia mashtaka waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo Imran Khan chini ya sheria za kupambana na ugaidi.

    Uchunguzi wao unajiri baada ya kuwashutumu polisi na mahakama kwa kumzuilia na kumtesa msaidizi wake wa karibu.

    Hali ya wasiwasi imetanda nchini humo, huku wafuasi wa kiongozi huyo wa zamani wakikusanyika nje ya nyumba yake wakiapa "kuchukua hatua" iwapo atakamatwa.

    Tangu kuondolewa mamlakani mwezi Aprili, Bw Khan amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali na jeshi la nchi hiyo.

    Polisi walitangaza mashtaka hayo baada ya mwanakriketi huyo aliyegeuka kuwa mwanasiasa kushutumu mamlaka kwa kumtesa msaidizi wake wa karibu, ambaye yeye mwenyewe anazuiliwa kwa tuhuma za uchochezi.

    Soma zaidi:

  14. Raila Odinga kuwasilisha kesi ya kupinga uchaguzi wa Ruto leo

    Je, Mahakama ya Juu zaidi itaweka historia nyingine inapojitayarisha kusikiliza na kuamua ombi la urais la Kiongozi wa Azimio Raila Odinga?

    Hilo ndilo swali kuu ambalo wengi wanatafakari huku mahakama kuu nchini ikijiandaa kusikiliza hoja kutoka kwa kundi la mawakili kuhusu ombi la kupinga ushindi uliokabidhiwa Naibu Rais William Ruto baada ya Wakenya kupiga kura tarehe 9, Agosti 2022.

    Odinga amepinga matokeo ya urais na ana hadi leo saa nane kuwasilisha ombi lake. Mkenya mwingine yeyote ambaye hakuridhika na matokeo ya uchaguzi anaweza pia kuwasilisha ombi hilo.

    Bw Odinga, mgombea mwenza wake Martha Karua, na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka jana walisalia na msimamo, wakisisitiza kwamba azma yao katika mahakama ya upeo itaonyesha ulimwengu jinsi ushindi wao "uliibiwa".

    Soma zaidi:

  15. Ukraine na Urusi: Usalama kuimarishwa katika kinu cha kinyuklia cha Zaporizhzhia

    Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Marekani zimesisitiza haja ya kuhakikisha usalama wa mitambo ya nyuklia inayotishiwa na mzozo wa Ukraine.

    Katika mazungumzo ya simu siku ya Jumapili, viongozi hao wanne pia walisisitiza kuinga mkono Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi.

    Moscow na Kyiv zimeshutumiana kwa kushambulia kinu cha nyuklia kinachoshikiliwa na Urusi, na hivyo kuzua hofu ya kutokea maafa.

    Wakati huo huo, Rais Volodymyr Zelensky aliwataka raia wa Ukraine kuwa waangalifu kabla ya sherehe za Siku ya Uhuru.

    "Urusi inaweza kujaribu kufanya jambo la kuchukiza, haswa la kikatili," alisema katika hotuba ya wikendi.

    "Moja ya malengo muhimu ya adui ni kutudhalilisha," aliongeza, lakini "tunapaswa kuwa na nguvu za kutosha ili kupinga uchochezi wote".

    Siku ya Uhuru wa Ukraine mnamo Jumatano, Agosti 24, pia itaadhimisha miezi sita tangu Urusi kuivamia Ukraine.

    Mzozo huo ulikuwa mada ya mkutano wa Jumapili uliowaleta pamoja Boris Johnson wa Uingereza, Rais wa Marekani Joe Biden, mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz.

    Kufuatia hitimisho lake, walihimiza kujizuia kwa kijeshi kuzunguka kituo cha nyuklia cha Zaporizhzhia kinachodhibitiwa na Urusi kusini mwa Ukraine, ambapo mapigano mapya yamesababisha hofu ya maafa zaidi kuliko yale ya Chernobyl mnamo 1986.

    Viongozi hao walikaribisha makubaliano - yaliyoidhinishwa na Rais wa Urusi Vladimir Putin siku ya Ijumaa - kuruhusu wakaguzi wa Umoja wa Mataifa kutembelea kiwanda hicho katika siku zijazo.

    Soma zaidi:

  16. Natumai hujambo