Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Wanajeshi wa Ukraine hawatasalimu amri Severodonetsk - meya wa jiji

Taarifa zaidi za sasa kutoka Severodonetsk - ambayo ilisemwa hapo awali na mkuu wa kijasusi wa kijeshi wa Ukraine kuwa kitovu cha sasa cha mzozo huo.

Moja kwa moja

  1. Habari za hivi punde, Wanajeshi wa Ukraine hawatajisalimisha huko Severodonetsk - meya wa jiji

    Wanajeshi wa Ukraine hawatajisalimisha huko Severodonetsk - meya wa jiji

    Taarifa zaidi za sasa kutoka Severodonetsk - ambayo ilisemwa hapo awali na mkuu wa kijasusi wa kijeshi wa Ukraine kuwa kitovu cha sasa cha mzozo huo.

    Vita ‘’vikali’’ vya mitaani vinaendelea huko, anasema meya wa jiji Oleksandr Stryuk.

    Lakini wanajeshi wa Ukraine hawataondoka katika mji huo wa mashariki ambao ni muhimu kimkakati, alinukuliwa na shirika la habari la UNIAN akisema.

    ‘’Hali inabadilika kila saa,’’ Stryuk anaongeza - lakini anaapa kuna ‘’nguvu na njia za kutosha’’ za kurudisha jiji kikamilifu kutoka kwa Warusi.

  2. Kurejeshwa kwa raia wa Rwanda walio Msumbiji kwazua hofu

    Mkataba wa kurejeshwa nchini humo uliotiwa saini wiki iliyopita kati ya Msumbiji na Rwanda umezua hofu miongoni mwa wakimbizi wa kisiasa wa Rwanda wanaoishi katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.

    Mkataba huo ulitiwa saini na mawaziri wa sheria wa nchi hizo mbili katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali.

    Takriban wakimbizi 3,000 wa Rwanda wanaishi Msumbiji, kulingana na mamlaka ya hapa.

    Wale waliokimbia kutoka Rwanda kwa sababu za kisiasa wanahofia kwamba mkataba huo ungetumiwa kuhalalisha urejeshwaji wao wa kulazimishwa.

    Waliomba kutotambuliwa au kutoa maoni zaidi kuhusu mkataba huo.

    Mnamo Septemba mwaka 2021, mfanyabiashara wa Rwanda Revocant Karemangingo aliuawa kwa kupigwa risasi katika mji mkuu wa Msumbiji, Maputo, chini ya hali isiyoeleweka.

    Alikuwa mkosoaji mashuhuri wa Rais wa Rwanda Paul Kagame.

  3. Masharti ya kuachiliwa kwa Besgye yalikuwa makali sana - jaji Uganda

    Mahakama kuu katika mji mkuu wa Uganda, Kampala, imeamua kuwa masharti ya kuachiwa kwa dhamana yaliyowekewa kiongozi mkongwe wa upinzani Kizza Besigye yalikuwa makali kupita kiasi na ukiukaji wa haki.

    Dkt Besigye amekuwa kizuizini tangu Mei 24.

    Alishtakiwa kwa kuchochea ghasia baada ya kujaribu kuhamasisha watu katika jiji la Kampala kupinga kupanda kwa gharama ya maisha.

    Uamuzi huo wa mahakama unafuatia pingamizi la mawakili wa mwanasiasa huyo kuhusu dhamana ya pesa taslimu ya $8,000 (£6,400) iliyowekwa na mahakama ya hakimu mkazi.

    Dkt Besigye alikuwa amekataa kulipa kiasi hicho na akazuiliwa gerezani hadi Juni 16.

    Jaji wa Mahakama ya Juu Micheal Elubu alisema masharti ya dhamana hayafai kuwekwa juu kiasi cha kutoweza kufikiwa au kutoa adhabu.

    Alirekebisha takwimu hadi $800 na kudumisha masharti mengine yaliyowekwa na hakimu wa kesi.

    Wanaharakati sita wanawake ambao waliandamana siku chache baada ya Dk Besigye kukamatwa wakitaka aachiliwe na dhidi ya kupanda kwa gharama ya bidhaa muhimu pia wako kizuizini kwa sasa.

    Walishtakiwa kwa kuchochea ghasia na walirejea Jumanne kwa ajili ya kusikilizwa kwa ombi lao la dhamana.

    Wanajumuisha Mbunge Anna Adeke, Naibu Meya wa Kampala, Doreen Nyanjura, na Susan Nanyonjo, mama wa mtoto wa miezi mitatu.

    Soma zaidi:

  4. Urusi inadai kushambulia maeneo mapya lengwa

    Urusi inadai kuharibu majengo ya viwanda ya kiwanda ambacho kilikuwa kikirekebisha magari ya kijeshi ya Ukraine katika eneo la Kharkiv.

    Katika taarifa za asubuhi, Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema ndege nyingine ya kijeshi ya Ukraine pia imetunguliwa.

    Vifaru vingine 18 vya Ukraine pia vimeharibiwa na ‘’raia’’ 450 wameuawa, Urusi inadai.

    Haikuwezekana kwa BBC kuthibitisha madai hayo kwa uhuru.

    Moscow ilizindua ‘’operesheni yake maalum ya kijeshi’’ kufuatia tuhuma za uwongo kwamba Ukraine imevamiwa na ‘’Wanazi’’.

    Soma zaidi:

  5. Ndege ya Lavrov yakatazwa kibali cha kuruka hadi Serbia

    Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov ameghairi ziara yake nchini Serbia.

    Nchi kadhaa jirani zilizuia ndege yake kupita katika anga yao kwa kukataa kuidhinisha ‘’kuruka juu’’, maafisa walisema.

    Mashirika ya habari ya Urusi yamemnukuu msemaji wa wizara hiyo Maria Zakharova akisema: ‘’Wajumbe wa Urusi walipaswa kufika Belgrade kwa mazungumzo. Lakini Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wa Nato walifunga anga zao.’’

    ‘’Diplomasia ya Urusi bado haijajifunza jinsi ya kutuma kwa usafiri wa anga wa papo hapo, chanzo cha kidiplomasia cha Urusi kililiambia shirika la habari la Interfax.

    Lavrov anasema sasa atamwalika mwenzake wa Serbia Nikola Selakovic kumtembelea mjini Moscow, na kuongeza: ‘’Hakuna mtu atakayeweza kuharibu uhusiano wetu na Serbia’’.

    Soma:

  6. Ramaphosa: Sijawahi kuiba pesa popote

    Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametetea kwa nguvu uadilifu wake baada ya kushutumiwa kuhusika katika utekaji nyara na hongo.

    Wiki iliyopita, mkuu wa zamani wa ujasusi Arthur Fraser alisema kesi hiyo inahusiana na madai ya jaribio la wizi wa $4m (£3.2m) mnamo mwaka 2020 katika moja ya mali ya rais na madai ya juhudi za kuficha kilichotokea.

    Rais kisha alithibitisha kuwa kulikuwa na wizi katika shamba lake huko Limpopo ‘’ambapo mapato yatokanayo na uuzaji wa wanyamapori yaliibiwa’’.

    Lakini maswali yaliibuka kwa nini alikuwa na pesa hizo.

    Akiongea na wafuasi wake wikendi, Bw Ramaphosa alieleza kuwa kama mkulima alinunua na kuuza ngombe mara kwa mara na mara nyingi watu walilipa pesa taslimu.

    Aidha, alikanusha kuwa kiasi kilichoibiwa kilikuwa karibu $4m.

    ‘’Yote haya yalikuwa pesa kutokana na mauzo ya wanyama... sijawahi kuiba pesa popote... na sitafanya hivyo.’’

    Bw Ramaphosa alichukua nafasi ya Jacob Zuma kama mkuu wa nchi mwaka wa 2018 baada ya Zuma kulazimika kujiuzulu kutokana na madai ya ufisadi.

    Rais ameweka suala la kupambana na rushwa kuwa kipaumbele cha serikali yake.

    Lakini dhamira yake katika hili imetiliwa shaka kwani matumizi mabaya ya fedha za serikali, haswa juu ya pesa zilizotengwa kwa ajili ya kupambana na Covid-19, yameendelea wakati wa urais wake.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Ujasusi wa Uingereza: Urusi yahamishia mifumo ya ulinzi katika kisiwa cha nyoka

    Ujumbe wa ujasusi wa kijeshi wa Uingereza unaoripoti kuhusu hali katika Ukraine unasema kuwa baada ya kupoteza meli ya Moskva, jeshi la Urusi limehamisha mifumo yao ya ulinzi wa mashambulizi ya anga, ikiwemo mifumo ya Tor na Pantsir , na kuipeleka katika Kisiwa cha nyoka kilichopo katika Bahari nyeusi.

    "Huenda, silaha hizi zimetengenezwa kwa ajili ya kutoa ulinzi wa mashambulio ya anga kwa meli za kivita za Urusi karibu na kisiwa cha Zmeiny ," Ujasusi wa Uingereza unasema. Kwa maoni yake, hatua za jeshi la Urusi karibu na Zmeinoye "zilisaidia kufunga eneo la mwambao wa Ukraine na kuzuia kuanzishwa tena kwa biashara ya majini, ikiwemo kusafirisha nafaka za Ukraine nje."

    Ukraine na nchi za Magharibi wanaishutumu Urusi kwa kuzuia mauzo ya nje ya chakula kutoka katika bandari za Ukraine.

    Nchi nyingi duniani hutegemea nafaka kutoka Ukraine, ambapo ukosefu wake unatishia baa kubwa la njaa.

    Taarifa ya mkuu wa ujasusi wa Uingereza pia ilisema kuwa Jumapili asubuhi Urusi ilifanya shambulio la kombora kutoka majini la Kh-101 kwenye miundo mbinu ya leri mjini Kyiv katika kile kilichokuwa ‘’jaribio la usambazaji wa silaha za Magharibi kwa jeshi la Ukraine katika maeneo ya vitani."

    Urusi inadai kwamba shambulio la Jumapili katika Kyiv liliharibu vifaru vilivyotolewa na nchi za Magharibi kwa Ukraine. Lakini kulingana na Kyiv, kiwanda cha ukarabati wa magari ndiokilichoharibiwa kidogo, na kwamba hapakuwa na zana za kijeshi. Maafisa wa Ukraine waliwaalika waandishi wa habari kwenye kiwanda hicho na kuwaonyesha kiwango cha uharibifu uliofanyika.

    Kuhusu hali katika jimbo la Donbass, Uingereza imeandika kuwa mapigano makali yanaendelea katika Severodonetsk, na "Vikosi vya Urusi vimeendelea na mashambulizi vikisonga kuelekea Sloviansk, vikijaribu kuzingira vikosi vya Ukraine.

    Unaweza pia kusoma:

    • Mzozo wa Ukraine: Usambazaji wa silaha za Magharibi nchini Ukraine unavyobadili hali ya mapambano ya vita
    • MLRS: Kwanini Ukraine inazitaka 'kwa udi na uvumba' Silaha hizi?
  8. Lagos okadas: Nigeria yaharibu teksi 2,000 za pikipiki

    Zaidi ya pikipiki 2,000 za zilizochukuliwa zimeharibiwa katika jiji la Nigeria, Lagos, kufuatia baada ya kupigwa marufuku kwa pikipiki hizo zinazojulikana kama okada.

    Hatua hiyo imetokana na tukio la kushambuliwa kwa mwanamume mmoja na watu wanaoshukiwa kuwa waendeshaji pikipiki mwezi uliopita,

    Sunday David, mhandisi wa sauti mwenye umri wa miaka 38, aliuawa katika mtaa wa soko la Lekki baada ya kutofautiana kuhusu nauli.

    Kifo chake kilizua hasira na kuwalazimu mamlaka kuchukua hatua ya kupiga marufuku uchukuzi huo.

    Mkewe, Grace Bolu, aliyejawa na majonzi alihoji ni vipi atawatunza watoto wake wawili. "Mimi ni mtumishi wa serikali tu. Mume wangu anafanya kila kitu. Nitafanyaje? Mshahara wangu wa kulipa ada ya shule ni kiasi gani, kulipa kodi?" aliambia BBC.

    Marufuku hiyo imezua maoni tofauti kutoka kwa wakaazi wa eneo hilo huku wengine wakisema wahudumu wa pikipiki hizo huziendesha kwa njia hatari, huku wengine wakisema kuendesha okada kunatoa ajira muhimu kwa vijana.

    Fundi anayeishi Ikeja, Wasiu Adekoya, alisikitishwa na unyonge wa waendeshaji okada. "Wao [waendesha pikipiki] wanateka nyara watu. Kile ambacho serikali ilifanya ni sawa. Hatutaki matatizo katika jimbo la Lagos.

    Lakini waache watoe mabasi zaidi ili kuongeza upungufu." Mkazi mwingine aliyejitambulisha kama Mchungaji Abraham aliomba kuhurumiwa, akisema kuendesha okada kunatoa mapato muhimu kwa wengi.

  9. Tanzania yasitisha uamuzi wa kuondoa marufuku ya usafirishaji wa wanyamapori

    Serikali ya Tanzania imesitisha uamuzi tata wa kuondoa marufuku ya usafirishaji wanyamapori nje ya nchi.

    Hatua ya kuondoa marufuki hiyo ilitangazwa siku mbili zilizopita na ilikuwa imekosolewa vikali na wanaharakati.

    Sheria hiyo ilibuniwa mwaka 2016 ili kusaidia kuzuia wanyama wanaolindwa kusafirishwa nje ya nchi na wawindaji haramu.

    Mamlaka ya wanyamapori ilikuwa imepanga kuruhusu mauzo ya nje kwa muda wa miezi sita ili wafanyabiashara waweze "kuondoa akiba ya wanyama" ambao hawakuweza kuuza.

    Lakini Waziri wa Utalii na Maliasili wa Tanzania, Pindi Chana alisema marufuku hiyo itarejeshwa hadi uamuzi mwingine utakapotolewa.

    Tanzania inajulikana kwa mbuga zake za wanyamapori zinazovutia idadi kubwa ya watalii.

  10. Papa awaombea waathiriwa wa shambulio la kanisa la Nigeria

    Papa Francis amewaombea wahanga wa shambulizi dhidi ya kanisa moja nchini Nigeria ambapo waumini wasiopungua 25 waliuawa na watu wenye silaha.

    Taarifa ya Vatican ilisema amefahamu kuhusu vifo vya makumi ya watu. Shambulio hilo lilifanyika katika mji wa kusini wa Owo, katika jimbo la Ondo.

    Maafisa huko wameonya kwamba idadi ya waliojeruhiwa inaweza kuongezeka.

    Wanasema kasisi mmoja na washiriki wengine wa kanisa hilo walitekwa nyara na watu hao wenye silaha, ambao hawakujulikana ni nani.

    Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari, amelaani shambulio hilo na kulitaja kuwa la "chuki".

    Wiki moja iliyopita, mkuu wa kanisa la Methodist nchini humo alitekwa nyara na aliachiliwa huru baada ya kulipwa fidia.

  11. Baba yake Mtanzania aliyekwama katika mgodi wa madini awasili Burkina Faso

    Baba yake Mtanzania Marco Aristablos Bwire, mmoja wa wachimbaji wa madini 8 waliokwama katika mgodi wa Perkoa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha ghafla mwezi Aprili, amekwenda Burkina Faso, imetangaza huduma ya mawasiliano ya Burkina Faso.

    Bw Sosthène Aristablos Bwire alikutana na Waziri wa madini tarehe 3 Juni, Jean Alphonse Some, ambaye mkalimani wake aliripoti kuhusu taarifa hii:

    “Wakati aliposikia habari mbaya, alijisikia vibaya sana, hakutarajia mshituko wa aina hiyo, kwa bahati mbaya hii ilitokea, na akahisi maumivu yote ambayo baba anaweza kkuyahisi kwa familia yake.”, alisema mkalimali

    Kulingana na waziri wa madini, Wizara za mambo ya nje kupitia balozi zao zilisaidia kuwasiliana na familia za wachimba migodi wa Tanzania na Zambia waliokuwa wakifanya kazi katika mgodi nchini Burkina Faso.

    “Wizara ya madini ilihakikisha kwamba walipata tiketi za ndege na hivyo ndivyo familia ya mnmoja wao ilivyoweza kufika nchini hapa nchini Burkinafaso. Familia ya Mzambia ilihisi kwamba ilikuwa ni mapema sana na alitaka kusubiri kidogo kabla ya kuja. Serikali tofauti zilisaidia hili, kwahiyo kwa familia ya Tanzania, leo ni halisi. Tunahisi maumivu yaokwasababu sote ni Waafrika, na sote ni makaka.”

    Ripoti ya hivi karibuni kuhusu hali inaonyesha kuwa mchakato wa kusukuma maji unazoroteshwa na matope yaliyopo chini ya mgodi. Pampu zinazotumiwa kuondoa maji mgodini hupasuka mara kwa mara.

    Mafundi wanajaribu kutafuta suluhu nyingine za kuondoa maji katika mgodi.

    Miili ya wachimba migodi sita kati ya wanane waliokwama imeopolewa katika kipindi cha wiki kadhaa, baada ya waokoaji kupata chumba cha uokozi wa wachimba migodi kikiwa kitupu.

    Wachimba migodi (Mmoja Mtanzania, Mmoja Mzambia na sita Waburkinabè) walikuwa wakifanya kazi katika mgodi wa kina kirefu cha zaidi ya mita 500. Serikali inasema kwamba operesheni imekuwa ikiendelea kwa ajili ya kuwasaka wengine wawili waliosalia.

  12. Korea Kusini na Marekani zarusha makombora kutoa onyo kwa Korea Kaskazini

    Korea Kusini na Marekani zimerusha makombora manane siku ya Jumatatu, kujibu msururu wa makombora ya balistiki yaliyorushwa na Korea Kaskazini siku iliyotangulia.

    Haya yanajiri huku Pyongyang ikiendelea kuzidisha majaribio yake ya makombora.

    Rais wa Korea Kusini Yoon Suk-yeol alisema serikali yake itajibu vikali chokochoko zozote kutoka kwa jirani yake wa kaskazini.

    "Tutahakikisha hakuna ufa hata mmoja katika kulinda maisha na mali ya watu wetu," alisema.

    Akizungumza katika hafla ya kumbukumbu ya vita huko Seoul, aliongeza kuwa mipango ya nyuklia na makombora ya Korea Kaskazini "inafikia kiwango cha kutishia sio tu amani kwenye Rasi ya Korea lakini pia Kaskazini Mashariki mwa Asia na ulimwengu", kulingana na Yonhap.

    Marekani na Korea Kusini mara kwa mara hufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi, ambayo mara nyingi huikasirisha Korea Kaskazini.

    Mapema Jumatatu, saa chache baada ya Korea Kaskazini kurusha makombora kadhaa kwenye pwani yake ya mashariki, washirika hao wawili walirusha Mifumo minane ya Makombora ya kujibu mashambulizi (ATACMS) - moja kutoka Marekani na saba kutoka Korea Kusini.

    Wachambuzi wanasema hatua hiyo ni ya Korea Kusini kuonyesha uwezo wake, kwa usaidizi wa silaha za Marekani.

    Hili ni tukio la pili la kulipiza kisasi kutoka kwa Marekani na Korea Kusini ndani ya wiki kadhaa, huku hatua sawa na hiyo ikifanywa wiki iliyopita baada ya Pyongyang kurusha makombora mara tu mfululizo mara baada ya ziara ya Rais wa Marekani Joe Biden katika eneo hilo.

    Soma zaidi:

  13. 'Serengeti Girls' wa Tanzania wafuzu kwa Kombe la Dunia

      • Author, Alfred Lasteck
      • Nafasi, BBC News, Dar es Salaam

    Timu ya taifa ya wanawake chini ya miaka 17 ya Tanzania ‘Serengeti Girls’ imefuzu kushiriki michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika Oktoba mwaka huu nchini India.

    Timu hiyo imefuzu baada ya kuibuka na ushindi wa jumla wa mabao 5-1 dhidi ya Cameroon. Serengeti ilipata ushindi wa bao 1-0 leo, bao lililowekwa kimiani na Neema Paul.

    Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Cameroon, timu hiyo ilishinda kwa mabao 4-1.

    Tanzania sasa imeungana na Morocco na Nigeria kuiwakilisha Afrika na kukamilisha idadi ya timu 16 zitakazoshiriki fainali hizo za Dunia kati ya Oktoba 11-30 mwaka huu katika miji mitatu nchini India zikiwa fainali za saba tangu michuano ilipoasisiwa mwaka 2008.

    Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kufuzu fainali hizo kwa timu za soka. Hadi kufuzu, Serengeti ilizing’oa Botswana, Burundi na kumalizia kwa kuitoa Cameroon.

    Hata hivyo, kinara wa mabao wa hatua ya kufuzu ni Mtanzania, Clara Luvanga ambaye amefunga jumla ya mabao 10.

  14. Uingereza kutuma kombora la kwanza la masafa marefu Ukraine

    Uingereza inatuma makombora yake ya kwanza ya masafa marefu nchini Ukraine, waziri wa ulinzi amesema, licha ya tishio kutoka kwa Urusi kwa nchi za Magharibi.

    Ben Wallace alisema mfumo wa roketi wa M270 utasaidia Ukraine kujilinda dhidi ya Urusi.

    Serikali ya Uingereza haijathibitisha ni silaha ngapi zitatumwa, lakini BBC inafahamu kuwa mwanzoni zitakuwa tatu.

    Uamuzi huo uliratibiwa na Marekani, ambayo ilitangaza wiki iliyopita pia kuwa inasambaza mfumo wa roketi.

    Hatua hiyo ya Marekani tayari imeikasirisha Moscow na siku ya Jumapili Rais wa Urusi Vladimir Putin alitishia kupanua orodha ya maeneo ambayo Urusi itashambulia nchini Ukraine ikiwa nchi za Magharibi zitapeleka silaha za masafa marefu Kyiv.

    Serikali ya Uingereza ilisema kuwa wanajeshi wa Ukraine watapewa mafunzo ya jinsi ya kutumia virutubishi nchini Uingereza katika wiki zijazo.

    Akitangaza hatua hiyo, Bw Wallace alisema Uingereza ilikuwa ikichukua nafasi kubwa katika kuwapa wanajeshi wa Ukraine "silaha muhimu wanazohitaji ili kulinda nchi yao dhidi ya uvamizi wa Urusi".

    Alisema: "Kadiri mbinu za Urusi zinavyobadilika, ni lazima uungwaji mkono wetu kwa Ukraine. "Mifumo hii yenye uwezo mkubwa wa kurusha roketi itawawezesha marafiki zetu wa Ukraine kujilinda vyema dhidi ya matumizi ya kikatili ya mizinga ya masafa marefu, ambayo majeshi ya Putin yametumia kiholela kushambulia miji."

    Uingereza na Marekani zimeongoza katika kusambaza silaha kwa Ukraine, lakini kuipa kwa roketi za masafa marefu kunaashiria mabadiliko makubwa, alisema mwandishi wa BBC wa masuala ya ulinzi Jonathan Beale. Pia ni utambuzi kwamba Ukraine inajitahidi kushindana dhidi ya silaha kali za Urusi, aliongeza.

    Mfumo wa Uingereza wa roketi nyingi unaweza kurusha makombora 12 kutoka ardhini hadi angani ndani ya dakika moja na unaweza kulenga shabaha ndani ya maili 50 (km 80) kwa usahihi wa uhakika - mbali zaidi kuliko mizinga inayomilikiwa na Ukraine hivi sasa.

    Ni sawa na mfumo ambao Marekani inatuma, M142 High Mobility Artillery Rocket System (HIMARS).

    Wiki iliyopita Washington ilisema itasambaza virusha roketi vinne vya HIMARS kwa Ukraine - ya kupata hakikisho kwamba zitatumika kwa madhumuni ya kujihami pekee na sio kulenga shabaha ndani ya Urusi.

    • Mzozo wa Ukraine: Usambazaji wa silaha za Magharibi nchini Ukraine unavyobadili hali ya mapambano ya vita
    • MLRS: Kwanini Ukraine inazitaka 'kwa udi na uvumba' Silaha hizi?
  15. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja leo Jumatatu 06.06.2022.