Dkt.Tedros achaguliwa tena kuwa mkuu wa WHO
Tedros Adhanom Ghebreyesus wa Ethiopia amechaguliwa tena kuwa mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa muhula wa pili wa miaka mitano.
Matokeo ya kura ya siri yalikuwa ni utaratibu kwa vile alikuwa mgombea pekee.
Akifungua Mkutano wa 75 wa Afya Ulimwenguni huko Geneva, Dk Tedros, ambaye ameongoza mwitikio wa ulimwengu dhidi ya janga la Covid, alisema virusi vya corona vimeubadili ulimwengu, na kuwaacha wengi bado wanateseka.
Akiyazuia machozi alipokuwa akizungumza, pia alitoa wito wa kukomeshwa kwa vita, ambayo alisema "inatikisa na kuvunja misingi ambayo jamii ziliisimamia".
Alikumbuka uzoefu wake wa kwanza kama mtoto wa vita nchini Ethiopia, ambayo inakabiliwa tena na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe katika eneo lake la kaskazini la Tigray, ambako ni asili yake.
Mkuu huyo mwenye umri wa miaka 57 amekuwa katika mzozo na serikali ya Ethiopia baada ya kumshutumu kwa kuunga mkono vikosi vya Tigray - tuhuma ambayo ameikanusha hapo awali.
Alikuwa Waziri wa Afya wa Ethiopia - ambapo alipokea sifa kwa juhudi zake za kudhibiti magonjwa kama vile malaria na VVU/UKIMWI - na waziri wa mambo ya nje kabla ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuongoza WHO mwaka 2017.
- Umakini kwa Ukraine unaonesha upendeleo kwa watu weupe dhidi ya weusi, Mkuu wa WHO asema
- Wanawake waliolipa gharama ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Ethiopia