Urusi yasema ina wanunuzi wa nishati wa kutosha bila nchi za Magharibi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi anasema nchi hiyo ina wanunuzi wa kutosha wa mafuta na gesi yake nje ya nchi za Magharibi
Moja kwa moja
Hifadhi ya silaha haramu yapatikana katika oparesheni ya usalama Kenya
Polisi katika kaunti ya Marsabit mashariki mwa Kenya wanasema wamepata hifadhi kubwa ya silaha nzito wakati wa operesheni ya usalama inayoendelea katika eneo hilo.
Washukiwa saba walifikishwa mahakamani leo Jumatano wakikabiliwa na mashtaka ya kupatikana na silaha hizo haramu ambazo ni pamoja na bunduki na guruneti.
Waendesha mashtaka waliomba washukiwa hao kuzuiliwa kwa siku 14 zaidi huku polisi wakikamilisha majaribio ya bunduki hizo ambazo maafisa wa usalama wanaamini kuwa zimetumika katika wimbi la mapigano ya kikabila hivi majuzi katika kaunti ya Marsabit.
Makumi ya watu wameuawa wakati wa ghasia hizo zinazolaumiwa kwa uchochezi wa kisiasa na mizozo ya muda mrefu ya mpaka.
Serikali imeweka amri ya kutotoka nje kwa mwezi mmoja alfajiri hadi jioni ya Marsabit ikijaribu kudhibiti msururu wa mauaji ya kulipiza kisasi.
Mahusiano na Putin hayawezi tena kuwa kawaida - msemaji wa Waziri Mkuu wa Uingereza

Chanzo cha picha, Sputnik/Mikhail Metzel/Reuters
Maelezo ya picha, Rais wa Urusi, Vladimir Putin Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson na mwenzake wa Uswidi wamesema uhusiano na Vladimir Putin kamwe hauwezi kuwa wa kawaida kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Johnson alikutana na Waziri Mkuu wa Uswidi Magdalena Andersson mapema ili kutia saini ahadi mpya ya usalama kati ya Uingereza na Uswidi.
Msemaji wa Johnson alisema baadaye viongozi wote wawili "wamesisitiza kwamba uhusiano na Putin hauwezi kamwe kuwa wa kawaida", kulingana na Reuters.
Msemaji huyo pia alisema viongozi hao walikubali misukosuko ya baada ya uvamizi wa Putin "imebadilisha kimsingi usanifu wa usalama wa kimataifa", shirika la habari linaripoti.
Bei ya mafuta barani Ulaya inaweza kupanda kufuatia hatua ya hivi punde ya Ukraine
Nchi za Ulaya ambazo zinategemea zaidi mafuta ya Urusi zinafuatilia kwa karibu hatua ya hivi punde zaidi ya Ukraine, ambayo inasema itasitisha usambazaji wa gesi asilia kupitia baadhi ya mtandao wake wa mabomba ambayo husafirisha theluthi moja ya mafuta yanayowasilishwa barani humo.
Ingawa athari kwa kiasi halisi cha gesi inayoletwa bado haijabainishwa, hatua hiyo inaashiria kwamba bei inaweza kupanda kwa mujibu w Nathan Piper, mkuu wa utafiti wa mafuta na gesi katika Investec, aliambia BBC
Anasema athari za kuimarishwa kwa vifaa vinavyoongeza bei zinakuja wakati Ulaya inapojaribu kujaza akiba hadi majira ya joto, kabla ya msimu wa baridi ujao.
Umoja wa Ulaya umekuwa ukizingatia kwa wiki kadhaa jinsi ya kujiondoa kutoka kwa nishati ya Urusi, huku baadhi ya nchi wanachama zikigawanyika juu ya mkakati sahihi.
Jumuiya hiyo imeahidi kupunguza uagizaji wa gesi kutoka nje kwa thuluthi mbili ifikapo mwisho wa 2022, lakini imezitaka nchi kujenga hifadhi zao.
Maelezo zaidi:
Urusi yasema ina wanunuzi wa nishati wa kutosha bila nchi za Magharibi

Chanzo cha picha, Getty Images
Akijitenga na Uingereza na Uswidi kwa muda, waziri wa mambo ya nje wa Urusi anasema nchi hiyo ina wanunuzi wa kutosha wa mafuta na gesi yake nje ya nchi za Magharibi, huku nchi za Umoja wa Ulaya zikijaribu kupunguza utegemezi wao kwa nishati ya Urusi.
Sergei Lavrov alisema: "Wacha Magharibi walipe zaidi ya ilivyokuwa wakilipa kwa Shirikisho la Urusi, na iwaeleze idadi ya watu wake kwa nini wanapaswa kuwa masikini zaidi."
Lavrov alikuwa akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari baada ya mazungumzo na mwenzake mjini Muscat, Oman.
Kama ambavyo tumekuwa tukiripoti, EU imependekeza kupiga marufuku kabisa uagizaji wa mafuta kama sehemu ya kuimarisha vikwazo vyake.
Tayari imeahidi kupunguza uagizaji wa gesi kutoka nje kwa theluthi mbili ifikapo mwisho wa mwaka, na inapanga kukomesha mafuta ghafi kwa muda wa miezi sita na bidhaa zilizosafishwa ndani ya miezi sita.
Video ya IS video yasemekana kuonyesha mauaji ya wakristo wa Nigeria

Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Iswap, ambayo inahudumu zaidi kaskazini-mashariki mwa Nigeria, hivi karibuni imepata hasara kubwa kufuatia mashambulizi ya kijeshi. Kundi la Islamic State limechapisha video ambayo inasadikiwa kuonyesha raia 20 waumini wa Kikristo wakiuawa katika jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Akizungumza kwa lugha ya Kihausa, mmoja wa wanamgambo walofunika nyuso zao alionyesha kisu akisema ilikuwa ni kulipiza kisasi mauaji ya viongozi wa kundi hilo Mashariki ya Kati mapema mwaka huu.
BBC haijaweza kuthibitisha maudhui ya video hiyo au mahali ambapo picha hiyo ilipigwa.
Ilichapishwa kwenye chombo cha habari kilichounganishwa na IS na inaonyesha makundi matatu ya mateka wakiwa wamevalia mavazi ya kiraia.
Mamlaka bado haijatoa maoni kuhusu video hiyo.
Wanamgambo wa IS, wanaoendesha harakati zao katika eneo la Ziwa Chad kwa jina la Islamic State West Africa Province (Iswap), pamoja na kundi jingine la wanamgambo wa Kiislamu, Boko Haram, hivi karibuni wamepata hasara kubwa kutokana na mashambulizi ya jeshi la mataifa mbalimbali.
Kampeni hizo za kijeshi siku za nyuma kwa kawaida zimekuwa zikifuatiwa na video za propaganda kutoka kwa makundi yenye itikadi kali.
Soma:
Karibu wanajeshi 26,350 wa Urusi wameuawa, yasema Ukraine

Chanzo cha picha, Reuters
Urusi imepoteza wanajeshi 26,350 tangu ilipoivamia Ukraine tarehe 24 Februari, Wizara ya Ulinzi ya Ukraine ilisema katika sasisho lake la hivi punde.
Ukraine inadai jumla ya hasara iliyopata Urusi ni pamoja na:
- Vifaru 1,187
- Magari 2,856 ya kivita
- Mifumo 528 ya kivita
- Mifumo 185 ya kurushia roketi
- Mifumo minane ya ulinzi wa anga
- Ndege 199
- Helikopta 160
- Ndege 290 zisizo na rubani
- Makombora 94 ya meli
- Meli 12 au boti
- Magari 1,997 na malori
- Vitengo 41 maalum vya vifaa
BBC haijaweza kuthibitisha madai haya.
Unaweza pia kusoma
KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
Hatima ya Halima Mdee na wenzake kujulikana leo

Wajumbe wa Baraza kuu Chadema wanaendelea na kikao jijini Dar es salaam miongoni mwa mambo watakayojadili ni pamoja na rufaaa za wabunge 19 wa viti maalumu waliofukuzwa.
Miongoni mwao ni pamoja na aliyekuwa mwenyekiti wa baraza la wanawake BAWACHA Halima Mdee.
Kwa mujibu wa uongozi wa Chadema, Katibu Mkuu wa chama John Mnyika hakuwasilisha majina ya wateule wa viti maalum NEC, na hawakutoa idhini ya kada yoyote kuapa Bungeni.

Baada ya uchaguzi wa Oktoba 2020 kuisha, vyama vikuu vya upinzani nchini Tanzania vilijikuta katika njia panda ya kisiasa, si upande wa Tanzania Bara pekee, hadi Zanzibar.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kulikuwa na kitendawili cha ikiwa wapeleke majina ya Wabunge wa viti maalum ama la.
Kitendawili hiki kilikuwa na jawabu tofauti kutoka kwa wafuasi wa chama hicho na wachambuzi wa siasa.
Mambo yaligeuka baada ya kundi la Wabunge 19 wanawake kutoka Chadema kufanya uamuzi wenye utata wa kwenda Bungeni na kuapishwa na kuwa wabunge wa Bunge la 12.
Wabunge hao 19 wa viti maalumu walituhumiwa kupeleka majina yao wenyewe bila idhini ya chama jambo ambalo linatafsiriwa kama usaliti .



Katika mkutano huu pia wamehudhuria wageni mbalimbali mshuhuri wakiwemo wenyeviti wa vyama vingine vya siasa akiwemo James Mbatia NCCR Mageuzi, Hashim Rungwe - Chauma, na wawakilishi toka ACT wazalendo na CUF Mgeni wa Heshima kwenye mkutano huo ni Robert Kyagulanyi maarufu Bob wine mwanasiasa wa upinzani kutoka nchini Uganda.
'Mshambuliaji wa kijihadi' wa Somalia ahusika na shambulio karibu na uwanja wa ndege

Chanzo cha picha, EPA
Maelezo ya picha, Wabunge wanampigia kura rais siku ya Jumapili - wagombea 39 wanawania nafasi hiyo Bomu la kujitoa mhanga limelipuliwa katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu. Mlipuko huo ulilenga kituo cha ukaguzi kwenye barabara inayoelekea kwenye uwanja wa ndege wa jiji hilo.
Kundi la wanamgambo wa Kiislamu, al-Shabab, limedai kutekeleza shambulio hilo.
Siku ya Jumapili, wabunge wanatazamiwa kumchagua rais ajaye wa nchi.
Kura hiyo, ambayo imeahirishwa mara kadhaa, itafanyika ndani ya jumba la ndege kwenye uwanja wa ndege. Al-Shabab hufanya mashambulizi mara kwa mara mjini Mogadishu.
Mwezi uliopita shambulio la kurushia mawe lililenga bunge siku chache tu baada ya wabunge kuapishwa.
Wanajeshi wajeruhiwa baada ya mlipuko mkubwa kukumba mji mkuu wa Somalia
Mlipuaji wa. kujitoa mhanga kufa ameripotiwa kulenga magari katika kituo cha ukaguzi cha barabra kuu ya kuelekea uwanja wa kimataifa wa ndege wa Aden Adde.
Shambulio hilo katika eneo linaloitwa makutano ya Kilometa-Nne linasemekana kusababisha majeruhi kadhaa, wakiwemo wanajeshi na raia, kwa mujibu wa vyanzo vya ndani.
Eneo hilo liko chini ya kilomita tano kutoka uwanja wa ndege, ambapo wagombea wanaowania kiti cha urais wanatarajiwa kutoa hotuba zao za kampeni Bungeni.
Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika umeweka marufuku ya kutotoka katika eneo kambi ya ljeshi la anga la Afisyoni huko Hangara na maeneo ya jirani, ambapo uchaguzi wa urais utafanyika Jumapili.
Kuna wagombea 39 wanaonia uchaguzi wa urais wa Somalia, ambao tayari umecheleweshwa kwa zaidi ya mwaka mmoja, kutokana na ukosefu wa usalama nchini humo.
Mwezi uliopita, shambulio la risasi lilikatiza kikao cha bunge ambapo wabunge wapya walioapishwa walikuwa wameketi. Watu kadhaa walijeruhiwa.
Hungary: Vikwazo vya mafuta vya Umoja wa ulaya dhidi ya Urusi vitaharibu uchumi

Chanzo cha picha, EPA
Umoja wa ulaya unalenga kupiga marufuku kabisa uangizaji wa mafuta kama sehemu ya vikwazo zaidi dhidi ya Urusi. Lakini sio kila mwanachama wa umoja wa Ulaya (EU) anaunga mkono hatua hiyo.
Nchi mwanachama Hungary inasema vikwazo vya mafuta dhidi ya Urusi "vitaharibu" uchumi wa Hungary.
Waziri wa Mambo ya Nje Peter Szijjarto alisema Tume ya Ulaya haina suluhu la "matatizo makubwa ambayo yatajitokeza kwa nchi ya Hungary", licha ya mazungumzo ambayo yamekuwa yakifanyika, Reuters iliripoti.
Aliongeza kuwa makubaliano kuhusu vikwazo vya mafuta vitafanya kazi tu ikiwa vitaelekezwa kwenye usafirishaji wa mafuta ya baharini, na usafirishaji wote wa mafuta ya Urusi kupitia mabomba ungesamehewa kikamilifu
Mwandishi wa habari wa Al Jazeera auawa Vikosi vya Israel vikishambulia mji wa Jenin

Chanzo cha picha, Reuters
Mwandishi wa habari wa Al Jazeera Shereen Abu Aqleh ameuawa kwa kupigwa risasi alipokuwa akiripoti kuhusu uvamizi wa vikosi vya usalama vya Israel katika mji wa Jenin, Ukingo wa Magharibi.
Kituo cha habari cha Qatar kimesema Abu Aqleh, 51, alipigwa risasi "makusudi" na wanajeshi wa Israel. Mwandishi mwingine alipigwa risasi na kujeruhiwa.
Jeshi la Israel lilikanusha kuwa vikosi vyake vinawalenga waandishi wa habari. Ilikuwa inaangalia "uwezekano" kwamba "inawezekana walipigwa na wapiganaji wa Kipalestina" wakati wa kurushiana risasi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Yair Lapid amekitaja kifo cha Abu Aqleh kuwa cha kusikitisha na kusema kuwa imejitolea kufanya uchunguzi wa pamoja na Mamlaka ya Ndani ya Palestina.
"Wanahabari lazima walindwe katika maeneo yenye migogoro na sote tuna jukumu la kupata ukweli," aliongeza.
Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar Lolwah al-Khater alisema Abu Aqleh alipigwa risasi "wazi" akiwa amevalia mavazi maalu na kufofia kumtambua kama mwandishi wa habari.

Chanzo cha picha, Aljazeera
Wizara ya afya ya Palestina imethibitisha kifo cha Abu Aqleh na kusema kuwa kabla alikimbizwa hospitalini akiwa katika hali mbaya baada ya kupigwa risasi. Shereen Abu Aqleh alikuwa mtu mashuhuri katika kituo cha habari cha Kiarabu cha Al Jazeera ambaye amekuwa akiangazia mzozo wa Israel na Palestina kwa miaka 15.
Mwandishi wa habari wa Al Jazeera Nida Ibrahim alisema alikuwa "mwandishi wa habari anayeheshimika sana" na kwamba habari hiyo "ilikuwa mshtuko kwa waandishi wa habari ambao wamekuwa wakifanya kazi naye."
Wimbi la mashambulizi ya Waarabu na Wapalestina wa Israel nchini Israel katika wiki za hivi karibuni limesababisha vifo vya Waisrael 17 na Waukraine wawili. Takriban Wapalestina 26 wameuawa - ikiwa ni pamoja na washambuliaji waliopigwa risasi na kufa wakati wa kutekeleza mashambulizi, au wanamgambo na raia waliouawa wakati wa mashambulizi na makabiliano ya Israeli katika Ukingo wa Magharibi.
Rihanna kuzindua bidhaa zake za kifahari za urembo barani Afrika

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwanamuziki Robyn Rihanna Fenty maarufu kama Rihanna ametangaza kuwa bidhaa zake za urembo za Fenty Beauty na Fenty Skin zitaanza kupatikana katika nchi nane za Afrika kuanzia mwisho wa mwezi huu.
Katika chapisho lake katika mtandao wa kijamii, nyota huyo wa muziki wa pop alisema "amekuwa akiungojea huu wakati" na kwamba huu ni "mwanzo tu".
Bidhaa hizo za urembo zitapatikana Botswana, Ghana, Kenya, Namibia, Nigeria, Afrika Kusini, Zambia na Zimbabwe.
Ruka X ujumbeRuhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya njeMkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe
Rihanna, alizindua Fenty Beauty mwaka 2017 kwa ushirikiano na kampuni ya bidhaa za kifahari ya LVMH (Moët Hennessy Louis Vuitton).
Rihanna ana utajiri wa thamani ya $1.7bn (£1.2bn), huku makadirio ya $1.4bn yakitokana na thamani ya Fenty Beauty.
Kampuni hiyo iliripotiwa kutengeneza kiasi cha $100m (£72m) katika siku zake 40 za kwanza.
Kampuni yake imetengeneza pesa nyingi zaidi kuliko bidhaa zingine za urembo zilizoanzishwa na watu mashuhuri kama vile Kylie Jenner's Kylie Cosmetics, KKW Beauty ya Kim Kardashian na Kampuni ya Honest ya Jessica Alba, kwa mujibu wa jarida la Forbes.
Marekani: Urusi yarusha makombora ya kasi 'hypersonic ' zaidi ya 10 tangu vita kuanza
Pentagon inaamini kwamba Urusi imetumia silaha zake za hypersonic takriban 10 hadi 12 tangu kuanza kwa vita nchini Ukraine, kwa mujibu wa afisa mkuu wa ulinzi.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne, afisa huyo alisema Marekani haina "hesabu kamili" ya kutumwa kwa silaha hiyo.
Urusi inadai kuwa kombora la Kinzhal ambalo linaweza kulenga shabaha hadi kilomita 2,000 (maili 1,240) na linaweza kuruka kwa kasi ya zaidi ya kilomita 6,000 kwa saa, lilirushwa kwa mara ya kwanza kwenye shabaha nchini Ukraine mwezi Machi.
Hivi karibuni, maafisa wa Ukraine walidai kuwa silaha hiyo ilitumiwa huko Odesa mwishoni mwa juma.
Afisa huyo wa Marekani, hata hivyo, alisema kuwa "hana chochote cha kuashiria" kwamba zilitumiwa dhidi ya sehemu zilizokuwa zinalengwa katika jiji hilo.
Ruka X ujumbeRuhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya njeMkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe
Waomba hifadhi wa Uingereza wajificha kukwepa kupelekwa Rwanda

Chanzo cha picha, Getty Images
Watu wanaohukumiwa kuingia Uingereza kinyume cha sheria wanakabiliwa na kupelekwa Rwanda kwa ajili ya makazi mapya.
Mashirika ya misaada yanasema waomba hifadhi kadhaa nchini Uingereza wamejificha kwa sababu ya hofu kuwa watatumwa Rwanda.
Chini ya mkataba uliotiwa saini mwezi uliopita, watu wanaohukumiwa kuingia nchini kinyume cha sheria wanakabiliwa na kupelekwa Rwanda kwa ajili ya kupata makazi mapya.
Shirika la Msalaba Mwekundu na Baraza la Wakimbizi linasema tishio la kuondolewa limewafanya baadhi ya wale wanaotafuta hifadhi kujidhuru; mmoja amejaribu kujiua.
Mashirika ya kutoa misaada yamekosoa mipango ya serikali ya Uingereza kuwa ni ukiukaji wa wajibu wa kutoa huduma.
Ofisi ya Mambo ya Ndani ya London inasema inachukua kila hatua kuzuia kujidhuru au kujiua.Inasema inatumai sera yake itadhoofisha mtindo wa biashara wa wafanyabiashara wa watu.
- Rwanda: Tupo tayari kuwapokea waomba hifadhi kutoka Uingereza
- Wahamiaji Rwanda: Uingereza inaweza kutuma watu wa kwanza 'ndani ya wiki kadhaa'
Miili ya watu 44 yapatikana kwenye vifusi huku mapigano yakiendelea Ukraine

Chanzo cha picha, MAKSIM STRELNIK
Miili ya raia 44 imepatikana kwenye vifusi vya jengo lililoporomoka katika mji wa Izyum nchini Ukraine huku vita vya kuwania udhibiti wa eneo hilo vikiendelea.
Jengo hilo la ghorofa tano liliporomoka mwezi wa Machi huku wakazi wakijificha kwenye vyumba vya chini kutokana na kushambuliwa kwa makombora na Urusi.
Lakini waokoaji wameweza tu kulifikia jengo hilo, afisa mmoja wa eneo hilo aliambia BBC.
Na kuna hofu kwamba idadi ya vifo inaweza kuongezeka zaidi, kwani jengo lingine katika barabara hiyo hiyo pia lililengwa.
"Tunajua pia kulikuwa na watu mle ndani. Kazi ya utafutaji inaendelea na nadhani tutajua idadi zaidi ya waathiriwa hivi karibuni," meya wa Izyum Valeriy Marchenko aliambia BBC.
Urusi ilitwaa udhibiti wa mji wa Izyum tarehe 1 Aprili na wanajeshi wameuteka mji huo tangu wakati huo.
Hakuna vifaa maalum vya kufukua kifusi na kila kitu kinafanywa kwa mikono. Wale wanaofanya kazi hiyo wanaweza tu kufanya hivyo wakati makombora yanaposimamishwa, kwa mujibu wa gavana wa mji wa Kharkiv Oleh Synyehubov.
Izyum, inayojulikana kama lango la kuelekea Donbas, ni sehemu ya eneo la zamani la Ukraine linalozalisha makaa ya mawe na chuma na mji muhimu kwa wanajeshi wa Urusi.
Elon Musk kumrudisha Donald Trump Twitter

Chanzo cha picha, Getty Images
Elon Musk anasema ikiwa ombi lake la kununua Twitter litafaulu atabatilisha marufuku ya Donald Trump kutoka kwenye mtandao huo.
Mtu tajiri zaidi ulimwenguni alikubali zabuni ya $44bn (£34.5bn) na bodi ya Twitter mwezi uliopita.
Lakini alisema haikuwa mpango uliokamilika na kwamba ingekamilika katika kipindi cha miezi miwili hadi mitatu ijayo.Uamuzi wa Twitter wa kumpiga marufuku rais huyo wa zamani wa Marekani ulikuwa "upotovu wa kimaadili na wa kijinga mtupu", Bw Musk aliambia gazeti la Financial Times.
Mnamo Januari 2021, Twitter ilisema akaunti ya Bw Trump "ilisitishwa kabisa... kutokana na hatari ya kuchochea ghasia zaidi" kufuatia kuvamiwa kwa jengo la Capitol nchini Marekani.Lakini mmiliki wa Tesla alisema, "Ningebadilisha marufuku ya kudumu lakini bado similiki Twitter kwa hivyo hili sio jambo ambalo hakika litatokea."Alisema marufuku hiyo haikunyamazisha Bw Trump, lakini kwa kumfanya ahamie kwenye tovuti yake ya 'Truth' ya Kijamii, iliongeza sauti yake kati ya wale walio mbali zaidi wa kulia.
Alidokeza kuwa Bw Trump alikuwa amesema awali hatarejea kwenye Twitter hata akaunti yake ikirejeshwa.
Bw Musk alisema alikuwa amezungumza na mwanzilishi mwenza wa Twitter Jack Dorsey juu ya suala la kuwafungia watumiaji nje ya akaunti zao za mitandao ya kijamii kujibu tweets za kuudhi."Mimi na yeye tuna mawazo sawa kwamba marufuku ya kudumu inapaswa kuwa nadra sana na kuhifadhiwa kwa akaunti ambazo ni za roboti au akaunti za kashfa," alisema.
Putin anajiandaa kwa vita vya muda mrefu- Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images
Vladmir Putin anajiandaa kwa vita vya muda mrefu nchini Ukraine, huku hata ushindi katika eneo la mashariki hautamaliza mzozo huo, idara ya kijasusi ya Marekani imeonya.
Onyo hilo linakuja huku mapigano makali yakiendelea katika eneo la mashariki, ambako Urusi inajaribu kuchukua eneo.
Moscow ilielekeza nguvu mpya kwa wanajeshi wake kuteka eneo la Donbas baada ya Ukraine kukataa majaribio ya kuchukua mji mkuu wake wa Kyiv.
Lakini licha ya hayo, vikosi vyake vimesalia katika mkwamo, taarifa za kijasusi za Marekani zilisema.
Avril Haines, mkurugenzi wa ujasusi wa kitaifa, aliiambia kamati ya Seneti ya Marekani iliyosikiza Jumanne kwamba Bw Putin bado ana nia ya "kufikia malengo zaidi ya Donbas", lakini kwamba "anakabiliwa na kutofautiana kati ya matarajio yake na uwezo wa sasa wa kijeshi wa kawaida wa Urusi".
Aliongeza kuwa rais wa Urusi "pengine" alikuwa akitegemea msaada wa Marekani na EU kwa Ukraine kudhoofika huku mfumuko wa bei, uhaba wa chakula na bei ya nishati ikizidi kuwa mbaya.
Hata hivyo, rais wa Urusi anaweza kugeukia "njia kali zaidi" huku vita vikiendelea - ingawa Moscow ingetumia tu silaha za nyuklia ikiwa Bw Putin ataona "tishio lililopo" kwa Urusi.
Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Ulinzi Scott Berrier aliambia kikao hicho kwamba Warusi na Waukraine walikuwa "katika mkwamo kidogo".
Katika mapigano ya hivi punde zaidi, Ukraine inadai kutwaa tena makazi manne katika eneo la kaskazini-mashariki la Kharkiv.
Cherkasy Tyshky, Ruski Tyshky, Rubizhne na Bayrak wote yalinyakuliwa kutoka kwa Urusi, vikosi vya silaha vya Ukraine vilisema.
Rais Volodymyr Zelenskiy alisema mafanikio ya Ukraine yanasukuma hatua kwa hatua vikosi vya Urusi kutoka Kharkiv, ambayo imekuwa ikishambuliwa tangu vita hivyo.
Lakini alisema Waukraine "hawapaswi kuunda mazingira ya shinikizo nyingi za maadili, ambapo ushindi unatarajiwa kila wiki na hata kila siku".
Unaweza pia kusoma
KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
Hujambo, karibu katika taarifa zetu za moja kwa moja leo 11.05.2022
