Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Serikali ya Tanzania yafungulia magazeti manne yaliokuwa yamefungiwa
Magazeti yaliokuwa yamefungiwa ni Mwanahalisi, Mawio, Mseto na Tanzania Daima.
Moja kwa moja
Wafungwa watoroka jela Ethiopia
Takriban nusu ya wale waliotoroka kutoka jela nchini Ethiopia mapema asubuhi ya Jumatano bado hawajapatikana.
Kwa jumla, wafungwa 130 walitoroka jela katika mji wa Nefas Mewcha katika eneo la Amhara.
Walisaidiwa na wale wanaodai kuwa wanachama wa wanamgambo wa Fano ambao wamekuwa wakipigana pamoja na serikali katika vita dhidi ya waasi katika eneo jirani la Tigray.#
Kamishna wa polisi wa eneo hilo, Tekola Ayifokeru, aliambia BBC watu hao waliokuwa na silaha, ambao walisafiri kwa magari matatu, pia walivamia ghala la kuhifadhia silaha na kupora. Alisema wafungwa 65 wamekamatwa, washambuliaji 16 wameuawa na polisi watatu wamejeruhiwa.
Kamanda huyo alisema kuwa jaribio kama hilo lilifanywa wiki iliyopita kwenye gereza la takriban kilomita 325 (maili 200) kusini-magharibi mwa Nefas Mewcha katika jiji la Finote Selam.
Wafungwa kutoka kituo hicho walikuwa wamehamishwa hadi Nefas Mewcha, ambako inashukiwa walitumia simu za rununu zilizoingizwa gerezani kwa njia haramu kupanga tukio hilo.
Mtalii aungana tena na meno yake aliyoyapoteza miaka 11 iliyopita
Mtalii aliyepoteza jino lake bandia wakati alipokuwa akitapika ndani ya debe la kutupa takataka usiku alipokuwa anakunywa pombekatika eneo laBenidorm alipigwa na butwaa wakati alipoyapata tena baada ya miaka 11.
Paul Bishop, mwenye umri wa miaka 63, alisema "aliugua " baada ya kunywa kilevi cha cider alipokuwa ametoka nje kujiburudisha usiku katika tafrija katika hoteli nchini Uhispaniamwaka 2011.
Baada ya meno hayo ya Paul kupatikana katika dangula la takataka, Mamlaka za Uhispania zilitumia rekodi za vipimo vya vinasaba DNA kumtafuta hatimaye makazi yake ya Stalybridge, yaliyoko Greater Manchester.
Akikumbuka matukio ya usiku ule zaidi ya muongo mmoja uliopita, Paul aliambia kipindi cha BBC North West Tonight: "Nilikuwa nimemaliza kilevi change cha pombe ya cider na nikaamua kutapika "debe la takataka kilikuwa ndio kitu kilichokuwa karibu nami.
"Wakati tulipoelekea kwenye baa iliyofuata, Rafiki yangu alinigeukia na akaniuliza meno yako yako wapi ."
Serikali ya Tanzania yafungulia magazeti manne yaliokuwa yamefungiwa
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Tanzania Nape Nnauye ametoa leseni kwa magazeti manne ambayo yalikuwa yamefungiwa.
Waziri Nape ametoa leseni hizo leo wakati akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali ya habari .
Magazeti yaliokuwa yamefungiwa ni Mwanahalisi, Mawio, Mseto na Tanzania Daima.
"Agizo la Rais ni sheria na inapaswa kutekelezwa, leo nitatoa leseni kwa magazeti manne yaliyokuwa yamefungiwa ambayo ni Mwanahalisi, Mawio, Mseto na Tanzania Daima kwa sababu ni vizuri kuondoka kwenye maneno tufanye vitendo hivyo tuanze na ukurasa upya sasa mwenye maneno yake aseme mwenyewe, kifungo kimetosha kikubwa kazi iendelee”. Amesema waziri huyo.
Pia, Waziri Nape ameagize Idara ya Habari Maelezo kwa kushirikiana na wahariri na taasisi zingine za habari ndani ya muda mfupi kuandaa kikao cha wadau wa habari kujadili marekebisho yaliyopelekwa Serikalini ya sheria ya habari.
“Kwenye hicho kikao mwisho wake tutatengeneza kamati ndogo ambayo itatokana na waandishi wa habari tushauriane tupitie kifungu hadi kifungu tuone ni namna gani wapi tunakubaliana halafu tupeleke marekebisho bungeni ya kupitia upya sheria ya habari' amesema waziri Nape
Uganda yasema agizo la ICJ la kulipa fidia halikufikiwa kwa haki
Serikali ya Uganda inasema uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki ya kuamuru nchi hiyo kuilipa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo $325m kama fidia haukufikia kiwango cha haki kilichotarajiwa.
Katika taarifa yake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kiryowa Kiwanuka alisema nchi hiyo inapinga na inakataa kunyooshewa kidole cha lawama askari wa Uganda kwa makosa licha ya mahakama kukiri kuwepo kwa makundi mengine yenye silaha nchini DRC.
Alitaja uamuzi wa mahakama kuwa ni kushindwa kuthamini masuala ya Afrika na kwamba hautoi mchango wowote katika juhudi za sasa za kutatua masuala ya usalama yanayoendelea huko.
Vikosi vya Uganda kwa sasa viko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wakati huu kwa idhini ya Kinshasha kupigana dhidi ya waasi wa Islamic State, Allied Democratic Force (ADF).
Serikali ya Uganda pia ni sehemu ya kufadhili ujenzi unaoendelea wa barabara ya kilomita 200 ili kuimarisha biashara kati ya nchi hizo mbili.
Mnamo mwaka wa 1999, DRC iliwasilisha kesi mbele ya ICJ dhidi ya Uganda kwa vitendo vya uvamizi wa silaha katika eneo lake kinyume na mikataba ya Umoja wa Mataifa na AU kati ya 1998 na 2003.
Wakati huo, Uganda haikuomba idhini ya serikali ya Congo kuingia.
Katika kilele cha mzozo huo, zaidi ya nchi tisa za Kiafrika ziliingizwa kwenye mapigano.
Kufuatia uamuzi wa mahakama siku ya Jumatano, Uganda sasa italazimika kulipa fidia hiyo kwa awamu ya $65m kila tarehe 1 Septemba, kuanzia mwaka huu.
Mvutano wa Ukraine: Urusi yaanza mazoezi ya kijeshi na Belarus
Urusi na Belarus zinaanza siku 10 za mazoezi ya pamoja ya kijeshi huku kukiwa na hofu inayoendelea ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Belarus ni mshirika wa karibu wa Urusi na ina mpaka mrefu wa kusini na Ukraine.
Marekani imetaja mazoezi hayo - ambayo yanaaminika kuwa ndiyo makubwa zaidi ya Urusi kupelekwa Belarus tangu Vita Baridi kama hatua "ya kuongezeka kwa mvutano huo".
Urusi imekanusha mara kwa mara mpango wowote wa kuivamia Ukraine licha ya kuwa na wanajeshi zaidi ya 100,000 kwenye mpaka.
Lakini Marekani na nchi nyingine za Magharibi zimeonya kwamba shambulio linaweza kutokea wakati wowote.
Moscow inasema haiwezi kukubali kwamba Ukraine - jamhuri ya zamani ya Soviet yenye uhusiano wa kina wa kijamii na kiutamaduni na Urusi - siku moja inaweza kujiunga na muungano wa ulinzi wa Magharibi wa Nato na imedai kwamba hilo litakataliwa. Imekuwa ikiunga mkono uasi wa kutumia silaha mashariki mwa Ukraine tangu 2014.
Mazungumzo ya kidiplomasia yenye lengo la kutuliza mvutano huo yanatarajiwa kote Ulaya siku ya Alhamisi.
Waziri Mkuu wa Libya anusurika jaribio la mauaji
Waziri Mkuu wa Libya Abdulhamid al-Dbeibah amenusurika katika jaribio la mauaji lililofanywa na watu wasiojulikana.
Gari lake lilishambuliwa kwa risasi lilipokuwa likiendeshwa katika mji mkuu, Tripoli, mapema siku ya Alhamisi.
Watu wenye silaha walikimbia eneo la tukio.
Pande zinazozozana zimekuwa zikigombea udhibiti wa Libya, na bunge lenye makao yake mashariki mwa nchi hiyo litapiga kura baadaye siku ya Alhamisi kumchagua waziri mkuu atakayechukua nafasi ya serikali ya umoja wa kitaifa.
Bw Dbeibah amesema kuwa atapuuza matokeo ya kura hiyo.
Uchaguzi wa kuichagua serikali mpya uliahirishwa Disemba mwaka jana lakini hakuna kura inayotarajiwa mwaka huu
Abiria akamatwa uwanja wa ndege wa Heathrow kwa shutuma za kubaka ndani ya ndege
Abiria mmoja alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Heathrow baada ya mwanamke mmoja kusema alibakwa kwenye ndege wakati wa safari ya usiku ya kuvuka Atlantiki kutoka New Jersey.
Mwanamke huyo alisema alishambuliwa na mwanaume mwenye umri wa miaka 40 huku wengine wakiwa wamelala kwenye ndege kutoka Newark tarehe 31 Januari.
Maafisa walipanda ndege ya United Airlines baada ya kutua saa 06:39 GMT na kumkamata mtu huyo ambaye ameachiliwa huru kwa ajili ya uchunguzi.
Polisi wa Met walisema mwanamke huyo alikuwa akiungwa mkono na maafisa maalum.Msemaji alisema Met wanafahamu kuhusu "tukio la ndege inayoingia".
The Enigma: Almasi nyeusi yenye umri wa mabilioni ya miaka yauzwa kwa dola milioni 3.16
Almasi nyeusi yenye umri wa mabilioni ya miaka inayoaminika kuwa almasi kubwa zaidi iliyokatwa duniani, imeuzwa kwa £3.16m.
Kwa jina la The Enigma, jiwe hilo la thamani ya karati 555.55 ambalo lina uzito sawa na ndizi, lilitarajiwa kuingiza zaidi ya £4.4m.
Dalali Sotheby's alisema "mnunuzi amechagua kutumia cryptocurrency kwa ununuzi."
Kuna nadharia zinazoshindana kuhusu asili ya jiwe, ikiwa ni pamoja na kwamba lilibebwa duniani na asteroid.
Baada ya mnada huo, mjasiriamali wa sarafu fiche Richard Heart alienda kwenye mitandao ya kijamii kudai kuwa yeye ndiye mnunuzi wa The Enigma.
Aliwaambia wafuasi wake zaidi ya 180,000 wa Twitter kwamba "mara tu malipo yanapopitishwa na milki kuchukuliwa" jiwe hilo la thamani litaitwa jina la "almasi HEX.com", akimaanisha jukwaa la blockchain aliloanzisha.
Jiwe hilo ni mojawapo ya aina ngumu zaidi za almasi ya asili.
Carbonados ni nadra sana na zimewahi kugunduliwa nchini Brazil na Jamhuri ya Afrika ya Kati pekee.
Kwa sababu vina osbornite, madini yanayopatikana tu kwenye vimondo, vinaaminika kuwa vinatoka angani.
Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja hii leo tarehe 10 Februari 2022