Wasichana waliorudi shuleni hawaruhusiwi kwenda na watoto wao darasani

Waziri wa Elimu nchini Tanzania, amenukuliwa na vyombo kadhaa vya Habari nchini, akisema, agizo la serikali la kuwaruhusu wanafunzi wa kike waliokatisha masomo kwa kupata ujauzito kurudi shuleni, halimaanishi kwamba wanafunzi hao waruhusiwe kuingia darasani na watoto wao.

Moja kwa moja

  1. Tumefika mwisho wa taarifa zetu za moja kwa moja, mpaka Jumatatu panapo majaaliwa

  2. Wabunge wa Uganda wasusia vikao juu ya kuzuiliwa na kuteswa kwa wapinzani

    Wabunge wa upinzani nchini Uganda wamesusia vikao vya bunge wakidai serikali iwaachie wanasiasa wa upinzani ambao walikamatwa wakati wa kapeni za uchaguzi na baada ya uchaguzi mkuu wa rais na wabunge mwaka 2021.

    Hilo limejiri hapo jana katika kikao cha bunge baada ya naibu Spika wa bunge kuwataka wasubiri hadi wiki ijayo.

    Kulingana na mwandishi wa BBC Issaac Mumena, karibu wabunge wote wa vyama vya upinzani nchini Uganda waliondaka jana kwenye kikao cha bunge huku wakiwa wanaimba nyimbo za kutaka serikali kuwachia huru wafungwa wa kisiasa, na kupinga serikali inavyoendelea na unyanyasaji wa watuhumiwa kwa kuwaweka korokoroni baadhi yao bila kufikishwa mahakamani.

    Kiongozi wa wabunge wa upinzani bungeni Mathias Mpuuga alipingana na Naibu Spika Anita Among alipotoa ripoti ya kupotea kwa watu na wengine kuzuiliwa bila kufunguliwa mashitaka na kuteswa.

    Alitaka bunge kuzungumzia swala hilo lakini naibu Spika akawafahamisha mpaka wiki ijayo kwa kuwa anachukua hatua ya kumuelezea Spika.

    Wabunge wa upinzani wanadai hawawezi kuendelea kuhudhuria vikao vya bunge wakati wenzao wanateswa magerezani

    Baadhi ya wabunge wa chama tawala cha NRM waliobaki bungeni waliwalaumu wenzao wa upinzani kwa kutoka nje kwani na wao hawafurahishwa na vikosi vya usalama kuwatesa watuhumiwa.

    Kwa upande wao ingekuwa bora zaidi kama wangesubiri siku ya Jumanne wiki ijayo kama walivyoshauriwa na naibu Spika.

    Waziri wa mambo ya ndani wa Uganda alikanusha ripoti ya kuteswa watuhumiwa na kusema anakwenda kutowa ripoti siku ya Jumanne wiki ijayo.

    Mwaka jana Rais Museveni aliwaonya walinda usalama na kuwataka kuacha kuwatesa watuhumiwa ili kusema wanachotaka, lakini bado vitendo vya unyanyasi wa watuhumiwa vinaendelea.

    Hivi karibuni mwandishi wa vitabu na mwana harakati wa kutetea haki za binadamu Kakweza Rukirabashaija alilalamika mahakamani jinsi alivyoteswa na kikosi cha kumlinda Rais alipokamatwa, na madaktari wa Idara ya magereza walithibisha kuteswa kwake walipotakiwa na mahakama kufanya uchunguzi.

    Hii hapa ni video ya wabunge wakiwa nje ya bunge.

    Ruka X ujumbe
    Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

    Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

    Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

    Mwisho wa X ujumbe

  3. Kenya: Mpiga mbizi aliyekuwa akiopoa maiti zilizotupwa mtoni ajificha

      • Author, Ferdinand Omondi
      • Nafasi, BBC News, Nairobi
    Takriban miili 25 imepatikana hadi sasa kutoka kwa Mto Yala
    Maelezo ya picha, Takriban miili 25 imepatikana hadi sasa kutoka kwa Mto Yala

    Mpiga mbizi ambaye amekuwa akisaidia kuopoa maiti kutoka Mto Yala magharibi mwa Kenya amejificha baada ya kutishiwa maisha yake, shirika la kutetea haki za binadamu linasema.

    Anasema amehusika katika kuopoa miili isiyopungua 25 tangu katikati mwa mwaka jana.

    Wakati timu ya BBC ilipozuru eneo hilo katika kaunti ya Siaya mwezi uliopita, mzamiaji huyo alieleza jinsi baadhi ya maiti alizopata zikiwa zimefungwa viungo vyao pamoja, huku nyingine zikiwa kwenye magunia.

    Wakati huo alisema baadhi ya maafisa wa polisi hawakufurahishwa na hatua ya yeye kuzungumza na wanaharakati wa haki za binadamu na waandishi wa habari kuhusu hali hiyo.

    Alitakiwa asizungumze na vyombo vya habari - na polisi pia wanapinga kauli zake, wakisema miili imegunduliwa kwa zaidi ya miaka miwili.

    Shirika la Haki Africa linasema mwanamume huyo sasa ametishwa na polisi.

    Mpiga mbizi huyo hivi majuzi aliitwa na polisi, akazuiliwa kwa saa nane na kunyanganywa simu yake, shirika hilo la kutetea haki za binadamu lilisema katika taarifa ya mkurugenzi wa Haki Africa Hussein Khalid ambapo aliiambia BBC kuwa, shirika hilo limeamua kumficha kwasababu ya wasiwasi wa ustawi wake.

    Lakini Kamanda wa Kaunti ya Siaya Michael Muchiri anasema hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi.

    Mpiga mbizi huyo amekuwa akifanya kazi vizuri na maafisa wake na polisi "hawawezi kumtishia mtu ambaye amekuwa msaada mkubwa kwetu," alisema kati ya miili hiyo iliyopatikana na mpiga mbizihuyo, miwili hadi sasa imetambuliwa kufuatia taarifa za hivi punde na vyombo vya habari.

    Katika visa vyote viwili, wanaume hao walikuwa wameripotiwa kutoweka ndani ya miezi mitatu iliyopita - na wote wawili walikuwa wameonekana mara ya mwisho wakiwa hai zaidi ya kilomita 200 (maili 124) kutoka Mto Yala, na kuzua maswali kuhusu jinsi walivyofika huko.

    Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamehoji iwapo kuna uwezekano wowote wa polisi kuhusika katika vifo hivyo.

    Vikosi vya usalama kwa kawaida huwa miongoni mwa washukiwa wa kwanza wakati kunapotokea vifo vinavyotiliwa mashaka na matukio ya kutoweka - hasa ikizingatiwa kuwa kesi zilizoandikwa kwa kina zinazohusishwa moja kwa moja na maafisa.

    Lakini mamlaka imewataka wananchi kuacha uvumi huo na kusubiri uchunguzi ukamilike.

    Wiki iliyopita, mwanapatholojia mkuu alikamilisha uchunguzi wa miili 17, lakini matokeo bado hayajatolewa hadharani.

  4. Afrika Kusini yatengeneza toleo lake la chanjo ya corona ya Moderna

    Kwa sasa Afrika ina idadi ndogo zaidi ya chanjo za Covid duniani

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Kwa sasa Afrika ina idadi ndogo zaidi ya chanjo za Covid duniani

    Wanasayansi nchini Afrika Kusini wametoa nakala yao ya chanjo ya Moderna Covid, hatua ambayo wanasema inaweza kusaidia kuongeza viwango vya chanjo barani Afrika.

    Kwa sasa bara hili lina idadi ndogo zaidi ya watu wanaopata chanjo ya Covid.

    Kampuni inayoendesha chanjo hiyo mpya - Afrigen Biologics - inasema inatumai kuanza majaribio ya kimatibabu mnamo mwezi Novemba.

    Moderna hapo awali ilisema haitakubali hataza kwenye chanjo yake, ikiruhusu wanasayansi huko Cape Town kutengeneza toleo lao la chanjo.

    Watafiti hao waliungwa mkono na Shirika la Afya Duniani (WHO).

    Petro Terblanche, mkurugenzi wa Afrigen Biologics, alisema walikuwa wanaanza kidogo, lakini wana malengo ya kuongeza kasi siku zijazo.

    "Tumetumia mpangilio ambao ni sawa na chanjo ya Moderna 1273," aliiambia BBC.

    "Hii ni sehemu ya mpango wa kimataifa wa kujenga uwezo katika nchi za kipato cha chini na cha kati ili kujitegemea."

    Chanjo inayonakiliwa ni ile ya RNA iliyotengenezwa na kampuni ya Kimarekani ya Moderna.

    Pfizer-BioNTech pia ilitengeneza chanjo yake kwa kutumia teknolojia hiyo hiyo.

    Zilikuwa baadhi ya chanjo za kwanza za Covid kuidhinishwa kutumika kote ulimwenguni.

    Aina hii ya chanjo hufundisha seli jinsi ya kutengeneza protini ambayo itasababisha mwitikio wa kinga ndani ya miili yetu, badala ya kuweka vijidudu dhaifu au visivyotumika mwilini.

    Mwanasayansi mkuu wa kampuni hiyo, Dk Caryn Fenner, alitaja mafanikio hayo " kuwa muhimu sana."

    "Inaweka uwezo mikononi mwetu kuweza kutengeneza chanjo zetu wenyewe kwa siku zijazo, kuwa tayari kwa magonjwa zaidi ya milipuko, kutoa nyenzo za majaribio ya kimatibabu katika ardhi ya Afrika na kisha kuangalia magonjwa mengine ya umuhimu barani Afrika."

    Nchi nyingi za Afrika zimechanja kikamilifu chini ya asilimia 10 ya watu wake, ikilinganishwa na asilimia 60 Amerika Kaskazini,asilimia 63 Ulaya na asilimia 61 kote Asia.

    Licha ya kuwa na viwango bora zaidi barani Afrika, Afrika Kusini imechanja asilimia 27 pekee ya watu wake.

    Soma zaidi:

  5. Wasichana waliorudi shuleni hawaruhusiwi kwenda na watoto wao darasani

      • Author, Aboubakar Famau
      • Nafasi, BBC News, Dodoma
    Mwanafunzi mzazi akiwa na mtoto wake darasani

    Waziri wa Elimu nchini Tanzania, amenukuliwa na vyombo kadhaa vya Habari nchini, akisema, agizo la serikali la kuwaruhusu wanafunzi wa kike waliokatisha masomo kwa kupata ujauzito kurudi shuleni, halimaanishi kwamba wanafunzi hao waruhusiwe kuingia darasani na watoto wao.

    Profesa Adolf Mkenda ambae ndiye waziri wa elimu amesema kufanya kunaweza kuwasumbua wanafunzi wengine wakiwa darasani.

    Kauli hii ya waziri Mkenda, inakuja siku chache baada ya makala iliyofanywa na BBC inayomuonesha binti mmoja akiwa darasani na mwanaye.

    Esnath Gedion kutoka jijini Mbeya, tangu shule kufunguliwa, amekuwa akiingia darasani na mwanaye mwenye umri wa miezi minne, baada ya kukosa mtu wa kukaa na mtoto wake nyumbani.

    Serikali ya Tanzania mwishoni mwa mwaka jana iliondoa marufuku ya kuzuia wanafunzi wa kike waliokatiza masomo kwa kupata ujauzito kurudi shuleni.

    Hata hivyo, licha ya kuwepo kwa fursa hiyo, baadhi ya wanafunzi wamejikuta katika wakati mgumu baada ya kukosa watu wa kuwaachia watoto nyumbani, hivyo baadhi kulazimika kuingia na watoto wao darasani.

    Baadhi ya wadau wa elimu, wanasema, serikali ilitakiwa kuweka miundombinu rafiki kwanza kwa wanafunzi hao na watoto wao.

    Baadhi ya wanafunzi hao, wamerudi shuleni kupitia mradi wa Alternative Education Pathway, ambao ni wezeshi na hauna masharti magumu kwa wanafunzi kama vile kuvaa sare darasani.

    Mratibu wa elimu ameiambia BBC kwamba, miongoni mwa mapendekezo waliyowasilisha serikalini ni pamoja na kuweka vituo vya kulelea watoto ili wanafunzi hao wapate muda mzuri wa kusoma.

    Hata hivyo, mpaka sasa, hatma ya mabinti wanaokabiliwa na changamoto ya ulevi kama vile Esnath, haijulikani.

  6. Boti ya kifahari ya Jeff Bezos itasababisha daraja la kihistoria kuvunjwa

    Jeff Bezos

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Jeff Bezos

    Rotterdam imethibitisha kuwa itabomoa daraja la kihistoria ili kuruhusu boti kubwa iliyojengwa kwa ajili ya mwanzilishi wa Amazon Jeff Bezos kupita.

    Boti hiyo ya kifahari iliyovunja rekodi inajengwa na kampuni ya Uholanzi ya Oceanco na ilihusishwa na Bw Bezos mwaka jana.

    Chombo hicho kinaripotiwa kuwa na urefu wa futi 417 (127m) na kirefu sana kutoshea kupitia Daraja la Koningshaven.

    Msemaji wa meya alithibitisha mpango huo kwa wanahabari, huku Bw Bezos akitarajiwa kufikisha hoja hiyo kupitia kampuni Oceanco.

    Ripoti ziliibuka kwenye vyombo vya habari vya Uholanzi siku ya Jumanne kwamba sehemu ya kati ya daraja hilo la jiji la Uholanzi, inayojulikana na wenyeji kama De Hef, itaondolewa kwa muda ili kuruhusu mashua ya urefu wa futi 130 (40m) kupita.

    Daraja la kihistoria kuvunjwa
    Maelezo ya picha, Boti ya kifahari ya Jeff Bezos itakayosababisha daraja la kihistoria kuvunjwa

    Hatua hiyo ina utata kwasababu daraja hilo la chuma lina historia ya siku nyingi, na sasa ni mnara wa kitaifa.Hapo awali ilifanyiwa ukarabati mkubwa ambao ulisababisha kutotumika kutoka mwaka 2014 hadi 2017, wakati maafisa walisema haitavunjwa tena.

    Shirika la habari la AFP lilinukuu afisi ya meya ikisema ajira zilizotokana na ujenzi wa chombo hicho ndio zilizochochea mpango huo, na kuahidi kuwa daraja hilo litajengwa upya katika hali yake ya sasa."Ndio njia pekee ya kuelekea baharini," msemaji wa meya aliongeza.

    Maoni hayo yaliungwa mkono na kiongozi wa mradi wa mamlaka ya eneo la Rotterdam Marcel Walravens, ambaye alisema haitakuwa jambo la maana kumaliza ujenzi wa boti mahali pengine.

    Aliiambia tovuti ya Rijnmond mradi huo "ni muhimu sana"kwa mtazamo wa kiuchumi na akataja sifa ya Rotterdam kama"mji mkuu wa bahari barani Ulaya".

    "Ujenzi wa meli na shughuli ndani ya sekta hiyo ni nguzo muhimu ya manispaa," alisema.

    Jeff Bezos
    Maelezo ya picha, Jeff Bezos

    Maelezo kuhusu agizo la boti hiyo ya kifahari inayojengwa na kampuni ya Oceanco yaliibuka mwaka jana.Kampuni hiyo bado haijasema lolote kuhusu wateja wake lakini wasifu wa Bloomberg kuhusu Bezos mnamo mwaka 2021 ulionekana kuthibitisha uvumi kwamba angekuwa mmiliki.

    Chombo hicho kinachojulikana kama Y721, kitakuwa kikubwa zaidi cha aina yake duniani, kulingana na shirika la Boat International.

    Inasemekana kujivunia sifa nyingi za kifahari.

    Hata hivyo, hatua hiyo ilikosolewa na mwanasiasa wa eneo Stephan Leewis kupitia mtandao wa Twitter, ambaye alielezea "kubomoa mnara wetu wa kitaifa" kama "daraja hiyo imepitiliza".

    Forbes inakadiria kuwa mwanzilishi wa Amazon ana thamani ya zaidi ya $175bn (£130bn) na kwa sasa inamtaja kuwa tajiri wa tatu duniani.

    Kando na kuwa gwiji katika wa tasnia ya biashara ya mtandaoni, Bezos pia anamiliki gazeti la Washington Post na kampuni ya anga za mbali ya Blue Origin.

    Soma zaidi:

  7. Kocha wa Misri anataka mechi ya fainali ya Afcon dhidi ya Senegal kuahirishwa

    Wachezaji wa Misri wakisherehekea ushindi wa nusu fainali dhidi ya wenyeji Cameroon

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Wachezaji wa Misri wakisherehekea ushindi wao wa mechi ya nusu fainali dhidi ya Cameroon

    Kocha msaidizi wa Misri Diaa al-Sayed anataka fainali yao ya Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Senegal ichezwe Jumatatu badala ya Jumapili ili wapate siku ya ziada ya kupumzika.

    Mafarao waliwashinda wenyeji Cameroon siku ya Alhamisi kwa mikwaju ya penalti, ukiwa ni ushindi wao wa tatu mfululizo.

    Senegal, ambao wameshinda michezo zao zote ndani ya dakika 90, walishinda Burkina Faso 3-1 Jumatano.

    "Naomba CAF fainali ichezwe Jumatatu," Al-Sayed alisema.

    ''Senegal wana siku moja ya ziada ya kupumzika''

    Al-Sayed alikuwa akizungumza na vyombo vya habari kwa sababu kocha wa Misri Carlos Queiroz alitolewa nje kwa kadi nyekundu wakati wa mechi.

    Mechi ya kutafuta mshindi wa nafasi ya tatu kati ya Cameroon na Burkina Faso ulipaswa kuwa Jumapili pia, lakini sasa itachezwa Jumamosi.

    Mnamo 2019 nusu fainali zote mbili zilichezwa siku moja.

    Tarehe ya fainali iksogezwa itachelewesha wachezaji kurejea kwenye vilabu vyao.

  8. Chokoleti za KitiKat zaondolewa madukani kwa kuhofiwa kuwa na 'vipande vya kioo'-Afrika Kusini

    Chokoleti za KitKat ni maarufu sana katika nchi za Kiafrika

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Chokoleti za KitKat ni maarufu sana katika nchi za Kiafrika

    Kampuni ya kutengeneza vyakula ya Nestlé imezirudisha kwa hiari baadhi ya chokoleti zake za KitkKat nchini Afrika Kusini baada ya kubaini kuwa zina vipande vya kioo wakati wa kukagua usalama.

    Kampuni hiyo ilisema hakuna mteja aliyelalamika lakini hatua za kuzuia zinachukuliwa baada ya tatizo hilo kubaini.

    Inasema kwa sasa inachunguza kitu gani hasa kilitokea katika chokoleti hizo kuona ikiwa chokoleti imeathirika, itabidi kuangalia nambari ya uzalishaji nyuma ya kifungashio.

    Wateja ambao walikuwa wamenunua chokoleti zilizo na namba za utambulisho zilizoorodheshwa wameombwa kuzirejesha.

    Utambulisho huo ni:

    • Nestlé KitKat 2 Finger Milk 36x20g UTZ MB yenye nambari ya uzalishaji "13590177" nyuma ya kifungashio"13600177", "13620177", "13630177", "13640177", "20010177" na "20100177" na
    • Mini Bag Milk 32x200g UTZ yenye nambari ya uzalishaji "20120177", "20010177" "20020177" na "20030177", "13620177", "13600177" na "13610177" inayoonekana nyuma ya kifungashio.

    Yeyote anayeshuku kuwa alitumia chocolate zenye utambulisho huo ameombwa kuonana na daktari.

    Nestlé inasema itaimarisha ukaguzi wake wa ubora ili kuhakikisha visa kama hivyo havitokei tena.

  9. Nigeria yafichua washukiwa wanaofadhili ugaidi

    Nigeria has turned to financial regulators to help in the fight against terrorism

    Chanzo cha picha, AFP

    Nigeria inasema imegundua zaidi ya makampuni 120 na watu 96 wanaohusishwa na ufadhili wa ugaidi.

    Waziri wa habari, Lai Mohammed, alisema watu 45 wanaoshukiwa kufadhili ugaidi wamekamatwa na hivi karibuni watachukuliwa hatua za kisheria.

    Alisema shirika la uhalifu wa kifedha la Nigeria lilipata dola milioni 750 za Kimarekani (£550m) katika sarafu za ndani na nje zilizohusishwa na ufisadi.

    Mwezi uliopita, Tume ya Usalama na Ubadilishanaji wa fedha nchini Nigeria iliongeza uwezo wa mamlaka kufuatilia uhusiano wa kifedha na makundi yanayoshukiwa kuwa ya kijihadi.

    Rais Muhammadu Buhari, ambaye sasa yuko katika muhula wake wa pili, alichaguliwa kwa ahadi ya kupambana na ufisadi na kurejesha kiasi kikubwa cha fedha zilizoibwa kutoka Nigeria.

    Soma:

    • Fahamu kundi linaloihangaisha Nigeria licha ya kuwa na jeshi kubwa
    • Boko Haram: Hizi ndizo sababu sita za serikali ya Nigeria kushindwa kuliangamiza kundi la kigaidi la Boko Haram
    • Fahamu kwanini Nigeria, Mali, Burkina faso ,Niger, Chad na Cameroon zinalemewa na makundi yaliyojihami
  10. 'Tofauti' kati yangu na Mikel Arteta ilisababisha niondoke Arsenal -Pierre-Emerick Aubameyang

    Aubameyang aliachiliwa kutoka katika kandarasi yake ya Arsenal siku ya Jumatatu bila kujitokeza kufuatia suala la kinidhamu mwezi Disemba.

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Pierre-Emerick Aubameyang amesema "tofauti" kati yake na kocha wa Arsenal Mikel Arteta ilichangia uamuzi wake wa kuihama klabu hiyo na kujiunga na Barcelona.

    Mshambulizi huyo wa Gabon alikamilisha uhamisho wa bila malipo kwenda Barca siku ya Jumatano baada ya kufungiwa nje ya kikosi cha The Gunners.

    Kuondoka kwa Aubameyang kulikuja baada ya kuvuliwa unahodha wa Arsenal kufuatia utovu wa nidhamu.

    "Nadhani ilikuwa shida upande wake tu [Arteta]," mchezaji huyo wa miaka 32 alisema wakati wa uzinduzi wake Nou Camp siku ya Alhamisi.

    "Alifanya uamuzi. Siwezi kusema mengi zaidi. Hakuwa na furaha, japo nilikuwa mtulivu sana lakini ndio hivyo tena."

    Aubameyang aliachiliwa kuondoka Arsenal siku ya Jumatatu bila kujitokeza kufuatia suala la kinidhamu mwezi Disemba.

    Aubameyang na Arteta

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mshambulizi huyo wa zamani wa Borussia Dortmund hapo awali mnamo mwezi Machi alikosa mechi ya ushindi dhidi ya Tottenham kaskazini mwa London kwa sababu ya "ukiukaji wa itifaki ya kabla ya mechi".

    Lakini ana matumaini ya kufufua mchezo wake huko Barca kabla ya mechi ya kwanza dhidi ya Atletico Madrid siku ya Jumapili.

    "Ni kweli kwamba ilikuwa miezi migumu na nadhani soka huwa na mambo haya wakati mwingine," aliongeza Aubameyang.

    "Lakini kama itabidi niseme kitu kuhusu mada hii [kuondoka Arsenal], ni kwamba sikuwahi kufanya lolote baya kwa upande wangu, lakini nadhani hayo yamepita na ninataka kufikiria kuhusu hali yangu ya sasa."

    Aubameyang alifunga mabao 92 katika mechi 163 alizochezea Arsenal kufuatia uhamisho wake wa pauni milioni 56 kutoka Dortmund Januari 2018, akiwasaidia The Gunners kushinda Kombe la FA 2020 na kumpa Arteta medali ya fedha katika msimu wake wa kwanza kushikilia usukani.

    Mkataba wake Barcelona utaendelea hadi Juni 2025 na unajumuisha chaguo la kukubali kuondoka mnamo Juni 2023, pamoja na kifungu cha ununuzi cha euro milioni 100 (£83.4m).

  11. Uokoaji wa mtoto wa miaka 5 aliyeanguka kisimani waikumba Morocco

    Mamlaka za mkoa zilileta mashine nzito katika jaribio la kumuokoa mtoto huyo

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Mamlaka za mkoa zilileta mashine nzito katika jaribio la kumuokoa mtoto huyo

    Juhudi za kumuokoa mtoto nchini Morocco ambaye alianguka katika kisima karibu na mji wa Chefchauone zinaelekea ukingoni.

    Mtoto huyo , ambaye vyombo vya Habari vya eneo hilo vimemtambua kuwa wa miaka mitano , Rayan , alidaiwa kucheza karibu na kisima hicho katika mji wa kaskazini wa Tamrout , yapata kilomita 100 kutoka mji wa Chefchaouen.

    Rayan anaaminika kuanguka mita 32 kupitia mwanya mdogo wa shimo hilo. Operesheni ya uokoaji ikiongozwa na idara ya kuwalinda raia , imekuwa ikiendelea tangu siku ya Jumanne.

    Uokoaji wa mtoto huo unakaribia, msemaji wa serikali Mustapha Baitas alisema siku ya Alhamisi jioni.

    ''Mioyo yetu ipo na família na tunaomba kwamba atajiunga não hivi karibuni’’.

    Licha ya kuanguka vibaya, picha zilizoingizwa katika kisima hicho zinaonesha kwamba mvulana huyo bado yuko hai na ana fahamu, licha ya kwamba anaonekana kujeruhiwa kichwani.

    Wafanyakazi wa uokoaji wameshusha maski ya hewa , chakula na maji ndani ya kisima hicho na kikosi cha matibabu pia kipo katika eneo hilo, tayari kusaidia na kumtibu mtoto.

    Ndege aina ya helikopta pia imewasili katika eneo hilo ili kumpeleka hospitali punde tu atakapookolewa kutoka kwa kisima.

    Maelfu ya watu wamekuwa wakitazama picha za uokoaji huo kutoka kwa mitandao ya kijamii , na kundi kubwa la watazamaji limekongamana katika eneo hilo.

  12. Natumai hujambo. Ikiwa siku ya Ijumaa tunakuletea habari za moja kwa moja kutoka kote duniani