Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Roketi ya Elon Musk SpaceX inaelekea kugongana na mwezi

Roketi iliyorushwa na kampuni ya uvumbuzi wa anga za juu ya bilionea Elon Musk inakaribia kugonga ndani ya mwezi na kulipuka.

Moja kwa moja

  1. Na kufikia hapo twakamilisha matangazo haya ya moja kwa moja. Hadi kesho kwaheri

  2. Malawi yatangaza maeneo kadhaa kuwa hatari baada ya mafuriko makubwa

    Rais wa Malawi Lazarus Chakwera imetangaza baadhi ya sehemu za nchi hiyo kuwa maeneo ya majanga, baada ya watu 19 kuuawa katika mafuriko yaliyosababishwa na dhoruba ya kitropiki Ana.

    Vifo hivyo vimeripotiwa katika takriban wilaya tano kusini mwa Malawi, ambapo zaidi ya watu 50 pia walijeruhiwa kwa viwango tofauti.

    Hadi kambi 44 zimewekwa kusaidia maelfu ya watu waliofurushwa makwao

    Dhoruba hiyo pia imesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu, ikiwa ni pamoja na kiwanda kikuu cha kuzalisha umeme nchini.

    Umeme umeanza kurejeshwa katika baadhi ya maeneo ya nchi baada ya huduma hiyo muhimu kukatizwa kote nchini siku ya Jumanne.

    Taarifa iliyotolewa siku ya Alhamisi na ofisi ya rais imetangaza kuwa wilaya zote ambazo zimeathirika katika sehemu ya kusini ni maeneo ya majanga na hatua hiyo imeanza kutekelezwa mara moja.

  3. DCI yamkamata mshukiwa mkuu wa mauaji ya shabiki maarufu wa soka Kenya

    Maafisa waIdara ya upelelezi wa makosa ya jinai (DCI) nchini Kenya wamemkamata mshukiwa mkuu wa anayetuhumiwa kuhusika na mauaji ya shabiki maarufu wa kandanda Isaac Juma huko Mumias, magharibi mwa nchi hiyo, kulingana na taarifa za gazeti la Daily Nation mtandoni.

    DCI imenukuliwa ikisema: mshukiwa huyo mwenye umri wa miaka 27 alikamatwa nyumbani kwake Mumias na makachero wao baada ya uchunguzi wa awali kumhusisha na mauaji hayo.

    Isaac Juma alidungwa kisu nyumbani kwao katika eneo la magharibi mwa Kenya Jumatano usiku, kulingana na vyombo vya habari.

    Bw Juma alifahamika sana kwa kutumia mwili wake kama sanamu wakati wa mechi nchini kenya.

    Aliwahi kusafiri nje ya nchi na timu ya taifa.

    Katika mahojiano na televisheni ya Citizen nchini humo mwaka 2018, alisema ana matumaini kwamba timu ya Kenya itafuzu kwa mechi za Afcon ambazo kwa sasa zinaendelea nchini Cameroon.

  4. Rais wa Burkina Faso aliyeondolewa madarakani 'anaendelea vizuri'

    Rais wa Burkina Faso aliyeondolewa madarakani Roch Kaboré anaendelea vyema, afisa wa ngazi ya juu wa chama chake amesema.

    Haya yanajiri siku kadhaa baada ya mapinduzi ya kijeshi ambayo yamelaaniwa vikali na jamii ya kimataifa.

    Bw Kaboré anazuiliwa katika jumba la kifahari la rais chini ya kizuizi cha nyumbani, yuko katika hali nzuri kimwili na ana daktari anayeweza kumsaidia, kulingana na mwanachama mkuu wa chama chake, People's Movement for Progress (MPP).

    Kwa saa kadhaa siku ya Jumatatu, hatima ya rais huyo aliyeondolewa madarakani haikufahamika, huku habari zinazokinzana zikisambaa kuhusu kukamatwa, kufukuzwa nje au hata jaribio la mauaji.

    Mkutano wa kilele wa kanda ya Afrika Magharibi Ecowas utafanyika Ijumaa kujadili hali ya Burkina Faso baada ya Bw Kaboré kupinduliwa, na uwezekano wa vikwazo dhidi ya jeshi.

  5. Mwandishi wa Uganda anayetuhumiwa kumtusi rais aachiliwa

    Mawandishi wa Uganda aliyetuhumiwa kumtukana rais na familia yake ameachiliwa baada ya kukamatwa tena muda mfupi baada ya mahakama kumwachilia kwa dhamana.

    Kakwenza Rukirabashaija "alitupwa" na wanajeshi kwenye lango la nyumba yake mashariki mwa Uganda siku ya Jumatano, wakili wake alisema.

    Mke wa mwandishi huyo pia alithibitisha kuachiliwa kwake.

    Wakili wake alisema mwandishi huyo alikuwa mgonjwa na amepelekwa hospitali kwa matibabu.

    Mwandishi huyo aliyeshinda tuzo alishtakiwa kwa mawasiliano ya kuudhi baada ya kutuhumiwa kumtusi Rais Yoweri Museveni, na mwanawe, Lt Gen Muhoozi Kainerugaba, kwenye Twitter.

    Alifanikiwa kupata dhamana kutoka kwa mahakama ya Kampala kabla ya kukamatwa tena katika mazingira yasiyoeleweka.

    Wakili wake alisema "alitekwa nyara" akitoka gerezani na wanaume waliokuwa wamevalia nguo za kawaida na kupelekwa eneo lisilojulikana.

    Mwandishi huyo alishinda tuzo kwa riwaya yake ya kejeli ya 2020 The Greedy Barbarian ambayo inaelezea ufisadi wa hali ya juu katika nchi ya kubuni.

  6. Raia wa Rwanda ambao hawajachanjwa hawataruhusiwa maeneo ya umma - Waziri Mkuu

    Raia wa Rwanda na wakazi lazima wawe wamepewa chanjo kamili dhidi ya Covid ili kuruhusiwa kufika maeneo ya umma, taarifa iliyotolewa na Waziri Mkuu inasema.

    Amri ya kutotoka nje usiku itaanza saa sita usiku, na vilabu vya usiku na matamasha ya muziki yamepangwa kufunguliwa tena.

    Takriban watu milioni saba kati ya milioni 13 wamechanjwa kikamilifu nchini Rwanda, wakati zaidi ya watu milioni nane wamepata chanjo ya kwanza.

    Rwanda ni mojawapo nchi za Afrika zilizo na viwango vya juu vya watu waliochanjwa ikilinganishwa na idadi ya watu wake, na ya kwanza katika Afrika Mashariki.

    Lakini uamuzi wa Jumatano usiku unamaanisha kuwa mamilioni ya watu bado wanahitaji kupata chanjoya pili ili kufikia maeneo ya umma.

    Ingawa chanjo ni ya hiari, kumekuwa na ripoti za watu kupewa chanjo kwa lazima, na wengine wamekimbilia nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi ili kuepuka chanjo.

    Msemaji wa serikali alikiri kwa shirika la utangazaji la Ufaransa, RFI, kwamba baadhi ya mamlaka "zinaweza kuwa na bidii sana" katika kampeni zao lakini haikuwa sera ya serikali.

  7. Shabiki maarufu wa Kenya auawa

    Wakenya wanaomboleza kifo cha shabiki maarufu ambaye amekuwa akiuchora mwili wake kwa rangi mbali mbali wakati wa mechi.

    Isaac Juma alidungwa kisu nyumbani kwao katika eneo la magharibi mwa Kenya Jumatano usiku, kulingana na vyombo vya habari .

    Bw Juma alifahamika sana kwa kutumia mwili wake kama sanamu wakati wa mechi nchini kenya.

    Aliwahi kusafiri nje ya nchi na timu ya taifa.

    Katika mahojiano na televisheni ya Citizen nchini humo mwaka 2018, alisema ana matumaini kwamba timu ya Kenya itafuzu kwa mechi za Afcon ambazo kwa sasa zinaendelea nchini Cameroon.

    Wakenya kwenye mitandao ya kijamii wamekuwa wakimkumbuka jina lake maarufu- Kenya One, kama alivyofahamiwa na mashabiki wake.

    "Ulikuwa mtu mwema, mchangamfu na uliburudisha‘’ , alisema Abu Rumi kwenye ujumbe wake wa Twitter.

    "Tutakukosa kusema kweli uungaji mkono wako ambao haukuyumba kwa soka ya Kenya, Omwami. Ulikuwa mfuasi aliyejitolea! Ulale salama !," @SallyBolo aliandika.

  8. Rais wa Zambia akosolewa kwa safari za nje za 'mara kwa mara'

    Rais wa Zambia Hakainde Hichilema ameshambuliwa na upinzani kutokana na safari zake za mara kwa mara nje ya nchi.

    Bw Hichilema Jumatano alifanya safari yake ya tisa nje ya nchi tangu achukue wadhifa huo mwezi Agosti. Safari yake ya hivi punde zaidi ni ziara ya siku mbili nchini Afrika Kusini kwa mazungumzo na mwenzake Cyril Ramaphosa pamoja na kuhudhuria uzinduzi wa kitabu.

    Lakini chama cha upinzani cha Kisoshalisti kimetilia shaka safari hiyo baada ya mkutano wake na Bw Ramaphosa kutajwa kuwa wa kawaida.

    "Kwa hiyo, ni nini hasa madhumuni ya safari ya Rais Hichilema nchini Afrika Kusini ikiwa mkutano na Rais Ramaphosa ni wa kawaida tu? Je, mkutano na Rais Ramaphosa ni kificho tu cha shughuli zake binafsi?" Rais wa Chama cha Kisoshalisti Fred M’membe aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.

    Hata hivyo, Bw Hichilema alielezea safari yake katika msururu wa machapisho kwenye mtandao wa Facebook.

    Alithibitisha kufanya mazungumzo baina ya nchi hizo mbili na Bw Ramaphosa ambayo yalilenga "maendeleo, amani na usalama wa kikanda na kuimarisha uhusiano wetu wa kiuchumi na baina ya nchi mbili".

    Pia alithibitisha kushiriki katika uzinduzi wa kitabu kilichoandikwa na Greg Mills, kiitwacho Expensive Poverty, Why Aid Fails And And How It Can Work.

    Akiwa katika upinzani, Bw Hichilema mara nyingi alikosoa safari za nje zinazofanywa na mtangulizi wake Edgar Lungu.

  9. Ndovu amkanyaga mtalii hadi kumuua nchini Uganda

    Mtalii amekanyagwa hadi kuuawa na ndovu katika mbuga ya Wanyama nchini Uganda baada ya kuondoka kwenye gari alilokuwa akisafiria.

    Marehemu, amaye ni raia waSaudia, alikuwa akipita kwnye mbuga ya taifa ya wanyama ya Murchison Falls National Park iliyopo katika jiji la Arua pamoja na wenzake wakati waliposimama kujisaidia.

    Kundi la ndovu waliokuwa na hasira kwa watalii hao na marehemu, ambaye alikuwa amekwenda mbali zaidi ya gari, hakuweza kurejea.

    Tukio hilo lilitokea Jumanne usiku lakini liliripotiwa Jumatano.

    Maafisa wa mbuga ya Wanyama walithibitisha tukio hilo na walisema upelelezi unaendelea.

    Walisema kuwa hatua zinachukuliwa kuzuwia matukio ya aina hiyo kutokea tena.

    Mahsmabulio ya Wanyama yamekuwa yakiripotiwa katika kipindi cha nyuma katika mbuga za Wanyama za Uganda.

  10. Roketi ya Elon Musk SpaceX inaelekea kugongana na mwezi

    Roketi iliyorushwa na kampuni ya uvumbuzi wa anga za juu ya bilionea Elon Musk inakaribia kugonga ndani ya mwezi na kulipuka.

    Chombo kinachosaidia roketi kulipuka kwa Falcon 9 kilikwenda katika anga za juu mwaka 2015, lakini baada ya kukamilisha safari yake, hakikuwa na mafuta ya kutosha ya kukirejesha duniania na badala yake kilibakia katika anga za juu.

    Mtaalamu wa masuala ya anga za juu Jonathan McDowell ameiambia BBC News kuwa itakuwa mara ya kwanza kwa roketi isiyoongozwa kugongana na mwezi.

    Lakini anasema athari yake itakuwa ndogo.

    Roketi hiyo iliachwa katika obit ya juu miaka saba iliyopita baada ya kukamilisha kazi ya kutuma setilaiti ya hali ya hewa katika safari ya maili milioni.

    Ilikuwa ni sehemu ya mpango wa uvumbuzi wa anga za juu wa Bw Musk - SpaceX, ambayo ni kampuni ya kibinafsi ambayo lengo lake kuu ni kuwawezesha binadamu kuishi katika sayari nyingine.

    • Elon Musk: Fahamu siri sita za ufanisi wa kibiashara kutoka kwa mtu tajiri zaidi duniani
    • Mpango wa kupeleka watu wakaishi Mars
    • Jeff Bezos: Fahamu safari ya dakika 11 kwenda angani iliofanywa na bilionea
  11. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya mubashara kwa leo tarehe 27.01.2022