Polisi nchini Nigeria wawakamata watu 4 kwa ''kula nyama ya watu''

Washukiwa hao walikamatwa baada ya maafisa wa upelelezi kupata maiti katika jengo ambalo halijakamilika huku baadhi ya sehemu za mwili zikiwa zimetolewa.

Moja kwa moja

  1. Mpaka hapa tumefika mwisho wa matangazo ya moja kwa moja ya kurasa wetu wa BBC Swahili, Wikiendi njema

  2. Watu watatu wauawa na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Kiislamu Msumbiji

    Watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Kiislamu wamewaua watu watatu katika wilaya ya Nangade na Ibo katika mashambulizi kaskazini mwa jimbo la Cabo Delgado ambayo yamesababisha watu wengine wengi kukimbia makazi yao, ripoti zinasema.

    Mali zinadaiwa kuharibiwa huko Ibo, na samaki kuibwa.

    Licha ya mamlaka kujitolea kuweka wanajeshi kutoka Rwanda na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) katika eneo hilo, pamoja na tangazo la kuharibiwa kwa ngome kuu za wanajihadi, vikundi vidogo vya wanamgambo hao vinaendelea kushambulia sehemu ya jimbo hilo.

  3. Uganda kuteketeza dozi 400,000 za chanjo za covid

    m

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Uganda inatarajia kuteketeza chanjo 400,000 za virusi vya corona ambazo hazijatumika, zilizokuwa zimetolewa kwa matumizi kaskazini mwa nchi hiyo.

    Dozi nyingi ambazo hazijatumika ni Moderna na Astrazeneca.

    Dozi hizo zinatajwa kuisha muda wake, kwa mujibu wa gazeti la mtandaoni la Uganda, Monitor.

    Hatua hii inakuja wakati nchi imefikia chini ya nusu la lengo lake la kutoa chanjo kwa watu milioni 22, chanzo hicho hicho kilisema.

    "Moderna imeganda sana - inapaswa kuyeyushwa. Kabla ya matumizi, wakati haikutumika huko Acholi tuliipeleka hadi Magharibi mwa Uganda lakini hatukuweza kuitumia kabla ya siku 30," tovuti ya habari nchini Uganda Nile Post inamnukuu Waziri wa Afya Jane Aceng alisema.

    Alihusisha uchukuaji mdogo wa chanjo na taarifa za kusadikika za kiafya, iliendelea.

  4. Ethiopia yakataa kumuunga mkono bosi wa WHO kwa madai ya ‘kuunga mkono’ TPLF

    m

    Ethiopia ilisema jana kuwa haitaunga mkono kuchagulia tena kwa Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus wa taifa hilo kwa muhula wa pili kama mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), huku ikimtuhumu kuunga mkono kundi lililopigwa marufuku.

    Katika barua ya Bodi ya Utendaji ya WHO, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia ilisema Dkt. Tedros, mwenyewe kama waziri wa zamani wa mambo ya nje, anatishia uadilifu wa shirika la WHO kwa sababu amejiunga na kundi lililopigwa marufuku katika nchi yake ya asili.

    "Hajafikia uadilifu na matarajio ya kitaaluma yanayohitajika kutoka kwa afisi na wadhifa wake," ilisema barua hiyo iliyotumwa kwa Bodi, ambayo kwa sasa inaongozwa na Dkt Patrick Amoth, Daktari wa Uzazi na Magonjwa ya Wanawake na Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya ya Kenya.

    "Amekuwa akiingilia masuala ya ndani ya Ethiopia, ikiwa ni pamoja na uhusiano wa Ethiopia na jimbo la Eritrea ... anaendelea kama mwanachama hai na mfuasi wa TPLF ambalo linatajwa kama kundi la kigaidi na bunge la Ethiopia.

    " Ethiopia ilisema inataka Bodi, chombo chenye wanachama 34 wa WHO, kuchunguza mienendo ya Dk Tedros kwa kukiuka "wajibu wake wa kitaalamu na kisheria."

  5. Man Utd lazima wamalize katika nafasi tatu za juu, asema Ronaldo

    m

    Cristiano Ronaldo anasema kumaliza nje ya nafasi tatu za juu kwenye Ligi ya Premia halitakubalika kwa Manchester United huku Ralf Rangnick akihangaika kuibadilisha timu yake ambayo haikufanya vizuri.

    Bosi huyo wa muda wa Ujerumani ameimarisha kikosi chake kichukue mikoba kutoka kwa Ole Gunnar Solskjaer aliyetimuliwa lakini United wako katika nafasi ya saba, pointi 22 nyuma ya viongozi Manchester City.

    Mchezaji bora wa dunia mara tano Ronaldo ametoa wito wa kubadilishwa kwa fikra ndani ya chumba cha kubadilishia nguo ili kushughulikia hali mbaya ya United, ambayo ilisababisha kupoteza kwa bao 1-0 kutoka kwa Wolves katika mechi yao ya hivi karibuni ya ligi.

    "Manchester United inapaswa kushinda ligi au iwe ya pili au ya tatu," aliiambia Sky Sports.

    "Sioni nafasi nyingine kwa Manchester United. "Moyoni mwangu, sikubali kwamba mawazo yetu yawe chini ya kuwa katika nafasi tatu za juu kwenye Ligi Kuu, kwa maoni yangu.

    "Nadhani ili kujenga mambo mazuri wakati mwingine lazima uharibu vitu vichache. Mwaka mpya, maisha mapya, natumani Manchester inaweza kuwa katika kiwango ambacho watu wanataka, haswa mashabiki. Tuna uwezo wa kubadilisha mambo sasa.

  6. Mahakama yamsafisha askofu kwa mashtaka ya ubakaji wa mtawa, India

    m

    Mahakama ya India imemuondolea mashtaka askofu mmoja aliyeshtakiwa kwa kumbaka mtawa mmoja kati ya mwaka wa 2014 na 2016 katika kesi ambayo ilishtua jumuiya kongwe za Kikristo nchini humo.

    Franco Mulakkal, mwenye umri wa miaka 54, alikamatwa kutoka jimbo la kusini la Kerala mwaka wa 2018.

    Alikuwa amekanusha madai hayo.

    Kesi hiyo ilizua maandamano makubwa baada ya mtawa huyo kudai kuwa Kanisa Katoliki lilipuuza malalamishi yake.

    Vatikani ilikuwa imemwondolea askofu kazi zake kwa muda.

    Siku ya Ijumaa, mahakama ya mjini Kottayam ya Kerala ilimkuta hana hatia ya mashtaka. "Upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka yote dhidi ya mshtakiwa," alisema Jaji wa vikao vya ziada vya Kottayam (ASJ) G Gopakumar.

    Mawakili wa mtawa huyo walisema watapinga uamuzi huo katika mahakama kuu.

    Lakini timu ya wanasheria ya askofu huyo ilisema "imesambaratisha ushahidi wote" dhidi yake. "

    Ni kesi yenye changamoto kubwa. Ni lazima ipelekwe kwenye mahakama kuu. Ni sawa," Raman Pillai, ambaye aliongoza timu ya utetezi ya Bw Mulakkal, aliambia BBC Hindi.

    "Lakini mahakama ilisema hakuwa na hatia. Ni wazi, ushahidi ambao ulitolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka ulitupiliwa mbali. Hii ina maana kwamba shtaka lilikuwa la uongo. Hakukuwa na ubakaji hata kidogo," aliongeza.

    Bw Mulakkal alikuwa askofu wa dayosisi ya Jalandhar katika jimbo la kaskazini la Punjab.

    Mshitaki wake ni wa Wamisionari wa Yesu, huko Kerala ambalo ni sehemu ya dayosisi ya Jalandhar. Alidai kuwa askofu huyo alimbaka mara 13 na mashambulizi hayo yalitokea alipotembelea nyumba ya watawa alikokuwa akiishi katika jiji la Kottayam, Kerala.

  7. DRC yawafukuza Wanyarwanda waliotoroka chanjo ya Covid-19

    m

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Takriban Wanyarwanda 100 ambao walikimbilia kisiwa kilichopo Ziwa Kivu katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kuepuka kupata chanjo za Covid wamerudishwa nchini kwao

    Hata hvyo watu wawili wanadaiwa kutoonekana katika kundi hilo la Wanyarwanda 101 huku operesheni ya kuwasaka inaendelea.

    Afisa wa Kisiwa cha Idjwi, Roger Ntambuka, aliiambia BBC kwamba mamlaka iliweza kufanya mazungumzo na Wanyarwanda hao ili kuwarejea nyumbani kwao.

    "Hakukuwa na sababu ya Wanyarwanda hawa kubaki hapa. Tuliweza kuwashawishi," alisema.

    m

    Chanzo cha picha, AFP

    Alisema raia hao wa Rwanda , ambao ni wanawake, wanaume na watoto, waliondoka kuelekea nyumbani kwa boti.

    Gavana wa jimbo la magharibi mwa Rwanda alisema hakuwa na habari kuhusu Wanyarwanda waliokimbia na haijabainika kama mamlaka ilihusika katika kuwarejesha nchini kwao.

    Wiki iliyopita mamlaka ya Burundi iliwafukuza zaidi ya Wanyarwanda 10 waliokuwa wameingia nchini humo kukwepa chanjo ya lazima ya corona na kuwarudisha nyumbani.

    Raia wa Rwanda lazima wapewe chanjo ili kuruhusiwa kutumia usafiri wa umma, kwenda kwenye maeneo ya starehe(bar) na migahawa au kuhudhuria hafla za umma.

  8. Habari za hivi punde, Australia yafuta visa ya Novak Djokovic

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Australia imefutilia mbali visa ya nyota wa tenisi Novak Djokovic kwa mara ya pili mfululizo kuhusu haki yake ya kusalia nchini humo bila chanjo.

    Uamuzi wa Waziri wa Uhamiaji Alex Hawke unamaanisha kuwa Djokovic sasa anakabiliwa na hatari ya kufukuzwa nchini humo.

    Hata hivyo, Mserbia huyo mwenye umri wa miaka 34 bado anaweza kukata rufaa nyingine ya kisheria kubaki nchini humo.

    Mcheza huyo wa tenisi nambari moja kwa upande wa wanaume alipangiwa kucheza katika mashindano ya wazi ya Australian Open, yatakayoanza Jumatatu.

    "Leo nimetumia uwezo wangu... kufuta visa aliyokuwa nayo Bw Novak Djokovic kwa misingi ya afya na utaratibu mzuri, kwa msingi kwamba ilikuwa ni kwa manufaa ya umma kufanya hivyo," waziri huyo alisema katika taarifa yake.

    Hatua hiyo pia inamaanisha Djokovic huenda akakabiliwa na marufuku ya miaka mitatu ya kupata visa mpya ya Australia.

    Visa ya Djokovic ilifutwa kwa mara ya kwanza muda mfupi baada ya kuwasili Melbourne tarehe 6 Januari, baada ya maafisa wa Kikosi cha mpaka wa Australia kusema "ameshindwa kutoa ushahidi ufaao" ili kupokea msamaha wa chanjo.

    Kulikuwa pia na msukosuko mkubwa kutoka kwa baadhi ya Waaustralia, ambao wameishi chini ya vizuizi virefu na vikali vya Covid, kwamba Djokovic alikuwa ameruhusiwa kuingia licha ya kutokuwa na chanjo.

  9. Dwarka: Jiji la kale la India lililozama baharini

    TH

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mji wa kale wa India wa Dwarka, unasemekana kuzama chini ya Bahari ya Arabia. Sasa, wanaakiolojia wa chini ya maji wanatafuta misingi ya kuta zake za jiji ili kuthibitisha kuwepo kwake.

    moja ya vituo saba vya hija takatifu nchini India, mji wa Dwarka sio tu wa umuhimu wa kidini, bali pia wa akiolojia.

    Umwilisho wa zamani wa jiji hilo, unaojulikana katika Epic Mahabharata kama ufalme wa kale wa Krishna, ulienea karibu kilomita 84 kama jiji lenye ngome ambapo Mto Gomti na Bahari ya Arabia hukutana. Kulingana na maandishi, jiji hilo la zamani lilizama chini ya Bahari ya Arabia baada ya kifo cha Krishna.

    Katika nusu ya pili ya karne iliyopita, wanaakiolojia walifanya majaribio ya kupata uthibitisho wa kimwili wa jiji lililozama karibu na pwani ya Dwarka ya kisasa ili waweze kuthibitisha kuwepo kwake bila shaka.

    Matokeo yake, vitu vingi vya kale vimegunduliwa chini ya maji kama vile mawe na nguzo; hata hivyo, umri kamili wa matokeo haya bado unajadiliwa. Sasa, wanakiolojia wanapanga kuchimba chini ya maji ili kutafuta misingi ya kuta za jiji la kale. Iwapo watapata eneo kamili la makazi hayo, litakuwa na umuhimu mkubwa wa kihistoria kwa India.

  10. Wanyarwanda waliotoroka chanjo ya Covid nchini mwao wamerejeshwa nyumbani

    th

    Chanzo cha picha, AFP VIA GETTY IMAGES

    Mfalme wa Kisiwa cha Ijwi huko Kivu Kusini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo anasema Wanyarwanda zaidi ya 100 waliokuwa wamekimbia nchi yao kukwepa chanjo ya Covid-19 walirejeshwa nchini Rwanda siku ya Alhamisi.

    Katika mahojiano na BBC, Mfalme Roger Ntambuka alisema wameweza kuwashawishi kurejea nyumbani, waliyokuwa wamesafiri kuanzia mwendo wa saa kumi na moja jioni, katika mashua waliyopangiwa, pamoja na wajumbe waliofuatana nao.

    "Hakukuwa na sababu ya Wanyarwanda hawa kubaki hapa. Tuliweza kuwashawishi," aliongeza. Alisema raia hao walikuwa ni pamoja na watoto, wanawake na wanaume.

  11. Polisi nchini Nigeria wawakamata watu 4 kwa ''kula nyama ya watu''

    TH

    Chanzo cha picha, NIGERIA POLICE

    Polisi katika jimbo la Zamfara kaskazini-magharibi mwa Nigeria wanasema wamewakamata watu wanne wanaodaiwa kuhusika na ulaji nyama za watu na kuuza sehemu za binadamu- jambo ambalo ni nadra sana katika eneo hilo.

    Kamishna wa polisi katika jimbo hilo Ayuba Elkanah aliwaambia waandishi wa habari katika mji mkuu Gusau siku ya Alhamisi kwamba washukiwa hao walikamatwa baada ya maafisa wa upelelezi kupata maiti katika jengo ambalo halijakamilika huku baadhi ya sehemu za mwili zikiwa zimetolewa.

    Ilikuwa ni katika harakati za kufanya uchunguzi wa kupotea kwa mvulana wa miaka tisa. Washukiwa hao wakiwemo wanaume wawili na wavulana wawili walikamatwa wiki iliyopita, kulingana na mkuu wa polisi, na kwamba washukiwa wengine wa genge hilo wanasakwa.

    Mkuu huyo wa polisi alisema hadi sasa uchunguzi umebaini kuwa mara mbili kiongozi wa genge hilo aliwalipa washukiwa wengine watatu kiasi cha Naira Laki Tano (sawa na $1,207) kwa ajili ya sehemu za binadamu.

    Kuhusika na uuzaji wa sehemu za binadamu na ulaji nyama si jambo la kawaida katika jimbo la Zamfara. Lakini ni moja wapo ya maeneo ya Nigeria yaliyokumbwa zaidi na wimbi la mauaji na utekaji nyara kwa ajili ya fidia na magenge yenye silaha huku mamlaka zikikabiliwa na ukosoaji kwa kushindwa kukabiliana na ghasia hizo.

    Hata hivyo, wakati wa mkutano na waandishi wa habari Alhamisi kamishna wa polisi Ayuba Elkanah alisema vikosi vya usalama pia vimewaokoa watu kumi na saba waliotekwa nyara hapo awali kutoka jimbo jirani la Niger na kupelekwa Zamfara.

    Alisema vikosi vya usalama vilivyokuwa kwenye doria pia vimefanikiwa kupata baadhi ya silaha ikiwa ni pamoja na vifaa vya kurusha roketi kutoka kwa genge moja baada ya makabiliano ya risasi karibu na msitu.

    Wiki iliyopita, takriban watu 200 waliripotiwa kuuawa wakati wa msururu wa uvamizi katika vijiji kadhaa jimboni humo.