Rwanda: Maafisa wa zamani wa waasi wa FDLR wahukumiwa kifungo cha miaka 10 jela
- Author, Yves Bucyana
- Nafasi, BBC Swahili
Mahakama mjini Nyanza imewahukumu Ignace Nkaka (La Forge Fils Bazeye), msemaji wa zamani wa FDLR, na Lt Kanali Jean Pierre Nsekanabo (Abega), afisa wa zamani wa upelelezi, kifungo cha miaka 10 jela.
Mahakama iliwapata na hatia ya kuwa wanachama wa shirika la kigaidi, ingawa wakati wa vikao vya kesi walikiri kuwa katika kundi la waasi bila kujua ni kundi la kigaidi.
Mnamo tarehe 12/2018, wawili hao walikamatwa kwenye mpaka wa Bunagana baina ya Uganda na DR Congo wakitokeana mjini Kampala kwa tuhuma za kushiri mkutano wa kuvuruga usalama wa Rwanda.
Kesi yao imekuwa ikiendelea kwa zaidi ya miaka miwili.
Walishtakiwa kwa makosa ya jinai ikiwa ni pamoja na kuwa katika kundi haramu la kijeshi lenye lengo la kuangusha utawala wa Rwanda ,na kufanya mauaji ya wananchi.
Mahakama haikuwakuta na hatia kwa mashtaka hayo.Jaji amesema kwamba hata ingawa mwendeshamashtaka alisema kwamba walikuwa katika ngazi za juu za FDLR lakini hawakuwa katika nafasi ya kuchukua maamuzi yoyote kuhusu mipango ya kundi hilo ya kuhujumu usalama wa Rwanda.
Kundi la FDLR lilikiri kuhusika na mashambulio kadha wa kadha dhidi ya Rwanda kwanzia mwaka 98 hadi 2012 ambapo watu wengi walipoteza maisha yao,na mali nyingi kuteketezwa.
Awali waasi hao wa zamani wa FDLR waliomba mahakama kuwaachilia huru na kuwarudisha katika maisha ya kawaida kama ilivyotokea kwa waliokuwa wapiganaji wengine wa FDLR waliorejea Rwanda baadhi wakawekwa katika taasisi za serikali pamoja na jeshi la taifa.
Kuhusu hilo,mahakama imesema wao hawakurudi nchini Rwanda kwa hiari yao kama ilivyokuwa kwa wapiganaji wengine.
Jaji wa mahakama amesema wamepunguziwa adhabu na kuhukumiwa kifungo cha miaka 10 jela kutokana na wao kurahisishia vyombo vya sheria katika kesi hiyo pamoja na kutoa taarifa muhimu kwa vyombo vya usalama kuhusu hali ya makundi ya waasi mashariki mwa DR-Congo.
Ignace Nkaka maarufu kama La Forge Fils Bazeye aliyekuwa msemaji wa kundi la FDLR na Luteni Kanali Jean Pierre Nsekanabo maarufu Abega Camara hawakupwepo mahakamani na mawakili wao hukumu hiyo ilipotolewa.Mahakama imesema wana siku 30 za kukata rufaa.