Hekalu la miaka 4,500- lililopotea lapatikana Misri

Wanaakiolojia nchini Misri wanasema wamepata moja ya uvumbuzi muhimu zaidi katika miongo kadhaa.

Moja kwa moja

Ambia Hirsi

  1. Mpaka hapa tumefikia mwisho wa matangazo ya moja kwa moja ya ukurasa wa BBC Swahili, tukutane tena hapo kesho.

  2. Nato yaionya Urusi dhidi ya uvamizi wa kijeshi Ukraine

    Wanajeshi wa Urusi

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Urusi

    Mkuu wa Nato ameitaka Urusi kuwa wazi kuhusu mipango yake ya kijeshi kufuatia hatua yake ya kuongeza idadi ya wanajeshi katika mpaka wake na Ukraine.

    Jens Stoltenberg alisema kwamba idadi kubwa ya wanajeshi imeonekana katika mpaka wa taifa hilo na jirani yake Ukraine katika wiki za hivi karibuni.

    Alizungumza huku kukiwa na madai kwamba Urusi huenda inapanga kuivamia Ukraine.

    Moscow imepinga madai hayo na kulalamika kuhusu ongezeko la vitendo vya NATO katika eneo hilo.

    Akizungumza baada ya mazungumzo na waziri wa masuala ya kigeni wa Ukraine mjini Brussels, bwana Stoltenberg alisema kwamba kitu muhimu ni kuzuia hali ya wasiwasi kusambaa na kutodhibitika.

    Aliionya Urusi dhidi ya kuchukua uamuzi wowote wa uchokozi

    Bwana Stoltenberg alisema: Tunaona idadi kubwa ya wanajeshi isiyo kuwa ya kawaida , na tunajua kwamba Urusi imetaka kutumia uwezo wake kama huo awali kutekeleza vitendo vya uchokozi dhidi ya Ukraine.."

  3. Polisi wakutwa na hatia dhidi ya mauaji ya raia wa Uingereza nchini Kenya

    Family

    Chanzo cha picha, Alexander Family

    Mahakama ya Mombasa imetoa hukumu kuwa maofisa wanne wa polisi wana hatia ya kuua bila ya kukusudia katika kesi ya raia wa Uingereza Alexander Monson ambaye alikufa akiwa kizuizini huko Diani, mwaka 2012.

    Maofisa hao walikuwa mahakamani , kufuatia kesi hiyo ya mauji ya Alexander Monson, raia wa Uingereza, ambaye alikutwa amefariki karibu miaka 10 iliyopita akiwa mikononi mwa polisi katika mji wa pwani wa Diani.

    Jaji ametoa hukumu kuwa bwana Monson aliteswa na watu wasiofahamika nje ya gereza, lakini ndani ya mazingira ya mahakama.

    Watu hao wanafahamika na walalamikaji, na jaji hajaweza kuwajua na kusema kwa kuwa kuna sheria inayowata jeshi la polisi kuwa kimya.

    Maafisa hao wa polisi walifikishwa mahakamani mapema mwaka huu, baada ya kubainika kuwa Bw Monson alifariki baada ya kupigwa akiwa kizuizini na wala si kutokana na kutumia dawa za kulevya kupita kiasi kama polisi walivyodai awali.

    Bw Monson, ambaye wakati huo alikuwa na miaka 28, alikuwa mwana wa 12 wa Baron Monson na mrithi wa mali ya familia huko Lincolnshire, na alikuwa akiishi na mamake huko Diani, Kenya alipofariki.

    Baba yake, Lord Nicholas Monson, mtu wa tabaka la juu nchini Uingereza, ambaye aliwasili Kenya mwishoni mwa wiki iliyopita na kuhudhuria uamuzi wa mahakama.

  4. Zaidi ya watoto 6000 walikabiliwa na unyanyasaji Tanzania katika kipindi cha miezi tisa mwaka huu

    N

    Naibu waziri wa mambo ya ndani wa nchini Tanzania Khamis Chilo amelifahamisha Bunge la nchi hiyo kwamba jumla ya watoto 6,168 wa Tanzania walikabiliwa na aina tofauti za unyanyasaji kati ya Januari na Septemba mwaka 2021.

    Bw. Chiko alikuwa akijibu swali la Mbunge wa viti maalum Bi Esther Matiko siku ya Ijumaa ambaye alitaka kujua idadi ya watoto na waathirika wa ghasia nchini Tanzania katika kipindi hicho.

    Katika jibu lake, Bw Chilo alisema kati ya 6168 walioathirika wanawake walikuwa 5287 na wanaume wakiwa 881 akiongezea kwamba 3524 kati yao walibakwa huku 637 wakilawitiwa

    Bw. Chiko alisema karibu washukiwa 3,800 wamekamatwa na kesi 2,368 zinaendelea katika mahakama tofauti nchini na hukumu za kesi 88 zimetolewa.

    • Kwanini watoto wako wapo hatarini katika mtandao?
  5. Mwendesha mashtaka wa Libya apinga nia ya urais wa mwana wa Gaddafi kugombea urais

    Lakini bodi ya uchaguzi ilisema Saif al-Islam Gaddafi alikuwa amewasilisha nyaraka zote muhimu

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Lakini Tume ya uchaguzi ilisema Saif al-Islam Gaddafi alikuwa amewasilisha nyaraka zote muhimu

    Mwendesha mashtaka wa kijeshi nchini Libya, Mohamed Gharouda, ametaka mamlaka ya uchaguzi kusitisha utayarishaji wa makaratasi ya ugombea urais wa Saif al-Islam Gaddafi, mwana wa marehemu mtawala wa nchi hiyo Muammar Gaddafi.

    Mwendesha mashtaka pia aliomba ukaguzi wa makaratasi ya mbabe wa kivita Khalifa Haftar - ambaye pia anatafuta urais - usitishwe.

    Tume ya uchaguzi Jumapili ilisema kuwa Bw Gaddafi aliwasilisha stakabadhi muhimu kama mgombeaji urais katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi ujao.

    Lakini katika barua kwa tume ya uchaguzi, Bw Gharoda alionya kuwa tume hiyo itawajibikia matokeo ikiwa utayarishaji wa karatasi hautasitishwa.

    "Saif al-Islam na Khalifa Haftar wametuhumiwa kwa vitendo vya uhalifu" na maombi yao ya kugombea urais "lazima yakomeshwe hadi uchunguzi ukamilike," ofisi ya mwanasheria mkuu wa kijeshi inasema katika barua.

    Kujiandikisha kugombea kwa Bw Gaddafi, ingawa kulitarajiwa, kumewashtua watu nchini Libya na nje ya nchi kwa jukumu lake katika ukandamizaji wa kikatili wa uasi dhidi ya utawala wa babake.

    Bado anasakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwa tuhuma za uhalifu wa kivita uliofanywa mwaka 2011.

    Bw Haftar, ambaye anaongoza majeshi mashariki mwa Libya, anasakwa na mahakama ya Marekani kwa madai ya kuwatesa Walibya wakati wa vita.

  6. Wanawake wa Australia washtaki Qatar kwa upekuzi wa kuwavua nguo uwanja wa ndege

    Wanawake hao walitolewa kwenye ndege ya Qatar Airways huko Doha mwaka jana (picha ya faili)

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Wanawake hao walitolewa kwenye ndege ya Qatar Airways huko Doha mwaka jana (picha ya maktaba)

    Kundi la wanawake wa Australia ambao walivuliwa nguo na kupekuliwa katika uwanja wa ndege wa Doha wanaishtaki mamlaka nchini Qatar.

    Wanawake hao waliamriwa kuondoka kwenye ndege na kuchunguzwa iwapo walikuwa wamejifungua baada ya mtoto kupatikana kwenye pipa kwenye Uwanja wa Ndege wa Hamad Oktoba 2020.

    Walielezea kisa hicho kama shambulio lililoidhinishwa na serikali na tukio hilo lilizua ghadhabu kubwa.

    Baadaye Qatar iliomba msamaha na afisa mmoja wa uwanja wa ndege kupewa hukumu iliyosimamishwa jela.

    Lakini wanawake hao wanasema kesi zao zimepuuzwa.

    Walitolewa kwenye ndege ya Qatar Airways na walinzi waliokuwa na silaha kabla ya kuingizwa kwenye gari la wagonjwa kwenye lami ambapo walikaguliwa na wauguzi.

    Wanawake hao walisema hawakuridhia uchunguzi huo na hawakupewa maelezo ya kile kinachowatokea.

    Mmoja wa wanawake hao, ambaye hakutaka jina lake litajwe, aliiambia BBC kwamba "alifanyiwa uchunguzi wa kutisha zaidi wa kimwili".

    "Nilikuwa na hakika kwamba ningeuawa na mmoja wa wanaume waliokuwa na bunduki, au mume wangu angeuawa," alisema katika taarifa kutoka kwa wakili wake.

    Uchunguzi huo ulichukua kama dakika tano kabla ya kusindikizwa kurudi kwenye ndege yao.

    Wanawake kadhaa waliripoti kisa hicho kwa polisi baada ya kutua Australia, jambo lililozua hisia za umma na kulaaniwa na mataifa kadhaa.

  7. Kombe la Dunia 2022: Afrika Kusini 'iliyoibiwa' yataka mchezo wa marudiano na Ghana

    Wachezaji wa timu ya taifa ya Arika Kusini

    Shirikisho la Soka la Afrika Kusini (Safa) linatarajiwa kwasilisha malalamishi rasmi kwa Shirikisho la Soka Duniani FIFA kuhusu uchezeshaji wa mwamuzi katika mechi yao ya kufuzu kwa Kombe la Dunia dhidi ya Ghana Jumapili usiku.

    Ikihitaji sare ili kufika raundi ya tatu na ya mwisho ya kufuzu kwa Afrika, Afrika Kusini ilipoteza 1-0 baada ya Ghana kupiga penalti iliyozua utata.

    Ushindi huo mdogo wa Black Stars uliwawezesha kufuzu kwa hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia la Afrika kwa tofauti ndogo, na kuwaondoa Afrika Kusini kileleni mwa kundi hilo kwa idadi ya mabao.

    Mkwaju huo wa penalti ulitolewa baada ya kiungo wa Leicester City na Ghana, Daniel Amartey kuanguka kufuatia kile kinachosemekana kugongwa kidogo na mlinzi Rushine de Reuck, ambaye alilishwa kadi kwa ajili ya kosa hilo.

    "Tutawaandikia Caf [Shirikisho la Soka la Afrika] na Fifa - kwanza kuchunguza jinsi mchezo ulivyoendeshwa na pili kupinga baadhi ya maamuzi haya," Mkurugenzi Mtendaji wa Safa Tebogo Mothlante alisema Jumatatu.

    "Kama tulivyofanya jana usiku, tayari tumemfahamisha kamishna wa mechi kwamba tutawasilisha malalamiko rasmi."

  8. Hekalu la miaka 4,500- lililopotea lapatikana Misri

    Hekalu la kali

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wanaakiolojia nchini Misri wanasema wamepata moja ya uvumbuzi muhimu zaidi katika miongo kadhaa.

    Wamepata mojawapo ya mahekalu manne ya jua yaliyopotea na yaliyojengwa na mafarao wakiwa bado hai katika jaribio la kujigeuza kuwa miungu hai.

    Inaaminika kwamba mahekalu sita tu ya jua yalijengwa na mafarao wa Misri miaka 4,500 hivi iliyopita.

    Ni mbili tu kati ya hizo sita zimegunduliwa hadi sasa, kwa hivyo wanaakiolojia wanaelezea ugunduzi wa muundo wa tatu kama huo kuwa uvumbuzi mkubwa zaidi ndani ya miaka 50.

    Lilikuwa katika eneo la Abu Gorab kusini mwa Cairo na lingekuwa na ukubwa mbao umelingana kikamilifu na upinde wa mashariki-magharibi wa jua.

    Ingawa piramidi kubwa ziliundwa ili kuhakikisha hadhi ya farao kama mungu katika maisha ya baada ya kifo, mahekalu ya jua yalikuwa miundo midogo na ilikusudiwa kuwaweka kama miungu hai.

    Soma:

    • Kaburi la mwana wa Pharaoh lapatikana Misri
    • Misri yagundua makaburi ya kale yenye miili huko Luxor
    • Miili iliyohifadhiwa kwenye kaburi karne ya 16 yagunduliwa Misri
  9. Mwanafunzi wa Nigeria atuhumiwa kumpiga mhadhiri hadi kukosa fahamu

    Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ilorin nchini Nigeria amezuiliwa na polisi baada ya shutuma za kumpiga mhadhiri wa kike.

    Polisi wanasema mwanafunzi huyo alikuwa ameenda kumuona msimamizi kuhusu kazi yake ya mwaka wa mwisho wa mradi wakati kutoelewana kulipotokea.

    Inadaiwa alimvamia mhadhiri huyo ambaye alipata jeraha kichwani na kuzimia.

    Mhadhiri huyo amelazwa katika hospitali isiyojulikana huku mwanafunzi huyo akizuiliwa na polisi.

    Msemaji wa chuo hicho Kunle Akogun alithibitisha kisa hicho katika taarifa iliyowasilishwa kwa vyombo vya habari siku ya Jumapili.

    Alisema mhadhiri huyo anaendelea kupata nafuu.

  10. Mahakama ya Kenya kutoa uamuzi kuhusu mauaji ya raia wa Uingereza

    Alexander Monson alikuwa akiishi na mama yake nchini Kenya

    Chanzo cha picha, Monson Family

    Maelezo ya picha, Alexander Monson alikuwa akiishi na mama yake nchini Kenya

    Mahakama nchini Kenya inatarajiwa kutoa uamuzi wake iwapo maafisa wanne wa polisi wana hatia ya mauaji ya Alexander Monson, raia wa Uingereza, ambaye alipatikana amefariki karibu miaka 10 iliyopita akiwa mikononi mwa polisi katika mji wa pwani wa Diani.

    Maafisa hao wa polisi walifikishwa mahakamani mapema mwaka huu, baada ya kubainika kuwa Bw Monson alifariki baada ya kupigwa akiwa kizuizini na wala si kutokana na kutumia dawa za kulevya kupita kiasi kama polisi walivyodai awali.

    Bw Monson, ambaye wakati huo alikuwa na miaka 28, alikuwa mwana wa 12 wa Baron Monson na mrithi wa mali ya familia huko Lincolnshire, na alikuwa akiishi na mamake huko Diani, Kenya alipofariki.

    Baba yake, Lord Nicholas Monson, mtu wa tabaka la juu nchini Uingereza, ambaye aliwasili Kenya wikendi iliyopita atahudhuria uamuzi wa mahakama.

    Jamaa za Monson
    Jamaa za Monson

    Bw Monson alikamatwa kwa madai ya kuvuta bangi na licha ya polisi kusema alikufa kutokana na matumizi ya kupita kiasi, ripoti za uchunguzi wa sumu zilionyesha kuwa hakuna dawa zilizopatikana katika mfumo wake wakati wa kifo chake.

    Uchunguzi wa 2018 nchini Kenya ulibaini kuwa Bw Monson alipigwa hadi kufa na kwamba kumekuwa na jaribio la kuficha na vitisho dhidi ya mashahidi.

  11. Habari za hivi punde, Norwich City: Dean Smith atangazwa kuwa kocha mpya

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Norwich City imemthibitisha Dean Smith kama kocha mkuu mpya wa klabu hiyo kwa mkataba wa miaka miwili na nusu.

    Kocha huyo wa zamani wa Aston Villa, 50, anarithi mikoba ya Daniel Farke, ambaye alitimuliwa na Canaries wakiwa mkiani mwa Ligi ya Premia, pointi tano chini ya eneo salama katika jedwali .

    Craig Shakespeare, ambaye alifanya kazi na Smith katika Villa Park, ataungana naye kama msaidizi wake huko Carrow Road.

    "Kimekuwa kipindi kigumu cha siku saba," alisema Smith, ambaye alifukuzwa na Villa mnamo 7 Novemba.

    "Nimefurahi sana kurejea na kufanya kazi kwa Norwich City kwenye Ligi ya Premia.

    "Ni wazi, kumekuwa na kazi nzuri ambayo imefanyika katika klabu hii ya soka katika kipindi cha miaka minne na nusu iliyopita. Sasa ni kazi yangu na Craig kuendelea na kuboresha kazi hiyo kwa lengo kuu la kusalia katika Premier. Ligi."

    Mchezo wa kwanza wa Smith utakuwa nyumbani dhidi ya Southampton tarehe 20 Novemba.

    Ataweka historia ya kuwa mtu wa kwanza kuchukua usukani wa mechi mfululizo za Ligi Kuu dhidi ya mpinzani mmoja akiwa na timu tofauti, baada ya kutimuliwa na Villa kufuatia kushindwa na Saints.

  12. Serikali yaondoa uungwaji mkono wa mshiriki wa Miss SA nchini Israel

    Lalela Mswane ametakiwa kutoshiriki shindano la Miss Universe

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Serikali ya Afrika Kusini imeondoa uungaji mkono wa mshiriki wa Miss SA katika shindano la Miss Universe litakalofanyika Israel.

    Kumekuwa na wito wa kumtaka Bi Lalela Mswane kususia mashindano hayo licha ya waandalizi kusema kuwa haifai kuingizwa siasa.

    Wale wanaopinga kushiriki wa Afrika Kusini katika mashindano hayo wanalalamikia madai kwamba Israel ilitekeleza ukatili dhidi ya Wapalestina.

    Waafrika Kusini wanasema wanafahamu fika siasa za ubaguzi wa rangi hivyo basi hawaungi mkono kile kinachoendelea nchini Israel.

    Katika tarifa, Wizara ya sanaa na utamaduni nchini Afrika Kusini imesema kuwa "ukatili uliofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina umenakiliwa vyema" na haukuweza "kwa dhamiri njema kujihusisha na vile".

    Israel hapo awali ilikanusha kufanya ukatili na inakataa shutuma kwamba vitendo vyake dhidi ya Wapalestina ni sawa na ubaguzi wa rangi.

    Waziri Nathi Mthethwa ameelezea kwamba kujiondoa kwa Bi Mswane kungeweza kuwa vyema kwa hadhi ya kimataifa ya Afrika Kusini "ikilinganishwa na tukio la mara moja ambalo linaweza kuwa mbaya kwa mustakabali wake na hadhi yake ya umma kama mwanamke kijana, mweusi".

    "Jambo hili halijafanikiwa, hivyo basi uamuzi wa kuitenga hadharani kwa serikali na watu wa Afrika Kusini na msimamo wa mratibu wa shindano la Miss SA kuhusu suala hili", alisema.

    Shindano la Miss Universe limepangwa kufanyika tarehe 12 Desemba.

    Uhusiano baina ya nchi hizo mbili na Israel umezorota kwa miaka mingi, huku Afrika Kusini ikimuondoa balozi wake na kushusha hadhi ya ubalozi wake mwaka 2019.

  13. Katibu wa mashauri ya kigeni wa Marekani Blinken aanza safari yan chi tatu Afrika

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Katibu wa mashauri wa nchi za kigeni wa Marekani Antony J. Blinken leo ameanza ziara katika nchi tatu zaAfrika - Kenya, Nigeria, na Senegal .

    Ziara yake imeanza leo tarehe 15 hadi 20, mwezi huu na inalenga kukariri uhusiano wa nchi hiyo na washirika wa Afrika.

    Katika ziara hiyo, Blinken ataendeleza ushirikiano kati ya Marekani na Afrika kuhusu vipaumbele vya pamoja vya kimataifa, ikiwa ni pamoja na kukomesha janga la COVID-19 na kurejea kwenye uchumi wa kimataifa unaojumuisha zaidi, kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi , kuhuisha demokrasia na kuendeleza amani na usalama.

    Katibu Blinken ataanza safari yake jijini Nairobi, ambapo atakutana na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na Waziri wa Masuala ya Kigeni Balozi Raychelle Omamo.

    Katibu huyo na wawakilishi wa serikali ya Kenya watajadili maslahi ya pamoja ya nchi hizo kama wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na kushughulikia masuala ya usalama wa kikanda kama vile Ethiopia, Somalia, na Sudan. Katibu huyo ataendeleza ushirikiano kati ya Marekani na Kenya katika kukomesha COVID-19, kuboresha upatikanaji wa nishati safi na kulinda mazingira.

  14. Watatu wakamatwa chini ya Sheria ya Ugaidi baada ya mlipuko wa gari hospitalini jijini Liverpool

    Picha za gari lililoungua nje ya hospitali hiyo zimesambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii

    Chanzo cha picha, CARL BESSANT

    Maelezo ya picha, Picha za gari lililoungua nje ya hospitali hiyo zimesambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii

    Wanaume watatu wamekamatwa chini ya Sheria ya Ugaidi baada ya mtu mmoja kuuawa katika mlipuko wa gari nje ya Hospitali ya Wanawake ya Liverpool.

    Teksi iliyokuwa imembeba abiria mmoja ilisimama kabla ya saa 5:00 huku kukiwa na ukimya wa kitaifa wa dakika mbili kwa ajili ya Kumbukumbu ya Jumapili kuanza - na gari hiyo kulipuka.

    Abiria huyo aliyetangazwa kufariki katika eneo la tukio bado hajatambuliwa rasmi. Dereva alijeruhiwa na amelazwa hospitalini hali yake inaendelea vizuri.

    Wapelelezi kutoka Polisi wa Kukabiliana na Ugaidi Kaskazini Magharibi walisema wanaume watatu - wenye umri wa miaka 29, 26 na 21 - walizuiliwa katika eneo la Kensington jijini humo.

    Walisema wanaendelea kupeleleza kuhusu chanzo cha mlipuko huo na wanafanya kazi na Polisi wa Merseyside huku uchunguzi ukiendelea "kwa kasi".

    Idara ya usalama, MI5, pia inasaidia.

  15. FW de Klerk wa Afrika Kusini kuchomwa katika mazishi ya faragha

    Kumekua na hisia mseto kuhusu utawala FW de Klerk Afrika Kusini

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Kumekua na hisia mseto kuhusu utawala FW de Klerk Afrika Kusini

    Rais wa mwisho mzungu wa Afrika Kusini FW de Klerk, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 85 wiki iliyopita, atazikwa katika sherehe ya faragha siku ya Jumapili, kulingana na wakfu wake.

    “Wakfu wa FW de Klerk unawatangazia kuwa kuchomwa kwa FW de Klerk’ na mazishi yake itafanyika Jumapili Novemba,21,” ilisema taarifa.

    “Itakua shere ya faragha kwa familia na haitakua wazi kwa vyombo vya habari,” Wakfu huo uliongeza. Hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa.

    De Klerk aliingia madarakani mwaka 1989 chini ya utawala wa ubaguzi wa rangi, mfumo ambao ulihalalisha ubaguzi wa rangi, lakini baadaye akawa mtu muhimu katika kipindi cha mpito kuelekea demokrasia.

    Mwaka 1993, alipata Tuzo ya Amani ya Nobel na rais wa zamani Nelson Mandela kwa kusaidia kujadili kukomesha ubaguzi wa rangi.

    Kumekua na hisia mseto kuhusu utawala wake nchini Afrika Kusini.

    Alifariki Alhamisi baada ya kupatikana na saratani mapema mwaka huu.

    • Jinsi Mandela alivyowaleta pamoja De Klerk na Fidel Castro
    • FW de Klerk: Rais wa mwisho mweupe wa Afrika Kusini
    • FW de Klerk:Rais wa zamani wa Afrika Kusini afariki akiwa na umri wa miaka 85
    • Watu 20 wauawa katika shambulizi la wanamgambo nchini Burkina Faso

      th

      Chanzo cha picha, AFP

      Takriban watu 20 wameuawa katika shambulizi la wanamgambo katika eneo la mpaka wa kaskazini mwa Burkina Faso, mamlaka imesema.

      Kumi na tisa kati ya wahasiriwa wanasemekana kuwa maafisa katika jeshi la polisi na mmoja alikuwa raia.

      Wanamgambo hao walilenga ngome karibu na mgodi wa dhahabu huko Inata.

      Siku mbili kabla maafisa saba wa polisi waliuawa katika shambulio jingine katika eneo hilo, ambalo linapakana na Mali na Niger.

      Wanamgambo wa Kiislamu wenye uhusiano na al-Qaeda na kundi la Islamic State wanafanya kazi katika eneo la mpakani.

      Nchi hizo tatu, zikisaidiwa na Chad na Ufaransa, zimetuma mamia ya wanajeshi huko.

    • Covid: Austria yaanzisha ‘Lockdown’ kwa watu ambao hawajachanjwa

      th

      Chanzo cha picha, Getty Images

      Takriban watu milioni mbili ambao hawajachanjwa kikamilifu dhidi ya Covid-19 wamewekwa chini ya zuio la kutotoka nje nchini Austria huku nchi hiyo ikikabiliwa na kuongezeka kwa visa vya ugonjwa huo .

      "Hatuchukui hatua hii kirahisi, lakini kwa bahati mbaya ni muhimu," Kansela Alexander Schallenberg alisema.

      Watu ambao hawajachanjwa wataruhusiwa tu kuondoka nyumbani kwa sababu chache, kama vile kufanya kazi au kununua chakula.

      Takriban 65% ya wakazi wa Austria wamechanjwa kikamilifu - mojawapo ya viwango vya chini kabisa Ulaya Magharibi.

      Wakati huo huo, kiwango cha maambukizi ya siku saba ni zaidi ya kesi 800 kwa kila watu 100,000, ambayo ni moja ya juu zaidi barani Ulaya.

      Kwa ujumla, Ulaya imekuwa tena eneo lililoathiriwa zaidi na janga hili na nchi kadhaa zinaanzisha vizuizi na onyo la kuongezeka kwa visa vya ugonjwa huo

      Walakini, Uingereza, ambayo ina moja ya viwango vya juu zaidi vya maambukizi ya Covid, bado haijaleta vizuizi, licha ya viongozi wa afya kutaka sheria kama maski za lazima katika maeneo yaliyo na watu wengi na zilizofungwa zirudishwe ili kuepusha hali mbaya zaidi msimu wa baridi.

    • Joe Biden na Xi Jinping: Wanachotaka kutoka kwa mazungumzo

      th

      Chanzo cha picha, Getty Images

      Rais wa Marekani Joe Biden na Rais wa China Xi Jinping watafanya mkutano wa kupitia njia ya mtandao hivi leo Jumatatu huku mvutano kati ya nchi hizo ukizidi kuongezeka.

      Mataifa hayo makubwa yanayoshindana yalishangaza wengi wiki iliyopita kwa kutoa tamko la pamoja la kushughulikia mabadiliko ya hali ya hewa, katika mazungumzo huko Glasgow, Scotland.

      Lakini wasiwasi unaoongezeka wa makabiliano ya kijeshi juu ya Taiwan na umesababisha utulivu kuhusu tofauti zao .

      Mkutano wa tatu wa wawili hao utashughulikia mada kadhaa zenye utata

      Usalama wa mtandao, biashara na kutoeneza kwa silaha za nyuklia ni mada kwenye meza, vyanzo vinavyofahamu mazungumzo hayo viliviambia vyombo vya habari vya Marekani.

      Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa, Ikulu ya White House ilisema "viongozi hao wawili watajadili njia za kusimamia kwa uwajibikaji ushindani kati ya Marekani na PRC, pamoja na njia za kufanya kazi pamoja pale ambapo maslahi yetu yanalingana".

      Wawili hao wamezungumza mara mbili tangu Bw Biden aingie madarakani mwezi Januari, lakini wote wamekiri kuwepo kwa matatizo katika uhusiano huo.

    • Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja hivi leo Jumatatu tarehe 15 Novemba 2021