Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Watu tisa wameuawa katika mapigano Bukavu DRC

Radio Okapi inayofadhiliwa na Umoja wa Mataifa inaripoti kwamba "waasi walishambulia vituo vingi vya kijeshi na polisi huko Bukavu ... kwa lengo la kupora silaha".

Moja kwa moja

Esther Namuhisa

  1. Mpaka hapo ni tamati ya habari zetu za moja kwa moja kwa leo, tafadhali tukutane kesho majaliwa

  2. Watatu washikiliwa Tanzania kwa kufukua kaburi la mtu mwenye 'Ualbino'

    Jeshi la polisi nchini Tanzania linawashikilia watu wa tatu wa familia moja kwa madai ya kufukua mwili wa kijana mwenye ualbino ambaye alizikwa mwezi Julai mwaka 2020.

    Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoani Tanga Safia Jongo Jeshi hilo bado linaendelea na upelelezi na taarifa za awali zinaonesha sababu za tukio hilo ni Imani za kishirikina.

    Familia ya marehemu iligundua kutitia kwa kaburu la ndugu yao ambaye alizikwa toka mwezi Julai mwaka jana na kutoa ripoti kwa polisi na baada ya polisi kufukua kaburi hilo walibani mkono mmoja haukuwepo.

    Baada ya upelelezi mtuhumiwa mmoja kati ya watatu ambao tayari wamekamatwa alionesha wapi waliuficha.

    Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini Tanzania (LHRC), kimekemea vikali tukio hilo na kuwataka polisi kuharakisha upelelezi na washitakiwa wafikishwe kwenye vyombo vya sheria haraka iwezekanavyo.

    Mkurugenzi wa kituo hicho Bi. Anna Henga amesema tukio hilo ni la pili la kikatili kutokea dhidi ya watu wenye ualbino kwa mwaka huu nchini Tanzania.

  3. Rais Misri atangaza mwezi ujao serikali yake itahamia mji mpya uliojengwa kwa mabilioni ya dola

    Rais wa Misri Abdul Fattah al-Sisi ameelekeza mamlaka za Serikali kuanza kuhamia kwenye mji mpya wa kiserikali kuanzia mwezi ujao.

    Msemaji wa Rais Sisi alisema hatua hiyo itakuwa seheu ya majaribio ya miezi sita ya kuhamia makao mapya.

    Makao mapya ya kiutawala ya serikali yalianza yamejengwa kilometa 45 mashariki mwa jiji la Cairo.

    Mpango huo uliotumia mabilioni ya dola unalenga - kwa mujibu wa maofisa - kuepuka msongamano katika jiji la Cairo, ukichukua watu zaidi ya milioni 6.

    Pamoja na mji huo wa kiserikali utakaokuwa na maofisi ya kiserikali, pia eneo hilo litakuwa na makazi ya balozi mbalimbali pamoja na akazi ya Rais.

  4. Kampeni ya kutetea vazi la hijabu Ulaya yasitishwa

    Mashirika makubwa ya kutetea haki za binadamu barani Ulaya yametoa machapisho yao ya kampeni iliyohimiza heshima kwa wanawake wa Kiislamu walioamua kuvaa hijabu baada ya kupata upinzani nchini Ufaransa.

    Baraza la Ulaya lilitoa picha hizo wiki iliyopita kwa ajili ya kampeni kupinga ubaguzi dhidi ya Waislamu. Kauli mbiu kwenye tangazo ama chapisho moja ilisomeka: "Urembo uko katika utofauti kama vile uhuru uko kwenye hijabu".

    Wanasiasa kadhaa mashuhuri wa Ufaransa walilaani ujumbe huo na kusema kwamba hijabu haiwakilishi uhuru. Lakini baadhi ya wanawake wa Kiislamu ambao huvaa hijabu walisema kwamba hatua hiyo ilionyesha kutoheshimu utofauti na haki ya kuchagua cha kuvaa nchini Ufaransa.

    Waziri wa vijana wa Ufaransa, Sarah El Haïry, alisema alishtushwa na bango moja, ambalo lilionyesha picha iliyopasuliwa ya mwanamke mmoja aliyevaa hijabu, na mmoja asiyevaa.

    Rais wa Femyso, Hande Taner, alitetea kampeni hiyo siku ya Jumatano katika mahojiano yake na BBC. Alisema "kampeni yenyewe bado inaendelea" lakini akaongeza: "Kuhusu kwa nini tweet ilifutwa, siwezi kuzungumza kwa niaba ya Baraza la Ulaya."

    Bi Taner alisema "inasikitisha sana kwamba juhudi za vijana walio wachache zinashambuliwa na kuhujumiwa" na wanasiasa.

  5. Habari za hivi punde, Mwanamuziki wa Tanzania Vitali Maembe aachiliwa kwa dhamana

    Hatimaye mwanamuziki wa Tanzania Vitali Maembe ameachiliwa na polisi kwa dhamana siku moja tu baada ya kukamatwa.

    Kulingana na taarifa iliotiwa saini na katibu wa idara ya haki za binadamu katika chama cha ACT Wazalendo, Mbarala Maharagande, bwana Maembe alikamatwa na polisi katika eneo la Bagamoyo siku ya Jumanne na baadaye kuhamishwa hadi kituo cha polisi cha Kibaha.

    Kwa mujibu wa katibu huyo mwanamuziki huyo hatahivyo ametakiwa kuripoti katika kituo cha polisi mapema hapo kesho siku ya Alhamisi .

    Jeshi la polisi linadaiwa kumtuhumu kwa kutumia wimbo wake Kaizari kuwashutumu viongozi

    Mwanamuziki huyo anadaiwa kuwania kiti cha eneo bunge la Bagamoyo kwa tiketi ya chama cha ACT mwaka 2020.

  6. Britney Spears amlaumu mamake kwa kumdhibiti

    Mwanamuziki wa Marekani Britney Spears amemlaumu mamake kwa malezi ya kihafidhina ambayo yamedhibiti maisha yake kwa takriban miaka 13 .

    Babake nyota huyo Jamie ndiye mtu ambaye amekuwa akisimamia mipango ya kisheria ambayo nyota huyo hatakuwa na usemi kuhusu masuala yake ya kibinfasi na yale ya kifedha. Lakini akiandika katika mtandao , msanii huyo amesema lilikuwa wazo la mamake.

    ''Kile ambacho watu hawajui ni kwamba mamungu ndiye aliyempatia wazo hilo'' , alisema. Sitaweza kupata miaka hiyo iliopotea …aliharibu maisha yangu kisiri.

    Katika chapisho jipya lililofutwa katika mtandao wa Istagram, aliendelea: Unajua ulichokifanya. Babangu asingelijua kuhusu kunidhibiti. lakini usiku wa leo ninatabasamu nikijua nina maisha mapya mbele yangu.

    Chapisho hilo la Spears linaonekana kushinikizwa na hatua ya babake kuwasilisha ombi la kufutiliwa kwa maisha ya kumdhibiti nyota huyo.

    Mpangilio wa aina hii ya ulinzi wa kisheria ambao kwa kawaida hutolewa kwa watu ambao hawawezi kufanya maamuzi yao wenyewe, kama vile walio na matatizo ya kiakili au magonjwa mengine ya akili.

  7. Guardiola: Mechi hii ni muhimu kuliko ya Manchester United

    Mkufunzi klabu ya Manchester City Pep Guardiola amesema kwamba Manchester City wana fursa ya kupiga hatua muhimu katika awamu ya timu 16 bora katika kombe la klabu bingwa Ulaya wakati watakapokutana na Club Bruggeskatika uwanja wa Etihad jioni ya leo.

    Ni mechi ambayo raia huyo wa Uhispania anasema ni muhimu zaidi ya mechi ya Jumamosi kati ya timu hiyo na Manchester United .

    City ipo katika nafasi ya pili katika kundi A na pointi moja nyuma ya viongozi wa kundi hilo PSG .

    Ushindi wowote utaiweka timu hiyo pointi tano juu ya timu iliopo katika nafasi ya tatu Club Brugesambayo waliishinda 5-1 mwezi uliopita – huku ikiwa imesalia mechi mbili.

    ‘’Lazima tuwajibike zaidi ili kuweza kupata matokeo bora. Mechi hii itatupatia fursa nzuri ya kufuzu katika awamu ya timu 16 bora’’ , alisema Guardiola.

    ‘’Hii ni muhimu zaidi ya mechi ya Manchester United . Katika ligi ya premia kuna mechi nyingi hapa , ni mechi sita pekeena tumesalia na tatu. Mechi hizi ni muhimu sana’’.

  8. Kuuawa kwa watoto wawili wa marais wa zamani Liberia kwazua taharuki

    Watoto wawili wa marais wa zamani wa Liberia na afisa wa uhamiaji ndio waliuawa hivi karibuni nchini Liberia.

    Msemaji wa polisi Moses Carter ameithibitishia BBC siku ya Jumatano kuwa mauaji ya watoto wa aliyekuwa rais wa Liberia William R. Tolbert, Jr, yalitokea Jumatatu wiki hii.

    Mwili wa Mchungaji William R. Tolbert, III ulikutwa umetapakaa damu kitandani kwake , katika makazi yake yaliyopo kisiwa cha Bushrod, Monrovia.

    Baba yake aliuawa kikatili na mwili wake kukatwakatwa wakati wa mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Samuel Doe ambayo yalipindua utawala wake wa miaka tisa tarehe 12 Aprili 1980.

    Na kama marehemu baba yake, Mchungaji Tolbert alikuwa mhubiri na balozi wa amani wa Liberia.

    Kifo chake kimetokea siku moja baada ya mwili wa afisa wa uhamiaji wa kike, Maude Elliott, kupatikana ukiwa na majeraha makubwa na michubuko katika maeneo ya nyumbani kwake huko Monrovia magharibi mwa Brewerville.

    Mwezi Septemba, John Tubman, mtoto wa aliyekuwa rais pia William Tubman, aliuawa na mwili wake kupatikana nyumbani kwake.

    Mapema mwaka huu rais George Weah amekosolewa vikali na umma alipowataka kuweka kamera katika nyumba zao ili kujilinda.

  9. Mwanamuziki wa Tanzania 'Vitali Maembe' adaiwa kukamatwa

      • Author, Aboubakar Famau
      • Nafasi, BBC News, Dodoma

    Wakati taarifa za kukamatwa kwa msanii Vitali Maembe zikiendelea kusambaa, Jeshi la Polisi linaonekana kuwa kimya huku likisema linafuatilia taarifa hizo.

    Katika jitihada za kupata uthibitisho wa kukamatwa kwa msanii huyo, BBC imewasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani. Hata hivyo, jitihada za kupata uthibitisho hazikuzaa matunda.

    ”Asante kwa taarifa, tunazifuatilia” amejibu aliyepokea simu ya RPC na kusema RPC yuko kwenye kikao hivyo ameacha simu yake ofisini.

    Kwa upande wake, akinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari vya ndani hii leo, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Wanko Nyigesa amesema ameyasikia madai ya kukamatwa kwa msanii huyo hivyo anafuatilia ili kupata ukweli na kulitolea majibu.

    Wakati huo huo, Zitto Kabwe ambae ni Kiongozi wa Chama cha Kisiasa ACT Wazalendo, kupitia ukurasa wake wa Twitter, amelitaka Jeshi la Polisi kumuachia msanii huyo. Nawataka Jeshi la Polisi Tanzania kumwachia huru mara moja ndugu Vitalis Maembe.

    Haivumiliki na tunataka Vitalis aachiwe huru sasa hivi,” ameandika Zitto. Ikumbukwe kwamba Vitalis Maembe hutumia mziki wake, kueleza madhila wanayoyapata watu wa kawaida, huku akijichukua yeye kuwa sauti yao na kuwasilisha hoja hizo. Ingawa kazi yake, imekuwa ikinasibishwa na uanaharakati.

    Vile vile Vitalis Maembe ni miongoni mwa wasanii waliohitimu katika wa Chuo cha Sanaa Bagamoyo na kufanikiwa kupenyeza kazi zake za sanaa ndani na nje ya Tanzania.

  10. Watu tisa wauawa katika ghasia DRC-Gavana

    Akizungumza na chombo cha habari cha Théo KASI,gavana wa jimbo la kivu kusini, mashariki mwa DRC amesema watu tisa wameuawa katika operesheni ya kurejesha amani katika mji wa Bukavu.

    Miongoni mwa watu waliouawa , ni watu sita ambao walifanya mashambulizi pamoja na askari wawili na polisi.

    Watu 36 ambao walifanya uvamizi wamekamatwa , wakati uchunguzi ukiendelea.

    Ingawa hali ya maisha inaanza kurejea katika hali ya kawaida, baadhi ya maduka na ofisi zimeanza kufunguliwa tangu asubuhi.

    Askari wengi wamepelekwa kufanya doria katika mji huo .

    Wakazi wameiambia BBC kuwa walisikia milio ya risasi kuanzia majira ya saa saba usiku , na wakabaki ndani mpaka kulipokucha.

    Mwezi Septemba mwaka jana viongozi wa wapiganaji wapatao sabini walisaini mkataba wa kusitisha mapigano DRC , lakini serikali ilishindwa kuihusisha jeshi .

    Aidha makubaliano hayo hayakuweza kuleta amani katika eneo ambalo limekuwa na ghasia kwa miongo miwili, huko kusini mwa -Kivu.

  11. Marekani yawashauri raia wake kuondoka Ethiopia

    Ubalozi wa Marekani mjini Addis Ababa umesema kutokana na hali ya kiusalama ya nchi hiyo kuzorota kwa kiasi kikubwa , ubalozi unashauri raia wake kufikiria kuanza kujiandaa kuondoka katika nchi hiyo".

    Katika taarifa ambayo ameiandika kwenye kurasa ya Facebook ya ubalozi imetoa onyo kwa watu kusafiri kwenda Addis Ababa.

    Wakati huo huo , katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, wito kutaka hatua haraka zichukuliwe kuzuia ghasia kwa kuwa athari inayoweza kutokea Ethiopia itahatarisha eneo kubwa”.

  12. Taliban yapiga marufuku matumizi ya fedha za kigeni Afghanistan

    Taliban imepiga marufuku matumizi ya fedha za kigeni nchini Afghanistan, hatua ambayo itaathiri zaidi uchumi ambao unaporomoka.

    "Hali ya ya uchumi na matakwa ya taifa katika nchi yanahitaji raia wote wa Afghans kutumia fedha za Afghani katika biashara zao," Taliban ilisema.

    Hali ya kiuchumi bado haijatengamaa kutokana na kujiondoa kwa msaada wa kifedha wa kimataifa mara baada ya Taliban kuingia madarakani.

    Dola ya Marekani ilikuwa ikitumka zaidi katika masoko ya Afghanistan.

    Dola pia zimekuwa zikitumika mara nyingi katika biashara za maeneo ya mpakani mwa Afghanistan kama Pakistan.

    "Yeyote atakayekiuka sheria hii atakabiliwa na hatua za kisheria," taarifa zinasema.

    Baada ya Taliban kudhibiti taifa hilo mwezi Agosti, mabilioni ya dola yaliyokuwa nje ya nchi yalitaifishwa na Marekani.

    "Tunaamini kuwa ni muhimu kuendeleza vikwazo tulivyoviweka dhidi ya Taliban lakini wakati huo huo kutafuta namna ambayo tutaweza kutoa usaidizi wa kibinadamu wa raia wa Afghan. Na hicho ndicho tunachokifanya," Naibu waziri wa fedha Wally Adeyemo aliiambia kamati ya benki ya seneti nchini Marekani.

    • Vita Afghanistan: Watu wenye silaha wavamia harusi kuzuia muziki usipigwe
  13. Cleo Smith: Mtoto wa miaka minne aliyepotea siku 18 apatikana mzima wa afya

    Mtoto wa miaka minne aliyepotea siku 18 katika maeneo ya pembezoni ya kaskazini mwa Australia amepatikana akiwa mzima wa afya katika nyumba iliyokuwa imefungwa, polisi imesema.

    Oktoba 16, Cleo Smith aliwapotea familia yake katika eneo la kambi ambalo liko karibu na mji wa Carnarvon, na kuanza kufanya msako mkali.

    Mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 36 yuko kizuizini na anahojiwa na wapelelezi.

    Polisi waliivamia nyumba moja Carnarvon majira ya alfajiri siku ya Jumatano baada ya kupata fununu ya uwepo wa mtoto huyo.

    "Walimpata mtoto Cleo katika chumba kimoja katika nyumba hiyo," Kamishina Col Blanch ametoa taarifa ya polisi.

    "Afisa mmoja alimbeba mkononi na kuanza kumuuliza jina lake' alisema 'Mimi ni Cleo'."

    Mtoto huyo aliungana na familia yake, ambao walikuwa na hofu juu ya kupotea kwake.

    "Familia yetu imekamilika sasa," mama yake Ellie Smith,aliandika Instagram.

    Picha za video zinamuonesha mtoto huyo akitabasamu.

  14. Blatter na Platini washtakiwa kwa ufisadi katika soka

    Mamlaka ya Uswizi imewafungulia mashtaka maofisa wa zamani wa FIFA Sepp Blatter na Michel.

    Platin anashtakiwa kwa ulaghai na mwingine uhalifu unaohusisha rushwa katika soka.Mwendesha mashtaka wa Uswizi anasema Blatter, rais wa zamani wa FIFA, alihusika katika mchakato ambao ni kinyume na sheria kwa kutuma dola milioni 2.19 kwa Platini,ambaye alikuwa rais wa Umoja wa Ulaya mwaka 2011.

    Waendesha mashtaka wanasema kiasi hicho "kiliharibu rasilimali za FIFA na kumtajirisha Platin kinyume na sheria. Blatter na Platini wanakabiliwa na mashitaka hayo katika mahakama ya Bellinzona.

    Kama wakikutwa na hatia dhidi ya mashtaka yanayowakabili , watapewa hukumu ya kifungo cha miaka kadhaa au faini.

    Kesi hii ilifunguliwa mwezi Septemba 2015 baada ya shirikisho la soka la FIFA, lilipokabiliwa na tuhuma za ufisadi.

  15. Msaidizi wa rais wa zamani wa Zambia akamatwa kwa kuweka vizuizi

    Msaidizi wa rais wa zamani wa Zambia Edgar Lungu amekamatwa kwa makosa ya kuwatukana na kuwawekea vizuizi afisa kuchunguza nyumba yake.

    Msemaji wa rais wa zamani bwana Amos Chanda alikamatwa pamoja na mke wake na shemeji yake ambao walikuwa pamoja naye wakati wa tukio hilo.

    Bwana Chanda alihojiwa kwa saa nane kabla ya kutolewa kwa dhamana.

    Watu watatu wanashutumiwa kuwatukana na kuwawekea vizuizi afisa wa kupambana na rushwa wakati nyumba zao zikitakiwa kufanyiwa uchunguzi.

    Bw. Chanda hajasema lolote kuhusu mashtaka dhidi yake wakati wa ukaguzi na kuwashutumu maofisa kuwa wachawi na hajafanya kosa lolote.

    Kumekuwa na madai ya rushwa dhidi ya maafisa wa utawala uliomaliza muda wake wa rais Lungu.

  16. Milio ya risasi yasikika huku mapigano yakiripotiwa Bukavu DRC

    Milio ya risasi nzito na nyepesi imesikika huko Bukavu nchini DRC mapema Jumatano huku watu wasiojulikana wakidai kushambulia mji huo, maafisa wanasema.

    Mapigano kati ya jeshi la kifalme na washambuliaji katika mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini, yalianza mwendo wa saa saba usiku kuendelea hadi saa kumi asubuhi, wenyeji wanasema.

    Radio Okapi inayofadhiliwa na Umoja wa Mataifa inaripoti kwamba "waasi walishambulia vituo vingi vya kijeshi na polisi huko Bukavu ... kwa lengo la kupora silaha".

    Katika taarifa, gavana wa jimbo hilo Theo Kasi Ngwabidje alisema kuwa vikosi vya usalama vimekomesha mashambulio hayo ambayo "yalijaribu kuvuruga utulivu wa watu".

    Bw Ngwabidje alitoa wito kwa watu kuanza shughuli zao kama kawaida, lakini wenyeji wanasema kuwa jeshi linawataka watu kusalia nyumbani.

    • Mzozo wa DRC: Umwagikaji wa damu waendelea mashariki mwa DRC muda mfupi baada ya rais kutangaza 'hali ya kuzingirwa' kwa mikoa miwili
    • Fahamu kwanini Nigeria, Mali, Burkina faso ,Niger, Chad na Cameroon zinalemewa na makundi yaliyojihami
  17. Ethiopia 'yasikitishwa na hatua ya Marekani kusitisha mkataba wa biashara'

    Ethiopia imesema "imesikitishwa sana na hatua ya Marekani ya kuondoa mkataba wa mauzo ya bidhaa kwenda Marekani bila ushuru.

    “Tumesikitishwa sana na vitisho ambavyo Agoa [African Growth and Opportunities Act] imeviweka kwa kujiondoa sasa kwa kuzingatia serikali ya Marekani,” wizara ya biashara ya Ethiopia ilisema Jumanne.

    Marekani imepanga kusitisha mpango wa kutowatoza ushuru biashara kutoka Ethiopia, Mali na Guinea kutokana na masuala ya haki za binadamu na demokrasia.

    Siku ya Jumanne, Rais Joe Biden katika barua la bunge la Marekani alisema Ethiopia imekuwa ikikiuka haki za binadamu zinazotambulika kimataifa”.

    Kwa upande wa Mali na Guinea , nchi hizo zimekuwa katika mapinduzi katika miezi ya hivi karibuni.

    Lakini Jumanne, waziri wa Ethiopia amesema uamuzi huo inabidi ubatilishwe ifikapo Januari mosi mwakani.

    “Tunataka Marekani kuunga mkono jitihada zetu za kurejesha amani na utawala wa sheria – na sio kuwahukumu watu wetubali kukabiliana na jeshi la waasi,” wizara ilisema.

    "Serikali ya Ethiopia inazingatia kwa umakini madai yote ya haki za binadamu: tunafuatilia madai hayo na kufanya uchunguzi na tunhaidi kuhakikisha uwajibikaji unafanyika," aliongeza.

    • Mzozo wa Tigray Ethiopia: Blinken asema Marekani inasikitishwa na ukatili unaofanyika
    • Mzozo wa Tigray Ethiopia: Mataifa yenye nguvu za kiuchumi duniani yakemea 'ukiukaji wa haki za binadamu'
  18. Eswatini kufanya kongamano la kitaifa kutatua mgogoro

    Mfame Mswati wa Eswatini na rais wa Afrika Kusini wamekubaliana kufanya kazi kwa karibu na kuanzisha kongamano la kitaifa ili kutatua mgogoro unaosababisha maandamano Eswatini.

    Hatua hii inakuja baada ya mfalme kukutana na rais Cyril Ramaphosa, ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa Jumuiya ya maendeleo ya kusini (Sadc),kuzungumzia siasa na maendeleo ya usalama wa Eswatini.

    Hatua hii imekuja baada ya ghasia kadhaa kutokea kati ya wanaharakati wa demokrasia na vyombo vya usalama katika miezi ya hivi karibuni , ambazo zilisababisha vifo vya watu wapatao 30.

    Kuna wito mkubwa unaomtaka mfalme Mswati III kuruhusu demokrasia katika utawala wa kifalme uliobaki Afrika.

    Maandamano yalitokea mwezi uliopita baada ya vyombo vya usalama vya mfalme Mswati vilipojaribu kuwazuia wanaharakati kufanya maandamano.

    Mawasiliano ya intaneti yalizimwa baada ya picha za maandamano ya ghasia zilivyoanza kuenea katika mitandao ya kijamii.

    Mfalme Mswati alitoa agizo la shule kufungwa baada ya wanafunzi kugomea masomo, wakitaka elimu kuwa bure na kusitishwa kwa utawala wa kifalme.

    Rais Ramaphosa na mfalme Mswati wamewataka wadau wote kumaliza ghasia na kudumisha amani wakati mchakato wa kuanzishwa kwa mdahalo ukifanyiwa kazi.

  19. Kenya yataka kurejeshwa nchini kwa mwanajeshi wa Uingereza kuhusu mauaji ya raia wake

    Kenya ina nia ya kuiomba Uingereza kumsalimisha mwanajeshi wa taifa hilo anayedaiwa kuhusika na mauaji ya mwanamke mmoja raia wa Kenya miaka tisa iliyopita .

    Waziri wa ulinzi Eugene Wamalwa ameiambia kamati ya bunge kuwa serikali ya Uingereza imeahidi ushirikiano kamili.

    Bw. Wamalwa alisema mwili wa Agnes Wanjiru mwenye umri wa miaka 21 uligunduliwa baada ya wanajeshi wa Uingereza waliokuwa wakifanya mazoezi nchini Kenya kuondoka nchini.

    Wajumbe wa serikali ya Uingereza kwa sasa uko nchini Kenya ukifanya mazungumzo na wenzao wa Kenya, lakini wamekataa maombi yote ya mahojiano na BBC.

    Bw Wamalwa aliwaambia wabunge Jumanne kwamba alisoma ripoti ya uchunguzi iliyohitimisha kuwa Wanjiru aliuawa na wanajeshi wa Uingereza katika ardhi ya Kenya.

    Aliongeza kuwa serikali ya Kenya iliwasiliana na Uingereza baada ya taarifa ya Jumatatu ya mkuu wa polisi kwamba kesi hiyo imefunguliwa tena.

    Bw Wamalwa pia alisema amepata hakikisho la serikali ya Uingereza kwamba wale wanaosakwa kuhusiana na mauaji hayo, ambao alisema wanajulikana, watafikishwa Kenya kujibu mashtaka.

  20. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja hii leo Jumatano tarehe 3 Novemba 2021