Ndege ya UN yalazimika kubadili mkondo kufuatia mashambulio ya angani ya Ethiopia

Chanzo cha picha, Getty Images
Ndege ya misaada ya Umoja wa Mataifa ililazimika kughairi kutua Ijumaa huko Mekele, mji mkuu wa Jimbo la Tigray kwa sababu ya shambulio la angani la serikali, msemaji wa UN ameiambia BBC.
Awali serikali ilithibitisha kufanya shambulio la angani la hivi punde , ikisema inalenga waasi wa Tigray ambao wanadhibiti mji huo. Wanasema raia walilengwa.
Shirika la chakula la umoja wa mataifa,WFP linasema ndege yake ililazimika kurejea Addis Ababa kutokana na shambulio la hivi punde.
Ni siku ya nne mashambulio ya angani yanafanywa dhidi ya mji wa Mekelle huku mapigano yakipamba moto kati ya vikosi vya serikali kuu na vikosi vya jimbo hilo la kaskazini mwa nchi.
Serikali inasema ilishambulia eneo la mafunzo linalotumiwa na wapiganaji wa Tigraya lakini msemaji wa waasi anasema mahali paliposhambuliwa ni chuo kikuu mjini humo.














