Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Maelfu ya wanamgambo wa Boko Haram wajisalimisha Nigeria
Mamlaka nchini Nigeria zinasema sasa wanatoa wasifu kwa wale ambao wamejisalimisha kwa lengo la kuwapa ushauri nasaha.
Moja kwa moja
TAMWA yasikitishwa na udhalilishaji unaodaiwa kufanywa na polisi mkoani Tanga
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Martha Saranga
- Nafasi, BBC Dar es Salaam
Chama cha waandishi wa habari wanawake nchini Tanzania Tamwa kimeelezea kusikitishwa na udhalilishaji uliodaiwa kufanywa na baadhi ya askari polisi katika wilaya ya Handeni Mkoani Tanga.
Tamko hili linakuja baada ya mkuu wa wilaya hiyo Siriel Mchembe kuibua ukatili unaofanywa na baadhi ya askari polisi wanaodaiwa kuwashika sehemu za siri wasichana na kuwabaka kuwapiga na kuwalazimisha kuwa na mahusiano ya kimapenzi.
Mkurugenzi mtendaji wa Tamwa Dkt. Rose Reuben amesema hakuna aliye juu ya sheria na ndiyo maana askari wana dhamana ya kusimamia sheria hizi lakini cha ajabu baadhi wamekuwa wa kwanza kuzivunja.
Waziri Mkuu kuamua hatima ya Gwajima, Silaa na Polepole
Hatima ya wabunge watatu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Askofu Josephat Gwajima (Kawe), Jerry Silaa (Ukonga) na mbunge wa kuteuliwa Humphrey Polepole sasa iko mikononi mwa Waziri Mkuu wan chi hiyoKassim Majaliwa.
Wabunge hao leo walifika mbele ya kamati ya Maadili ya wabunge wa CCM na kuhojiwa kutokana na tuhuma zinazowakabili za kusema uwongo na kushusha hadhi ya Bunge.
Mwanzoni mwa wiki Bunge lilipitisha azimio la kuwapa adhabu Askofu Gwajima na Silaa kutohudhuria vikao vya mikutano miwili ya Bunge
Mwenyekiti wa kamati ya Maadili ya wabunge wa CCM, Hassan Mtenga amesema kazi bado inaendelea.
"Sisi tumemaliza kazi yetu na mapendekezo yanapelekwa kamati ya uongozi ya Bunge ambayo iko chini ya Waziri Mkuu, wakimaliza basi itajulikana nini kinafuata," amesema Mtenga.
Wapiganaji wa Tigray watuhumiwa kuwalenga raia
Wapiganaji katika eneo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia, kupora vituo vya afya na vituo vingine vya kibinadamu katika eneo jirani la Amhara, shirika la habari la AP linaripoti.
Mzozo wa miezi 10 kaskazini, ulioanza juu ya uongozi wa Tigray, sasa umeongezeka.
Kumekuwa na ripoti kadhaa za ukatili uliodaiwa kkutekelezwa na wanajeshi wa muungano na washirika wao katika eneo laTigray na AP wanaripoti kwamba kuna madai kwamba mashambulio ya Amhara ni kulipiza kisasi.
Shirika hilo la habari pia linasema vifaa vya matibabu katika hospitali ya mji wa Nefas Mewucha was vilivunjwa na bidhaa za tiba kuporwa.
"Ni uwongo kwamba hawalengi raia na miundombinu," msimamizi wa hospitali Birhanu Birhanu amenukuliwa akisema.
Wapiganaji wa Tigray wamekanusha madai kwamba raia wanalengwa.
Katika ujumbe wa Facebook siku ya Alhamisi ubalozi wa Marekani mjini Addis Ababa ulisema kuwa"visa vitatu vya uporaji wa misaada ya kibinadamu vimethibitishwa katika mabohari ya kijamii kaskazini mwa Amhara".
Ap pia anamnukuu mtu ambaye aliona nyumba ya watawa ya Karne ya Checheho ikishambuliwa kwa makombora.
Soma zaidi:
- Mzozo wa Tigray: Msaada mkubwa wa kibinadamu unahitajika
- Uchumi wa Ethiopia waathiriwa na mzozo wa Tigray
Mtu aliyejifanya Makamu wa Rais wa Zimbabwe akamatwa baada ya kutibiwa
Mwanamume mmoja raia wa Zimbabwe ameshtakiwa kwa ulaghai baada ya kujifanya Makamuwa rais wa nchi hiyo na kupata huduma ya matibabu bila malipo.
Mahakama katika mji mkuu wa Harare, alifahamishwa kuwa Marlon Katiyo, 35, alitembelea hospitali mbili mara kadhaa mwezi uliopita kupata matibabu ya maumivu ya kichwa akisema kwamba alikuwa, Makamu wa Rais Constantino Chiwenga.
Bwana Katiyo, amabye hajatoa tamko lolote kuhusiana mashtaka hayo alipewa matibabu ya bure.
Ombi la dhamana alilowasilisha linatarajiwa kusikizwa siku ya Ijumaa.
Uamuzi wa mapingamizi ya Mbowe na wenzake kutolewa Jumatatu
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Eagan Salla
- Nafasi, BBC Swahili, Dar es Salaam
Mahakama Kuu ya Tanzania kitengo cha makosa ya rushwa na uhujumu uchumi inatarajiwa kutoa maamuzi juu ya mapingamizi yaliyowasilishwa na upande wa utetezi juu usahihi wa hati ya mashitaka.
Jopo la mawakilii wanaomtetea Mbowe na wenzake liliweka mapingamizi hayo na kuitaka mahakama kujiridhisha kabla hatua nyingine yoyote.
Jaji Elinezer Luvanda ameahirisha shauri hilo hadi siku ya Jumatatu Septemba tarehe sita atakapotoa maamuzi juu ya mapingamizi hayo ya upande wa utetezi baada ya kusikiliza ushahidi, hoja za upande wa serikali na kutaka muda wa kujiridhisha kabla ya kutoa maamuzi.
Mbowe na wenzaje wanashitakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi, ugaidi na kupanga njama za kuwadhuru viongozi wa serikali akiwemo aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya.
Mwenyekiti huyo wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania anashikiliwa tangu mwezi Julai baada ya kukamatwa jijini Mwanza ambako alikuwa akiratibu kongamano la kudai katiba mpya.
Maelezo zaidi:
- Mahojiano Maalum na Rais Samia: Mashtaka dhidi ya Mbowe hayajachochewa kisiasa
- Freeman Mbowe: Bingwa wa mikakati ya siasa za upinzani anayewanyima usingizi watawala
Marekani yakaribisha uteuzi wa Obasanjo kuwa mwakilishi wa AU eneo la Upembe wa Afrika
Marekani imeunga mkono uteuzi wa rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo kuwa Mawakilishi wa Muungano wa Afrika katika eneo la Upembe wa Afrika.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield amesema Marekani itatoa ushirikiano kuelekea majadiliano ya kumaliza mzozo nchini Ethiopia ambako maelfu ya watu wameuawa na zaidi ya robo milioni kuishi katika mazingira ya njaa
Uteuzi wa Olusegun Obasanjo unakuja katika kilele cha mzozo wa miezi 9 katika jimbo la Tigray ambapo Umoja wa Mataifa unasema uhalifu wa kivita umefanywa, na sasa maelfu wanaweza kufa na njaa.
Utawala wa Waziri Mkuu Abiy Ahmed uko chini ya shinikizo kujadiliana na Chama cha Tigray People’s Liberation Front, ambacho Ethiopia imetambua kama shirika la kigaidi.
Zambia yamchagua spika wa kwanza mwanamke
Bunge la Zambia limemchagua mwanamke wa kwanza kuwa spika.
Nelly Mutti ambaye ni wakili alichaguliwa bila kupingwa na wabunge wapya chini ya utawala mpya unaoongozwa na Rais Hakainde Hichilema.
Majukumu ya spika ni pamoja na kuhakikisha mwenendo mzuri wa mijadala ya bunge pamoja na kuhakikisha wabunge wanadumisha nidhamu ya taasisi ya bunge.
Maelfu ya wanamgambo wa Boko Haram wajisalimisha Nigeria
Jeshi la Nigeria linasema karibu wanamgambo 6000 wa Boko Haram wakiwemo makamanda , wapiganaji na familia zao wamejisalimisha kwa mamlaka katika muda wa wiki chache zilizopita.
Cameroon pia ilikuwa imetangaza kujisalimisha kwa mamia ya ya wanamgambo Boko Haram nchini humo hivi karibuni.
Jeshi la Nigeria linasema kujisalimishwa kwa wingi kwa wanachama wa Boko Haram kunatokana oparesheni kali ya kijeshi inayoendesha dhidi ya wanamgambo hao kaskazini mashariki mwa nchi.
Kifo cha kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau mwezi Mei huenda kumechangia hali hiyo.
- Abubakar Shekau: Mambo 5 yanayothibitisha kifo cha kiongozi wa Boko Haram aliyeogopwa
Baadhi ya wafuasi hao huenda wamejisalimisha kwa mamlaka au walijiunga kundi pinzani la wapiganaji- Islamic State Afrika Magharibi, ISWAP.
Mamlaka nchini Nigeria zinasema sasa wanatoa wasifu kwa wale ambao wamejisalimisha kwa lengo la kuwapa ushauri nasaha.
Lakini Wanigeria wengine wana wasiwasi juu ya kuwaunganisha tena wapiganaji wa zamani katika jamii- wakitaja hatari zinazoweza kutokea.
Kulingana na Umoja wa Mataifa uvamizi wa Boko Haram ulianza 2009 -umesababisha vifo vya watu 300,000 na mamilioni ya wengine kuachwa bila makao Nigeria na nchi nyingine kadhaa katika eneo la Ziwa Chad.
Kundi la kwanza la wanajeshi wanawake lahitimu Saudia
Kundi la kwanza la wanajeshi wa kike wa Saudia wahitimu kutoka Kituo cha Mafunzo ya Jeshi cha Wanawake Jumatano, baada ya kumaliza wiki 14 za mafunzo ya kimsingi yaliyoanza Mei 30.
Kulingana na gazeti la Arab News, Meja Jenerali Adel Al-Balawi, mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Vikosi vya Jeshi, alitoa hotuba ambayo alisema: “Kituo hiki kina ujumbe muhimu, ambao unazingatia kutoa programu bora za mafunzo na mitaala na mazingira bora ya kujifunzia.
“Inafanya hivyo kulingana na viwango vya ubora wa kimataifa ambavyo vinakidhi mahitaji. Hii inakusudia kuboresha utendaji wa jumla, ambako kutasaidia kufikia malengo ya wizara hapo baadaye."
Saudi Arabia imefungua usajili wa makurutu wanawake mnamo Februari mwaka huu.
Watu sita wafariki baada ya kuingia kinyemela kwenye mgodi Burkina Faso
Wachimbaji sita haramu walifariki baada ya kuteleza kwenye mashimo ya zamani ya mgodi wa dhahabu nchini Burkina Faso.
Wengine saba walijeruhiwa paada ya polisi kurusha vitoa machozi, manusura wanasema.
Polisi walisema wachimbaji hao walikfariki kutokana na ukosefu wa oksijeni kwenye mmigodi hiyo na hawakutoa tamko lolote kuhusu utumiaji wa vitoa machozi.
Maafisa wanasema migodi iliharibiwa na magari kuteketezwa na watu wa eneo hilo baada ya tukio hilo.
Uchimbaji haramu ni kawaida nchini Burkina Faso na serikali imekuwa ikihimiza umma kushirikiana na mamlaka kuipiga vitauovu huo.
Mtu mmoja awachoma visu watu sita New Zealand
Maafisa wa polisi nchini New Zealand wamempiga risasi na kumuua mtu mwenye itikadi kali aliyezua vurugubaada ya kuwachoma kisu na kuwajeruhi watu sitakatika duka moja la mjini Auckland Newzealand.
Waziri mkuu Jacinda Ardern alisema kwamba tukio hilo lilikuwa shambulio la kigaidilililotekelezwa na raia mmoja wa Sri Lankaambaye alikuwa akichunguzwa na polisi.
‘’Mshukiwa huyo ambaye hadi kufikia sasa hajatambuliwa , alichochewa na kundi la Islamic State IS’’ , alisema bi Ardern.
Polisi walimuua katika kipindi cha sekunde sitinisiku ya ijumaa.
‘’Kile kilichotokea leo , kilikuwa kitendo cha chuki ni makosa sana,’’ bi Ardern alisema katika mkutano na vyombo vya habari.
‘’Lilitekelezwa na mtu binafsi , sio dini’’.
Aliongezea kwamba , alisikia uchungu mwingi kusikia kuhusu shambulio hilo.
Kati ya watu sita waliojeruhiwa , watatu wako katika hali mahututi huku mmoja akiwa katika hali mbaya, kwa mujibu wa maafisa wa Afya.
‘’Wafanyakazi wa hospitali wanafanya kila kitu kulinda maisha yao’’, alisema meya wa mji wa Auckland Phil Goff akizungumza na BBC.
‘’Sote tumetishiwa na kilichotokea. Lakini haki ilikuja wakati mzuri kwa mshukiwa’’, aliongezea.
Je shambulio hilo lilifanyika vipi?
Lilifanyika katika duka la CountDownkatika duka la jumla la Lynn Mall katika wilaya ya New Lynn Ijumaa mchana
Mshambuliaji alidaiwa kuchukua kisu kikubwa kutoka katika rafu ya dukana kuanza kuwachoma kisu watu waliokuwa karibu naye .
Uchunguzi wa polisi ulikuwa umefungwa wakati huo.
Wasichana watano wa shule watoroka kutoka kwa watekaji nyara wa Nigeria
Wasichana watano kati ya makumi ya wanafunzi waliotekwa nyara kutoka shule moja ya upili katika jimbo la Zamfara kaskazini mwa Nigeria wametoroka kutoka kwawatekaji nyara wao .
Watu waliojihami kwa bunduki walishambulia shule yao katika mji wa Kaya-Maradun Jumatano na kuwateka zaidi ya wanafunzi 70 - wengi wao wakiwa wasichana - na mfanyikazi mmoja mwandamizi.
Wazazi wa wanafunzi hao waliiambia BBC kwamba watoto hao waliweza kutoroka wakati watu hao waliojihami walipokuwa wakiwagawanya katika vikundi kwa harakati zaidi kuelekea msituni. Walirejea nyumbani usiku sana.
Polisi wa Zamfara walithibitisha tukio hilo lakini walisema kwamba wasichana wa shule "waliokolewa" bila kutoa maelezo.
Vikosi vya usalama vinasema wanajaribu kupata makumi ya wanafunzi wengine ambao bado wameshikwa mateka .
Rais wa Burundi ashutumiwa kwa kumkosoa mwandishi wa habari
Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, ameshutumiwa kwa kumshambulia kwa maneno mwandishi wa habari aliyeangazia hali ya ugonjwa wa corona nchini humo.
Rais alikuwa amesema Esdras Ndikumana, ambaye ni mwanahabari wa kituo cha Ufaransa RFI, alikuwa akichafua taswira ya Burundi kutokana na habari yake.
Hata hivyo, Waandishi Wasio na Mipaka (RSF) walisema kuwa "matamshi hayo yana uzito mkubwa na hatari" ni "ukumbusho wa kusikitisha wa uhuru wa vyombo vya habari jinsi ulivyo dhaifu nchini Burundi."
Shirika la habari la RFI lilielezea "tuhuma za rais kama "zisizo na msingi na za kipuuzi."
Mkuu wa RSF Afrika Arnaud Froger alimsihi rais " kutotengeneza uadui pasipo na haja" na kuongeza kwamba anachostahili kufanya ni "kupambana na janga hilo badala ya kukabiliana na waandishi wa habari".
Siku za nyuma, kumekuwa na wasiwasi juu ya uhuru wa vyombo vya habari nchini Burundi.
Wauguzi wa Kenya kufanya kazi Uingereza
Wauguzi wasio na ajira na wahudumu wa afya kutoka Kenya watapata nafasi ya kufanya kazi nchini Uingereza kama sehemu ya mpango mpya ulioombwa na Serikali ya Kenya na kuzinduliwa na Rais Kenyatta wakati wa ziara yake huko London.
Katika mpango wa kushirikishana maarifa na utaalam, wataalamu wa afya wa Kenya na mameneja wa afya watafaidika na njia maalum ya kufanya kazi nchini Uingereza.
Waziri wa Leba Simon Chelugui alisema serikali imeanza kusafirisha wafanyikazi na wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu nje ya nchi hatua inayolenga kutatua tatizo la uhaba wa wauguzi 62,000 nchini Uingereza.
''Tunasafirisha wauguzi wa Kenya kwenda kufanya kazi nje ya nchi. Mwezi uliopita tulikuwa London na Rais Uhuru Kenyatta na tulifanya mazungumzo na serikali ya Uingereza, ambayo ilikubali kuchukua wahudumu 20,000 kutokana na uhaba wao wa wauguzi 62,000 ambao wamepata mafunzo nchini Kenya,” alisema alipojitokeza kwenye mkutano wa Kamati ya Bunge inayoshughulikia Kazi na Ustawi wa Jamii huko Mombasa.
Makubaliano hayo yako wazi kwa wafanyikazi wa ziada wa afya wa Kenya ambao wana sifa lakini hawana kazi, kuhakikisha mchakato huo unakuwa ni wenye faida kwa Kenya.
Awamu ya kwanza ya wauguzi itaondoka Kenya kufikia Oktoba 15.
Watu 12 wafariki DR Congo kutokana na mgodi uliovuja sumu Angola
Karibu watu 4,500 wameugua kusini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufuatia kuvuja kwa sumu kutoka kwa mgodi wa almasi katika nchi jirani ya Angola, waziri wa mazingira anasema.
Eve Bazaiba alisema watu 12 walikuwa wamefariki dunia.
Alisema kuwa DR Congo itauliza fidia ya uharibifu uliosababishwa lakini haikutaja kiasi.
Hata hivyo, hadi kufikia hivi sasa hakuna aliyesema chchote kujibu hayo hasa kutoka kwa kampuni ya madini.
Mwezi uliopita kulikuwa na uvujaji wa kutoka eneo la uhifadhi wa bidhaa za vyuma vizito uliosababisha mto kuwa na rangi nyekundu, samaki, viboko na wanyama wengine wakafa.
Muungano wa Ulaya kurudisha mamilioni ya chanjo za corona Afrika
Muungano wa Ulaya utarudisha mamilioni ya dozi ya chanjo za Johnson & Johnson zilizotengenezwa Afrika Kusini katika bara la Afrika.
Mjumbe maalum wa Muungano wa Afrika Strive Masiyiwa amewambia waandishi wa habari kwamba chanjo zote zinazotengenezwa “zitabakia Afrika na kusambazwa Afrika”.
“Swala limerekebishwa na limerekebishwa kwa njia chanya ,” amesema.
Hii inafuatia ukosoaji kwamba chanjo zinasafirishwa kutoka bara la Afirka ambalo lina viwango vya chini vya uchanjaji duniani.
Chini ya asilimia 3 ya idadi ya watu wa Afrika ndio waliochanjwa chanjo dhidi ya Covid-19.
Uganda inamshikilia msomi wa Rwanda kwa tuhuma za ujasusi
Vikosi vya usalama nchini Uganda vinamshikilia Makamu mkuu wa chuo Kikuu cha kibinafsi -Victoria University kwa madai ya ujasusi na kuishi nchini humo kinyume cha sheria, amesema msemaji wa jeshi Brigadia Jenerali Flavia Byekwaso.
Dkt. Lawrence Muganga, ambaye ni mzaliwa wa Rwanda alichukuliwa na maafisa ambao hawakuwa wamevaa sare kutoka katika ofisi yake mjini Kampala Alhamisi mchana.
Haijulikani iwapo kukamatwa kwake kuna uhusiano na Rwanda, ambayo ni nchi jirani na Uganda.
Mahusiano baina ya nchi hizo mbili wakati mwingine huwa ya wasi wasi- huku pande mbili zikilaumiana kila upande kuingilia maswala ya ndani ya nchi ya mwenzake.
Jenerali Byekwaso aliiambia BBC kwamba uchunguzi ulikuwa umeanza.
Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja hii leo ikiwa ni tarehe 03/09/2021