Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

'Kwanini nilimrusha mwanangu kwa watu nisiowajua kabisa'

Mama ambaye alimrusha mtoto wake kwa kundi la watu akiwa katika jengo la ghorofa lililokuwa likiteketea mjini Durban Afrika Kusini ameiambia BBC namna ambavyo anashukuru wale walioweza kumuokoa binti yake.

Moja kwa moja

Esther Namuhisa

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo haya mubashara. Kwaheri.

  2. Waasi wa Tigray wanazuia misaada, kuajiri wanajeshi wa watoto

    Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amekilaumu kikundi cha waasi cha TPLF kwa kushambulia maeneo yanakopitishwa misaada ya kibinadamu kwenye eneo linalokabiliwa na vita la Kaskazini mwa Tigray.

    Kikundi cha TPLF, kilichokuwa kinatawala jimbo la Tigray, na kufurumushwa mwenzi November na jeshi la Ethiopia, kimeungana sasa na vikundi vingine vya kijeshi na kuanzisha kundi la waasi la Tigray Defence Force (TDF).

    Waasi hao wanashikilia mji mkuu wa Mekelle tangu mwezi uliopita huku serikali ya Ethiopia ikiondoa vikosi vyake na kutangaza kusitisha mapigano ili kuruhusu shughuli za kilimo kufanyika na kutolewa kwa misaada ya kibinadamu.

    Lakini TPLF inataka kufanyika kwa makubaliano kupitia mazungumzo yatakayokuwa na sharti litakalojumuisha kuondolewa kabisa kwa vikosi vya Eritrea na vikosi vya Amhara.

    Katika taarifa yake, Waziri Mkuu Abiy alitupia lawama pia Jumuiya za kimataifa kwa kukalia kimya kile alichokisema kitendo cha TPLF kuwatumia watoto kama wanajeshi.

    Kikundi cha TPLF kilisema wiki hii kwamba kimeteka miji ya Korem na Alamata, kusini mwa Tigray mpakani mwa Amhara.

    Serikali ya Amhara imewarejesha wanajeshi wake wastaafu ili kusaidia wakati huu ambapo mapigano yanazidi kushamiri katika eneo la mpaka huo.

    Jumatatu hii, Marekani ilisema ina wasiwasi na hali ya usalama katika mpaka Amhara-Tigray na kusisitiza wito wake wa kufanyika kwa makubaliana ya kusitishwa kwa mapigano.

    Kuna hofu kwamba kuendelea kwa mapigano hayo kutazuia juhudi za kupeleka misaada ya kibinadamu kwa maelfu ya watu walioathirika na mapigano hayo.

    Wiki iliyopita Umoja wa mataifa ulisema mapigano hayo yamesababisha baa la njaa lililowakumba na kuathiri zaidi ya watu 400,000.

  3. Uporaji Afrika Kusini: Lori za Msumbiji zachomwa moto

    Lori zinazomilikiwa na raia wa Msumbiji zimeporwa na kuchomwa moto na waandamanaji katika nchi jirani ya Afrika Kusini, chama cha wasafirishaji mizigo Msumbiji kinasema.

    Shirikisho la Chama cha Usafiri Barabarani (Fematro) linasema hakuna majeruhiwa au vifo vilivyoripotiwa miongoni mwa madereva.

    Kisa hicho kilitokea mjini Durban, mkoa wa KwaZulu-Natal, ana kwengineko mkoani Gauteng, alisema Constantino Jotamo, mkurugenzi wa Fematro director.

    "Tunatafuta maelezo zaidi kuhusu kile kilichotokea," alisema

    Madereva wanahofia hali huenda ikaendelea kuwa mbaya zaidi katika siku zijazo.

    "Siku chache zilizopita zimekuwa ngumu sana,” anasema Rui Muianga, dereva wa lori katika barbara ya Maputo-Johannesburg.

    Siku ya Jumanne, ni magari matatu pekee ya usafiri wa umma ziliondoka Msumbiji hadi Afrika Kusini

  4. Dozi laki tatu za chanjo ya Corona kuingia Tanzania

      • Author, Munira Hussein
      • Nafasi, BBC Africa

    Tanzania inatarajia kuingiza dozi laki tatu za chanjo ya Covid-19 kutoka katika mpango wa COVAX ambao unalenga kusaidia nchi maskini.

    Waziri wa Afya bi. Doroth Gwajima amesema kuwa wanatarajia kuingiza dozi hizo kisha kuanza kugawa kwa wahudumu wa afya na kada zingine ambao ni mstari wa mbele katika kupambana na corona.

    ‘’Tumeshakamilisha taratibu zote za mpango wa Covax, na tunarajia kupokea asilimia ishirini ya chanjo ambayo ndio inayotolewa bure kisha Serikali tunafanya mpango wa kuongeza fedha kupata hizo asilimia zilizobaki.’’ Anasema Gwajima.

    Ameongeza pia Tanzania itaanza kutoa takwimu mpya za mwenendo wa corona kila baada ya wiki mbili na kuchapisha katika mtandao kama inavyoshauriwa na shirika la afya duniani.

    Kuhusu taarifa ya kukosena kwa mitungi ya gesi katika baadhi ya maeneo, amesema kuwa suala hili linatokana na watu wa maeneo hayo kutokuchukua tahadhari za Corona, hali ambayo imesababisha kuongeza kwa wagonjwa na uhitaji zaidi wa mitungi ya gesi.

    • Je taifa la Tanzania linakabiliwa na mlipuko uliojificha?
    • 'Kila anayekufa sio mgonjwa wa corona' asema Magufuli
  5. Fawzia kuwa mgombea pekee wa urais Somalia

    Mbunge mwanamke ametangaza kugombea wadhifa wa urais katika uchaguzi mkuu wa rais unaokuja.

    Fawzia Yusuf Adam anakuwa mwanamke pekee kati ya wagombea 10 , ambao wanatarajiwa kupigiwa kura Oktoba 10.

    Bi. Adam ni msaidizi wa zamani wa waziri mkuu na aliwahi kuwa waziri wa mambo ya nje.

    Atawania dhidi ya kiongozi aliyeko madarakani Mohamed Abdullahi Mohamed, anayejulikana kwa jina la utani la Farmajo, na wengine wawili waliowahi kuwa marais na wengineo.

    Bi Adam anasema atapumua na kuweka Somalia mpya.

    Viongozi wa Somalia wamekubaliana kuwa na uchaguzi mwezi Oktoba baada ya kusubiri kwa muda.

    Uchaguzi ulicheleweshwa kutokana na baadhi ya viongozi kushindwa kushiriki katika mazungumzo ya uchaguzi ambapo walisababisha maandamano kutotea.

    Uchaguzi wa Somalia huwa unafanyika na wawakilishi wa koo kabla ya siku ya kupiga kura.

  6. 'Kwanini nilimrusha mwanangu kwa watu nisiowajua kabisa'

    Mama ambaye alimrusha mtoto wake kwa kundi la watu akiwa katika jengo ambalo lilikuwa na moshi wa moto mjini Durban Afrika Kusini ameiambia BBC namna ambavyo anashukuru wale walioweza kumuokoa binti yake.

    “Jambo ambalo nililofanya ni kuwaamini watu ambao siwajui kabisa,” Naledi Manyoni alisema, aliongeza kusema kuwa yeye na binti yake Melokuhle wanaendelea vizuri baada ya tukio lile.

    BBC ilimpiga picha mama huyo akirusha mwanae mdogo Melokuhle wakati ghasia na uporaji ukiendelea katika mji wa Durban, siku ya Jumanne.

    Watu waliokuwa katika maduka ya chini waliwasha moto katika jengo ambalo bi Manyoni alikuwa amemtembelea mshirika mwenzie.

    Walikuwa katika gorofa la 16, wakati walipoanza kuhisi kuna moshi .

    Lifti zilikuw ahazifanyi kazi kwa sababu ya moto, hivyo bi Manyoni aliamua kutumia ngazi kushuka akiwa na mwanae.

    Hata hivyo hakuweza kufika gorofa la chini kwa kuwa kulikuwa na eneo ambalo lilikuwa limezuiwa.

    Aliweza kufika kwenye korido la gorofa la pili na kuomba watu wamsaidie kumdaka mwanae.

    “Kile nilichokuwa nawaza ni mwanangu aishi ,” alisema.

    Zima moto walifika katika eneo la tukio dakika 20 baada ya watu kuanza kuokoa wakazi wa eneo hilo - na hivyo ndivyo bi Manyoni alivyoweza kuwa na mtoto wake.

    Aliiambia BBC kuwa alifanikiwa kurudi katika gorofa alilokuwa anaishi saa sita usiku.

  7. Mshindi wa Miss Tanzania aenguliwa Miss World

    Maswali mengi yameibuka mtandaoni nchini Tanzania baada ya picha za mshindi wa pili wa taji la ulimbwende nchini humo kushirikishwa kuwa ndio atawakilisha Tanzania katika mashindano ya dunia.

    Huku taarifa zinasema Miss Tanzania, bi. Rose Manfere hataweza kushiriki mashindano ya urembo wa dunia yanayotarajiwa kufanyika Desemba 2021 nchini Puerto Rico na badala yake aliyekuwa mshindi namba mbili, Juliana Rugimisa ataliwakilisha taifa hiyo.

    Gazeti la Mwananchi limeandika , sababu iliyopelekea hatua hiyo kufikiwa ni baada ya kamati ya Miss Tanzania kuvunja mkataba na mlimbwende wa Tanzania mwaka 2020/2021 kwa kuwa Miss Rose Manfere alikiuka baadhi ya masharti ya mkataba.

    “Manfere bado ni miss Tanzania hajavuliwa taji, kuna makosa yalitokea amevunja mkataba lakini maamuzi ya kamati yameona kwamba asivuliwe taji lakini asiwe mwakilishi wa Tanzania kwenye Miss World kwa mwaka huu, Juliana ataenda kama mwakilishi wa Miss World Tanzania kwani mkataba unasema mshindi wa kwanza akishindwa kutekeleza majukumu yake kama mkataba unavyomwambia mshindi wa pili ndio atakuwa mwakilishi wa Miss World Tanzania, lakini Manfere bado ni Miss Tanzania, " Mwananchi imemnukuu mwakilishi wa kamati ya mandaalizi ya mashindano hayo, Azama Mashango .

  8. Tahadhari yatolewa kuhusu bunduki inayofanana na kitu cha kuchezea watoto

    Kampuni ya bunduki imekosolewa kwa kutengeneza bunduki inayofanana na silaha bandia ya kuchezea watoto.

    Culper Precision alisema silaha hiyo ya iliyopewa jina la Block19, ilitengenezwa ili kumpa raha mtumiaji wakati akiwa katika michezo ya kupiga risasi.

    Lakini mtengenezaji wa mwanasesere raia wa Denmark aliiandikia kampuni huyo kuacha kutengeneza silaha hiyo inayofanana na michezo ya kuchezea watoto ya 'Lego bricks'.

    Wafanya kampeni za kudhibiti matumizi ya bunduki wameeleza ubaya na hatari ya silaha hiyo.

    Shannon Watts, wa kundi la usalama wa bunduki katika kila mji limesema taasisi yake inahusishwa na Lego katika kutengeneza bunduki aina ya Block19 wiki iliyopita.

    Na kampuni ya Denmark imetuma barua kwa kampuni ya Culper Precision kutaka silaha hizo kusitishwa kutengenezwa.

    Bi Watts alikosoa kampuni hiyo ya bunduki ambayo iko Utah, wakisema ni hatari kwa watoto na inaweza kuwapelekea kutumia silaha hata kama bunduki haifanani na kitu cha kuchezea watoto.

    Culper Precision ilitoa taarifa ya kuamua kuzindua silaha hii ya Block19 na kuonesha jinsi bunduki inaweza kutumika na kila mtu na kufurahia kupiga risasi.

    Na kuongeza kuwa silaha hiyo inaweza kununuliwa na wale tu ambao wanaruhusiwa kisheria kumiliki bunduki.

    Rais wa Culper Precision bwana Brandon Scott aliliambia gazeti la Washington Post kuwa itakuwa na mazungumzo na wakili ili kuamua kama wataridhia maombi waliyopata kutoka Lego.

    Silaha hiyo inaonekana kuwa imeondolewa kwenye tovuti ya mtengenezaji wa bunduki.

  9. Julius Malema afungiwa kutumia Twitter kwa muda

    Kiongozi wa upinzani wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) nchini Afrika Kusini bwana Julius Malema amezuiwa kwa muda kuandika katika akaunti yake ya Tweeter kwa kukiuka miongozo ya Twitter, vyombo vya habari vya ndani vimeripoti.

    Mbuyiseni Ndlozi, mbunge na mwanachama wa chama cha EFF, Jumanne aliweka picha ya ujumbe ambao unaonesha kuwa bwana Malema amezuiwa kwa muda kuandika kwenye twitter.

    Bwana Malema amezuiliwa kuandika na kushiriki ujumbe wa wengine kwenye akaunti yake ya twitter kwa muda wa takribani saa 12.

    Bwana Malema alitishia kuhamasisha wafuasi wake kushiriki katika vurugu kubwa ambazo zinapinga kufungwa kwa Zuma, zilizoanzia KwaZulu-Natal na jimbo la Gauteng .

    “Hatutaki askari mtaani kwetu ! La sivyo, tunaungana na wanaoandamana.Wapiganaji wote wote wanapaswa kuwa tayari...hawawezi kutuua sisi sote. Tunataka suluhu ya kisiasa katika tatizo la kisiasa na sio wanajeshi ,” bwana Malema aliandika kwenye Tweeter akipinga wanajeshi kukabiliana na maandamano.

    Rais Cyril Ramaphosa alitoa agizo kwa wanajeshi kwenda katika majimbo mawili kusaidia kuzuia ghasia zilizosababishwa na kufungwa kwa rais wa zamani wa nchi hiyo Jacob Zuma.

    Bwana Ramaphosa alitoa onyo kwenye mitandao ya kijamii dhidi ya wanaoweka maudhui au taarifa za uongo na uchochezi mtandaoni.

    Mamlaka imesema watu wapatao 12 wanachunguzwa kwa kuhamasisha vurugu kupitia mitandao ya kijamii.

    Waziri wa kushughulia masuala ya polisi Beki Cele alisema wanafanyia uchunguzi ujumbe wa Twitter na binti wa Zuma, Dudu Zuma-Sambudla, kukosoa utendaji wa sheria.

    Akaunti ya Dudu ilishirikishwa mtandaoni ilikuwa inaikosoa serikali na kusifia au kuwahamasisha waandamanaji wanaopinga kufungwa kwa baba yake.

  10. Ghasia Afrika Kusini:Vifo vyaongezeka na kufikia 72

    Watu wapatao 72 wameuawa na zaidi ya watu 800 wamekamatwa katika ghasia hizo zilizoanza kama maandamano alhamisi iliyopita kupinga kwenda jela kwa rais wa zamani wa nchi hiyo Jacob Zuma.

    Aidha tume ya Umoja wa Afrika imelaani ghasia zinazoendelea Afrika Kusini zilizosababisha watu 72 kuuawa.

    Waandamanaji waligeuza maandamano hayo na kuwa ghasia mwishoni mwa wiki, wakichoma moto, kufunga barabara kuu na kuvamia na kupora maduka.

    "Mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, amelaani vikali vurugu hizo ambazo zimesababisha vifo vya raia na matukio mabaya ya uporaji wa mali ya umma na ya kibinafsi, uharibifu wa miundombinu, ikiwemo kusitishwa kwa huduma muhimu katika eneo la Kwazulu-Natal, Gauteng na maeneo mengine ya Afrika Kusini," tume imeeleza katika taarifa yake.

    Mamia ya wanajeshi yalitumwa kusitisha ghasia na uporaji Afrika Kusini kudhibiti machafuko hayo yaliyoibuka siku tano zilizopita.

    "Mwenyekiti ametoa wito wa jitihada za haraka kufanyika ili kurejesha amani na utulivu katika taifa hilo kwa kuzingatia utawala wa sheria. Alifafanua kuwa kushindwa kufanya hivyo athari itakuwa kubwa si kwa taifa hilo pekee bali kwa ukanda wote ," tume iliandika katika taarifa yake.

    • Rais wa zamani wa Afrika Kusini ajisalimisha mwenyewe polisi
    • Maandamano yashika kasi Afrika Kusini baada ya kukamatwa kwa Zuma
  11. Waziri azua gumzo baada ya kumnunulia mke wake gari

    Wafuasi vijana wa chama cha mabadiliko ya kidemokrasia(Congress for Democratic Change ) nchini Liberia wamepata hasira baada ya waziri mdogo katika ofisi ya rais kuonekana katika video akiwa anamzawadia mke wake gari la gharama huku akilimwagia shampeni.

    Tukio hilo liliripotiwa kuwa sherehe ya kuzaliwa kwa mke wake.

    Chama hicho cha vijana kimeelezea kitendo alichokifanya James Emmanuel Potter wiki iliyopita ni cha kizembe kwa kuonesha utajiri aliokuwa nao.

    Wamesema jambo kama lile linakanganya na kwenda tofauti na kanuni na itikadi za kuanzishwa kwa chama chake.

    Wafuasi hao wanamshutumu ofisa huyo ambaye ni msimamizi wa vifaa katika ofisi ya urais - kwa kutojali uhalisi wa wakati huo, katika moja ya nchi masikini zaidi Afrika.

    Lakini msaidizi huyo wa waziri alijibu baada ya kukosolewa na kuandika katika Facebook kuwa anafanya kazi ili kupata mshahara wa kumuwezesha kupata chochote kitakachompendeza.

    Hii ni video iliyowekwa Facebook ikimuonesha waziri mdogo huyo akimzawadia mke wake gari :

    Mtumiaji mmoja wa wa Facebook alimkosoa naibu waziri kwa kusema kitendo cha bwana Potter,kumnunulia mke wake Audi SUV na kumwaga shampeni ya gharama wakati wananchi wanaangaik na maisha. Je huyu ni maskini?"

    "Sababu moja kuwa maskini kwasababu ya ajira za serikali. Wanaishi maisha ya kifahari kwa gharama za watu maskini kuhangaika!" mtu mwingine aliandika.

    Wakati wengine walimtetea afisa huyo, akisema hakuna tatizo kwa mume kumnunulia mke wake gari . Anafanya kazi na naamini kipato chake kinamwezesha kununua gari hili dogo, acheni chuki".

  12. Habari...Karibu katika taarifa zetu za moja kwa moja leo ikiwa ni Jumatano 14/07/2021.