Maduka zaidi ya 200 yateketea soko la Kariakoo

Tathmini za awali zinaonesha kuwa maduka zaidi ya 220 yametekeketea kwa Moto.

Moja kwa moja

Esther Namuhisa

  1. Kufikia hapa hatuna la ziada kwa leo, tukutane kesho panapo majaaliwa!

  2. Watu 5 washikiliwa Nigeria kwa mapenzi ya jinsia moja

    Polisi wa kiislamu nchini Nigeria imewakamata watu watano wanaotuhumiwa kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

    Watu hao wamekama twa kaskazini mwa nchi hiyo kwa kukiuka sheria zinazokataza mapenzi ya jinsia moja.

    Mbali na kukatazwa kisheria, mapenzi ya jinsia moja ni kosa kwa sharia za kiislamu ambazo zinatumiwa karibu katika majimbo mengi ya kaskazini mwa nchi hiyo, likiwemo la Kano.

    Bodi ya Polisi wa kiislam katika jimbo la Kano alisema walivamia katika maficho ya watu hao katika eneo la Kumbotso baada ya kupata malalamiko kuhusu vijana hao.

    Kwa mujibu wa sheria za kawaida za nchi hiyo, ukipatikana na hatia ya kushiriki mapenzi ya jinsia moja nchini humo, unahukumiwa kifungo cha kwenda jela mpaka miaka 14 au kuhukumiwa kifo kwa sheria za kiislamu.

    Vitendo vya kutiwa mbaroni na kushitakiwa kwa watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja nchini Nigeria vimeongezeka tangu kupitishwa kwa sheria mpya mwaka 2014. Ingawa ni mara chache sana wanahukumiwa.

  3. Safaricom yashitakiwa kwa ubaguzi

    safari

    Chanzo cha picha, AFP

    Kampuni ya mtandao mkubwa wa simu, Safaricom imetakiwa kulipa fidia ya dola $60,000 (£42,000) kwa kukataa kumuajiri mwanaume ambaye haoni.

    Wilson Macharia alituma maombi ya huduma kwa wateja katika kampuni ya Safaricom na licha ya kualikwa kwenda kusaini mkataba wa ajira, hakupewa kazi hiyo kwasababu kampuni hiyo haina vitendea kazi vinavyoweza kumsaidia kufanya kazi yake huku haoni.

    Safaricom ilikanusha madai hayo ya kibaguzi , ikidai kuwa kampuni haina vitendea kazi au mifumo ya kufanyia kazi kwa walemavu wa macho.

    Mahakama ya Kenya imetoa hukumu kuwa Safaricom imeminya haki ya bwana Macharia kwa kushindwa kuwa na utu na kumnyima fursa ya kazi.

    Jaji alisema Safaricom, ilifahamika fika kuwa mtu aliyeomba kazi alikuwa haoni, badala ya kumtaarifu wakati wa mchakato lakini walifikia mpaka hatua ya kusaini mkataba, na baadae kumwambia kuwa walituma mualiko kimakosa.

  4. Watu 45 wauawa katika ghasia za kumuunga mkono Zuma

    45

    Chanzo cha picha, EPA

    Watu wapatao 45 wamefariki kwenye ghasia zinazoendelea katika maeneo mbalimbali nchini Afrika Kusini, tangu kujisalimisha kwa rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma wiki iliyopita.

    Karibu watu 800 wamekamatwa katika ghasia hizo zilizoanza kama maandamano alhamisi iliyopita kupinga kwenda jela kwa Zuma.

    Lakini waandamanaji waligeuza maandamano hayo na kuwa ghasia mwishoni mwa wiki, wakichoma moto, kufunga barabara kuu na kuvamia na kupora maduka.

    south

    Jeshi limepelekwa katika maeneo mbalimbali kuongeza nguvu na kusaidiana na Polisi kuzima ghasia hizo.

    Waziri wa Polisi Bheki Cele amewaambia waandishi wa habari jana leo kwamba uporaji unaendelea na ipo hofu kwamba, kuna baadhi ya maeneo yatakuwa na uhaba wa bidhaa za msingi.

    • Rais wa zamani wa Afrika Kusini ajisalimisha mwenyewe polisi
    • Maandamano yashika kasi Afrika Kusini baada ya kukamatwa kwa Zuma
  5. Umoja wa Ulaya waidhinisha mafunzo ya kijeshi Msumbiji

    mm

    Chanzo cha picha, AFP

    Umoja wa Ulaya (EU) umeidhinisha mafunzo ya kijeshi nchini Msumbiji ili kuvisaidia vikosi vya kijeshi na kuwalinda raia.

    Ina mpango wa kutoa mafunzo na kusaidia jeshi katika kuimarisha usalama kaskazini mwa Cabo Delgado, ambako kuna vurugu zinazosababishwa na mashambili ya kigaidi tangu mwaka 2017.

    Zoezi hilo litajumuisha mafunzo ya kijeshi pamoja na maandalizi ya operesheni haswa mafunzo ya kukabiliana na ugaidi, na mafunzo ya kuwalinda raia.

    Mpango huo utachukua muda wa miaka miwili.

    “Katika kipindi hiki, malengo ya mkakati huo yatasaidia jeshi la Msumbiji kuunda kikosi cha kukabiliana na suala hilo ” taarifa kutoka baraza la umoja wa ulaya imeeleza.

    Ni zaidi ya miaka mitatu iliyopita, zaidi ya watu 2,800 wameuawa katika vurugu zilizosababisha watu kuuawa na vilevile watu wapatao 900,000 kukimbia makazi yao.

  6. Marekani yahofia mvutano kuongezeka Tigray

    ethiopia

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Marekani imesema kuwa ina wasiwasi mkubwa juu ya mvutano na ripoti za mapigano yanayoendelea katika eneo la Tigray, Magharibi mwa Ethiopia.

    Wasiwasi huo umekuja baada ya Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa ulaya, Josep Borrell, ambaye amezitaka nchi wanachama kuzingatia kuweka vikwazo juu ya mgogoro huo.

    Marekani imesisitiza kuwepo na makubaliano ya kusitisha mapigano, ingawa mapigano yameripotiwa katika maeneo ya Tigray na Amhara eneo ambalo lina ghasia.

    Wapiganaji wa kundi la kisiasa la Tigray People’s Liberation Front (TPLF), sasa wanadai kuwa wamechukua mji wa Korem na Alamta wakiwa wanaelekea eneo la kusini.

    Kuna wasiwasi kuwa mapigano yanaweza kuendelea na kupunguza jitihada za kutoa misaada ya kibinadamu kwa mamilioni ya raia walioathirika na janga hilo.

    Maelfu wanaaminika kuuawa ndani ya miezi nane ya vita, huku zaidi ya watu milioni mbili wamelazimika kukimbia makazi yao.

    Mwezi uliopita , wapiganaji wa TPLF wameweza kuchukua miji muhimu - ukiwemo mji mkuu katika eneo la Tigray. Serikali ilitangaza kusitisha mapigano na kuondoa majeshi yake.

  7. Maduka zaidi ya 200 yateketea soko la Kariakoo

      • Author, Humphery Mgonja
      • Nafasi, BBC Field Producer
    Maelezo ya video, Maduka yapatayo 200 yateketea na moto soko la Kariakoo

    Tathmini za awali zinaonesha kuwa maduka zaidi ya 220 yametekeketea kwa Moto.

    Serikali imeagiza masoko yote na vituo vya mabasi kuwa na huduma za zima Moto ili kupunguza changamoto zinazotokea majanga kama hayo.

    Mwisho wa Juma lililopita Soko la Kariakoo liliungua huku bado chanzo cha Moto huo hakijafahamika.

    Humphrey Mgonja kafika kariakoo na kuandaa taarifa ifuatayo

  8. Chama cha upinzani Afrika kusini chakemea kutumwa kwa jeshi kupambana na waandamanaji

    sa

    Chanzo cha picha, EPA

    Chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) kimelaani kupelekwa kwa wanajeshi katika majimbo yaliyokumbwa na ghasia ya Gauteng na KwaZulu-Natal.

    Katika taarifa iliyotolewa muda mfupi baada ya hotuba Rais Cyril Ramaphosa kwa taifa , EFF ilitoa wito wa "kutumiwa kwa suluhisho la kisiasa katika ghasia zilizoenea".

    south

    Chanzo cha picha, Reuters

    Chama hicho kilisema kupelekwa kwa wanajeshi mitaani sio suluhisho la machafuko ya wenyewe kwa wenyewe na kwamba haitakuwa sehemu ya uamuzi wowote wa kuhalalisha kupelekwa kwa jeshi.

    EFF imesema mawakili wake wataandika barua kwa rais kujua "msingi wa kisheria wa kupelekwa kwa wanajeshi". Iliongeza kuwa itachukua "hatua zinazofaa" ikiwa rais atashindwa kujibu barua hiyo kwa masaa 12.

    m

    Chanzo cha picha, Reuters

    m

    Chanzo cha picha, Getty Images

  9. Ndege ya Uganda yachelewesha safari kwa kuishiwa mafuta Tanzania

    tz

    Abiria wanaokwenda Uganda kwa kutumia ndege aina ya Uganda Airlines walichelewa kuondoka jana jioni katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini, Dar es Salaam nchini Tanzania kwa saa kadhaa baada ya kuishiwa mafuta, gazeti la Daily Monitor limeandika.

    Ndege hiyo ilieleza sababu ya kuchelewesha safari yake ni kutokana na kuchelewa kupokea mafuta ambayo walikuwa wameyaagiza.

    Aidha uongozi wa kampuni hiyo ya ndege iliandika taarifa katika mitandao ya kijamii kuomba radhi kwa tukio lililotokea na kuhaidi tukio hilo kutojirudia siku zijazo.

  10. Watekaji wamuachia huru kiongozi maarufu wa kiislamu Nigeria

    nigeria

    Kiongozi maarufu wa kiislamu, Emir Alhassan Adamu, ambaye alitekwa Jumamosi na wanaume wenye silaha kaskazini magharibi mwa Nigeria katika jimbo la Kaduna, ameachiwa huru.

    Ndugu zake kumi na mbili ambao walichukuliwa pia , wameachiwa pia.

    Haijawekwa wazi namna Emir Adamu alivyopata uhuru wake lakini mtoto wake wa kiume ameiambia BBC kuwa watekaji hawakulipwa fedha.

    Kumekuwa na matukio mengi ya utekaji kaskazini mwa Nigeria na kukiwa na wanafunzi zaidi ya 1,000 wakiwa wametekwa kutoka shuleni au vyuoni tangu mwezi Desemba.

    Ingawa watu wengi wanaotekwa uachiwa huru mara baada ya watekaji kulipwa fedha, ingawa mpaka sasa tisa wamefariki na watu wapatao 200 hawajulikani walipo.

    Utekaji nyara kwa ajili ya kupata fedha imekuwa biashara inayokuwa kwa kasi , na inasadikiwa kuwa wahuni hao huwa wanapata msaada kutoka kwa wanaijeria wenye wadhifa wakiwemo wakala wa usalama.

  11. Mke wa rais wa Ghana kurudisha marupurupu yake

    ghana

    Mke wa rais wa Ghana anataka kurejesha fedha za marupurupu anayopatiwa tangu rais aingie madarakani mwaka 2017, baada ya wananchi kulalamikia mshahara wake.

    Vilevile Rebecca Akufo-Addo alisema hatakubali mshahara ambao ulipitishwa na bunge hivi karibuni.

    Alisema katika taarifa yake kuwa aliamua kurudisha fedha zote ambazo alipewa kama ruzuku ambazo ni dola 151,618.

    Alisema alikuwa hajaomba kulipwa na amepokea tu kutokana na wadhifa wake ingawa si rasmi.

    Alisema ameamua kurudisha fedha hizo kutokana na maoni mabaya ambayo yametolewa na baadhi ya wananchi na kwa upande mwingine haipendezi , na kama inamuwasilisha kuwa fisadi, mbinafsi na mwanamke ambaye hajali maslahi ya raia wa Ghana”.

    Mke wa rais na mke wa makamu wa rais wa Ghana
    Maelezo ya picha, Mke wa rais na mke wa makamu wa rais wa Ghana

    Wiki iliyopita,raia wa Ghana ameelezea kutokubaliana na maamuzi ya wabunge ya kuthibitisha mishahara ya wake wa rais na makamu wa rais kutokana na jukumu lao wanalopewa.

    Wake hao walipangiwa kulipwa kiasi cha dola $3,500 (£2,500) kila mwezi , kiwango sawa na wanacholipwa mawaziri kufuatiwa mapendekezo yaliyotolewa na kamati ya bunge mwaka 2019.

    Mke wa rais na mke wa makamu wa rais wamekuwa wanapokea marupurupu kwa miaka mingi kutokana na nyadhifa zao.

  12. Habari...Karibu katika taarifa zetu za moja kwa moja leo ikiwa ni Jumatatu 13/07/2021.