Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Jeshi kukabiliana na waandamanaji wanaopinga kufungwa kwa Zuma

Afrika Kusini imepeleka jeshi kukabiliana na ghasia zilizotokea baada ya kufungwa kwa rais wa zamani wa taifa hilo Jacob Zuma.

Moja kwa moja

Esther Namuhisa

  1. Kufikia hapa tunatamatisha matangazo yetu mubashara kwa leo. Tukutane kesho panapo majaaliwa!

  2. Maafisa Usalama wapelekwa Kaskazini mwa Kenya kudhibiti mapigano ya kikabila

    Timu maalumu ya wana usalama imepelekwa Kaskazini mwa nchi hiyo, ikiwa ni wiki moja toka kuzuka kwa mapigano ya kikabila katika eneo la Marsabit.

    Mapigano hayo yamesababisha vifo vya watu 10, maelfu ya wengine kuyakimbia makazi yao huku mamia ya mifugo ikielezwa kuibiwa.

    Katika mapigano hayo ya sasa yamesababisha pia baadhi ya nyumba kuchomwa moto na shule kadhaa zikifungwa, wakati huu ambao wanafunzi wakiendelea na mitihani yao ya mwisho.

    Chanzo cha mapigano hayo inadaiwa pamoja na mambo mengine ni yanatokana na kugombea rasilimali.

    Kwa miaka kadhaa sasa kumekuwa kukizuka kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe na kuathiri mamia ya watu katika eneo hilo ,la mpakani mwa Ethiopia.

    Mwaka 2015 Umoja wa Mataifa ulisema takriban Wakenya 310 waliuwawa na wengine zaidi ya 215,000 kulazimika kuyakimbia makaazi yao 2015 kutokana na machafuko ya aina hiyo.

  3. Umoja wa Mataifa: Kiwango cha njaa chaongezeka duniani

    Umoja wa Mataifa unaonya kuwa viwango vya njaa duniani vinaongezeka kwa kasi. Ripoti iliyotelwa na mashirika matano ya Umoja wa Mataifa inasema asilimia kumi ya idadi ya watu ulimwenguni hawapati vyakula venye virutubishi vya kutosha hiyo ikiwa ni zaidi ya watu milioni mia nane.

    Ripoti hiyo inaongeza kuwa bara la Afrika ndilo lilioathirika zaidi huku humusi moja ya Waafrika wakiwa hawana chakula cha kutosha. Janga la Corona linatajwa kusababisha hali ya upataikanaji wa chakula kuwa mbaya zaidi kwani imesababisha uchumi kusuasua na kuhujumu upatikanaji wa chakula.

    Mashirika hayo yanasema mlo ulio na virutubishi huwa wa gharama na watu wasiopungua bilionio tatu hawawezi kumudu. Yanataka hatua kuchukuliwa kupunguza gharama ya vyakula vyenye virutubishi na kulinda mfumo wa mzunguko wa chakula.

  4. Jeshi kukabiliana na waandamanaji wanaopinga kufungwa kwa Zuma

    Afrika Kusini imepeleka jeshi kukabiliana na ghasia zilizotokea baada ya kufungwa kwa rais wa zamani wa taifa hilo Jacob Zuma.

    Maduka yalivamiwa na majengo yalichomwa moto siku ya Jumatatu, wakati Zuma akisikiliza kesi yake katika mahakama ya juu.

    Watu wapatao sita wameuawa na 200 kukamatwa tangu ghasia hizo zianze wiki iliyopita.

    Zuma amehukumiwa kwa kosa la kuidharau mahakama baada ya kushindwa kuhudhuria kesi yake ya madai ya rushwa wakati wa utawala wake.

    Zuma mwenye umri wa miaka 79, ambaye alikanusha kuhusika katika madai ya rushwa, lakini alienda mwenyewe polisi wiki iliyopita ili kuanza kfungo chake cha miezi 15.

    Akiwa anatarajia kifungo chake kupunguzwa katika mahakama ya katiba. Hata hivyo wataalamu wa sheria wanasema nafasi ya kushinda ni ndogo sana.

    Kesi hiyo imeibua matukio ambayo hayakutarajiwa nchini humo ambapo hawajawahi kushuhudia kuona rais wa zamani akifungwa gerezani.

    Jumatatu ,picha za video zilionesha maduka makubwa yakichomwa moto katika mji wa Pietermaritzburg, katika eneo alikotokea Zuma, KwaZulu-Natal, na watu wakifanya maandamano.

    Ghasia zilienea mpaka Johannesburg, katika jimbo la Gauteng.

    Jumapil , waandamanaji walionekana wakiandamana katika maeneo ya biashara ya mjini Johannesburg.

    Jeshi limesema limeagizwa kwenda kusaidia kupunguza ghasia ambazo zimekuwa zikiendelea kwa siku kadhaa.

    Rais Cyril Ramaphosa amesisitiza utulivu , akisema hakuna maelezo juu ya vurugu hizo.

    Zuma alikamatwa kawa kukaidi maelezo ya kutoa ushaidi juu ya kesi ya rushwa ilyokuwa inamkabili wakati yuko madarakani.

    Alihudhuria mara moja tu kwenye uchunguzi wa kile kilichojulikana kama madai ya kuporwa kwa mali za serikali.

  5. Magazeti yaweka kampeni kupinga mswada tata dhidi ya vyombo vya habari Nigeria

    Raia wa Nigeria wataona vichwa vya habari vinavyofanana katika magazeti yote nchini humo kwa siku ya Jumatatu Julai 12 na Julai 13.

    Hii ikiwa ni kampeni ya tasnia ya habari iliyoanzishwa na wahariri, waandishi na wamiliki kupinga kutangazwa kwa miswada itakayodhoofisha uhuru wa vyombo vya habari nchini humo.

    Taarifa hiyo ikiwa na neno la 'taarifa kufungiwa' na picha inayomuonesha mtoto akiwa katika nguzo za gerezani zinazomfunga mdomo.

    Baraza la habari nchini Nigeria (NPC), na tume ya utangazaji ya taifa (NBC) imetoa orodha ya mswada ambao utamtaka mwandishi au mmiliki wa chombo cha habari kulipishwa faini ya dola $12,100 kwa kutoa habari isiyo na ukweli na kutokuwa huduma isiyokuwa na viwango bora.

    Kama mswada huo utapitishwa na kuwa sheria, wale watakao kamatwa watafungwa gerezani kwa kipindi cha miaka mitatu.

    Mwezi uliopita mwenyekiti wa Jumuiya ya kitaifa wa seneta ya tume ya vyombo vya habari na utangazaji, seneta Ajibola Basiru, alitetea mswada huo.

    "Ukweli ni kwamba mtu anayesimamia shughuli za vyombo vya habari kama redio, televisheni haimaanishi kuwa anataka kuminya uhuru wa vyombo vya habari, "alisema.

    Jumuiya ya waandishi wa habari (NUJ), Chama cha wahariri Nigeria (NGE) na Jumuiya ya wamiliki wa magazeti (NPAN) wanaamini kuwa sababu ya marekebisho ya sheria hiyo ni kutaka kuwa na uwezo wa kudhibiti na kufuatilia kile watakachokichapisha, " ambapo pia inawanyima jamii haki ya kusikilizwa au kusikia kile kilicho haki yao’", walisema.

    Kampeni hii itadumu kwa muda wa siku mbili.

  6. Maelfu waandamana kulaani kushuka kwa uchumi Cuba

    Maelfu ya raia wa Cuba wamejumuika katika maandamano makubwa kuwahi kufanyika kwa miongo dhidi ya serikali ya kikomunisti. Picha za mitandao ya kijamii yanaonesha kuwa vyombo vya usalama vinawapiga na kuwashikilia baadhi ya waandamanaji.

    Wameandamana mijini, ukiwemo mji mkuu Havana wakiimba na kupaza sauti kuishutumu serikali wanayoitaja ya kidikteta na kutaka uhuru. Wacuba wameghadhabishwa na kuporomoka kwa uchumi, kubanwa kwa uhuru na haki za kiraia na jinsi maafisa nchini humo wanavyolishughulikia janga la Corona.

    Waandamanaji hao wanataka mpango wa utoaji wa chanjo kuharakishwa baada ya Cuba kuripoti zaidi ya wagonjwa elfu saba wa maambukizi ya Corona kwa siku na vifo visivyopungua 47 jana Jumapili.

    Mwaka jana, uchumi wa Cuba ambao kwa kiasi kikubwa unadhibitiwa na serikali ulipungua kwa asilimia kumi na moja ukitajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita. Uchumi huo unasemekana umeathirika vibaya hivyo kutokana na janga la Corona na vikwazo vilivyowekwa na Marekani dhidi ya taifa hilo.

    Maelfu ya wafuasi wa serikali pia wameandamana baada ya rais kuwahimiza kulinda mapinduzi wakiangazia maandamano ya kutaka ukombozi yaliyofanyika mwaka 1959 na kupelekea utawala wa Kikomunisti Cuba. Rais Miguel Diaz Canel amesema maandamano hayo ni uchochezi kutoka kwa mamluki anaodai wamekodishwa na Marekani kuliyumbisha taifa hilo.

    Akilihutubia taifa kupitia televisheni Rais Canel amesema maagizo ya kuanza mapambano mitaani yashatolewa kwa wanamapinduzi ili kulilinda taifa. Mwanadiplomasia mwandamizi wa Marekani katika Amerika ya Kusini Julie Chung ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa wanatiwa wasiwasi mkubwa na wito huo wa mapambano na kuongeza kuwa wanawaunga mkono raia wa Cuba wanaotaka kuandamana kwa amani lakini wakati huo huo wanatoa wito wa kuwepo utulivu na kulaani ghasia za aina yoyote.

    Mmoja wa waandamanaji hao aliyejitambulisha kwa BBC kama Geovanis Gonzalez amesema hawawezi tena kustahimili ugumu wa maisha kwani hawana chakula, dawa wala uhuru. ''Tuko hapa kwasababu ya kupinga ukandamizaji dhidi ya watu. Wanatunyima chakula ili tufe. Havana inaporomoka. Hatuna makazi, hatuna chochote lakini wana fedha za kujenga mahoteli na sisi twafa njaa "

    Maandamano ya kupinga serikali yalianzia mjini San Antonio de los Banos kusini magharibi mwa mji mkuu Havana lakini muda mfupi yalisambaa kote nchini humo. Watu walitumia mitandao ya kijamii kuonesha moja kwa moja kwa moja maandamano hayo huku waandamanaji wakimshutumu vikali rais.

  7. Wanafunzi wenye corona wafanya mtihani wa taifa Rwanda

    Wanafunzi wa shule za msingi wameanza mitihani ya taifa siku ya Jumatatu wakati taifa likikabiliana na wimbi baya la mlipuko wa corona.

    Wizara ya elimu imesema wanafunzi waliopata maambukizi ya virusi vya corona wataweza kufanya mitihani katika vyumba tofauti.

    “Bahati ni kuwa hakuna ambaye yuko mahututi”, waziri wa elimu bi. Valentine Uwamariya alikiambia chombo cha habari cha taifa.

    Wanafunzi wanafanya mitihani katika vituo 1,021 katika taifa zima, karibu zaidi ya mia moja zaidi ya miaka miwili iliyopita, ili kuruhusu watu wakae kwa mbalimbali.

    Wanafunzi wenye virusi vya corona wanapaswa kusindikizwa na wazazi au mlezi kwenda kwenye kituo cha mtihani na kumrudisha nyumbani, wizara imeagiza.

    Maofisa wa afya wa Rwanda walithibitisha wiki iliyopita uwepo wa dalili za wimbi la Delta , wakati taifa likiwa na wastani wa wagonjwa 800 kila siku katika wiki nne zilizopita.

    “Kuna wagonjwa mahututi zaidi na vifo zaidi... na hatujawahi kufikia hapa kabla.” Waziri wa afya alisema wiki iliyopita.

  8. Zanzibar yaanza kutoa Chanjo kutoka China

      • Author, Munira Hussein
      • Nafasi, BBC Africa

    Wahudumu wa afya visiwani Zanzibar wameanza kupokea dozi ya kwanza ya chanjo ya covid-19.

    Serikali ya Zanzibar imethibitisha kuwa dozi za Sinocav kutoka nchini China zimeanza kutolewa kwa awamu ya kwanza huku awamu ya pili ikitarajiwa kufanyika baada ya wiki mbili kutoka sasa.

    ‘’Tumeanza kutoa chanjo wiki iliyopita kwa wahudumu wetu wa afya, tunawapa chanjo ya Sinovac kutoka China ambayo imepitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

    Tuna wahudumu wa afya elfu sita lakini kwa sasa tutaanza na nusu yao,’’ Katibu wa wizara ya Afya Zanzibar Dkt Omary Dadi Shajak ameieleza BBC.

    Kwa mujibu wa Dkt Shajak chanjo hiyo awali ilipangwa kutolewa kwa mahujaji waliokua waende Makka, lakini kutokana na kuzuiwa kwa mahujaji kutoka nje ya Saudi Arabia, Wizara hiyo imeamua kutumia chanjo kwa wahudumu wa Afya.

    Mpango huo wa chanjo hata hivyo unawalenga wahudumu wa afya wa Zanzibar pekee. Dkt. Shajak ameongeza pia chanjo ya pamoja na Tanzania bara itatolewa kwa utaratibu maalum kupitia mpango wa Covax.

  9. Uporaji na machafuko yanaendelea kabla ya kesi ya Zuma

    Maandamano yenye ghasia yameendelea nchini Afrika Kusini usiku kucha na Jumatatu asubuhi juu ya kufungwa jela kwa rais wa zamani Jacob Zuma.

    Duka moja kubwa huko Pietermaritzburg, katika mkoa wa KwaZulu-Natal lilichomwa moto Jumatatu asubuhi wakati uporaji na uharibifu wa mali ukiendelea Jumatatu asubuhi.

    Picha za jengo hilo likiteketea moto na usumbufu uliosababishwa na maandamano hayo zimesambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii:

    Makumi ya watu wamekamatwa na barabara zimefungwa wakati vikosi vya usalama vikishughulikia vurugu zinazoendelea.

    Maandamano hayo yanaendelea huku mahakama ya kikatiba ikisikiza rufaa ya Zuma dhidi ya kifungo chake kwa kukaidi agizo la mahakama.

    Korti inafanya tathmini ya uamuzi wake wa hapo awali na huenda ikatoa maagizo baadaye ikiwa hukumu hiyo itatekelezwa.

    • Maandamano yashika kasi Afrika Kusini baada ya kukamatwa kwa Zuma
    • Jacob Zuma: Rais wa zamani wa Afrika Kusini ambaye uongozi wake ulikumbwa na utata mwingi
  10. Afrika Kusini yashtushwa na kuwasili kwa wanajeshi wa Rwanda nchini Msumbiji

    Afrika Kusini yashtushwa na kuwasili kwa wanajeshi wa Rwanda nchini Msumbiji

    Waziri wa Ulinzi wa Afrika Kusini Nosiviwe Mapisa-Nqakula amesema wanajeshi wa Rwanda hawakutakiwa kuwasili Msumbiji kabla ya wale wa serikali za eneo hilo .

    Waziri huyo alisema haikukubaliwa na wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) kwamba wanajeshi wa Rwanda wangefika kwanza.

    "Inasikitisha kwamba kuja huko kunafanyika kabla ya kupelekwa kwa wanajeshi wa Sadc, kwa sababu kando na uhusiano wowote kati ya Rwanda na Msumbiji, mtu angetegemea Rwanda kwenda Msumbiji kwa muktadha wa agizo lililotolewa na wakuu wa nchi katika eneo la Sadc, " alisema.

    Waziri huyo alisema hili lilikuwa suala la pande mbili, "hali ambayo hatuna udhibiti juu yake"

    Wanajeshi wa Sadc wanatarajiwa kuwasili Msumbiji Alhamisi.

    Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi alithibitisha kuwasili kwa wanajeshi wa Rwanda kusaidia vita dhidi ya wapiganani wa kundi la kigaidi ambalo limekuwa likifanya mashambulio katika wilaya za Kaskazini mwa nchi hiyo katika mkoa wa Cabo Delgado, tangu Oktoba 2017.

    • Kwanini ni vigumu kukabiliana na kundi la IS Msumbiji?
    • Cabo Delgado: Uhusiano uliopo kati ya mali asili,uasi na mapigano nchini Msumbiji
  11. Simba watwaa ubingwa kwa mara ya nne mfululizo

      • Author, Eagan Salla
      • Nafasi, BBC Swahili, Dar es Salaam

    Klabu ya soka ya Simba nchini Tanzania imetwaa kwa mara ya nne mfululizo taji la ubingwa wa ligi kuu wa soka Tanzania bara baada ya kujikita kileleni wakiwa na alama 79 huku wakiwa wamesaliwa na michezo miwili kukamilisha msimu wa 2020/21.

    Simba walijitangazia ubingwa baada ya kumalizika kwa mchezo wake dhidi ya Costal Union ambapo waliibuka na ushindi wa mabao mawili yaliyowekwa kimiani kipindi cha kwanza na nahodha John Bocco na Chris Mugalu .

    Alama walizojikusanyia Simba haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote ya ligi kuu kwa idadi ya michezo iliyosalia wakiwemo watani wao wa jadi Yanga ambao wako nafasi ya pili.

    Simba imekuwa na rekodi nzuri kwenye michuano ya ndani pamoja na ile ya kimataifa, wengi wakifungamanisha matokeo mazuri ya uwanjani na uwekezaji mkubwa alioufanya bilionea Mohamed Dewji kwenye klabu hiyo yenye makao yake makuu mitaa msimbazi kariakoo, jijini Dar es Salaam.

  12. Watu 11 wauawa na radi wakijipiga picha ‘selfies’ India

    Radi imepiga na kuua takribani watu 11 na wengine kujeruhiwa huko Jaipur kaskazini mwa India siku ya Jumapili.

    Watu hao walikuwa wakijipiga picha (selfie ) kwenye mvua wakiwa juu ya jengo eneo ambalo ni maarufu katika kivutio cha utalii.

    Watu 27 walikuepo katika jengo hilona wakati kuta za ngome wakati tuko hilo likitokea – na baadhi waliripotiwa kuruka mpaka chini.

    Radi huua watu wapatao 2,000 nchini India kwa wastani kila mwaka.

    Afisa mkuu wa polisi aliviambia vyombo vya habari kuwa watu wengi waliouawa katika jengo hilo walikuwa vijana.

    Jumapili peke yake, wameshuhudia zaidi ya vifo tisa vikiripotiwa katika jimbo la Rajasthan ambako Jaipur ipo , kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani.

    Kiongozi wa jimbo hilo , Ashok Gehlot,alitangaza kutoadola 6700 sawa na 500,000 rupees kama fidia kwa familia zilizopoteza wapendwa wao.

    Msimu wa mvua kubwa nchini India, hunyesha Juni mpaka Septemba.

    Mamlaka ya hali ya hewa nchini India (IMD) imesema vifo vya radi vimeongezeka mara mbili nchini humo tangu miaka ya 1960 – sababu inayotajwa ni mabadiliko ya tabia nchi.

    Takwimu zinasema matukio ya radi yanaongezeka kwa 30%-40% tangu mwanzoni na katikati ya mwaka -1990.

  13. Shirikisho la FA lakemea ubaguzi wa rangi dhidi ya Marcus Rashford, Jadon Sancho na Bukayo Saka

    Shirikisho la soka nchini Uingereza limelaani ubaguzi wa rangi dhidi ya wachezaji wa England Marcus Rashford, Jadon Sancho na Bukayo Saka baada ya fainali ya siku ya jumapili ya kombe la Euro 2020 walioshindwa na Italia kupitia mikwaju ya penalti.

    Wachezaji wote watatu walikosa kufunga magoli yao ya penalti katika mchuano huo walioshindwa mabao 3-2 na walilengwa katika mitandao ya kijamii baada ya mchuano huo. Polisi wa eneo la Metropolitan wanachunguza ubaguzi huo na wamesema ‘Hautavumiliwa’ FA imesema ‘imeshangazwa’ na matusi hayo ya ubaguzi wa rangi. Wachezaji wa England wamekuwa wakipiga magoti katika michano ya Euro kuangazia vita vyao dhidi ya ubaguzi wa rangi katik timu yao .

    "Tutafanya kila tuwezalo kusaidia wachezaji walioathiriwa huku tukisisitiza adhabu kali zaidi kwa kila mtu anayehusika. "Tutaendelea kufanya kila tuwezalo kumaliza ubaguzi ndani ya michezo, lakini tunasihi serikali ichukue hatua za haraka na kuleta sheria inayofaa ili unyanyasaji huu uwe na adhabu za kudumu kimaisha kwa wahusika.

    "Makampuni ya mitandao ya kijamii yanahitaji kuchukua hatua na kuwajibika kwa kuwapiga marufuku wanyanyasaji kutoka kwa majukwaa yao, kukusanya ushahidi ambao unaweza kusababisha kushtakiwa na kusaidia kufanya majukwaa yao kutotumiwa kwa dhuluma hizi’ Rashford aliangazia matukio ya kibaguzi aliyopokea kwenye mitandao ya kijamii mnamo Mei baada ya kupoteza fainali ya Ligi ya Uropa na Manchester United.

    Mwaka jana Sancho alikuwa miongoni mwa wachezaji nyota waliolalamika dhidi ya ubaguzi wa rangi kufuatia mauaji ya George Floyd na afisa wa polisi huko Minneapolis. Kampuni za mitandao ya kijamii zimekosolewa kwa kukosekana kwa hatua juu ya unyanyasaji wa kibaguzi kwenye majukwaa yao, na mnamo Aprili Instagram ilitangaza zana ya kuwezesha watumiaji kuchuja moja kwa moja jumbe za matusi kutoka kwa wale ambao hawawafuati.

    Kufuatia matukio kadhaa vya unyanyasaji mitandaoni, vilabu kadhaa, wachezaji, wanariadha na mashirika ya michezo walishiriki katika siku nne za kususia mitandao ya kijamii mnamo Aprili kuhamasisha kampuni kuchukua misimamo mikali dhidi ya unyanyasaji wa kibaguzi na kijinsia.

    • England yashindwa na Italia 3-2 kupitia penalti
  14. Habari...Karibu katika taarifa zetu za moja kwa moja leo ikiwa ni Jumatatu 12/07/2021.