Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari apongeza kukamatwa kwa Nnamdi Kanu

Ni mara ya kwanza rais amezungumza juu ya kukamatwa huko tata na kurudishwa Nigeria kwa kiongozi huyo anayetaka kujitenga kwa jimbo anakotoka

Moja kwa moja

Dinah Gahamanyi

  1. Na kufikia hapo tumetamatisha matangazo yetu ya moja kwa moja kwa leo .Hadi hapo kesho panapo majaaliwa

  2. Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari apongeza kukamatwa kwa Nnamdi Kanu

    Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amevipongeza vyombo vya usalama na ujasusi kwa kumkamata kiongozi kundi lililopigwa marufuku la Biafra, Nnamdi Kanu na uvamizi wa nyumba ya mwanaharakati mashuhuri wa Yoruba, Sunday Adeyemo.

    Ni mara ya kwanza rais amezungumza juu ya kukamatwa huko tata na kurudishwa Nigeria kwa kiongozi huyo anayetaka kujitenga kwa jimbo anakotoka .

    Rais Buhari alizilimbikizia sifaidara za usalama nchini Nigeria kwa hatua hiyo .

    Katika taarifa Bw Buhari alisema vyombo vya usalama vilionyesha umahiri mkubwa, uwezo na usiri katika kutekeleza oparesheni hizo Lakini hakusema mahali ambapo Nnamdi Kanu aliamatwa.

    Bwana Buhari pia alipongeza uvamizi wenye utata wa makazi ya mwanaharakati maarufu wa yoruba Sunday Adeyemo ambapo kikosi maalum cha polisi kiliwaua watu.

    Alimshutumu Adeyemo kwa kufanya vitendo vya ugaidi na kuvuruga amani kwa kisingizo cha kulinda haki za watu wake .

    Wakati huo huo, Bunge la Uingereza linatarajiwa kuanza mjadala juu ya kumrudisha kiongozi wa ipob, Nnamdi Kanu kwenda Nigeria.

    Katika ratiba iliyochapishwa kwenye tovuti yake, bunge lilisema litajadili hali iliyozingira kusafirishwa kwa Bw Kanu kwenda Nigeria kinyume na mapenzi yake miongoni mwa maswala mengine.

  3. Dkt Masaga: Matumizi ya Oksijeni yameongezeka hivi sasa Bugando

    Moja ya hospitali zilizothibitisha kukabiliwa na uhaba wa mitungi ya oksijeni ni hospitali Kuu ya Rufaa ya Bugando iliyopo jijini Mwanza, kaskazini magharibi mwa Tanzania inayohudumia Kanda ya Ziwa.

    Kaimu mkurugenzi wa hospitali hiyo Dkt Fabian Masaga amezungumza na mwandishi wa BBC, Martha Saranga aliyeanza kuelezea hali ilivyo hospitalini hapo.

    Katika hatua nyingine rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewasisitiza Watanzania kuchukua hatua dhidi ya janga la virusi vya corona.

    ''Hili wimbi la tatu liko kwenye nchi na hakuna la kuficha tayari tuna wagonjwa kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na mikoa mingine, hata Dodoma kwa kiasi kidogo sana lakini wapo''.

    Rais Samia ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Watanzania, mkoani Morogoro, Mashariki mwa Tanzania.

  4. Rais wa zamani wa Zambia Kenneth Kaunda azikwa

      • Author, Shingai Nyoka
      • Nafasi, BBC News, Harare

    Baba wa taifa la Zambia Kenneth Kaunda amezikwa katika eneo la kumbukumbu ya marais wa zamani baada ya Mahakama Kuu kukataa ombi kutoka kwa mmoja wa wanawe kuhusu mahali anapopaswa kuzikwa.

    Shujaa huyo katika mapambano ya ukombozi wa kusini mwa Afrika kutoka kwa ukoloni, Kaunda alipewa heshima kamili za kijeshi katika mazishi ambayo yalileta pamoja vyama pinzani vya kisiasa na viongozi kutoka ukanda huo.

    Kaunda alifariki mwezi uliopita, akiwa na umri wa miaka 97.

    Jeneza lake lililosheheni taji la maua lilishushwa kaburini kwa saluti ya mlio wa bunduki na gwaride la ndege kupaa.

    Hapo awali Rais Edgar Lungu aliwaongoza wanafamilia na wanasiasa katika ibada ya mwisho ya mazishi.

    Wakati Kaunda anatambuliwa kwa kujenga taifa lenye amani, katika kifo chake familia yake mwenyewe iligawanyika juu ya mahali pake pa mwisho pa kupumzika.

    Wengine walisusia mazishi hayo wakipinga. Kulingana na wao, alikuwa ametaka kuzikwa sio kati ya marais wa zamani lakini kwenye shamba lake karibu na mkewe.

    Mahakama ilikataa ikitaja suala la maslahi ya Umma. Hatahivyo ripoti zinaonesha kuwa anaweza kufukuliwa na kuzikwa tena baadaye.

    • MSF yasitisha shughuli zake Tigray kwa sababu ya ‘ghasia za kutamausha’

      Shirika la matibabu la MSF limesitisha kazi yake katika baadhi sehemu za eneo lenye vita la Ethiopia la Tigray wiki mbili baada ya wafanyikazi wake watatu kuuawa huko.

      Katika taarifa, MSF imetaka "uchunguzi wa haraka juu ya mauaji hayo na inasisitiza kuwa wafanyikazi wa misaada wanaruhusiwa kufanya kazi zao kwa usalama".

      "Karibu wiki mbili tangu mauaji ya wenzetu, hakuna mtu aliyedai kuhusika na mazingira kuhusiana na vifo vyao bado hayajafahamika," mkurugenzi wa operesheni wa MSF Teresa Sancristoval amesema.

      Alielezea uamuzi wa kusimamisha kazi huko Abi Adi, Adigrat na Axum kama "chungu sana lakini ni lazima".

      "Mauaji ya wenzetu - María, Tedros na Yohannes - ni mfano mbaya wa kupuuza kabisa maisha ya binadamu ambayo timu zetu zimeshuhudia katika mzozo huu," Bi Sancristoval alisema.

      "Viwango vya unyanyasaji dhidi ya raia na unyama uliofanywa huko Tigray ni wa kushangaza kabisa."

    • Mzozo watokota juu ya iwapo Zuma atakamatwa au la

      Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma lazima ajisalimishe kwa polisi au akabiliwe na kukamatwa kulingana na hukumu ya wiki iliyopita ya mhakama ya katiba kwasababu alipatikana na hatia ya kutoheshimu agizo la mahakama.

      Haijafahamika wazi hatahivyo ni nini kitakachotokea kwake.

      Msemaji wa wakfu wa Jacob Zuma Mzwanele Manyi ameiambia BBC kuwa haamini kwamba Bw Zuma atakamatwa.

      "Kulingana na sisi hakuna kukamatwa kutakakotokea kwasababu mtu wa kumkamata amereodiwa akisema anasubiri mchakato ukamilike" alisema.

      Bw Manyi alisema kuwa waziri Bheki Cele aliiandikia mahakama akisema kuwa atasubiri mchakato utakaomuongoza katika utekelezaji wa kukamkamata.

      Mawakili wa rais huyo wa zamani wamekwenda kwenye mahakama ya juu zaidi kuzuia kukamatwa kwake.

      Lakini Bw Cele pia amesema kuwa ataheshimu uamuzi wa Mahakama ya katiba.

      Profesa wa Sheria ya katiba katika Chuo kikuu cha Cape Town Pierre De Vos ameiambia BBC kwamba kama muda wa mwisho wa kujisalimisha ambao ni siku ya Jumatano aliopewa hautaheshimiwa, atakuwa tena amefanya kitendo cha kutoheshimu agizo la mahakama na uhalali wa mfumo wa sheria utakuwa umetishiwa.

    • Wapenzi wa jinsia moja kusherehekea ’Gay pride’ kwa mara ya kwanza

      Jumuiya ya wapenzi wa jinsia moja nchini Rwanda , wametangaza kuwa wanatarajia kusherehekea siku siku ya Wapenzi wa jinsia moja, ikiwa katika hatua ya kuungana na wenzao duniani katika mwezi unaofahamika kama "Gay Pride amaLGBT Pride", sherehe zinazofanyika mwezi wa Julai

      Katika mwezi wa Gay pride, wapenzi wa jinsia moja pamoja hunaji kujiamini kwao, utu, usawa na kuongeza muonekano na kufahamika kwao duniani.

      Wanatarajiwa kuonesha kufurahia haki za binadamu miongoni mwa watu wa jamii ya LGBTQ nchini Rwanda, pamoja na kuhamasisha umma kuhusu maumbile yao na kuuhamasisha umma wa wanyarwanda kuwakubali walivyo.

      LGBTQ nchini Rwanda

      Nchini Rwanda Jamii yaLGBTQ imeendelea kupanuka, huku wakiwa na chama chao kiitwacho ’Isange Rwanda’.

      Wapenzi wa jinsia moja nchini humo wanasema kuwa changamoto kubwa inayo wakabili hasa ni jinsi wanavyochukuliwa na jamii ya Wanyarwanda kwa ujumla kwani baadhi yao wamelazimika kuficha mwenendo wao wa kijinsia kwa kuhofia kuchukiwa na kudharauliwa na watu.

    • Polisi abaki ‘’kinywa wazi’’ huku wezi wa kutumia pikipiki wakimuibia simu ya mkononi

      Video ya polisi wa usalama barabarani katika mji mkuu wa Kenya Nairobi, akiibiwa siku yake ya mkononi na wanaume watatu waliokuwa kwenye pikipiki imekuwa ikisambazwa sana kwenye mitandao ya kijami.

      Picha ya video hiyo iliyorekodiwa na dashcam, sinamuonesha afisa huyo akizungumza kwa simu yake kabla ya mwendesha pikipiki kupita na abiria ambaye alinyakua simu kutoka kwa polisi.

      Wanaume hao wawili walitoweka kwenye msururu wa magari na kumuacha polisi akionekana hana la kufanya.

      Haijawa wazi ni wapi hasa video ya tukio hilo ilichukuliwa ,lakini video inaonesha ilichukuliwa mwezi wa Julai.

      Unyakuaji wa simu za mkononi, mikoba na vipuli unaofanywa na wezi wanaotumia pikipiki umekithiri jijini Nairobi.

      Maafisa wamekuwa wakiwaonya watu kuwa macho wakati wanapotembea kwenye mitaa ya jiji la Nairobi.

      Uhalifu kama vile ujambazi na utekaji nyarapia umeongezeka wiki huku polisi wiki hii wakitangaza kuunda kikosi maalum cha kukabiliana na uhalifu huu.

    • Zimbabwe yatoa noti ya thamani ya juu zaidi

      Kuanzia Jumatano nchini Zimbabwe itasambazwa noti mpya ya dola 50, ikiwa ndio yenye thamani kubwa zaidi kuwahi kutolea Zimbabwe tangu mwaka 2019.

      Dola 50 ya Zimbabwe ina thamani ya dola $0.60.

      Noti mpya ilizunduliwa Jumanne na benki kuu ilisema kuwa itasambaza dola milioni 360 za Zimbabwe kupitia benki.

      Imetolewa huku nchi hiyo ikikabiliwa na mfumuko wa bei ambao umewafanya watu kutembea lundo la noti.

      Noti mpya ina picha ya shujaa wa kupambana na ukoloni Mbuya Nehanda.

      Zim Live imetuma ujumbe wa twitter:

    • Ni kwanini Rais Kenyatta anafungua miradi usiku?

      Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amekosolewa na raia wa nchi hiyo kwa kuzindua miradi wakati wa saa za amri ya kutotoka nje usiku.

      Rais Kenyatta amezindua hospitali tano usiku wa Jumanne na kueleza kuwa ilikuwa ni muhimu kufanya hivyo usiku ili kuhakikisha ufanisi katika utoaji wa huduma.

      Alisema kuwa hospitali katika jiji mji mkuu, Nairobi, zinapaswa kufanya kazi saa 24 na alihitaji kufuatilia hilo.

      Rais pia amesefafnua kuwa uzinduzi wa mchana ungekiuka miongozo ya watu kukaa mbali.

      "Kama mlivyojionea wenyewe, haingewezekana kwenda na kufanya kile tulichofanya leo, wakati wa mchana kwasababu ya idadi ya watu ambao wangekuwa pale ," aliwaambia wandishi wa habari.

      Wakenya kwenye mitandao ya kijamii wamemshutumu Bw Kenyatta kwa kutoheshimu sheria zake mwenyewe

      "Kwanini Uhuru Kenyatta anafungua miradi usiku! Kwanini anakiukasa za amri ya kutotoka nje usiku? Haheshimu sheria zake mwenyewe pia, mbali na amri za mahakama ," Ongoma alituma ujumbe wa twitter.

      Rais Kenyatta anapaswa kesho kupelekwa katika mahakama ya sheria kwa kuvunja sheria ya saa za kutotoka nje usiku," Miqdad Abdissalam aliandika..

      "Sasa Uhuru anapaswa kuondoa amri ya kutotoka nje usikukwani pia yeye anaona umuhimu wa kufanya kazi saa za ziada usiku," Ahmad Salim alituma ujumbe wa twitter.

      Amri ya kutotoka nje usiku nchini Kenya imewekwa kuanzia saa nne usiku hadi saa kumi alfajiri katika mji mkuu Nairobi na baadhi ya maeneo ya nchi inaanza saa moja jioni.

    • Euro 2020: England kuvunja mwiko wa miaka 55 leo?

      Kocha wa England Gareth Southgate amewataka wachezaji wa timu hiyo kuweka historia kwa kuichapa Denmark na kutinga fainali ya michuano ya Euro 2020 kwa mara ya kwanza.

      England wanawakabili Denmark katika nusu fainali ya Euro 2020 mbele ya mashabiki 60,000 katika dimba la Wembley na iwapo itatinga fainali, itakuwa fainali ya kwanza ya England kwenye michuano mikubwa tangu ifanye hivyo mwaka 1966.

      "Hatuna historia nzuri kwenye soka, kama tunavyojiaminisha wakati fulani, alisema Southgate. "Wachezaji hawa wanapiga hatua kubwa sana."

      Mara ya mwisho England kufika fainali kwenye michuano mikubwa ilikuwa miaka 55 iliyopita walipotwaa kombe la dunia. Lakini hawajawahi kuvuka hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ya Ulaya. Imewahi kucheza nusu fainali tano za Euro na Kombe la dunia, lakini ni nusu fainali moja tu ya kombe la dunia mwaka 1966 waliyofuzu na kutwaa kombe moja kwa moja.

      Katika fainali za kombe la dunia za mwaka 2018 waliishia nusu fainali baada ya kuondoshwa na Croatia.

      Dalili na mazingira yanaipa nafasi England Kutinga fainali.

      Kwa kikosi chake sasa, chenye mchanganyiko kinachoongozwa na nahodha wake Harry Kane, kuna kila dalili ya kufanya vyema mwaka huu kwenye michuano ya Euro 2020, angalau kwa kutinga fainali.Pamoja na hilo huwezi kupuuza safari ya Denmark hadi kufika hatua ya nusu fainali, walianza kupoteza michezo yake miwili ya kwanza, lakini ikashinda mitatu mfululizo dhidi ya Urusi, Wales na Czech.

      Denmark ambayo ilishawahi kutwaa taji hilo la Ulaya mwaka 1992, inapambana kwa ajili ya nyota wake, Christian Eriksen, ambaye katika hatua ya makundi alianguka uwanjani kwa tatizo la moyo.

      Dalili njema ya kwanza na muhimu kwa England haina majeraha na inao nyota wake wote baada ya Bukayo Saka kupona. Lakini pia inaonekana kuwa na ukuta mzuri, haijaruhusu bao hata moja katika mechi zote tano ilizocheza mpaka kufikia hatua ya nusu fainali, huku mlinda mlango wake, Jordan Pickford akitarajiwa kuwa kipa aliyecheza mechi nyingi za michuano hiyo mwaka huu bila kuruhusu bao.

      Mpinzani wake Gianluigi Donnarumma wa Italia, ameruhusu bao moja jana dhidi ya Hispania katika mchezo mwingine wa nusu fainali.

      Mbali na kikosi kizuri, dalili nyingine muhimu kwa England, ni kushinda dhidi ya timu kubwa, ikivunja mwiko wa miaka 55 ya kusubiri kuiondoa Ujerumani kwenye hatua ya mtoano. Iliondosha Ujerumani kwenye hatua ya 16 bora, lakini huko nyuma haikuwahi kufanya hivyo.

      Kucheza katika uwaja wa Wembley ambao ni nyumbani mbele ya watazamaji 60,000 kunazidi kuwapa nguvu England huku watazamaji wengine zaidi ya milioni 20.9 wanatarajiwa kufuatilia mechi hiyo kupitia TV wakiwa nyumbani, kwenye migahawa, hoteli na sehemu maalumu zilizotengezwa kwa ajii ya mashabiki wake kutazama mitaani.

      Kwa masharti ya Corona yaliyopo England, ni mashabiki wachache sana wa Denmark watakaoweza kuingia nchini humo kuipa nguvu timu yao .

      Iwapo England itapita itakutana na Italia katika fainali ya kihistoria itakayochezwa Julai 11 itakayopigwa pia katika dimba la nyumbani kwa England, Wembley. Italia imeondosha Hispania kwa matuta katika mchezo uliochezwa usiku wa jana.

    • Walichokisema Mke na watoto wa Nabii TB Joshua wakimuomboleza

      Viongozi na watu mbali mbali maarufu wamekuwa wakielekea katika makao makuu ya Kanisa la Nabii na muasisi wa kanisa la Synagogue Church of All Nations TB Joshua kwa siku ya pili kutoa heshima na rambi rambi zao kufuatia kifo chake.

      Temitope Balogun Joshua aliyefahamika zaidi kama TB Joshua alifariki dunia mwezi uliopita akiwa na umri wa miaka 57.

      Katika siku ya pili ya mchakato wa mazishi yake mke wake Evelyne na watoto wake watatu Sarah, Promise and Heart walipata fursa ya kumzungumzia maisha ya TB Joshua.

      Kulingana na mke wake Evelyn Joshua, alishuhudiaTB Joshua akikua ‘’kutoka kuwa na kusanyiko la waumini 8 wa kanisa hadi kuwa na kanisa lililojaa umati wa watu na kuwa na wafuasi kote duniani "

      ‘’Alinifunza kuwa mwanamke niliye leo. Kwa dhahabu kuwa dhahabu lazima ipitie moto. Ninataka tu kukushukuru kwa kuwa baba mwema wa watoto wetu.", alisema mjane Everlyne.

      Watoto wake TB Joshua , Sarah, Promise na Heart walimsifu baba yao mpendwa kwa kuwa mtu aliyejitolea kumtumikia Mungu " kwa heshima bila uwoga."

      "Aina ya upendo uliotuonesha hatukuwahi kuuona maishani mwetu. Kama kuna mtu yeyote aliyeishi maisha ya kushangaza ni wewe. Baba yangu alikuwa na utu ambao kwa namna ambayo sikuwahi kuelewa kamwe ," alisema binti yake Sarah.

      Mchakato wa mazishi wa kumuenzi na kumkumbuka TB Joshua ulianza Jumatatu kwa kuwashwa kwa mishumaa.

      Muhubiri huyo wa televisheni aliyekuwa maarufu Afrika, anatarajiwa kuzikwa Ijumaa wiki hii, katika mazishi ya faragha.

    • Hali ya tahadhari yatangazwa New York kufuatia ghasia za bunduki

      New York Governor Andrew Cuomo ametangaza hali ya tahadhari kufuatia kuongezeka ghafla kwa visa vya ufyatuaji risasi katika jimbo hilo.

      Gavana alisema kuwa zaidi ya watu 51 wameuawa baina ya wikendi ya Julai 4.

      Kumekuwa na ongezeko kubwa la vifo vitokanavyo na mashambulio ya bunduki kote nchini Marekani, ambapo vifo 200 vilitokea mwishoni mwa juma pekee katika maeneo mbali mbali ya Marekani.

      Agizo hilo litakwenda sambamba na kutengwa kwa dola milioni 138.7 kwa ajili ya mipango ya kuingilia kati na kuzuia ghasia za bunduki.

      Kuanzia mwezi Mechi hadi Mei mwaka jana, 2020, kulikuwa na ongezeko la mashambulizi na uhalifu wa kutumia bunduki katika jimbo la New York State na katika maeneo mengi ya Marekani.

      Gavana aliamua kuchukua uamuzi wa kuongeza usalama katika maeneo yenye hatari ya kiusalama, pamoja na kutoa mafunzo ya kazi kwa watu wanaoishi katika maeneo masikini.

      IMwezi Machi, shirika la ujasusi la Marekani FBI lilitoa ripoti ya awali ya takwimu za mwaka 2020 zilizoonesha kupanda kwa asilimia 25 kwa mauaji -ikilinganishwa na mwaka uliopita . ongezeko hilo limeendelea kupanda katika mwaka 2021.

      nchini Marekani vifo vingi vya nyumbani huthusishwa na bunduki .

    • Rais Samia na Blinken wazungumzia haki za kisiasa na uhuru wa raia Tanzania

        • Author, Yusuph Mazimu
        • Nafasi, BBC Swahili

      Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan Jumanne hii amefanya mazungumzo na Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken , mazungumzo yaliyojikita zaidi kwenye masuala ya ugonjwa wa Covid-19, Demokrasia na mazingira ya kufanya biashara Tanzania.

      Msemaji wa Waziri Blinken, Ned Price amesema viongozi hao wamezungumzia kuhusu umuhimu wa haki za kisiasa, uhuru wa raia, pamoja na juhudi za ushirikiano katika kuhakikisha masula ya demokrasia, amani, uhuru na mustakabali wa maisha ya watanzania.

      Moja ya haki inayolalamikiwa kuminywa ni mikutano ya kisiasa ya vyama vya siasa, licha ya mikutano ya wabunge na madiwani kuruhusiwa lakini katika maeneo yao.

      Kwa zaidi ya miaka mitano sasa nje ya nyakati za uchaguzi, vyama vya siasa nchini havijafanya mikutano ya hadhara ya siasa. Rais Samia hivi karibuni alipoulizwa na waandishi wa habari, alieleza kwamba, kwa sasa anajielekeza zaidi kwenye kuifungua nchi hiyo na kujenga uchumi.

      'Nilisema siku hiyo nazungumza bungeni kwamba nitakaa na wenzangu wanasiasa tuone tunakwendaje na siasa zetu katika mustakabali mpana wa taifa letu', alisema Rais Samia.

      Katika mtandao wake wa Twitter, Blinken amesifu jitihada za Rais Samia katika kukabiliana na janga la Corona.

      Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya Tanzania, Bwana Blinken amesifu pia jitihada za Rais Samia katika kuimarisha demokrasia na azma yake ya kukutana na kushirikiana na vyama vya siasa pamoja na kusimamia uhuru wa vyombo vya habari.

      Hata hivyo Chama kikuu cha Upinzani nchini humo (CHADEMA), kinaeleza kwamba hakijataarifiwa rasmi ni lini Rais huyo atakutana nao, licha ya maombi yao ya kuonana nae yalikubaliwa.

      Kwa sasa joto la kisiasa nchini humo limejielekeza kwenye kupatikana kwa Katiba mpya, ambapo mbali na wanaharakati na makundi mengie, vyama vya siasa nchini humo vimekuwa vikipiga kelele kutaka Katiba mpya ya nchi hiyo, kufuatia mchakato wake kusimama kwa zaidi ya sita.

      Kuhusu la Katiba mpya, kama ilivyokuwa kwa mikutano ya siasa, Rais Samia alisema apewe muda kwanza kuhusu kwa kuwa anajenga uchumi wa nchi hiyo kwa sasa.

      Mbali na hilo, na kuhaidi kwamba Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Serikali ya Marekani, taarifa ya Ikulu ya nchi hiyo inasema Rais Samia ametoa mwaliko kwa Rais Joe Biden wa Marekani kutembelea Tanzania ili kuimarisha zaidi uhusiano baina ya nchi hizo.

    • Hujambo na karibu tena kwa matangazo yetu mubashara leo Jumatano tarehe 07.07.2021