Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tanzania kutengeneza chanjo yake ya corona
Taarifa ya Serikali iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya wa nchi hiyo, Profesa Abel Makubi imesema chanjo hiyo itatengenezwa kupitia kiwanda chake kipya ambacho kipo kwenye mchakato wa kuanzishwa
Moja kwa moja
Dinah Gahamanyi
Rashford amtumia mvulana wa miaka ,9, zawadi ya kushitukiza
Mvulana mwenye umri wa miaka 9 amesema "nilikuwa mwenye furaha" baada ya mchezaji soka Marcus Rashford kumtumia zawadi ya kushitukiza akimmshukuru kwa kazi yake ya msaada.
Jacob, kutoka St Helens katika eneo la Merseyside, alihamasishwa na juhudi za mshambuliaji wa England za kukabiliana na umasikini miongoni mwa watoto na kuanza kuendesha kampeni ya inayoitwa Fare Share.
Familia yake imesema kuwawali "shtushwa sana " wakati kifaa cha michezo ya kpmpyutacha PlayStation 5 na barua kutoka kwa Rashford vilipowasilishwa kwenye mlango wao.
"Sisi ni wakarimu kwasababu ni kitu sahihi kufanya", ilisema barua.
Rashford, 23, aliongoza kampeni ya kukabiliana na umasikini kwa watoto wakati wa mlipuko wa virusi vya corona.
Shabiki huyo wa Manchester United, Jacob alitaka kusaidia na akawaomba watu kumdhamini huku akikimbia kuchangisha pesa, alisema baba yakeJohn Worthington.
Mvulana huyo, ambaye huchezea timu mbili za soka Kaskazini mwa nchi, alifungua akaunti ya Instagram, na baba yake ili kuendelea shughuli hiyo ya uchangishaji.
Rashford alitambua juhudi za mvulanaJacob ndipo alipomtumia baba yake ujumbe kumuuliza ni wapi anaweza kutuma zawadi.
Bw Worthington alisema: "Sikutarajia mzigo uje haraka sana, kwahiyo ulipowasili Jumatano, nilifikiria , 'Hii ni nini?'.
Afghanistan: Wanajeshi wa serikali wakimbilia Tajikistan wakiwatoroka wapiganaji wa Taliban
Zaidi ya wanajeshi 1,000 wa Afghanistan wamekimbilia nchi jirani ya Tajikistan baada ya kukabiliana na wanamgambo wa Taliban, maafisa wamesema.
Wanajeshi walikimbilia mpaka wa nchi hiyo jirani ili "kuokoa maisha yao wenyewe", kulingana na taarifa ya walinzi wa mpaka wa Tajikistan.
Vurugu zimeongezeka nchini Afghanistan, na Taliban wamekuwa wakifanya mashambulizi na kuchukua maeneo zaidi katika wiki za hivi karibuni.
Kuzidi kwa mashambulizi yao kumejiri wakati huu ambaokipindi cha miaka 20 ya huduma za jeshi la Nato kinafika tamati .
Idadi kubwa ya vikosi vya kigeni vilivyobaki nchini Afghanistan vimeondolewa kabla ya tarehe ya mwisho ya Septemba, na kuna wasiwasi kwamba jeshi la Afghanistan litaporomoka .
Chini ya makubaliano na Taliban, Marekani na washirika wake wa Nato walikubaliana kuondoa wanajeshi wote kwa ahadi ya wanamgambo kutoruhusu al-Qaeda au kikundi kingine chochote chenye msimamo mkali kuhudumu katika maeneo wanayodhibiti.
Kamati ya Usalama ya Kitaifa ya Tajikistan, ambayo inasimamia usalama wa mpaka, ilisema kwamba wanajeshi wa Afghanistan walitafuta hifadhi mapema Jumatatu asubuhi baada ya kupigana na wanamgambo wakati wa usiku, kulingana na shirika la habari la serikali la Tajikstan, Khovar.
"Walinzi wa mpaka wa Tajik kwa sasa wanadhibiti hali katika mpaka wa Tajikistan na Afghanistan," ilisema.
Taliban sasa inadhibiti karibu theluthi moja ya Afghanistan, na inaendelea kukamata maeneo zaidi kila siku.
Mikoa ya Badakhshan na Takhar, ambayo inapakana na Tajikistan, imeshuhudia harakati za hivi karibuni za Taliban kuteka maeneo makubwa
Hii ni mara ya tatu kwa wanajeshi wa Afghanistan kukimbilia Tajikistan katika siku tatu zilizopita na kisa cha tano katika wiki mbili zilizopita. Imefikisha jumla ya wanajeshi waliorejea Tajikistan kufika takriban 1,600.
Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani anasisitiza kuwa vikosi vya usalama vya nchi hiyo vina uwezo kamili kuwazuia waasi, hata hivyo kumekuwa na ripoti za wanajeshi zaidi wanaotafuta hifadhi nchini Pakistan na Uzbekistan kutoroka vita.
Nchi za jirani, pamoja na zile za Asia ya Kati, zinajiandaa kwa wakimbizi ikiwa vita vitaendelea nchini Afghanistan .
Lyse Doucet, mwandishi mkuu wa BBC wa kimataifa, anasema hali ya hofu na kutojua hatima ya maisha yao inatawala watu wengi nchini Afghanistan.
"Hawana uhakika kuhusu nchi yao inaelekea wapi, hawana uhakika kuhusu kijiji chao au mji au jiji, na hawana uhakika juu ya maisha yao wenyewe na hatima ya familia zao," alisema.
Hata hivyo msemaji wa Taliban Suhail Shaheen aliambia BBC kuwa Taliban hawahusiki na ongezeko la vurugu hivi karibuni.
Alisisitiza kwamba wilaya nyingi zipo chini ya Taliban kupitia upatanishi baada ya wanajeshi wa Afghanistan kukataa kupigana.
Vikosi vinavyoongozwa na Marekani viliondoa Taliban madarakani nchini Afghanistan mnamo Oktoba 2001. Kikundi hicho kilikuwa kikimpa hifadhi Osama Bin Laden na viongozi wengine wa al-Qaeda waliohusishwa na mashambulio ya 9/11 huko Marekani ambayo yalisababisha uvamizi huo.
Rais Biden amesema kujitoa kwa Wamarekani ni haki kwani vikosi vya nchi yake vimehakikisha Afghanistan haiwezi kuwa ngome ya wanajihadi wa kigeni kupanga njama dhidi ya nchi za Magharibi tena.
Kuondolewa kwa majeshi Tigray hakumaanishi Ethiopia imeshindwa - Abiy
Waziri mkuu wa Ethiopia anasema kuondolewa kwa wanajeshi na maafisa wa serikali kutoka eneo la kaskazini mwanchi -Tigray haipaswi kuonekana kama ishara kwamba upande wa serikali ulishindwa vita.
Abiy Ahmed alisema kuwa mzozo wa miezi nane dhidi ya waasi wa Tigray umewadhoofisha waasi.
Alisema jeshi la kitaifa bado lina uwezo wa kupigana lakini alisisitiza umuhimu la kuwa na amani ili Ethiopia iweze kuendelea.
Katika hotuba yake bungeni hakujibu orodha ya masharti ya waasi wa TPLF ili kuwe na usitishaji mapigano kati ya pande hizo mbili
Mamia ya maelfu ya raia huko Tigray wanakabiliwa na hali kama ya baa la njaa kutokana na mzozo na mashirika ya misaada yanaomba kuwafikia bila vizuizi
Miaka 10 ya Sudan Kusini: ‘Kwangu Kenya ni nyumbani’ – John Mayen
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Roncliffe Odit
- Nafasi, BBC Nairobi
Kwa zaidi ya miaka 26, John Chol Mayen kutoka Sudan amekuwa akiishi Kenya. Kijana huyo mwenye asili ya Sudan Kusini alizaliwa katika mpaka wa Kenya na Ethiopia baada ya wazazi wake kutoroka vita Sudan Kusini.
Baadaye walihamia kambi yawakimbizi ya Kakuma, kaskazini-magharibi mwa Kenya ambapo alilelewa. John anakumbuka vyema maisha yake ya utotoni.
‘’Utoto wangu ulikuwa na changamoto si haba, maisha hayakuwa rahisi katika kambi ya wakimbizi. Hapo si kama nyumbani, maisha ni tofauti kabisa. Hakuna vitu vya kuchezea, hakuna uhuru wa kucheza kama watoto wa kawaida. Maisha ni tofauti kabisa.’’
Baadaye wazazi wake walihamia mjini Eldoret ambapo John alianza masomo yake ya chekechea na baadaye shule ya msingi. Na licha ya changamoto alizopitia, John alijikakamua na kufaulu mtihani wake wa kitaifa na kujiunga na shule ya upili.
Ni wakati huo akiwa katika shule ya upili ambapo taifa la Sudan Kusini lilijipatia uhuru wake.
‘Ilikuwa mwaka 2011, nilikuwa shuleni wakati huo, tukaitwa tukaambiwa lazima tutoke ili tukapige kura ya kujipatia uhuru, mimi na wanafunzi wenzangu kutoka Sudan Kusini tukaenda eneo la Railways jijini Nairobi ili kupiga kura,’ anakumbuka John.
Wakati huo, zaidi ya asilimia 99 ya raia wa Sudan Kusini walipiga kura ya maoni ili kujitenga na taifa la Sudan. Na hapo ndipo taifa jipya kabisa barani Afrika, Sudan Kusini, lilipozaliwa.
Kijana huyu wa nne kwa familia ya watoto nane, anasema licha ya kwamba alikuwa na umri mdogo kuelewa mambo kadhaa, lakini tamko la uhuru wa Sudan Kusini lilileta shangwe kwa nafsi yake.
‘Kujua tu kwamba sasa taifa letu lina uhuru, na ile fikira ya uwezekano wa kurudi nyumbani, hiyo ilikuwa pindi ya furaha kweli.’
Miaka minne baadaye, John Mayen alijiunga na Chuo Kikuu cha Daystar jijini Nairobi, Kenya, ambapo alisomea taaluma ya hisabati. Alifuzu na kuhitimu chuoni mwaka 2020.
Lakini wakati Sudan Kusini inapoadhimisha miaka 10 ya uhuru, John Mayen anasherehekea nini?
‘Kwangu mimi ni furaha tu kujua kwamba taifa letu liko huru. Sasa watu wetu wana nafasi ya kujiendeleza kiuchumi, kielimu, kijamii na hata kifamilia.’
John anasema licha ya kwamba bado taifa hilo changa zaidi barani Afrika halijafikia upeo wake kamili, lakini kuna matumaini makubwa ya siku za usoni.
Yeye binafsi anatamani kupata kazi nchini Sudan Kusini ili aweze kutumia taaluma aliyojifunza nchini kenya katika kuboresha maisha ya watu wa Sudan Kusini.
Lakini wakati akijiunga na ndugu, jamaa na marafiki kuadhimisha miaka hiyo 10 ya uhuru, John Mayen anasema kwake yeye binafsi, Kenya ndio nyumbani.
‘Kenya imenipa elimu, Kenya imenipa upendo, mambo ambayo sijawahi kuyafurahia nchini Sudan Kusini,’ anasema John, huku akiangua kicheko.
‘Hata ikiwezekana, nitaoa hapa hapa Kenya.’
Watu wenye silaha waishambulia hospitali, shule na kituo cha polisi chini ya saa 24 nchini Nigeria
Watu wenye silaha wameilenga hospitali, shule na kituo cha polisi chini ya saa 24 nchini Nigeria.
Mzazi ambaye binti yake alitekwa nyara ameiambia BBC kuwa wanafunzi 140 walichukuliwa kutoka kwenye shule ya Bethel Babstist majira ya asubuhi Jumatatu.
Shambulio hili linafuatia shambulio lingine kwenye hospitali iliyopo karibu ambako watu 8 wakiwemo akiwemo mtoto mchanga mmoja walichukuliwa.
Mwandishi wa BBC wa Nigeria Mayeni Johns anasema, mzozo wa utekeji nyara unaongezezeka kwa kasi nchini Nigeria.
Wakati taarifa zikijitokeza za utekaji nyara katika eneo la shule liyopo katika mji wa Zaria, duru zimeiambia BBC kuhusu utekaji nyara uliofanyika katika eneo la shule lililopo chini ya umbali wa dakika 30 kutoka hospitali hiyo.
Idadi kamili ya wanafunzi waliochukuliwa kutoka Shule ya Bethel Baptist haijafahamika bado, lakini kiongozi wa kijamii na mzazi aliyezungumza na BBC wamesema ni zaidi ya watoto mia moja.
Mama ambaye binti yake mwenye umri wa miaka 15 ni miongoni mwa wanafunzi wasiojulikana walipo, anasema watu wenye silaha walivunja uzio na kuingia ndani sehemu ya nyuma ya shule saa nane usiku.
Taarifa za utekeji nyara zimekuwa zikiongezeka kote nchini Nigeria, huku uchumi wa taifa hilo ambalo linategemea mafuta ukianguka kufuatia janga la Covid 19.
Kaskazini magharibi mwa Nigeria, shule na vyuo vikuu mara nyingi hulengwa na watekaji kwa ajili ya kikombozi.
Zaidi ya wanafunzi elfu moja wamekwisha kutekwa nyara tangu mwezi wa Disemba na 9 wameuawa.
Wanafunzi 22 bado hawajulikani walipo, baadhi yao wakiwa ni wadogo hadi wenye umri wa miaka mitatu.
Mishumaa kuwashwa kwa ajili ya marehemu Nabii TB Joshua
Tukio la kuwasa mishumaa litaanzisha utararibu wa mazishi ya aliyekuwa muhubiri mashuhuri wa Nigeria, na muasisi wa kanisa la Synagogue Church of All Nations (SCOAN) aliyefariki mwezi uliopita.
Mchungaji TB Joshua alifariki tarehe 5 Juni akiwa na umri wa miaka 57, siku chache kabla ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa.
Hatahivyo kanisa lake bado halijafichua ni nini kilichosababisha kifo chake.
Taarifa iliyotolewa na kanisa lake - Synagogue Church of All Nations imesema: "Mungu amemchukua mtumishi wake Nabii TB Joshua nyumbani - sawa na mapenzi yake. Aliutumia muda wake wa mwisho duniani katika huduma ya Mungu. Alifanya alichopaswa kufanya, akakiishi na amekufa kwa ajili yake ."
"Nabii TB Joshua ameacha urithi wa huduma na kujitolea kwa ajili ya ufalme wa Mungu ambao utaendelea kuishi kwa vizazi ambavyo havijazaliwa ."
Mchakato wa kuwasha mishumaa utakuwa utakuwa ni sherehe ya kibinafsi , limesema kanisa la Synagogue Church of All Nations.
Tukio hilo linatarajiwa kuanza saa kumi na mbili unusu jioni Jumatatu kwa saa za Nigeria.
Litapeperushwa pia moja kwa moja kwenye chaneli ya TV ya kanisa hilo.
Kulingana na taarifa hiyo Kanisa hilo limewataka watu kubeba mishumaa kama ishara ya kuungana katika mpango wa ‘’kumheshimu’’ mtumishi wa Mungu - TB Joshua."
Mazishi yake yanatarajiwa kuwa ya faragha Ijumaa Julai 11, 2021.
Makombora ya Uchina yanayoitia tumbo joto Marekani
Marekani imesema kuongezeka kwa idadi ya silaha za nyuklia za uchina ni swala la kutia hofu na kuongeza kuwa Marekani inapaswa kuzungumza na Uchina sasa kuijua ni nini kinachoendelea.
Akizungumza na waandishi wa habari, Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani - Ned Price alisema, "China inahitaji kuzungumza na Marekani ili kufikia suluhu la kudumu juu ya silaha zake."
Gazeti la Washington Post linaripoti kwamba China ina zaidi ya magalamia moja ya kuhifadhi makombora aina ya silo ambayo yanaweza kutunzwa katika jangwa la magharibi.
Ned Price anasema Uchina imepata ugumu wa kuficha silaha zake, kulingana na Global Times.
Magala hayoya silaha Silos mara nyingi hutumiwa nchini China kuhifadhi makombora ya masafa marefu aina ya ballistic yanayoweza kupiga bara jingine. Makombora haya yana uwezo wa kupiga eneo la mbali na kuzalisha nishati nyingi. Ni silaha nzito za nyuklia.
TPLF wataka kutambuliwa kama serikali halali ili kusitisha mapigano Tigray
Waasi katika jimbo la Tigray nchini Ethiopia wamesema ili wasitishe mapigano katika eneo hilo, ni sharti watambuliwe kama serikali halali.
Kuondolewa kwa majeshi ya Eritrea katika eneo hilo, pia ni moja ya sharti.
Hapo awali mamlaka mjini Addis Ababa zilieleza kusitisha mapigano na maafisa wa serikali wakiondoka wakati ambapo waasi wamerejesha mikononi mwao enro kubwa la jimbo hilo.
Miezi minane ya mapigano kati ya waasi na majeshi ya serikali yamesababisha maelfu ya watu kuuawa huku zaidi ya watu milioni mbili wakiyakimbia makazi yao.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN), watu 400,000 wanakabiliwa na baa la njaa,hasa katika eneo la kaskazini mwa jimbo hilo.
Waasi hao wa TPLF awali walieleza kwamba kusitisha huko wanakokusema majeshi ya serikali ni danganya toto na kwamba wataendelea kuwafurusha maadui zao hao kutoka katika eneo hilo.
Pamoja na hilo waasi hao wameongeza orodha mpya ya masharti ili waweza kusititisha mapigano, ikiwemo kufanyika kwa uchunguzi huru kuhusu madai ya uhalifi wa kivita, kupelekwa kwa misaada ya kibinadamu na kurejeshwa kwa huduma muhimu kama umeme.
Mpaka sasa serikali ya waziri mkuu Abiy Ahmed mjini Addis Ababa imekataa kuzungumza na kukubaliana na viongozi wa TPLF na kuliweka kundi hilo kama miongoni mwa makundi ya kigaidi.
Watoto wachanga na wauguzi watekwa nyara Nigeria
Watu wenye silaha wamewateka nyara watoto wachanga, wauguzi na walinzi wa usalama katika hospitali iliyopo kaskazini magharibi mwa Nigeria, polisi imesema.
Idadi Kamili ya wale waliotekwa katika mji wa Zaria haijulikani.
Majambazi wa eneo hilo walifanya mashambulio ya mfulurizo kwenye kituo cha polisi na kituo cha taifa cha kifua kikuu na ukoma, kabla ya kutorokea msituni.
Afisa wa serikali katika eneo hilo amesema jeshi limeanza juhudi za kuwatafuta waathiriwa.
Takriban watu saba waliuawa katika shambulio kama hilo lililotekelezwa na watu wenye silaha mwishoni mwa juma katika jimbo la Kaduna.
Utekaji nyara kwa ajili ya kikombozi ni wa mara kwa mara nchini Nigeria.
Papa 'anaendelea vizuri' baada ya kufanyiwa upasuaji wa koloni
Papa Francis amefanyiwa upasuaji wa tatizo la utumbo mkubwa au koloni uliofanikiwa katika hospitali moja huko Roma, Vatican imesema.
Hali ya afya ya Papa Francis, 84, "inaendelea vizuri" baada ya kufanyiwa upasuaji ambao ilibidi apigwe ‘nusu kaputi’, msemaji wa Vatican Matteo Bruni amesema.
Ni mara ya kwanza Papa Francis kulazwa hospitalini tangu kuchaguliwa kwake kuwa kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki ulimwenguni mwaka 2013.
Mapema Jumapili, Papa ambaye ni raia wa Argentina alihutubia maelfu ya wageni katika uwanja wa St Peter's.
Katika taarifa iliyotolewa awali, Vatican ilisema Papa Francis alikuwa anatibiwa katika hospitali ya chuo kikuu cha Gemelli kwa tatizo la koloni.
Ugonjwa huo ni hali inayojumuisha vifuko katika ukuta wa utumbo mpana ambako kunaweza kusababisha kupungua kwa koloni.
Dalili zake ni pamoja na tumbo kuvimba, kuwa na maumivu na mabadiliko ya tabia za utumbo.
Vatican haikutoa maelezo zaidi kuhusu upasuaji huo au kipindi ambacho Papa anatarajiwa kuwa hospitalini.
Wakati wa ibada ya Jumapili katika Kanisa la Mtakatifu Petro, Papa alitangaza kuwa ataenda Slovakia mnamo mwezi Septemba baada ya kufanya ibada ya kusherehekea huko Budapest, mji mkuu wa Hungary.
Papa Francis mwaka 1936 huko Buenos Aires, na alipoteza sehemu ya pafu lake la upande wa kulia akiwa na umri wa miaka 21.
Pia aliwahi kupata tatizo la nyonga na siatika (ugonjwa wa mshipa wa nyuma ya paja), ambako kunasababisha uchungu kuanzia sehemu ya chini ya mgongo hadi miguuni.
Mwaka 2014, alilazimika kuahirisha shughuli zake kadhaa kwa sababu ya tatizo maradhi ya tumbo.
Tanzania kutengeneza chanjo yake ya corona
Tanzania imeanza mchakato wa kutengeneza chanjo yake ya virusi vya corona ili kupunguza gharama ya kuagiza chanjo hiyo nje ya nchi.
Taarifa ya Serikali iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya wa nchi hiyo, Profesa Abel Makubi imesema chanjo hiyo itatengenezwa kupitia kiwanda chake kipya ambacho kipo kwenye mchakato wa kuanzishwa.
Prof. Makubi hata hivyo hakueleza mchakato huo ambao umesharidhiwa na Rais Samia Suluhu Hassan upo katika hatua gani hasa na lini kiwanda kinatarajiwa kukamilika na kuanza kuzalisha chanjo.
Mpaka sasa hakuna nchi ya Afrika iliyoanza kutengeneza chanjo ya Corona, ingawa nchi za Uganda, Rwanda, Afrika Kusini na Senegal zilitangaza kuanza mipango ya kutengeza chanjo. Haifahamiki pia endapo Tanzania itashirikiana na nchi nyengine ama mashirika ya kimataifa
Tanzania inasema imechukua uamuzi huo kwa kuwa ina wataalamu waliobobea wa chanjo: "tuna wataalamu wakutosha kwa hiyo tunataka huo mchakato wa kuanza kutengeza chanjo zetu sio tu kwa ajili ya Covid-19 pekee yake, hata chanjo zingine hiki kiwanda kitaweza kuzalisha ili kupunguza gharama, lakini pia kuzifanya ziwe karibu na wananchi’, alisema Makubi siku ya Jumapili akiwa Dodoma.
Mbali na hilo nchi hiyo pia imetoa mwongozo mpya wa kukabiliana na kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona shuleni. Miongoni mwa mambo yaliyopitishwa wakati shule zikifunguliwa hii leo nchini humo ni;
- Walimu, wafanyakazi na wakufunzi kuvaa barakoa wakati wote wakiwa shuleni.
- Wanafunzi kuvaa barakao wakati wote wakiwa darasani.
- Na uwepo wa vifaa vya kunawia mikono, kuwekea taka na kutoewa kwa elimu kuhusu virusi hivyo.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Rais Samia, nchi hiyo ambayo kwa zaidi ya mwaka mmoja ilikuwa haijatangaza takwimu za ugonjwa huo ina wagonjwa zaidi ya 100 wa Corona, 70 wakiwa kwenye mitungo ya oksijeni.
Wakati huo huo, Tanzania tayari imeshatuma maombi ya kujiunga na mpango wa chanjo wa Covax kama ilivyoshauriwa na Kamati ya Wataalamu iliyoundwa na rais Samia kumshauri juu ya namna ya kukabiliana na janga la corona.
Mpango wa Covax ambao moja ya waratibu wake ni Shirika la Afya Duniani (WHO) unalenga kuhakikisha nchi masikini ulimwenguni zinapata chanjo hizo muhimu.
Unaweza pia kusoma:
- Virusi vya Corona: WHO yasema chanjo ya corona inaweza kufika Tanzania ndani ya wiki mbili
- Virusi vya Corona Tanzania: Tanzania kuna wagonjwa zaidi ya 100 wa wimbi jipya la corona
Hujambo na karibu kwa matangazo yetu mubashara leo Jumatatu tarehe 05.07.2021