Mkuu wa zamani wa ujasusi wa Israel afichua oparesheni za Mossad dhidi ya Iran

Yossi Cohen alitoa maelezo juu ya wizi wa stakabadhi za nyuklia za Iran

Moja kwa moja

Ambia Hirsi and Yusuf Jumah

  1. Mkuu wa zamani wa ujasusiwa Israel afichua oparesheni za Mossad dhidi ya Iran

    Yossi Cohen led Mossad for more than five years

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mkuu anayemaliza muda wake wa shirika la ujasusi la Israeli Mossad ametoa ufichuzi wa oparesheni za Mossad dhidi ya Iran katika mahojiano ya kipekee .

    Yossi Cohen alitoa maelezo juu ya wizi wa stakabadhi za nyuklia za Iran.

    Uvamizi wa ghala mnamo 2018 ulichukua maelfu ya nyaraka kutoka nchini humo kwenda Israeli.

    Alidokeza pia kuhusika kwa Israeli katika uharibifu wa kituo cha nyuklia cha Irani huko Natanz, na mauaji ya mwanasayansi wa nyuklia.

    Bwana Cohen alistaafu kama mkuu wa Mossad wiki iliyopita.

    Alizungumza na mwandishi wa habari Ilan Dayan kwenye kipindi maalum cha runinga cha Uvda cha Channel 12, kilichopeperushwa Israeli Alhamisi usiku.

    Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu alimteua Bwana Cohen kama mkuu wa Mossad mwishoni mwa mwaka 2015. Alijiunga na shirika hilo mnamo 1982 baada ya kusoma katika chuo kikuu huko London, na aliambia kipindi hicho kwamba alikuwa na "mamia" ya pasipoti katika kipindi chote cha kazi yake.

  2. Marekani yashtumu hatua ya Nigeria kuifungia Twitter

    TWITTER

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Marekani imelaaani vikali hatua ya serikali ya Nigeria kufungia mtandao wa Twitter nchini humo.

    Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani, Ned Price amesema hatua hiyo ya Nigeria si tu inakiuka uhuru wa demokrasia lakini pia inakandamiza uhuru wa kujieleza.

    Wiki iliyopita Nigeria iliamua kufungia mtandao huo kutoa huduma nchini humo baada ya mtandao huo kufuta moja ya chapisho la rais wa nchi hiyo, Muhammadu Buhari kwa madai lilikuwa ni la uchochezi.

    Pamoja na kufungiwa kwa mtandao huo, ili kuendelea kutumia mtandao huo, baadhi ya wanigeria wanatumia VPN

    Serikali yenyewe ya Nigeria ilisema kufungiwa kwa mtandao huo hakuna uhusiano wowote na kuondolewa ama kufutwa kwa chapisho la Rais Buhari.

    Chapisho hilo la Buhari lilieleza kuwashughulia watu wote hasa vijana ambao wamekuwa wakuharibu miundo mbinu ya serikali.

  3. Majaji sita waliokataliwa na rais Uhuru Kenyatta lazima wateuliwe-asema jaji mkuu wa Kenya Martha Koome

    Koome

    Chanzo cha picha, JUDICIAL SERVICE COMMISSION

    Jaji Mkuu Martha Koome amesisitiza wito wake kuwa majaji sita walioachwa kwenye orodha ya wale walioteuliwana rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ni lazima wateuliwe .

    Akizungumza wakati wa kuapishwa kwa Daniel Musinga kama rais wa Mahakama ya Rufaa, alisema wakati huo ulikuwa mchungu, kwa sababu majaji wanne - ambao waliteuliwa kwa korti ya Rufaa - walikuwa bado hawajateuliwa.

    Koome alisema Mahakama iko katika hatari ya kutekwa na idara na vile vile "watu ambao sitawataja".

    Koome pia alielezea wasiwasi wake kuhusu ufadhili mdogo wa Mahakama na akamuambia Spika wa Bunge la taifa Justin Muturi moja kwa moja, akisema kwamba mgao wa Sh37 bilioni ulikuwa mdogo sana kati ya Bajeti ya Sh3.6 trilioni iliyosomwa siku Alhamisi.

    Koome alisema Idara ya Mahakama ilikuwa ikifanya kazi katika "jumba la makavazi" ambalo lilikuwa katika hali mbaya na akashangaa kwa nini wizara ya Afya haijalitaja jengo hilo kama hatari ya kiafya lisilofaa kutumiwa

  4. Ethiopia yakanusha Jimbo la Tigray kukumbwa na baa la njaa

    Tigray

    Chanzo cha picha, AFP

    Serikali ya Ethiopia imekanusha taarifa kuwa jimbo la Tigray nchini humo limekumbwa na baa la njaa.

    Kauli hiyo imekuja muda mfupi baada ya Umoja wa Mataifa kutoa ripoti ya utafiti wake ikionya kwamba watu 350,000 katika jimbo hilo wanakabiliwa na hali mbaya ya njaa. Ripoti hiyo imeyataja pia maeneo jirani ya Amhara na Afar.

    Jimbo hilo limekuwa kwenye mapigano kwa zaidi ya miezi saba sasa, na kusababisha maelfu ya watu kuuawa na maelfu wengine kuyakimbia makazi yao.

    Serikali ya Ethiopia inasema ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa kuhusu uwepo wa baa la njaa kwenye eneo la Kaskazini mwa Tigray si za kweli.

    Msemaji wa masuala ya kigeni amesema serikali imekuwa ikipeleka vyakula katika maeneo hayo kwa ajili ya wenye uhitaji, na kuwapatia mbegu wakulima na pembejeo zingine kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa kilimo unaotarajiwa kuanza wiki chache zijazo.

    Umoja wa Mataifa na Jumuia ya Ulaya, mara kadhaa zimeonya na kuzitaka pande zinazozozana kusitisha mapigano ili kuruhusu misaada ya kibinadamu wakifkia mamilioni ya watu wenye uhitaji na kuepusha baa la njaa.

  5. Fahamu sababu za mwanamke kujifungua watoto wengi kwa pamoja

    Je uzazi wa watoto wengi kwa pamoja, ni jambo la hatari kwa mama na watoto?Soma zaidi

    Deaconess Doris Levi Wilson mwenye umri wa miaka 49 alipata watoto wasichana wanne na wavulana wawili Februari, 9, 2021.
  6. Uganda yarekodi viwango vya juu zaidi vya maambukizi ya virusi vya corona

    Doses of Uganda's first batch of Covid vaccine are fast running out

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Uganda imeandikisha viwango vya juu zaidi vya maambukizi ya virusi vya corona kuwahi kushuhudiwa nchini humo tangu janga la hilo lilipoanza.

    Watu 1,438 kati ya 8,478 waliambukizwa virusi kulingana na takwimu iliyotolewa na Wizara ya Afya siku ya Alhamisi. Vipimo vilifanywa tarehe 8 mwezi Juni.

    Nchini hiyo imekuwa ikikabiliwa na aina mpya ya virusi ambayo viligunduliwa kwanza nchini India, Uingereza, na Afrika Kusini ikiwemo kirusi kingine kilichogunduliwa China.

    Kuna wasi wasi visa vya maambukizi vinaendelea kuongezeka na hospitali huenda zikalemewa kwa kukosa vifaa tiba muhimu kama vile oksijeni.

    Shirika la ndege la kitaifa la Rwanda RwandAir limesitisha safari zake kwenda Uganda kutokana na ongezeko la maambukizi.

    Siku ya Jumatano, Milki ya Falme za Kiarabu zilisema kwamba wasafiri kutoka Uganda, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hawataruhusiwa kuingia nchini humo kuanzia Ijumaa hii.

    Zaidi ya watu 750,000 wamepewa chanjo ya corona nchini Uganda kufikia sasa.

    Nchi ilikuwa imepokea dozi 964,000 za chanjo ya AstraZeneca mnamo mwezi Machi, ambayo inaelekea kuisha.

  7. Mzozo waibuka Burundi juu ya 'Adhana'- wito wa Sala

    Waziri aliwaomba mashekhe kupunguza sauti ya Adhana wakati wa alfajiri

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Waziri aliwaomba mashekhe kupunguza sauti ya Adhana wakati wa alfajiri

    Viongozi wa Kiislamu nchi Muslim Burundi wamejitenga na kauli iliyotolewa na mmoja wao kumkosoa waziri wa mambo ya ndani aliyetoa wito kwa mashekhe kupunguza sauti ya adhana ya asubuhi ili isiwe kero kwa umma.

    Katika kikao cha pamoja na viongozi wa kidini, Waziri wa Mambo ya ndani wa Burundi Gervais Ndirakobuca aliwaomba viongozi kidini wasipige kelele wakati wa maombi ya usiku na kwa wenzao wa Kiislamu kupunguza sauti ya Adhana (wito wa sala) wakati wa alfajiri.

    Jumanne asubuhi Ndikumana Rashid, alisikika akimkaripia waziri na kumtaka afutilie mbali matamshi aliyotoa na kuomba msamaha.

    Bw. Rashid alisema kauli ya waziri ni shambulio la moja kwa moja dhidi ya dini ya Kiislamu.

    Wawakilishi wa Waislamu hata hivyo wamesema Bw. Rashid atawajibikia kauli yake kwa kumtukana waziri.

    Mkuu wa Baraza la Waislamu nchini Burundi Zuberi Mohamed, amesema hakuna mzozo kati ya Waislamu na serikali akiongeza kuwa wito wa sala jimbo la kawaida.

  8. Chuo cha kupambana na ugaidi chafunguliwa Ivory Coast

    Wanajeshi

    Chanzo cha picha, AFP

    Chuo cha kimataifa cha kupambana na ugaidi kimefunguliwa karibu na mji wa Abidjan huko Ivory Coast.

    Chuo hicho kinachofahamika kama AILCT, kilifadhiliwa na Ufaransa na Muungano wa Ulaya ,EU, na nchini zingine kinalenga kusaidia eneo hilo kukabiliana na wanamgambo wa kijihadi.

    Hafla ya ufunguzi wake iliongozwa na Waziri Mkuu wa Ivory Coast, Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo na Waziri wa Mambo ya nje wa Ufaransa.

    Chuo hicho ambacho kimejengwa eneo lenye minazi mingi karibu kilo mita 80 kutoka mjini Abidjan, kitatumika kutoa mafunzo ya kijeshi.

    Wanajeshi

    Chanzo cha picha, AFP

    Tayari dola milioni 27 sawa na (euro milioni 20) zimewekezwa katika mradi huo lakini fedha zaidi zinahitajika kuukamilisha ndani ya miaka miwili ijayo.

    Malengo matatu muhimu ni:

    • Kufundisha vikosi maalum vya majeshi katika mkoa huo.
    • Kuwapa mafunzo dhidi ya ugaidi maafisa, kama mahakimu, maafisa wa forodha na wahasibu.AILCT inataka kuunda mitandao ya wataalamu wanaojuana na kufanya kazi pamoja katika mipaka.
    • Kuunda kituo cha kimkakati cha kusoma.
    Tayari dola milioni 27 sawa na (euro milioni 20) zimewekezwa katika mradi huo

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Tayari dola milioni 27 sawa na (euro milioni 20) zimewekezwa katika mradi huo

    Uzinduzi wake unakuja siku chache baada ya Ufaransa kutangaza kwamba inakamilisha Operesheni ya Barkhane katika eneo la Sahel, ambalo linakabiliwa ukame kusini mwa Jangwa la Sahara.

    Eneo hilo linajumuisha Mali, Chad, Niger, Burkina Faso na Mauritania.

  9. Mkuu wa mkoa aliyetaka wananchi wabebe mabango kumkaribisha rais mashakani

    Rais Samia Suluhu

    Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania

    Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ametengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Albert Chalamila leo Juni 11, 2021.

    Chalamila amedumu kwenye nafasi hiyo kwenye mkoa wa Mwanza kwa siku 23 tu baada ya kuapishwa na Rais Samia Mei 19 mwaka huu baada ya kuhudumu kama mkuu wa mkoa wa Mwanza.

    Rais Samia amechukua hatua hiyo siku mbili kabla ya kuanza ziara yake ya siku tatu katika mkoa huo, ambapo pamoja na mambo mengine anatarajiwa kuzungumza na maelfu ya vijana kama alivyofanya wiki hii alipozunguza na maelfu ya wanawake mkoani Dodoma.

    Chalamila alikuwa anasifika kwa kutoa kauli tata hasa anapokuwa kwenye mijumuiko ya utekelezaji wa majukumu yake, tangu akiwa katika nafasi ya ukuu wa wilaya na baadae mkuu wa mkoa wa Mbeya.

    Siku mbili zilizopita Chalamila aliwataka wananchi wa mkoa wa Mwanza, wabebe mabango na kwenda nayo kwenye ziara ya Rais Samia hata kama yana ‘matusi’, kauli ambayo wengi wanaitafsiri kama ndiyo sababu ya kuondolewa kwake. huu.

    Ingawa hakuna uthibitisho wa hilo, lakini kauli hiyo inapingana na maagizo ya Rais aliyoyatoa hivi karibuni, akisema kwenye ziara yake mikoani akikuta mabango yoyote yamebebwa na wananchi, basi viongozi husika wa eneo hilo watawajibika ikiwemo kufutwa kazi.

    Hata hivyo Chalamila katika malezo yake ya awali kuhusu ziara ya Rais Samia mkoani Mwanza, alisema kauli ya Rais ilimaanisha mabango mengine, lakini mabango yenye nia njema hayajakatazwa kwa faida ya utatuzi wa jambo ama masuala ya maendeleo.

  10. RwandaAir yasitisha kwa muda safari zake Uganda -kunani?

      • Author, Dinah Gahamanyi
      • Nafasi, BBC Swahili
    RwandaAir

    Chanzo cha picha, RwandaAir

    Shirika la ndege la Rwanda, RwandAir imetangaza kuwa imesitisha kwa muda safari zake za ndege za kwenda na kutoka kwenye uwanja wa kimataifa wa ndege wa Uganda wa Entebbe mara moja.

    “Kutokana na kuongezeka kwa visa vya Covid-19 nchini Uganda, RwandAir inatangaza kusitishwa kwa safari zake za ndege za kuelekea na kutoka Entebbe kuanzia tarehe 10 Juni 2021, hadi tangazo lingine litakapotolewa,” Taarifa ya shirika hilo la ndege ya Rwanda lilisema.

    Ruka X ujumbe
    Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

    Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

    Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

    Mwisho wa X ujumbe

    Liliongeza kuwa : “RwandAir inaomba radhi kwa usumbufu uliosababishwa na hatua hiyo.”

    Shirika hilo lilisema kuwa wateja waliothiriwa ‘’wanaweza kupanga upya safari na kusafiri baadaye, pale safari hizo zitakaporejeshwa tena–au waombe kurejeshewa pesa zao za nauli.”

    Uganda imeshuhudia ongezeko la idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona, jambo lililowalazimisha maafisa kuweka sheria inayowataka watu kupunguza shughuli na matembezi yasiyo ya lazima kwa muda wawiki sita.

  11. Karibu katika matangazo ya moja kwa moja leo Ijumaa 11.06.2021