Biden amuonya Putin katika ziara yake ya kwanza ya kigeni
Biden alisema Moscow itakabiliwa na athari mbaya ikiwa itahusika katika "shughuli mbaya".
Moja kwa moja
Ambia Hirsi and Lizzy Masinga
Biden amuonya Putin katika ziara yake yake kwanza ya kigeni

Rais wa Marekani Joe Biden ameanza safari yake ya kwanza nje ya nchi yake kwa onyo kwa taifa la Urusi
Biden alisema Moscow itakabiliwa na athari mbaya ikiwa itahusika katika "shughuli mbaya".
Biden alithibitisha kuwa atatoa ujumbe wazi kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin, katika mahojiano na umati wa wanajeshi wa Amerika na familia zao jana, Jumatano, huko Mildenhall Air Force Base, ambapo ndege yake ilitua kabla ya kuelekea Cornwall, kusini magharibi mwa Uingereza.
Biden alisema: "Hatutafuti mzozo na Urusi.
Tunataka uhusiano thabiti. Ujumbe wangu uko wazi: Marekani itajibu kwa nguvu na kwa uthabiti ikiwa Urusi itajihusisha na shughuli zinazodhuru.
Mnamo Aprili, Putin alishutumu nchi za Magharibi kwa kujaribu "kuiwinda" Urusi, akiwaonya wasivuke "mstari mwekundu’
Katika kila kituo cha safari yake ya kwanza ya kigeni kama rais wa Marekani , Biden ameonekana kutoa ujumbe wa wazi kwamba "Marekani inarudi na nchi za demokrasia ulimwenguni kote zinashirikiana bega kwa bega mbele ya changamoto kubwa zaidi ambazo zinatishia siku zijazo
Zaidi ya watu 350,000 wanaishi katika mazingira ya njaa Ethiopia

Chanzo cha picha, Getty Images
Zaidi ya watu 350,000 wanaishi katika mazingira ya njaa nchini Ethiopia, kwa mujibu wa tathimini ya taasisi inayoangalia masuala ya usalama wa chakula.
The Integrated Phase Classification (IPC) imetumia viwango vinne vya kupima usalama wa chakula kutoka kiwango kidogo mpaka katika kiwango cha ''baa'' ikimaanisha njaa- ingawa ni kazi ya serikali kutangaza baa la njaa.
Tathimini hiyo ya IPC ilifanywa mji wa kaskazini wa Tigray, ambako kulikuwa na mapigano yaliyoibuka mwezi Novemba, na mikoa mingine ya Amhara na Afar kati ya Mei na mwezi Juni mwaka huu. Hii ni idadi kubwa ya watu tangu mwaka 2011 wakati njaa nchini Somalia''. Ripoti imeeleza.
Mgogoro huu mkubwa unatokana na athari za mizozo, pamoja na watu kuyakimbia makazi yao upatikanaji mdogo wa misaada ya kibinadamu, upotezaji wa mali ya mavuno na mapato, na masoko yasiyofaa au yasiyokuwepo.
Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na shirika la watoto Unicef wametaka kuchukuliwa hatua za haraka kushughulikia mgogoro huo. "Jamii za vijijini kaskazini mwa Ethiopia zimeathiriwa sana na mzozo.
Kenya yafungua anga lake kwa safari za Ndege za kuelekea na kutoka Somalia

Serikali ya Kenya leo Alhamisi imeondoa marufuku ya safari za ndege kuelekea na kutoka Somalia.
Wizara ya Mambo ya nje imesema mabadiliko hayo yamesukumwa na masilahi ya pande hizo mbili kwa matumaini kwamba kuhalalisha kabisa uhusiano wa pande mbili kutatokea.
"Serikali ya Kenya imezingatia maombi yaliyofanywa na imeamua kufungua tena anga ya Kenya kwa ndege zote zinazotokea Somalia na kutoka Kenya kwenda Somalia," ilisema taarifa hiyo.
Taarifa zaidi imesema kuwa masharti ya kupambana na Covid-19 yatahusu abiria wote kutoka Somalia wanaoingia Kenya, kama yaliyoainishwa mamlaka ya anga ya Kenya.
Hati inayoonesha hakuna maambukizi ya virusi vya corona kabla ya kuondoka au kuingia nchini itahitajika.
Hatua hii itakuja mwezi karibu mmoja baada ya KCAA, kupiga marufuku safari zote za kuelekea na kutoka Somalia wakati nchi hizo zikiwa zimeingia katika mvutano.
Marufuku hiyo imekuja siku kadhaa baada ya Qatar, kupitia mfalme Emir Sheikh Tamim Al Thani aliyesababisha kurejesha mahusiano ya kidiplomasia na Nairobi baada ya mzozo wa kidiplomasia uliodumu kwa miezi mitano.
Tarehe 31 mwezi Mei, serikali ya Kenya ilirejea marufuku yake dhidi ya safari za ndege kuelekea Somalia, ikisema kuwa hatua hiyo ilisababishwa na kuvunjika kwa mahusiano ya kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.
Ripoti ya UN imesema wanajeshi wa Somalia walipigana Tigray huku Ethiopia ikishtumiwa kwa mauaji ya kiholela

Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Mamilioni ya watu waliathiriwa katika mzozo wa Tigray Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa inadai kwamba wanajeshi kutoka Somalia walipigana kwa ushirikiano na Waeritrea katika eneo linalokumbwa na mzozo la Ethiopia-Tigray.
Ripoti ya Mwakilishi Maalum wa Umoja wa mataifa Mohamed Abdelsalan Babiker ilisema wanajeshi wa Somalia walipigana katika mstari wa mbele huko Tigray.
"Mbali na ripoti za kuhusika kwa wanajeshi wa Eritrea katika mzozo wa Tigray, mwakilishi huyo Maalum pia alipokea habari na ripoti kwamba wanajeshi wa Somalia walihamishwa kutoka kambi za mafunzo ya kijeshi huko Eritrea hadi mstari wa mbele huko Tigray, ambapo waliandamana na wanajeshi wa Eritrea wakati wakivuka mpaka wa Ethiopia, "inabainisha ripoti hiyo.
Ilisema kwamba wapiganaji wa Somalia waliripotiwa kuwapo katika mji mtakatifu wa Ethiopia wa Aksum. Serikali ya Somalia imekanusha kuhusika katika mzozo wa Tigray.
Eritrea haikushirikiana katika uchunguzi wa UN ambao ulizingatia zaidi hali ya haki za binadamu huko Eritrea.
Mwakilishi wa wa UN alisema ripoti yake ilitokana na uchunguzi na habari kutoka vyanzo tofauti.
Mnamo Februari, Shirika la Amnesty International lilishtumu wanajeshi wa Eritrea huko Aksum kwa kuua mamia ya watu haswa zaidi ya siku mbili mnamo Novemba ambayo inaweza kuwa ni uhalifu dhidi ya binadamu – madai ambayo mamlaka ya Eritrea ilitupilia mbali.
Mzozo wa Tigray uliibuka mnamo Novemba mwaka jana wakati serikali ya Ethiopia ilipoanzisha shambulio la kukiondoa chama tawala cha jimbo hilo TPLF madarakani baada ya wapiganaji wake kuteka kambi za jeshi za serikali huko Tigray.
Tangu mzozo ulipoibuka mwaka jana, maelfu ya watu wanafikiriwa kuuawa na mamilioni wanahitaji msaada wa kibinadamu.
wakati huo huo Serikali ya Ethiopia imeshutumiwa kwa kutekeleza mauaji ya kiholela ya kijana mmoja - katika ripoti mpya ya Human Rights Watch. Amanuel Wondimu Kebede mwenye umri wa miaka 17 aliuawa katika mkoa wa Oromia wa Ethiopia mnamo Mei mwaka jana- ni mmoja wa raia wengi waliokufa tangu mapigano yalipoanza katika eneo hilo miaka 3 iliyopita. Imesababisha wito wa uwajibikaji zaidi kwa vikosi vya usalama nchini humo.
Video iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii ilionyesha dakika za mwisho za Amanuel Wondimu Kebede .. Mikono yake ilikuwa imefungwa nyuma yake. Bunduki ilikuwa imetundikwa shingoni mwake ... uso wake ulikuwa na damu wakati alikuwa akizungumza na kamera.
Human Rights Watch inadai kwamba - dakika chache tu baadaye - vikosi vya usalama vya Ethiopia viliamuru kijana huyo ageuze kichwa chake… kabla ya kumpiga risasi mara mbili mbele ya mashahidi wasiopungua wanne.
Wakati huo, ilidaiwa kuwa Amanuel alikuwa amempiga risasi na kumjeruhi mtu mwingine - na vile vile alikuwa akihusishwa na mauaji ya mwandishi wa habari wa huko.
Hili pia limepingwa - na mashahidi wakisema alikuwa mwanafunzi mzuri ambaye alifanya kazi katika kanisa la eneo hilo.
Mzozo wa miaka mitatu kati ya serikali na Jeshi la Ukombozi la Oromo umewaacha raia wengi wamekufa. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanadai udhalilishaji unaofanywa na vikosi vya usalama, pamoja na kuzima kwa mawasiliano na mauaji ya kiholela.
Maelezo zaidi:
- Jukumu la Eritrea katika mzozo wa Ethiopia
- Mzozo wa Tigray Ethiopia: Jinsi askari alivyonusurika makabiliano ya risasi kwa saa 11
Kampuni ya Kenya ya parachichi yakabiliwa na madai zaidi ya unyanyasaji

Maelezo ya picha, Mudhikwa Musau anawatuhumu walinzi wa Kakuzi kwa ubakaji Wanawake wawili ambao wanasema walibakwa na walinzi katika shamba la Kakuzi nchini Kenya wamezungumza juu ya masaibu yao.
Madai yao yanakuja wakati kampuni hiyo ya kilimo inataka kuyashtaki makundi ya haki za binadamu ya Kenya juu ya kile inachosema ni madai ya uwongo ya unyanyasaji.
Wakosoaji wanasema kesi hiyo ya Kakuzi inakusudia kushinda mikataba ya hapo nyuma iliyopotea baada ya madula ya jumla kususia kuchukua bidhaa zake nchini Uingereza
Kampuni hiyo iliiambia BBC kwamba madai hayo mapya yanapaswa kuchunguzwa na haitawavumilia wanaofanya makosa.

Mudhikwa Musau, mwenye umri wa miaka 88, anaishi katika kijiji umbali wa dakika chache kutoka pembeni mwa miti iliyo katika ua la shamba kubwa la Kakuzi katikati mwa Kenya.
Anasema mnamo 2009 alibakwa kwa nguvu na mmoja wa walinzi wa kampuni hiyo. Akizungumza kwa lugha ya Kikamba, anaonyesha jinsi shambulio hilo lilivyotekelezwa .
"Nilikamatwa hivi na alikuwa akinishika hapa kama hivi. Nilizungushwa. Alisimama na kunikanyaga. Alinikanyaga shingoni. Alinishika shingo na kuligeuza. Alifunika mdomo wangu wakati nikipiga kelele . "
Mudhikwa Musau anasema alikwenda polisi baada ya kutoa malalamiko yake, lakini hakusikia tena kuhusu kesi hiyo.
Marium Wanja mwenye umri wa miaka sitini na tano pia amejitokeza. Anasema alizaa watoto wawili aliopata na walinzi wa Kakuzi miaka ya 1990.
Utakikumbuka vipi kipindi cha televisheni cha Keeping Up With the Kardashians?

Chanzo cha picha, Getty Images
Walionekana kuongoza hali ya watu kuwa wazi na hisia zao, na mojawapo ya mafanikio yao yalitokana na kuonekana kuwa wazi mbele ya kamera kuhusu hisia zao.
Waliibua gumzo juu ya urembo wa mwanamke. Kim alikuwa na athari kwa mtazamo wa dunia wa muonekano wa mwanamke mrembo.
Kipindi kilimuonyesha mara nyingi Kardashian katika "glam squad", akitoa huduma za kitaalamu za vipodozi, na mitindo ya nywele.

Chanzo cha picha, Getty Images
Walikuwa wa kwanza kuonesha jinsi mtu anavyoweza kujinadi binafsi katika mitandao ya kijamii.
Kim na Kylie ni miongoni mwa watu 10 wenye ufuasi mkubwa zaidi katika mitandao wa Instagram huku Kendall, Khloé na Kourtney wakiwa miongoni mwa watu 20 wenye ufuasi zaidi.
Walionyesha aina tofauti za familia. Mojawapo ya matokeo ya kufungua maisha yako kwa umma kwenye tamthilia ya maisha halisi ya Televisheni ni kwamba watazamaji wataona mzozo wa mahusiano yenu na wengi walivutiwa na namna walivyokuwa na mizozo lakini wakaendelea kuishi kama familia.
Mambo mengine yaliyoifanya familia ya Kardashian kuwa maarufu ni pamoja na:
- Shutuma ya kuwa na ‘’utata wa asili’’ na kuwa na utamaduni usiofaa
- Walikuwa na mapenzi tele – na talaka
- Kukosolewa kwa kujigamba kwa utajiri wao.
Pamoja na kukamilika kwa kipindi chao cha sasa, wamejipanga kimaisha.
Familia hii imesaini mkataba na huduma ya usajili ya Hulu na kipindi chao kitazinduliwa baadaye mwaka huu.
Maelezo zaidi juu ya kipindi hicho bado hayajafichuliwa, lakini kuna uwezekano mkubwa wa kusikia zaidi juu ya talaka ya Kim na Kanye.
Rais wa Kenya atangaza kazi kwa watengenezaji bunduki haramu

Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Zaidi ya silaha haramu 5,000 zilizojisalimishwa wakati wa msamaha zilichomwa moto mwaka jana Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametoa wito kwa watengezaji bunduki haramu kujiunga na kiwanda kipya cha utengenezaji silaha nchini.
Amesema salaha nyingi haramu zinazokamatwa na mamlaka za usalama zinatengezwa nchini.
Rais amewaahidi watengenezaji silaha "uthabiti" wa kazi "kukuza uchumi na kusaidia kudumisha usalama wan chi yako”.
Alisema wale wanaotaka kazi kuwasiliana na vyombo vya usalama kutoa huduma zao.
Mnamo mwezi Aprili Kenya ilizindua kiwanda cha silaha mbacho kilijengwa kwa gharama ya dola milioni 36.
Jaji Mkuu mwingine wa zamani Kenya amkosoa Rais Kenyatta

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Jaji Mkuu wa zamani wa Kenya David Maraga Hatua ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kuwakataa majaji sita waliopendekezwa na Tume ya Hudama za Mahakama,JSC, imeendelea kuzua hisia mseto.
Kiongozi wa hivi punde kutoa kauli yake kuhusiana na suala hilo ni Jaji Mkuu mshaafu David Maraga.
Katika mahojiano na Kituo cha Televisheni cha KTN, Bwana Maraga alisema: ''Hali kama hii ikiendelea nchini itaongozwa bila katiba''
Maraga amemtaka rais Kenyatta kuwateua majaji sita aliowaacha nje.
''Muda umewadia kwa bunge kumuondoa madarakani (Uhuru) akikiuka katiba'' aliongeza kusema.
Majaji hao sita ni miongoni mwa majaji 41 ambao walikuwa wamependekezwa kwa ajili ya uteuzi na Tume ya Huduma za mahakama nchini humo (JSC) miaka miwili iliyopita. Mmoja wa majaji hao alifariki.
Rais Kenyatta amekataa mapendekezo ya JSC licha ya maagizo mawili ya mahakama yaliyomtaka kufanya hivyo.
Nigeria yataka wenye mitandao ya kijamii kupata vibali vya ndani

Chanzo cha picha, AFP
Kampuni za mitandao ya kijamii ambazo zinataka kuendesha shughuli zao nchini Nigeria sasa zitahitajika kujisajili nchini humo na kupewa leseni na tume ya utangazaji.
Waziri wa mawasiliano,Lai Mohammed, ametoa tangazo hilo kufuatia hatua ya serikali kupiga Twitter marufuki siku tano iliyopita.
Mtandao huo wa kijamii ulifuta ujumbe wa Rais Muhammadu Buhari kwa kukiuka sheria zake lakini ofisi ya rais imepinga madai kwamba marufuku hiyo ilikuwa hatua ya kilipiza kisasi.
Baadhi ya vyombo vya habari vya kibinafsi nchini Nigeria vimepuuza amri ya kufunga akaunti zao za Twitter na kuamua kufikia mtandao huo kupitia mtandao wa VPN.
UN yataka usalama kuimarishwa DRC baada ya watu 19 kuuawa

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Uvamizi wa mara kwa mara unafanywa katika mkoa wa mashariki na kikundi cha waasi Watu 19 wameuawa katika msururu wa mauaji nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Madaktari wasiokua na mipaka au Médecins Sans Frontières wamesema raia 10 waliuawa baada ya hospitali kushambuliwa katika mji wa Boga mashariki mwa DRC siku ya Jumatatu.
Miili kadha iliripotiwa kupatikana baada ya wakulima kushambuliwa katika mpaka kati ya mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri.
Mashambulio ya mara kwa mara yamekuwa yakifanywa katika eneo hilo na Vikosi vya Allied Democratic au ADF– moja ya makumi ya makundi yaliyojihami mashariki mwa DRC.
Matthias Gillman, msemaji wa kikosi cha walinda usalama wa wa Umoja wa Mataifa - au Monusco – ametoa wito wa kupelekwa kwa maafisa zaidi wa polisi katika eneo hilo:
"Eneo hili limekuwa hatari kwa muda mrefu kwa sababu liko vijijini, ni vigumu kufika, ni kubwa na halina maafisa wa usalama wa serikali wanaohitajika, ndio sababu vikosi vya Monusco ... vinataka serikali kuimarisha uwepo wake.
- Kwanini hali ya usalama imeendelea kuwa tete nchini DRC?
- Namna ambavyo waasi wa Uganda walikuwa washirika wa IS nchini DRC
Morocco yahalalisha bangi ya dawa

Chanzo cha picha, Getty Images
Bunge nchini Morocco limeidhinisha sheria inayohalalisha ukuzaji wa bangi kwa ajili ya matumizi ya tiba na viwandani.
Lengo ni kuingia katika soko la kimataifa linalokua la kimataifa, kukuza kilimo na kutoa ajirahasa katika maeneo ya vijijini ambayo hayana maendeleo.
Morocco ni moja nchi zinazokuza bangi kwa kiwango kikubwa kwa matumizi haramu. Hii itasalia kuwa haramu chini ya sheria mpya.
Madhara ya Bangi
- Unaweza kusababisha kuchanganyikiwa na wasiwasi usio wa kawaida
- Ikivutwa na tumbaku, inaweza kuongeza hatari ya ugonjwa kama vile saratani ya mapafu
- Matumizi ya mara kwa mara yamehusishwa na hatari ya kupatwa na magonjwa ya kiakili
- Upungufu wa kudumu wa kiwango cha mtu kufikiria na kufahamu mambo, baada ya kutumia kwa muda mrefu
Maelezo zaidi:
- Fahamu nchi zinazotumia bangi kwa kiasi kikubwa
- Tanzania na Kenya zinaongoza kwa uvutaji wa bangi Afrika mashariki
Hujambo, haya ni matangazo mubashara leo Alhamisi 10.06.2021
