Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Serikali yaingilia kati sakata la kuahirishwa mchezo wa Simba na Yanga
Serikali ya Tanzania imeiagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kutoa taarifa kuhusu sakata la mechi ya watani wa jadi timu za Simba na Yanga
Moja kwa moja
Lizzy Masinga
Mwanafunzi bora mitihani ya taifa kidato cha nne ana ndoto ya kuwa daktari
Mshindi wa kwanza wa mitihani ya kumaliza kidato cha nne, KCSE2020 Robinson Wanjala Simiyu anatarajia kusoma udaktari katika Chuo Kikuu cha Nairobi.
Simiyu, kutoka Shule ya Sekondari ya Murang'a, alipata wastani wa A ya 87.334 kulingana na matokeo yaliyotolewa hivi karibuni.
Alisema alikuwa ameomba kusome udaktari na uhandisi lakini shauku yake iko kwenye udaktari.
Simiyu amewapa hamasa wenzake kufuata ndoto zao bila kujali changamoto wanazozipitia.
Simiyu alisoma Shule ya Msingi Gacie ambapo pia alifaulu kwa alama za juu zilizompa nafasi ya kwenda Shule ya Sekondari ya Murang'a.
Jumla ya wanafunzi 747,161 walifanya mitihani katika vituo 10,565 nchi nzima, kwa mujibu wa Dkt Mercy Karogo, Kaimu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la kitaifa la Kenya (Knec).
Waumini 40 watekwa msikitini wakati wa ibada ya Ramadhani Nigeria
Watu wenye silaha wamewateka waumini 40 kutoka kwenye msikiti wakati wa ibada ya usiku ya Ramadhani mjini Jibiya, Polisi wa jimbo la Katsina lililo kaskazini magharibi mwa Nigeria wamesema.
Tukio hilo lilitokea Jumapili usiku.
Msemaji wa polisi katika jimbo hilo Gambo Isah aliambia BBC timu ya pamoja ya waangalizi wa eneo hilo, polisi na wanajeshi waliwafukuza mara moja wale watu wenye silaha na kuwaokoa mateka wapatao 30.
Alisema watu 10 walikuwa bado hawajajulikana walipo.
Waumini walikusanyika ndani ya msikiti kwa ajili ya swala ya Thajjud-ambayo hufanywa wakati wa siku za mwisho za mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Watekaji walivamia msikiti, kufyatua risasi na kuwakamata watu kadhaa.
Utekaji nyara wa ukombozi unaofanywa na magenge ya wahalifu wenye silaha ni jambo la kawaida nchini Nigeria na Katsina likiwa moja ya majimbo yaliyoathirika zaidi.
Kabuga 'hana afya njema' kuendelea na kesi ya mauaji ya kimbari ya Rwanda
Mawakili wanaomuwakilisha anayedaiwa kuwa mfadhili wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda wameomba mashtaka dhidi yake yaondolewe kwa madai kuwa hayuko sawa kushtakiwa kwa sababu ya afya mbaya.
Félicien Kabuga, mwenye umri wa miaka 84, alikamatwa mwaka mmoja uliopita nchini Ufaransa na anazuiliwa Hague akisubiri kuhukumiwa katika mahakama inayoungwa mkono na UN nchini Tanzania.
Katika hati ya mahakama - Wakili wa Bw Kabuga anasema kuwa kuendelea kwa kesi hiyo kungekuwa ukiukaji mkubwa wa haki zake.
Wakati mmoja, mmoja wa watu tajiri zaidi nchini Rwanda, Bw Kabuga anadaiwa alisaidia kuunda wanamgambo wa Kihutu wa Interahamwe na anatuhumiwa kuchochea Wahutu kuua idadi ya watu kwa kutumia redio aliyokuwa nayo.
Afisa wa jeshi auawa katika shambulio Burundi
Takribani watu wanane akiwemo afisa wa jeshi la Burundi waliuawa Jumapili usiku kando ya barabara ya Bujumbura-Gitega karibu na eneo la Muramvya.
Vyombo vya habari vya nchini humo vinaripoti kama kuvizia wakati polisi wanasema lilikuwa tukio la ujambazi.
Mashuhuda wanasema hakuna kilichoibiwa kutoka kwa waathiriwa.
Kanali Onesphore Nizigiyimana ambaye aliwahi kutumikia Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia (UNSOM) na mfanyakazi wa benki kuu walikuwa miongoni mwa waliouawa, kulingana na tovuti ya habari ya iBurundi.
Watu wengine kadhaa walijeruhiwa na magari yalichomwa moto, tovuti hiyo iliripoti.
Serikali yaingilia kati sakata la kuahirishwa mchezo wa Simba na Yanga
Serikali ya Tanzania imeiagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kutoa taarifa kuhusu sakata la mechi ya watani wa jadi timu za Simba na Yanga uliotarajiwa kuchezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam tarehe 8 mwezi Mei.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa kikao cha Bunge mjini Dodoma.
''Jambo hili limevuta hisia za watanzania hata pia nje ya nchi kwa sababu timu hizi ndizo ambazo zimebeba sura ya michezo hasa mpira wa miguu Tanzania''.Alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
''Kufuatia kero hii tayari tumeagiza wizara ya habari , utamaduni na Michezo kuhakikisha kwamba wanatoa taarifa haraka sana kwa Watanzania, kuhusu mchezo wenyewe utachezwa lini, lakini pia vile viingilio ambavyo watanzania walilipia kuingia kwenye mchezo ule hatima yake ni nini''.
Amewasihi Watanzania hasa wapenzi wa michezo, kuwa waipe muda wizara ili kutoa taarifa ikishirikiana na taasisi inayoshughulikia mpira wa miguu (TFF) ili Watanzania wajue hatima ya suala hilo.
Baada ya kuahirishwa wa mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga uliotakiwa kuchezwa Mei 8 mwaka huu kulisababisha manung’uniko katika mitandao ya jamii lakini pia kutojua hatima ya waliolipa kiingilio katika mchezo huo kumezua siutafahamu.
Amesema tukio hilo limevuta hisia Kwa Watanzania ndani na nje kwa sababu timu hizi ndizo zimebeba taswira ya mpira wa miguu Tanzania.
Kenya kuchunguza madai ya unyanyasaji wa kijinsia
Maafisa wa polisi wa Kenya wanachunguza kisa cha polisi wa kike kulalamika juu ya dhuluma na unyanyasaji wa kijinsia, kwenye video iliyosambaa sana.
Kwenye video hiyo, afisa huyo anauliza aruhusiwe kujiuzulu "kwa amani" kutoka kwenye huduma hiyo, akisema alikuwa ameandika barua nyingi za kujiuzulu lakini zilikuwa bado hazijafika kwa mkuu wa polisi, Inspekta Jenerali Hilary Mutyambai.
Afisa huyo aliye katika mji wa pwani wa Mombasa alielezea kufadhaika kwake juu ya ukosefu wa haki na ufisadi na kitengo cha Mambo ya Ndani cha polisi - ambacho kinashughulikia malalamiko dhidi ya polisi - na akasema hawajafanya chochote kusaidia kesi yake.
Alisema kufadhaika namna hii ndio sababu maafisa wa polisi hujiua au kuua wengine.
“Maafisa wa polisi wanauana kwa sababu ya hii. Nisaidie tu kutoka kwenye kazi hii. "aliomba.
Siku ya Jumapili, Inspekta Jenerali wa polisi aliamuru uchunguzi huru juu ya suala hilo na ripoti itolewe ndani ya siku saba.
Taarifa yake ilichapishwa kwenye mtandao wa twitter
Waziri wa mambo ya ndani ya Kenya Fred Matiang'i hivi karibuni alitangaza mpango wa kupiga marufuku mahusiano ya kimapenzi miongoni mwa maafisa wa polisi- akilenga kupunguza idadi ya vitendo vya uhalifu.
Alisema kumekuwa na ongezeko la mauaji ya wapenzi miongoni mwa maafisa polisi miezi kadhaa iliyopita.
Walinda amani wa zamani wa Ethiopia waomba hifadhi Sudan
Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya walinda amani 100 wa zamani kutoka Ethiopia wametafuta ulinzi wa kimataifa na wameomba hifadhi nchini Sudan.
Walikuwa sehemu ya ujumbe wa UN uliofungwa hivi karibuni huko Darfur.
Hii inakuja baada ya walinda amani wengine wa Ethiopia awali kutoka eneo la mzozo la Tigray - kukataa kurudi Ethiopia kwa kuhofia kuteswa.
Kuna wasiwasi unaoongezeka juu ya madai ya ukatili uliofanywa wakati wa mzozo wa miezi sita huko Tigray.
Umoja wa mataifa umesema badala ya kurudi nyumbani wakati operesheni ya ujumbe wao ilipomalizika katika mkoa wa Darfur, karibu walinda amani 120 wa Ethiopia waliomba hifadhi nchini Sudan.
Maendeleo haya yanaweza kuhusishwa na mivutano ya kikabila ambayo imezidi nchini Ethiopia kutokana na mzozo katika eneo la kaskazini mwa Tigray.
Mwezi Februari huko Sudan Kusini kundi jingine la walinda amani wa Ethiopia ambao walikuwa asili ya Tigray walikataa kwenda nyumbani wakisema wanahofia kuteswa.
Kumekuwa na ripoti nyingi za ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa mzozo wa miezi sita. Jumamosi mkuu wa Kanisa la madhehebu ya Orthodox la Ethiopia - yeye mwenyewe wa kabila la Tigray - alisema ukatili huo ni mauaji ya kimbari.
Ajipiga risasi baada ya kuwauwa sita katika sherehe ya kumbukumbu ya kuzaliwa
Mwanaume mmoja mwenye silaha ajiuwa kwa risasi baada ya kuwapiga risasi na kuwaua watu sita katika sherehe za kumbukumbu ya kuzaliwa huko Colorado Springs siku ya Jumapili, polisi wameeleza.
Milio ya risasi ilisikika katika bustani ya nyumbani ambayo inahamishika ambapo familia ilikutana kusheherekea.
"Mshukiwa ambaye ni mpenzi wa msichana aliyekuwa anasheherekea siku yake ya kuzaliwa , alifika nyumbani hapo na kuanza kupiga risasi watu waliokuwa katika sherehe hiyo kabla ya kujiua yeye mwenyewe," idara ya polisi ya Colorado Springs imesema.
Sababu ya shambulio hilo halijafahamika mpaka sasa.
Watu wote waliopigwa risasi walikuwa watu wazima ingawa kulikuwa na watoto katika sherehe hiyo katika wakati huo.
Hawajatajwa majina watu waliopigwa risasi na hata mshambuliaji hajatajwa bado.
"Tukio la kikatili limepelekea watu sita kufariki na wengine kujeruhiwa.Watoto hawakujeruhiwa na mshukiwa huyo na wapo na ndugu zao sasa,"polisi wameeleza.
Meya wa Colorado Springs Mayor John Suthers ametaja kuwa uhalifu huo ambao hauna maana; Leo tumejikuta tunaomboleza kupoteza kwa wapendwa wetu na kuwaombea wale waliojeruhiwa kupona haraka na familia zilizopoteza wapendwa wao."
Mwezi Machi, watu 10 waliuawa katika shambulio la risasi ndani ya duka katika mji ulio mpakani mwa Colorado. Mshukiwa alikamatwa baadae na kukabiliana na mashtaka 10 ya mauaji.
Habari...karibu katika matangazo ya moja kwa moja ya ukurasa wa BBC Swahili leo ikiwa ni Jumatatu 10/05/2021