Rais Samia: Ili tuwakinge wazee tumeamua kuvaa barakoa

Kwa mara ya kwanza, toka aingie madarakani mwezi Machi mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan amevaa barakoa hadharani akiwa nchini humo.

Moja kwa moja

  1. Na huu ndio mwisho wa matangazo yetu mubashara. Tukutane tena wiki ijayo panapo majaaliwa.

  2. Mji wa Tanzania 'wakumbwa na uhaba wa mipira ya kondomu'

    KONDOMU

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mji wa Tanzania uliopo kusini magharini wa Mbeya unakabiliwa na upungufu wa mipira ya kondomu, wawakilishi wa serikali za mitaa wameonya, kulingana na gazeti la Mwananchi nchini humo.

    Inasemekana kuwa suala hilo lilizungumziwa katika mkutano wa baraza la serikali za mitaa Mbeya siku ya Ijumaa huku mkusanyiko ukiarifiwa kuwa kumekuwa na upungufu katika maeneo ya baa na mengineo ya burudani kwa takribani miezi minne.

    Wengine hawakusita kuonesha hofu yao kwamba hilo linaweza kusababisha kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya ukimwi.

    "Sasa hivi tuko katika mchakato wa kukabiliana na janga la ugonjwa wa Ukimwi lakini hakuna mipira ya kondomu katika vituo, sasa tutakuwa tunazuia nini?" diwani Adam Hussein amenukuliwa akisea hivyo.

    Hata hivyo afisa wa afya, Dkt. Jonas Lulandala, alijitahidi kuhakikishia madiwani kuwa suala hilo linashughulikiwa, gazeti la Mwananchi limesema.

    Alikiri kuwa kumekuwa na tatizo katika ugawaji wa mipira ya kondomu kwa miezi ya Februari na Machi lakini akasema kuwa hilo limetatuliwa na hivi karibuni mipira ya kondomu itakuwa inapatikana tena.

    Ikiwa itatumiwa vizuri, mipira ya kondomu inaweza kuwa stahiki kwa hadi asilimia 95 katika kuzuia usambaaji wa virusi vya Ukimwi, utafiti umebaini.

  3. Kenya yalegeza masharti ya kuingiza mahindi kutoka Tanzania

    Mahindi

    Chanzo cha picha, NMG

    Kenya imelegeza masharti ya kuingiza mahindi kutoka Tanzania baada ya agizo la rais la kuharakisha ukaguzi wa malori ya mahindi kutoka nchi jirani.

    Hatua hiyo inafuatia mazungumzo ya nchi mbili kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Rais Samia Suluhu wa Tanzania ambayo yalipelekea makubaliano ya kulegeza masharti kuwezesha usafirishaji wa bidhaa na utoaji huduma kati ya Kenya na Tanzania.

    Kuafuatia hutua hiyo, Mamlaka ya Kilimo na Chakula imepunguza mchakato wa kuidhinisha uingizaji wa bidhaa hadi siku moja huku wafanyabiashara wakihitajika kusajili na mamlaka husika na kuonesha nakala ya cheti cha usajili kwa mkaguzi mpakani.

    Hata hivyo, wale wanaonunua mahindi kutoka Tanzania bado watahitajika kuwa na cheti kinachoonesha kukidhi viwango vinavyohitajika kabla ya bidhaa hiyo kuruhusiwa kuingia Kenya.

    Hadi kufikia mwisho wa Machi mwaka huu, ni mfanyabiashara mmoja pekee ndiye ambaye alikuwa amekidhi viwango vinavyohitajika vilivyowekwa na serikali kuingiza mahindi kutoka Tanzania.

    Serikali iliweka kanuni hizo baada kuondoa marufuku ya kuingiza mahindi kutoka nchi jirani kwa wasiwasi kwamba huenda yana kiwango cha juu cha sumu kuvu.

  4. Rais Samia: Ili tuwakinge wazee tumeamua kuvaa barakoa

    Mkutano wa Wazee

    Chanzo cha picha, IKULU, TANZANIA

    Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa yeye na viongozi wengine wamevaa barakoa hii leo ili kuwalinda wazee na maambukizi ya corona.

    Katika mkutano na Wazee wa Dar es Salaam, takriban washiriki wote wamevaa barakoa.

    "Leo tumekuja tofauti, tumevaa vifunika uso. Wazee ndio kundi lililo hatarini zaidi kupata maambukizi ya corona...huu ni mkusanyiko mkubwa, tumeshindwa kuwatenganisha hivyo ili tuwakinge tumeamua kuvaa barakoa," amesema Rais Samia.

    Rais Samia pia amesema kamati aliyoiunda kumshauri juu ya hatua za kuchukua katika mapambano dhidi ya corona inakaribia kumpatia ripoti yake na amewaahidi wazee kuwa serikali yake itachukua hatua kuwalinda na janga hilo.

    "...Yale yote yanayofanya wazee wawe kundi hatari tutakwenda kuyashughulikia ili tuwakinge wazee wetu, lakini pia kuwafundisha mbinu za kujikinga wenyewe dhidi ya maradhi haya," amesema Rais Samia.

    Leo ni mara ya kwanza toka aingie madarakani mwezi Machi mwaka huu kwa Rais Samia kuvaa barakoa hadharani akiwa nchini humo.

    Kabla alivaa barakoa akiwa nchini Uganda alipokwenda kutia saini ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta mwezi uliopita na mapema wiki hii alivaa akiwa katika ziara yake nchini Kenya.

  5. Rais na viongozi wakuu wa Tanzania wavaa barakoa

    Rais Samia

    Kwa mara ya kwanza, toka aingie madarakani mwezi Machi mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan amevaa barakoa hadharani akiwa nchini humo.

    Kala alivaa Barakoa akiwa nchini Uganda alipokwenda kutia saini ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta mwezi uliopita na mapema wiki hii alivaa akiwa katika ziara yake nchini Kenya.

    Leo hii, katika mkutano wake na Wazee wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Rais Samia pamoja na viongozi wote wakuu alioambatana nao, kuanzia Makamu wa Rais Philip Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Waziri wa Afya Dorothy Gwajima na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wote wamevalia barakoa.

    Hii ni mara ya kwanza toka janga la corona liripotiwe nchini humo kwa uongozi wote wa juu kwa wakati mmoja kuonekana hadharani wakiwa wamevalia barakoa.

    Mtangulizi wa Rais Samia, hayati Rais John Magufuli hakuonekana hadharani akivalia barakoa na pia aliwataka wananchi wachukue tahadhari juu ya barakoa zinazotengenezwa nje ya nchi hiyo.

    Utawala wa Magufuli ulikosolewa vikali kwa kutochukua hatua stahiki kupambana na corona. Bi Samia ameonesha kuwa serikali yake itachukua hatua za tofauti na kwa kuanzia ameunda kamati maalumu ya kumshauri juu ya hatua stahiki za kuchukua katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

  6. Uuzaji wa nyama ya punda ruksa Kenya

    Punda

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Mahakama moja yaondosha marufuku ya kuchinja na kuuza nyama ya punda Kenya

    Mahakama moja nchini Kenya imebatilisha marufuku ya kuchinja na kuuza nyama ya punda nchini humo.

    Wizara ya kilimo iliweka marufuku hiyo mnamo mwezi Februari mwaka jana kwasababu ya wasiwasi wa kupungua kwa idadi ya punda baada ya wakulima na makundi la kijamii kufanya maandamano.

    Taifa hilo la Afrika Mashariki lilihalalisha biashara ya nyama ya punda mwaka 2012 kukidhi hitaji la nyama hiyo linalozidi kuongezeka China.

    Lakini wizara ya kilimo ikasema ilikuwa makosa kuchukua hatua hiyo kwasababu ilisababisha kupungua kwa idadi ya punda.

    Hata hivyo, baadhi ya wamiliki wa vichinjio vya punda walikwenda mahakamani wakisema kwamba hatua imesababisha upungufu wa ajira na mapato na ndio baadhi ya sababu zilizochangia kuondolewa kwa marufuku hiyo.

    Alhamisi, Jaji Richard Mwongo alikubaliana nao na kusema serikali ilishindwa kutetea kesi hiyo vilivyo.

    Kenya ina takriban punda milioni 1.2 ikilinganishwa na milioni 1.8 waliokuwepo miaka kumi ilyopita, kulingana na takwimu za serikali.

    Nchini Kenya, tangu mwaka 2012 thamani ya punda mkubwa imeongezeka zaidi ya mara nne na pia kumeongeza soko haramu la mnyama huyo huku mitandao ya kuchuna ngozi yake ikitafuta wahalifu kuiba punda.

    Watu wengi maeneo ya vijijini hutumia punda katika shughuli za kuchota maji na kubeba wa kuni.

  7. Malkia wa Zulu azikwa Afrika Kusini

    Malkia alizikwa kulingana na utamaduni ya ufalme wa Swati

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Malkia alizikwa kulingana na utamaduni ya ufalme wa Swati

    Malkia Mantfombi Dlamini Zulu wa jamii wa Zulu nchini Afrika Kusini amezikwa.

    Mazishi yake yalifanyika katika kasri lake la Kwakhangelamankengane mjini Nongoma nyakati za alfajiri. Ukumbusho wake ulifanyika usiku kucha.

    Alizikwa kulingana na utamaduni wa ufalme wa Swati. Mwili wa malkia ulifungwa kwa ngozi ya ng’ombe ambayo ulipewa ujumbe uliotumwa na kaka yake, Mfalme Mswati III wa Eswatini.

    Mazishi yalihudhuriwa na jamaa zake kutoka pande zote mbili za ufalme.

    Shughuli ya kumuaga rasmi itakayofadhiliwa na serikali itafanyikabaadaye leo.

    Baada ya Malkia Mantfombi kuzikwa, kilichosalia ni kumtafuta atakayeongoza ufalme wa Zulu.

    • Ufalme wa Zulu: Jinsi waasi wa ufalme na wanawafalme wanavyopigania uongozi
  8. Mdogo wake Kabila kupigiwa kura ya kuondolewa ugavana DRC

    drc

    Chanzo cha picha, AFP

    Maofisa wa jimbo la Tanganyika nchini Jamuhuri ya Demokrasia ya Congo inataka kumtoa madarakani gavana Zoe Kabila - ambaye ni mdogo wake aliyekuwa Rais wa zamani wa DRC Joseph Kabila.

    Hatua hii ya kumpigia kura ya kumuondoa madarakani iliungwa mkono maofisa ambao ni washirika wa Rais Félix Tshisekedi na kuongeza mpasuko kati ya kiongozi huyo na Kabila.

    Maofisa wa kambi ya Kabila waligomea suala hilo kwa mujibu wa gazeti la East African.

    Zoe Kabila alishutumiwa kwa uongozi mbovu na kushindwa kufanya kazi kwa ufasaha.

    Alikuwa ni gavana pekee miongoni mwa magavana 26 ambao walikuwa hawajasaini sheria iliyowekwa na Rais Tshisekedi kuhakikisha kuwa na serikali ya muendelezo.

    Rais Tshisekedi alisitisha muungano na chama cha Kabila - ambacho kilikuwa na wabunge wengi bungeni na kusababisha mvutano kuongezeka.

  9. Mwandishi wa habari Rwanda afungwa miaka 10 gerezani kwa mashtaka ya ugaidi

    The prosecution had demanded a life sentence for journalist Phocas Ndayizera
    Maelezo ya picha, Mwendesha mashtaka alitaka mwandishi wa habari Phocas Ndayizera kufungwa kifungo cha maisha.

    Mahakama ya Rwanda imemhukumu mwandishi wa habari Phocas Ndayizera na wengine sita kfungo cha miaka 10 gerezani kwa mashtaka ya ugaidi.

    Wamekutwa na hatia kwa kosa la kupanga kulipua eneo la umma katika mji mkuu wa Kigali na kula njama za kufanya ugaidi.

    Jaji alisema mahakama ingeweza kuwapa kifungo cha miaka 20 na 25 “lakini wamepewa miaka 10 kwasababu mpango wao haukufanikiwa na hivyo haukusababisha athari kwa umma”.

    Katika mkutano wa kwenye video uliofanyika Alhamisi mchana, wengine sita mahakama iliamuru waachiwe huru kwa mashtaka yanayowakabili.

    Mwezi Novemba 2018, mwandishi Phocas Ndayizera alipotea kwa siku saba kabla ya kufikishwa polisi wiki moja baadae wakati walipokamatwa kwa makosa ya kufanya mpango wa shambulio la mlipuko.

    Bwana Ndayizera na wenzake wamekanusha mashtaka hayo yote.

  10. Kenya kufanya sensa ya kwanza ya wanyama pori

    sensa

    Chanzo cha picha, AFP

    Kwa mara ya kwanza, mamlaka ya Kenya inazindua sensa ya wanyama pori siku ya Ijumaa.

    Zoezi hilo litazinduliwa rasmi mashariki mwa Kenya katika hifadhi ya taifa ya milima ya Shimba.

    Mamlaka ya wanyama pori (KWS) imesema sensa ya wanyama wa porini kitaifa imelenga kupata jumla ya idadi ya wanyama pori na eneo walipo.

    "Zoezi hili litabainisha idadi ya wanyama pori waliopo na kutambua vitisho vilivyowakabili katika hifadhi," huduma ya wanyama pori imeeleza.

    KWS na watafiti wa wanyama pori na taasisi ya mafunzo - taasisi huru ambayo inafanya utafiti wa hifadhi za wanyama pori na wanaowasimamia.

    Kenya ina hifadhi za wanyama pori katika maeneo mbalimbali ya nchi.

  11. Rais Kagame kuwa wa kwanza kuleta kiwanda chanjo ya mRNA barani Afrika

    kAGAME

    Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema taifa lake litakuwa la kwanza kuleta chanjo ya mRNA barani Afrika wakati bara hilo likipambana na janga la virusi vya corona.

    “Rwanda inafanya kazi na washirika ili kuwa ya kwanza kutengeneza chanjo ya mRNA barani Afrika,” Kagame amesema katika mkutano wa kwenye mtandao wiki hii katika mkutano ulioitishwa na jopo huru la kukabiliana na janga la corona ingawa hakutoa ufafanuzi.

    Waziri wa afya wa Rwanda, Luteni Kanali Dkt.Tharcisse Mpunga ameliambia shirika la utangazaji la Rwanda kuwa mjadala huo ulikuwa ni wa kuleta kiwanda cha chanjo Rwanda.

    “Hii inaweza kuwa hatua kubwa kwa Rwanda na Afrika kupata chanjo …tunategemea kuwa punde mijadala hii itazaa matunda”, Dkt Mpunga salisema Alhamisi usiku.

    “Ikiwa kama Afrika bado inategemea chanjo kutoka mabara mengine , tutakuwa nyuma kwenye foleni mara zote panapokuwa na uhaba”, Bwana Kagame alisema hayo kwenye mjadala ulioongozwa na aliyekuwa rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf na waziri mkuu wa zamani wa New Zealand Helen Clark siku ya Jumanne.

    Mamlaka ya Rwanda haijatoa ufafanuzi ya namna kiwanda hicho kitawekwa Rwanda.

    Makampuni ya dawa ya Marekani na Ujerumani - Pfizer Inc. na BioNTech SE - walishirikiana kutengeneza chanjo ya mRNA vkukabiliana na Covid-19, kama Moderna Inc.

    Afrika ina viwanda vichache vya uzalishaji wa aina yeyote ya chanjo na vile vilivyopo vingi huwa vinaweka vifungashio na kusambaza - ila sio kutengeneza wenyewe.

    Chanjo ya mRNA inatofautiana na usambazaji wake na kuwa mshirika wa utengenezaji na RNA, au kemikali inayofahamika kama ribonucleic, kulinda mwili dhidi ya vimelea vya magonjwa. Pfizer Inc., pamoja na BioNTech SE, ilianzishwa na chanjo ya mRNA kupambana na Covid-19, wakati Moderna Inc.ilithibitishwa kuwa bora zaidi ya zile zilizotengenezwa na makampuni mengine yanayotumia namna nyingine ya utengenezaji.

    “Nilikuwa na fursa ya kufanya mawasiliano na makampuni kadhaa ya chanjo haswa nikilenga mjumbe wa teknolojia ya RNA iliyotumika kwenye Moderna na Pfizer,” Kagame alisema mwezi uliopita.

    “Tumekuwa tukishiriki katika mijadala na baadhi ya viongozi wengine barani kwetu lakini tunataka kujadilina zaidi kuhusu hili na wengine.”

    Mwezi Februari, Rwanda ilianza kutoa chanjo kwa wahudumu ambao wako kwenye hatari ya maambukizi wakati taifa hilo likiwa na idadi ndogo ya chanjo, baadhi wakiwa wamepata chanjo ya Pfizer-BioNTech.

    Zaidi ya watu 350,000 wamepata chanjo ya corona nchini humo, wizara ya afya imesema.

    Zaidi ya dozi milioni 17 za chanjo ya corona zimepelekwa Afrika ambayo ina watu bilioni 1.3 ambapo kiwango kilichotolewa ni chini ya 2% ya dozi milioni 780 zilizotolewa duniani , WHO imesema.

  12. Habari...Karibu katika matangazo ya moja kwa moja ya ukurasa wa BBC Swahili leo ikiwa ni Ijumaa tarehe 07/05/2021