Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mzozo wa mrithi wa mfalme wa Wazulu waelekea mahakamani
Mke wa kwanza, Malkia Sibongile Dlamini, anapinga kutekelezwa kwa wosia wa mfalme uliomtaja mfalme ajaye - huku kukiwa na madai kwamba wosia wake wa mwisho unaweza kuwa ulighushiwa.
Moja kwa moja
Ambia Hirsi
Waziri wa biashara wa Burundi afutwa kazi kotokana na mauzo ya ndege
Waziri wa biashara, uchukuzi , viwanda na utalii, Immaculée Ndabaneze amefutwa kazi " kwa kuuweka uchumi haarini na kuchafua picha ya nchi ".
Alikamatwa kwa muda, akahojiwa na kuachiliwa Jumapili huku uchunguzi ukiendelea kuhusu madai hayo.
Bi Ndabaneze anakabiliwa na shutuma za ufisadi kuhusu mauzo ya ndege ya shirika la ndege la Burundi, Air Burundi.
Ndege hiyo iliuzwa kati ya mwezi Disemba 2020 na Januari 2021 “kwa mfanayabiashara wa Afrika Kusini kwa bei ya chini”, limeandika Shirika lisilo la kiserikali (NGO) linalopambana na ufisadi nchini Burundi, Olucome-Burundi kwenye ukurasa wake wa Twitter.
Bi Ndabaneze hajajibu lolote kuhusu tuhuma hizo dhidi yake.
Mahakama ya Ufaransa yaombwa kuachana na kesi ya mauaji ya kimbari ya Rwanda
Waendesha mashtaka nchini Ufaransa wameomba majaji kutupilia mbali mashataka dhidi wanajeshi watano wa Ufaransa wanaohusishwa na mauaji ya Watutsi wakati wa mauaji ya kibari ya Rwanda ya mwaka 1994.
Wachunguzi walisema hawakupata ushahidi wowote unaoashiria kuzembea kwa walinda amani wa Ufaransa.
Walikuwa wamelaumiwa kwa kuwatelekeza manusura wa jamii ya Watutsikatika eneo la Bisesero, kuchangia mauaji ya halaiki yaliyofanywa dhidi yao na Wahutu wenye misimamo mikali.
Mwezi Machi, ripoti kuu ya Ufaransa ilihitimisha kuwa Ufaransa ilikuwa na majukumu "mazito" yanayohusiana na mauaji ya kimbari ya Rwanda, lakini iliondoa hali hiyo.
Watu 800,000 wengi wao kutoka kabila la Tutsis waliuawa ndani ya zaidi ya miezi mitatu ya mwaka 1994.
Wanne wakamatwa katika msako wa unyanyasaji watoto unaoongozwa na Ujerumani
Polisi nchini Ujerumani wamewakamata wanaume watatu na wanne anazuiliwa Paraguay kwa madai ya kuendesha mtandao mkubwa zaidi wa kutumiana picha zinazohusisha watoto wanadhulumiwa kingono.
Oparesheni hiyo ya kimataifa, inayojumuisha vikosi kadhaa vya polisi, kutoka Uholanzi, Uswidi, Australia, Marekani na Canada inalenga mtandao wa uhalifu wa mtandaoni unaofahamika kama Boystown, ambao sasa umefutwa.
Maafisa wanasema mtandao wa Boystown ulikuwa umewasajili zaidi wa watumiaji 400,000.
Wanasema baadhi ya picha zinaonesha unyanyasaji mbaya wa kingono dhidi ya watoto wadogo.
Mtandao huo umekuwa ukiendesha shughuli zake katika wavu wa giza, eneo la mtandao ambalo haziwezi kufikiwa na injini kuu za utaftaji.
Shirika la upelelezi la Muungano wa Ulaya Europol limesama linatathmini mafanikio yaliyofikiwa katika oparesheni hiyo , na kuongeza kwamba "linatarajia kuwakama watu zaidi na kuwaokoa watoto zaidi kote duniani" kwa msingi huo.
Mitandao mingine kadhaa ya wanyanyasaji watoto kingono kupitia wavu wa gizapia imevunjwa, Europol imesema.
Rais Samia akutana na rais mstaafu wa Nigeria Olusegun Obasanjo
Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo amekutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Gerson Msigwa imesema viongozi hao wawili pia walijadili masuala ya usalama, ushirikiano wa kibiashara barani Afrika.
Bw. Obasanjo pia ametumia mkutano huo kumpongeza Rais Samia kwa kupokea usukani wa uongozi baada ya kifo cha Hayati Rais John Magufuli.
Pia ametoa salamu zake za rambi rambi kwa Tanzania kwa kuondokewa na rais Magufuli na na rais mstaafu Benjamin Mkapa.
DR Congo yatangaza kutokomezwa kwa mlipuko wa Ebola
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza kutokomezwa kwa mlipuko wa hivi karibuni wa ugonjwa wa Ebola uliosababisha vifo vya watu sita.
Tangazo hilo linakuja miezi mitatu baada ya ugonjwa huo kuripotiwa kuibuka tena huko Kivu Kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Shirika la Afya Dunia (WHO) limeangazia tangazo hilo katika Twitter yake Jumatatu.
Muda mfupi uliopita DRC ilipongezwa na Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Dr. Matshidiso Moeti
Katika taarifa shirika la watoto la Umoja wa Mataifa Unicef limesema hatua ya haraka iliyochukuliwa na serikali na washirika wake ilisaidia kudhibiti mlipuko.
Lilisema kuwa huo ulikuwa mlipuko wa tatu wa Ebola kukumba nchi hiyo chini ya mwaka mmoja.
Kabla ya kuanza kwa mlipuko huo Februarui 7, nchi hiyo ilikuwa imetangaza kumalizika kwa ule wa 11 uliosababisha vifo vya wati 55 kati ya visa 130 vya maambukizi vilivyothibitishwa kwa karibu miezi sita.
Tazama daraja la watembea kwa miguu lililo refu zaidi duniani
Spika Ndugai aendelea ‘kuwakingia kifua’ wabunge waliotimuluwa Chadema
Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amewatoa hofu wabunge 19 wa Chadema waliofutiwa uanachama wa chama hicho na kuwataka wafanye kazi bila hofu.
Bw. Ndugai amevionya baadhi vyama dhidi ya kuwanyanyasa wanawake na kuvitaka kufuata sheria kabla ya kumtaka achukue hatua ya kuwafukuza wabunge hao.
''Katibu Mkuu wa chama chochote huko ulikotoka anaandika tu barua kipeperushi kama hiki alafu mimi nakufukuza.Haiendi hivyo.'' alisema.
Tamko la Spika Ndugai limekuja wakati kukiwa na shinikizo kutoka kwa viongozi wa Chadema wakimtaka Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati suala hilo kwani kuwepo kwa wabunge hao bungeni ni kinyume cha Katiba.
Wabunge hao akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema, Halima Mdee walifukuzwa uanachama wa Chadema tarehe 27 mwezi Novemba, 2020 baada kwenda bungeni kuapishwa kuchukua nafasi za viti maalum bila idhini ya chama hicho.
Maelezo zaidi:
- Halima Mdee: Hatuondoki Chadema, tunakata rufaa
- Athari za kuwafukuza wanachama 19 wa Chadema
Apetamin: Instagram yakosolewa juu ya dawa ya kutengeza 'umbo namba nane'
Mamlaka ya Huduma Afya ya Kitaifa nchini Uingereza NHS, imetoa wito kwa mtandao wa kijamii wa Instagram kuwachukulia hatua watumiaji wake ambao akaunti zao zinatumika kuuza dawa "hatari " ambayo haijaidhinishwa kuwalenga wanawake na wasichana.
Uuzaji wa dawa aina ya Apetamin ni kinyume na sheria nchini Uingereza lakini, BBC imebaini kuwa zinapatikana madukani na mitandaoni.
Katika barua ya wazi wazi, viongozi wa NHS wameelezea wasi wasi wao kuhusu utangazaji wa bidhaa hizo na athari zake kwa afya ya mwili na akili.
Instagram inasema uuzaji wa dawa ambazo hazitumiki kwa ajili ya tiba "unaenda kinyume na sera zetu ".
Dawa ya Apetamin haijaidhinishwa kutumiwa Uingereza kumaanisha wadhibiti wa dawa hawajafanya uchunguzi kujiridhisha ikiwa inafikia viwango vya usalama na kwamba haistahili kuuzwa, kusambazwa au kutangazwa .
Madaktari wanasema utumiaji mbaya wa vichochea mlo vinaweza kusababisha uchovu mbaya, homa ya manjano, na hata ini kukosa kufanya kazi.
Pia unaweza kutazama:
Ethiopia yaorodhesha rasmi TPLF kama 'Kundi la kigaidi'
Baraza la mawaziri nchini Ethiopia limetaja chama tawala cha zamani cha Tigray Peoples Liberation Front (TPLF) party na kundi la Oromo Shene kama makundi ya kigaidi, Shirika la utangazaji wa Fana limeripoti.
Serikali imelaumu mashirika hayo kwa kuhusika na mashambulio yaliofanywa katika maeneo tofauti yakiwalenga raia kwa lengo la kulemaza mageuzi yaliyoanzishwa na nchini humo katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Mwezi Novemba mwaka jana, Ethiopia ilianzisha oparesheni ya kijeshi kaskazini mwa Jimbo la Tigray kuondoa madarakani TPLF kufuatia shambulio dhidi ya kambi za kijeshi katika eneo hilo.
Utawala wa Waziri Mkuu Abiy Ahmed umekumbwa na ghasia za kijamii zinazohusishwa na kundi la Shene.
Ethiopia inajiandaa kufanya uchaguzi mwezi Juni mwaka huu.
Soma zaidi:
- Mzozo wa Tigray: Waziri Mkuu wa Ethiopia Ahmed Abiy akiri kuwa vikosi vya Eritrea viko ndani ya Tigray
- Mzozo wa Tigray: Jukumu la Eritrea katika mzozo wa Ethiopia
Mzozo wa mrithi wa mfalme wa Wazulu waelekea mahakamani
Mzozo kuhusu ni nani atakayemrithi marehemu Mfalme wa Wazulu, Goodwill Zwelithini, sasa unaelekea mahakamani, vyombo vya habari vinaripoti.
Mke wa kwanza, Malkia Sibongile Dlamini, anapinga kutekelezwa kwa wosia wa mfalme uliomtaja mfalme ajaye - huku kukiwa na madai kwamba wosia wake wa mwisho huenda ulighushiwa.
Hatua hiyo ya kisheria inakuja siku kdhaa baada ya kifo cha Malkia Shiyiwe Mantfombi Dlamini Zulu.
Alikuwa ameteuliwa kushikilia wadhifa huo kwa muda tarehe 24 mwezi Machi baada ya Mfalme Zwethilini kufariki kutokana na matatizo yanayohusiana na ugonjwa wa kisukari akiwa na umri wa miaka 72.
Lakini katika kesi ya kupinga uteuzi wa Malkia Mantfombi kama mrithi wa Mfalme, Malkia Sibongile alitaka mahakama kutambua ndoa yake na na marehemu mfalme huyo kuwa halali. Pia anataka kupewa asilimia 50 ya usimamizi wa nyumba zake.
Siku ya Jumapili, Waziri Mkuu wa Zulu Mwanamfalme Mangosuthu Buthelezi alielezea hatua hiyo ya kisheria kama "aibu", alipokuwa akizungumza na Shirikala utangazaji la Afrika Kusini SABC.
"Baadhi ya wanafamilia wa kifalme wameshangazwa sana na kile alichofanya kwasababu bado anaomboleza. Wao, kama wajane wa Mfalme, na hatua ya kukimbilia mahakamani kwa njia waliofanya ni fedheha kwa familia ya ufalme." aliambia SABC.
Maelezo zaidi:
- Kifo cha mflame wa Wazulu Goodwill Zwelithin: Malkia achaguliwa kushikilia wadhifa kwa muda
- Mungu huzungumza kupitia kwangu adai mfalme wa Zulu
Hujambo na karibu katika matangazo haya mubashara kutoka BBC Swahili leo Jumatatu 03.05.2021