Rais Samia awa rasmi mwenyekiti mpya wa CCM

Rais Samia Suluhu Hassan amepata ushindi wa asilimia mia moja ya wapiga kura wote -avuka kigingi kingine cha Uongozi katika chama ambacho sehemu kubwa ya uongozi wake wa juu ni wanaume.

Moja kwa moja

  1. Na mpaka hapa ndio tunafikia mwisho wa matangazo haya ya moja kwa moja kwa leo, tukutane tena Jumatatu panapo majaaliwa.

  2. Ujerumani kurejesha sanamu za Nigeria zilizoporwa

    Sanamu

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Serikali ya Ujerumani imesema kuwa mwaka ujao itarajesha nchini Nigeria maelfu ya sanamu za kuchongwa zilizoibiwa wakati wa enzi ya ukoloni katika eneo la Benin katika jimbo la Edo – wakati wa operesheni ya wanajeshi wa Uingereza.

    Haya yanajiri baada ya kufikiwa kwa makubaliano baina ya viongozi wa kitamaduni wa Ujerumani na viongozi wa siasa ya kurejesha Nigeria sanamu hizo ambazo zimekuwa zikihifadhiwa katika makavazi ya Ujerumani.

    Waziri wa utamaduni wa Ujerumani, Monika Gruetters aliyasema hayo Alhamisi.

    Katika miaka ya hivi karibuni, Ujerumani imekuwa ikiangalia uwezekano wa kurejeshwa katika asili yake sanamu za kuchongwa zilizosambazwa katika baadhi ya makavazi ya nchi hiyo.

    Maelfu ya sanamu hizo yaliporwa wakati wa maangamizi ya kile ambacho kwa sasa kinaitwa Jiji la Benin City nchini Nigeria na kumekuwa ni miito ya mara kwa mara ya kutaka sanamu zilizoibiwa zirejeshwe Nigeria.

  3. CCM yapata Katibu mkuu mpya na Katibu wa itikadi na uenezi

    Daniel Chongolo anakuwa  katibu mkuu wa moya wa CCM kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Dk Bashiru Ally

    Chanzo cha picha, ISSA MICHUZI

    Maelezo ya picha, Daniel Chongolo anakuwa katibu mkuu wa moya wa CCM kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Dk Bashiru Ally

    Halmashauri Kuu ya CCM imemteua mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo kuwa katibu mkuu wa chama hicho tawala kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Dk Bashiru Ally.

    Shaka Hamidu Shaka, ndiye Katibu itikadi na uenezi mpya na kuchukua nafasi ya  Humphrey Polepole,

    Chanzo cha picha, ISSA MICHUZI

    Maelezo ya picha, Shaka Hamidu Shaka, ndiye Katibu itikadi na uenezi mpya na kuchukua nafasi ya Humphrey Polepole,

    Kikao hicho pia kimemteua Christina Mndeme kuwa naibu katibu mkuu Bara huku Abdallah Juma Sadala akiendelea kuhudumu nafasi hiyo upande wa Zanzibar.

    Katibu wa itikadi na uenezi iliyokuwa ikishikiliwa na Humphrey Polepole, sasa itashikiliwa Shaka Hamidu Shaka na katibu wa uchumi na fedha ni Frank Hawasi.

  4. Miili ya mwandishi na mwanamazingira waliouawa Burkina Faso yarejeshwa Madrid

    Inaaminiwa kuwa wapiganaji wa makundi ya jihadi walikua nyuma ya mashambulio hayo ya kuvizia.
    Maelezo ya picha, Inaaminiwa kuwa wapiganaji wa makundi ya jihadi walikua nyuma ya mashambulio

    Raia watatu wa kigeni walitoweka Jumatatu baada ya shambulio dhidi ya msafara wao karibu na eneo la hifadhi ya misitu asilia nchini Burkina Faso wamerejeshwa kwao.

    Mwandishi wa BBC nchni humo anasema wanajeshi 24 walibeba majeneza ya David Beriain, Roberto Fraile ana Rory Young across Torrejón hadi kwenye kituo cha kijeshi, huku familia zao, maafisa wa Uhispania na balozi wa Ireland wakitazama.

    Msemaji wa familia hizo alitoa shukran kwa kuwaleta Roberto na David “nyumbani .”

    Awali, Serikali ya Uhispania ilitangaza kuwa itawapatia tuzo ya medali wanaume hao wote wawili kwa utumishi bora kama madaktari- ambayo ni heshima ya juu zaidiya kiraia nchini Uhispania.

    Ramani inayoonesha maeleo yenye makundi ya Jihad katika kanda ya Sahel
    Maelezo ya picha, Ramani inayoonesha maeleo yenye makundi ya Jihad katika kanda ya Sahel

    Wanaume hao walikuwa wakichukua filamu ya kipindi kuhusu doria ya uwindaji haramu katika kanda ya Sahel , ambako kuna ukosefu wa usalama.

    Inaaminiwa kuwa wapiganaji wa makundi ya jihadi walikua nyuma ya mashambulio hayo ya kuvizia.

    Serikali za Uhispania na Ireland zimesema zitashirikiana na mamlaka za Burkina Faso kubaini ni nani aliyehusika na shambulio hilo.

  5. Rais Samia awa rasmi mwenyekiti mpya wa CCM

      • Author, Aboubakar Famau
      • Nafasi, BBC News, Dodoma
    CCM

    Chanzo cha picha, CCM

    Rais Samia Suluhu Hassan amepata ushindi wa asilimia mia moja ya wapiga kura wote -avuka kigingi kingine cha Uongozi katika chama ambacho sehemu kubwa ya uongozi wake wa juu ni wanaume.

    Wajumbe 1862 ambao ni sawa na asilimia 99 ya wajumbe wa Chama cha Mapinduzi .

    CCM wamekutana hii leo jijini Dodoma katika Mkutano Mkuu wa chama hicho na kumchagua rais Samia Suluhu Hassan kuwa mwenyekiti wa Chama hicho.

    CCM

    Chanzo cha picha, CCM

    Rais Samia anajaza nafasi hiyo baada ya kuachwa wazi na hayati John Pombe Magufuli ambae alifariki tarehe 17 mwezi Machi mwaka huu.

    Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa wajumbe wa chama hicho tawala kukutana baada ya kifo Dkt. Magufuli lakini pia ni kikao cha kwanza kwa Samia kuhudhuria kama rais wa Tanzania.

    MM

    Chanzo cha picha, CCM

    Hii ni hatua ya kihistoria katika chama hicho kuongozwa na mwanamke katika nafasi yake ya juu kabisa.

    Wengi wanasubiri kwa hamu kuona ni mabadiliko gani atakayofanya mwenyekiti mpya baada ya kukabidhiwa mikoba ya kukuongoza Chama hicho kikongwe Afrika Mashariki kwa miaka mitano.

    Mabadiliko yanayotarajiwa hivi sasa ni zaidi katika safu ya wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi.

    Mbali na kupigwa kura ya mwenyekiti, pia kumekuwa na upigaji kura ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kutoka nafasi mbili ambazo zilikuwa wazi.

  6. Malkia wa Zulu afariki dunia mwezi mmoja baada ya kuchukua majukumu ya kifalme

    zulu

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Familia ya kifalme ya Zulu nchini Afrika Kusini imetangaza kifo cha Malkia wake aliyekuwa anaongoza eneo hilo Shiyiwe Mantfombi Dlamini Zulu, mwezi mmoja tu baada ya kutawazwa kuchukua majukumu ya kifalme.

    Malkia Mantfombi, 65, alikuwa kiongozi wa mpito wa kabila la Zulu ambalo ndilo kubwa zaidi nchini Afrika Kusini baada ya kifo cha mume wake, Mfalme Goodwill Zwelithini.

    Waziri mkuu wa malkia huyo amesema kifo chake kimeshutua familia ambayo ipo kwenye masikitiko makubwa kwa kumpoteza.

    Mrithi kama mtawala wa eneo la Wazulu lenye watu milioni 11 bado hajatajwa.

    "Ni huzuni na masikitiko makubwa kwamba Familia ya Kifalme inatangaza kifo ambacho hakikutarajiwa cha Malkia Shiyiwe Mantfombi Dlamini Zulu, wa Wazulu," Mwanamfalme Mangosuthu Buthelezi, waziri wake mkuu amesema kwenye taarifa.

    Aliongeza kuwa anataka kuhakikishia watu kwamba hakutakuwa na "ombwe la uongozi kwa eneo la Wazulu".

    Malkia Mantfombi alilazwa hospitalini wiki moja iliyopita baada ya kuuguwa ugonjwa ambao haukujulikana, kulingana na vyombo vya habari vya Afrika Kusini.

    Alikuwa ameteuliwa kuchukua nafasi hiyo Machi 24, baada ya mume wake, 72, Mfalme Zwethilini, kufariki dunia akiwa hospitalini kwa ugonjwa wa kisukari na matatizo mengine.

    Mfalme huyo alikuwa ametawala eneo la Wazulu kwa karibu miaka 50 – na kumfanya kuwa mfalme aliyetawala kwa kipindi kirefu zaidi Afrika.

    Malkia Mantfombi alikuwa nani?

    zulu

    Chanzo cha picha, AFP

    Malkia MaDlamini Zulu alikuwa ameshikilia nafasi ya juu zaidi ya uongozi miongoni mwa wake wa mfalme kwasababu anatoka familia ya kifalme.

    Alikuwa dada ya Mfalme wa Eswatini, Mswati III – nchi pekee Afrika ambayo yote inaendeshwa kwa mfumo wa kifalme.

    Malkia MaDlamini Zulu na marehemu muwe wake walijaaliwa watoto wanane – ikiwa ni pamoja na vijana 5 wa kiume.

    Kijana wao mkubwa, 47, Mwanamfalme Misuzulu, ndiyo mwenye uwezekano mkubwa wa kuchukua uongozi kama mfalme, taarifa zinasema

  7. Daktari mkatoliki aliyepinga chanjo afariki kwa corona Kenya

    kenya

    Chanzo cha picha, Reuters

    Daktari maarufu nchini Kenya ambaye alikuwa mwanaharakati anayepinga chanjo ya virusi vya corona amefariki dunia kutokana na ugonjwa huo.

    Dkt. Stephen Karanja alisema hakuna haja ya kuwapa Wakenya chanjo dhidi ya ugojwa wa Covid-19.

    Badala yake, alihoji tiba ya kujifukiza na dawa zinazotumiwa ikiwemo hydroxychloroquine na zinc.

    Pia alisambaza dhana ya uwepo wa njama inayomuhusisha, Bill Gates na udhibiti wa idadi ya watu.

    Dkt. Karanja alifariki dunia Alhamisi katika hospitali moja ya kibinafsi mjini Nairobi.

    Hadi kufikia sasa zaidi ya watu 800,000 wamepata chanjo hiyo na hakujaripotiwa madhara yoyote.

    Kabla ya kifo chake, daktari Karanja alikuwa mwenyekirti wa Chama cha Madaktari Wakatoliki – waliomuelezea “kama shujaa kweli wa tiba.”

  8. CCM kumchagua mwenyekiti mpya bila shamrashamra

      • Author, Aboubakar Famau
      • Nafasi, BBC News, Dodoma
    SAMIA

    Chanzo cha picha, IKULU

    Maelfu ya wajumbe wa Chama cha Mapinduzi CCM wamekutana jijini Dodoma hii leo katika Mkutano Mkuu wa chama hicho.

    Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa wajumbe wa chama hicho tawala kukutana baada ya kifo cha aliyekuwa rais wa Tanzania John Pombe Magufuli ambaye pia ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa Chama.

    CCM

    Chanzo cha picha, IKULU

    Mbali na mambo mengine yatakayofanyika, lakini ajenda kuu ya mkutano huo ni pamoja na kuchaguliwa cha mwenyekiti mpya wa Chama ambapo tayari maandalizi yanaonekana kukamilika kwa kumkabidhi rais Samia Suluhu Hassan nafasi hiyo ya juu kabisa katika chama.

    Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa nafasi hiyo kushikiliwa na mwanamke.

    Tofauti na miaka mengine, mkutano mkuu unakuwa na shamra shamra na vifijo, mara hii inaonekana itakuwa tofauti huku Chama hicho kikisema bado kinaomboleza kifo cha aliyekuwa rais wa Tanzania.

  9. Kenya kufunga kambi za Kakuma, Dadaab kufikia Juni 2022

    kambi

    Kenya imethibitisha kuwasiliana rasmi na Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR na kutaarifu kuwa itafunga kambi za wakimbizi ya Dadaab na Kakuma ifikapo Juni 30, 2022.

    Waziri wa mambo ya nje wa nchini Kenya bwana Fred Matiangí ametangaza hayo baada ya kufanya mkutano na Filippo Grandi, mjumbe wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia wakimbizi.

    Dkt. Matiangí amesema kuwa timu ya maafisa wa serikali ya Kenya na Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa watafuatilia mchakato huo uliopangiwa kuanza Mei, 5, 2022.

    Mchakato wa sasa hivi unajumuisha kurejea katika nchi zao kwa hiari au kutoa kibali cha kufanyakazi au cha makazi bila malipo kwa wakimbizi kutoka jamii ya Afrika Mashariki.

    Wakati huo huo, Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limefurahishwa na mpango wa kupitiwa tena kwa mpango wa kufunga kambi hizo za wakimbizi.

    ‘’Sio kambi za kudumu za wakimbizi au kufungwa kwa haraka kwa kambi hizo au kukiuka kanuni ya kimataifa inayokataza nchi inayopokea wakimbizi kuwarejesha nchini mwao ambako wanaweza kuwa katika hatari ni suluhisho ya hili’’, UN imesema.

    Katika taarifa iliyotolewa na shirika hilo, imesema kuwa inaamini serikali ya Kenya na shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa katika kubaini machaguo mengine ya kuwahifadhi au kurejea kwa hiari kwa wanaotaka kwa namna heshima.

    Mnamo mwezi Machi, serikali ya Kenya ilikuwa imeipatia UN makataa ya mwisho ya kutafuta njia kwasababu inataka kufunga kambi hizo mbili ambazo ni makazi kwa wakimbizi 400,000.

    Muda mfupi baadae, Shirika la Amnesty International likajibu kwa kusema kuwa hatua ya kufungwa kwa kambi za Dadaab na Kakuma bila mpangilio unaoheshimu haki za wakimbizi, kutasababisha janga la kibinadamu wakati tayari dunia inakumbana na janga la virusi vya corona.

    Kenya imekuwa ikitoa makazi kwa wakambizi kwa zaidi ya miaka 30 na sasa hivi serikali inasema uwezo wake kuendelea kuwatunza hata kwa kuzingatia viwango vya chini kabisa vya kibinadamu vinavyokubalika imekuwa changamoto kwa nchi hiyo kuvifikia.

    Katibu Mkuu nchini Kenya Karanja Kibicho, aliongeza kuwa uamuzi wake wa kufunga kambi za Dadaab na Kakuma kufikia Juni 30, 2022 ‘ni kwa maslahi ya raia wa nchi yake’.

  10. Habari...Karibu katika matangazo ya moja kwa moja katika ukurasa wa BBC Swahili leo ikiwa Ijumaa tarehe 30/04/2021