Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Kenya yasitisha safari za ndege za abiria kwenda India

Kenya imesitisha kwa muda safari za ndege za abiria wanaotoka India. Waziri wa afya Mutahi Kagwe amesema hatua hiyo imechukuliwa kufuatia ongezeko la maambukizi ya Corona-kusini mwa Asia mwa taifa hilo.

Moja kwa moja

Esther Namuhisa

  1. Mpaka hapa tumefika mwisho wa matangazo ya moja kwa moja kutoka kurasa ya BBC Swahili, tukutane tena hapo Kesho.Shukrani

  2. Kenya yasitisha safari za ndege za abiria kwenda India

    Kenya imesitisha kwa muda safari za ndege za abiria wanaotoka India. Waziri wa afya Mutahi Kagwe amesema hatua hiyo imechukuliwa kufuatia ongezeko la maambukizi ya Corona-kusini mwa Asia mwa taifa hilo.

    Katazo hilo litaanza Jumamosi na kudumu kwa muda wa wiki mbili.

    Lakini ndege za mizigo zitaendelea kufanya kazi .

    Mtu yeyote anayewasili kutoka India kabla ya hapo atapimwa virusi vya corona na wakikutwa na corona watalazimika kujitenga na kukaa karantini kwa gharama zao wenyewe.

    Kwa sasa India inakabiliwa na janga kubwa la virusi vya corona.

    Hospitali zimelemewa kwa kuwa na wagonjwa wengi na ripoti za watu kufariki mitaani zikiongezeka.

    Zaidi ya wagonjwa 350,000 wa virusi vya corona wameripotiwa ndani ya saa 24 zilizopita – na hii kuwa rekodi mpya ya dunia.

    Mataifa ya Afrika yanategemea kupata chanjo kutoka India kwa kutumiwa mpango wa Covax . Ingawa ongezeko la maambukizi limesababishwa kupiga marufuku usafirishaji wa chanjo hizo na kuangazia watu wake kwanza.

    Malawi imepiga marufuku pia wasafiri wanaotoka India, pamoja na Bangladesh, Brazil na Pakistan kutokana kusambaa kwa virusi vya corona katika hayo mataifa.

  3. Watu watatu wakamatwa Tanzania wakidaiwa kuuza mishikaki ya nyama ya mbwa

    Gazeti la Mwananchi nchini Tanzania limeripoti kuhusu kukamatwa kwa vijana watatu wanaodaiwa kuuza mishikaki ya mbwa katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani eneo la Msamvu, Morogoro.

    Waliokamatwa kutokana na tuhuma hizo walikutwa wakichuna ngozi ya mbwa na kudai kuwa ni wauzaji mishikaki ni Hamza Rajabu (20), Omary Mohamed wote wakazi wa Msamvu na Mussa Juma (30) mkazi wa Mtawala.

    Vijana hao wamekamatwa wakiwa wanachuna ngozi ya mbwa tarehe 26 Aprili, 2021 katika daraja kuu la barabara iendayo Iringa eneo la relini.

    Kwa mujibu wa gazeti hilo wakazi wa eneo hilo wamesikitishwa na kulaani kitendo hicho na kutaka mamlaka kuchukua hatua kali dhidi yao.

    “Hawa watu wanafahamika kwa uuzaji wa mishikaki haswa majira ya usiku, ndio wamekuwa wakiuza mara nyingi, unawakuta kituo cha mafuta na stendi ya Dodoma. Watu tunakula na wanatuuzia mishikaki bila hata kujua kama ni ya mbwa ama la,” alisema Alexanda.

    “Tumesikia mmoja wa hao vijana ni wakala mkubwa wa wauza nyama za mishikaki hasa ya ile ya mia mia, kinachotakiwa ni kuepuka nyama za kununua mitaani, sio kila nyama unayoletewa unanunua, unatakiwa kuchukua nyama sehemu sahihi ukijua hii ni nyama ya mnyama fulani,” alisema dereva wa bodaboda eneo la Msamvu , Abdallah Pawa.

    Mfanyakazi wa stendi ya Msamvu, Samson Jonas alisema: “Idadi ya watu wanaoingia na kutoka hapa Msamvu ni wengi, huyu jamaa ni muuzaji na atafanya wale wafanyabiashara wa mishikaki kukosa wateja, kwani si wote wanaouza nyama ya mbwa, wapo wanaouza mishikaki ya ng’ombe, mbuzi au kuku.

  4. Tahadhari yatolewa dhidi ya dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi Kenya

    Zaidi ya pakti 24,000 za dawa za kupunguza makali ya virusi vya ukimwi zilizosambazwa katika majimbo 31 ​​nchini Kenya zina athari kubwa kwa wale wanaozitumia.

    Wanaharakati wa maswali ya HIV wanasema matumizi ya dawa hizo zenye thamani ya bilioni shilingi 1.2 yalisitishwa nchini humo mwaka 2019.

    "Kwa nini serikali inacheza na maisha ya watu? Tumewaambia mara nyingi sana kwamba dawa hizi hazifanyi kazi kwa sababu madhara ambayo yamehusishwa nayo. " Nelson Otuoma, mratibu wa kitaifa wa mtandao wa watu wanaoishi na VVU aliiambia BBC kwa simu.

    Dawa iliyosimamishwa ni ile ya Zidovudine / Lamivudine / Nevirapine. Dawa hizi ni miongoni mwa dawa zilizotolewa kama msaada kwa nchi kutoka kwa mfumo wa ule Global Fund na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Usaidizi wa Virusi vya HIV (PEPFAR).

    “Tumeshangazwa sana kwamba dawa hizi zilikuwa bado kwenye ghala kwa miezi. Walituambia kuwa zilikuwa zimeshaharibiwa.” Otuoma aliongeza.

    Kwa kawaida, dawa ya Nevirapine, utolewa kama dawa moja au kama mchanganyiko wa kipimo cha dawa tatu.

    Madhara ya dawa hii kwa kawaida ni maumivu ya tumbo, upele, uchovu, maumivu ya kichwa, kutapika na maumivu ya misuli, ambayo huenda baada ya mwezi mmoja.

    Nevirapine imehusishwa pia na uharibifu wa ini kwa watu wengine. Nchi nyingi zimesitisha matumizi yake kwa watu wanaishi na HIV.

    Shirika la Afya duniani WHO limesema kwamba matibabu ya msingi wa Nevirapine yalikuwa yameonesha kiwango kikubwa cha kutopunguza makali ya virusi vya ukimwi mwilini,

    Mwaka wa 2015, shirika hilo lilipendekeza nchi kutumia dawa ijulikanayo kama Dolutegravir kama tiba mbadala ya laini ya kwanza kwa watu wazima na vijana.

  5. Kituo cha runinga chafungiwa kwa kuonesha vibonzo vya ngono Kenya

      • Author, Roncliffe Odit
      • Nafasi, BBC Nairobi

    Mamlaka ya Mawasiliano nchini Kenya imeifungua kwa muda wa wiki nne runinga ya Mt. Kenya TV kwa kukikuka sheria na kanuni za maadili. Mamlaka hiyo imeitoza runinga hiyo faini ya Dola 5,000 za Marekani kwa kupeperusha kipindi cha vibonzo kilichokuwa na maudhui yasiyo na staha.

    Akitangaza adhabu hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Kenya Bi. Mercy Wanjau amesema walipokea malalamiko kwamba kituo hicho cha runinga kilipeperusha picha zisizofaa mnamo Aprili 19, 2021, saa nane mchana, kinyume na kanuni za utangazaji.

    Mt. Kenya TV inayopeperusha matangazo yake kwa lugha ya Kikuyu, inadaiwa kupeperusha vibonzo vya ngono katika kipindi chake ‘Mucii wa Ciina’ wakati ambapo watoto wengi wako nyumbani.

    Hii si mara ya kwanza kwa vyombo vya habari vya Kenya kufungiwa.

  6. UN yazichukua chanjo milioni 1.3 DRC kuepuka zisipite muda wake

    Shirika la Kimataifa linaloshughulikia masuala ya watoto-Unicef zimechukua zaidi ya dozi milioni mbili za chanjo ambazo zililengwa kwa ajili ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo ili zisipite muda wake.

    Chanjo hizi zinazosambazwa na mpango wa dunia wa Covax unaisha Juni 24, kwa mujibu wa Unicef.

    Dozi zipatazo milioni 1.3 kati ya dozi milioni 1.7 zitaenda kwenye mataifa mengine yakiwemo Senegal, Comoros, Ghana na Angola.

    DRC imechelewa kufanya kampeni za utoaji chanjo za AstraZeneca, ambazo walizipokea mwezi Machi, wakiwa na wasiwasi wa damu kuganda baada ya watu kupata chanjo hiyo.

    Wakati utoaji wa chanjo hiyo ulikuwa umepangwa kuanza Machi 15, na kuhaiirishwa mpaka Aprili 19.

  7. Uganda yasitisha matumizi ya vitamin C kutibu COVID-19

      • Author, Isack Mumena
      • Nafasi, BBC Swahili Kampala

    Wizara ya afya nchini Uganda imesitisha matumizi ya vitamin C katika kutibu virusi vya Covid-19 kutokana na matumizi mabaya ya wagonjwa.

    Vitamni C ndiyo moja ya dawa zilizokuwa zinatumiwa kWa wagonjwa wa covid-19 nchini Uganda kwa sababu zinasaidia kuendeleza chembe hai nyeupe(White blood cell) kupambana kuondoa virusi.

    Lakini baadhi ya wafanyakazi wa wizara ya afya wanaoshughulika na masuala ya utafiti, wanadai vidonge vya vitamn C vinapatikana kwa urahisi na hivyo watu hutumia kiholela kupita kiasi na kuleta madhara.

    Daktari Misaki Wanyegera ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya kupambana na virusi vya corona katika wizara ya afya nchini Uganda, amesema walichukua hatua ya kuondoa Vitamic C baada ya wagonjwa hospitalini kukutwa wakitumia hovyo vitamin hizo na kusababisha figo kushindwa kufanya kazi kutokana na matumizi mabaya.

    Kulingana na ushauri wa madaktari, matumizi ya Vitamin C kwa mgonjwa wa mafua ni tembe 2 kila baada ya saa 8, lakini watu wanatumia mara tatu ya hizo.

    Mwezi Januari kulikuwa na ukosefu wa Vitamin C za Gramu 100 kote nchini humo kutokana na matumizi mabaya.

  8. Afungwa jela kwa kuwapiga picha polisi wakikata roho

    Mwanaume mmoja nchini Australia amehukumiwa kifungo cha miezi 10 gerezani kwa kosa la kuwadhihaki na kuwapiga picha maafisa wa polisi wakati wakiwa wanakata roho katika ajali.

    Mwezi uliopita Richard Pusey alikutwa na hatia katika shitaka ambalo si kawaida kutokea kwa kusababisha hasira kwa umma pamoja na makosa mengine.

    Mwanaume huyo mwenye miaka 42-tayari alikuwa kizuizini kwa siku 300 na anakaribia kumaliza muda wake.

    Jaji aliyemuhukumu alisema, jambo aliliolifanya lilikuwa la kikatili na halikuwa na utu kabisa.

    Bado familia za wahanga wa tukio hilo hawakuridhishwa na muda wa kifungo alichopewa na kuchochea hasira kubwa kwa umma.

    Mwezi uliopita, Jaji Trevor Wraight alisema vyombo vya habari vimemtafsiri Pusey katika hali ambayo anaonekana kuwa mwanaume anayechukiwa zaidi nchini Australia.

  9. Rais wa Somalia aachana na mpango wake wa kuongeza muda madarakani

    Rais wa Somalia, Mohamed Abdullahi Farmajo, ameachana na mpango wake wa kuongeza muda wa kukaa madarakani kwa miaka miwili zaidi hatua ambayo kisiasa imesababisha machafuko mjini Mogadishu na kuleta mapigano ya kijamii kati ya wanajeshi wanaomuunga mkono na wale wanaompinga.

    Katika hotuba yake kwa taifa ,Rais Farmajo ametaka ufanyike uchanguzi mpya wa Rais kwa haraka na kupongeza jitihada za waziri mkuu ambaye muda mfupi uliopita alitengua utawala wa bwana Farmajo baada ya muda wake kumalizika mwezi Februari.

    Bwana Farmajo alisema angefika bungeni siku ya Jumamosi kurejesha mpango wa Septemba 17, mwaka 2020 wa kuongeza muda wa kukaa madarakani ambao ulipitishwa na wabunge Aprili 12.

    Makubaliano ya mwaka 2020 ni mchakato ambao unahusisha wazee wa ukoo katika kuchagua wajumbe ambao pia uchagua wabunge wa shirikisho ambao uchagua rais.

    "Ninatamani kuthibitisha ,kama nilivyofanya miaka iliyopita , kuwa tunahakikisha kuwa uchaguzi unafanyika Somalia kwa wakati uliopangwa na amani," alisema.

    Rais alisema pia kuwa vyombo vya usalama vinahakikisha usalama kwa raia unazingatiwa na kuzuia matukio yeyote ambayo yanaweza kupelekea taifa kuingia katika mapigano.

    Huku baadhi ya raia wakiwa wamekimbia ghasia na kumekuwa na hofu ya wanamgambo wa al-Shabaab.

  10. Habari...Karibu katika matangazo ya moja kwa moja ya kurasa wa BBC Swahili leo ikiwa ni Jumatano 28/04/2021.