Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Chadema yataka kuonana na Rais Samia

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Chadema kimeomba kuonana na rais wa nchi hiyo Samia Suluhu Hassan, kiongozi mkuu wa Chadema ameeleza.

Moja kwa moja

Dinah Gahamanyi, Yusuf Jumah and Ambia Hirsi

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo haya ya moja kwa moja. Hadi kesho kwaheri.

  2. Farmajo aongezewa miaka miwili kuongoza Somalia

    Bunge la Somalia limepiga kura siku ya Jumatatu ili kurefusha muhula wa rais kwa miaka miwili zaidi kuliongoza taifa hilo la upembe wa Afrika ili kuliruhusu kujiandaa kufanya uchagzuzi wa moja kwa moja.

    Spika wa bunge hilo Mohamed Mursal Sheikh amesema wabunge 149 walipiga kura kuidhinisha pendekezo hilo,mmoja akalipinga ilhali watatu hawakupiga kura.

    Rais wa sasa Mohamed Abdullahi Mohamed 'Farmaajo' ambaye amekuwa ofisini tangu 16 Februari 2017 amekuwa akishinikizwa na vyama vya upinzani na serikali za majimbo kuondoka madarakani baada ya kukamilika kwa muda wake wa kuhudumu .

    Utata huo kati yake na viongozi wa majimbo hayo umesababisha wasi wasi ya uwezekano wa taifa hilo kutumbukia katika mgogoro Zaidi wa kiasa na kiusalama baada ya mapigano ya muda mrefu ya wenyewe kwa wneyewe na mashambulizi ya kigaidi kutoka kwa kundi la Al shabaab kuhujumu jitihada za jamii ya kimataifa kuleta uthabiti nchini humo.

    Maelezo zaidi:

    • Je, Mohamed Farmajo ni nani?
  3. Freddie Kanoute 'Nililazimishwa kuwa wakala wa soka’

    Mshambuliaji wa zamani wa Mali Freddie Kanoute anasema hakutaka kamwe kuwa wakala wa soka.

    Kampuni ya Kanoute kwa jina 12 Management sasa inaziwakilisha timu kama Red Bull Salzburg na Patson Daka ya Zambia pamoja na Mali na Moussa Djenepo wa Southampton.

    Mchezaji huyo wa zamani wa Tottenham Hotspur na Sevilla anasema kushughulikiwa vibaya kwa wachezaji wachanga wa Kiafrika na mawakala wasio waaminifu kulimsukuma kuingia kwenye biashara hiyo,

    "Haijawahi kuwa ndoto yangu kuwa na kampuni ya uwakala au kuwa wakala lakini nililazimishwa au kusukumwa ndani yake," mchezaji huyo wa zamani wa Soka wa Afrika mwenye umri wa miaka 43 aliambia kipindi cha redio cha Newsday cha BBC World Service.

    "Nimekuwa nikishiriki katika maendeleo ya vijana barani Afrika. Kwa hivyo nakumbuka tangu 2005, 2006 wakati nilikuwa nikicheza, ni wazi nilikuwa na bidii sana.

    "Nilikuwa nikiwasaidia tu na vifaa na vitu kama msaada wa kimaadili."Lakini niligundua mapema sana, kwamba maajenti wengine walikuwa wanakuja na kuwapigia kelele wachezaji na kuwapeleka Ulaya. Halafu baada ya hapo hawakuwa wakitunza inavyofaa’"Wakati mwingine kuwatelekeza mara tu walipokuwa na shida. Kwa hivyo wachezaji hawa walikuwa wakituita wakisema" tusaidieni "na kadhalika."Kwa hivyo nilipomaliza taaluma yangu, nikasema nitaendelea kusaidia akademi lakini pia nitaanzisha kampuni yangu ya uwakala’."Karibu ninaangalia wachezaji ambao nimewajua tangu umri mdogo."

    Kanoute, ambaye alizaliwa Ufaransa na kuwachezea katika timu ya chipukizi kabla ya kubadilisha utaifa wake na huzuru Mali mara kwa mara na anasema sio tu kwa jili ya mambo ya soka pekee yanayompeleka huko.

  4. Kiongozi wa Sudan Kusini amfuta kazi mkuu wa jeshi

    Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amemfuta kazi mkuu wa jeshi na kumteua kama balozi wa nchi hiyo nchini Ubelgiji.

    Jenerali Johnson Juma Okot, ambaye alikuwa mkuu wa Jeshi la nchi hiyo ,South Sudan People’s Defence Forces (SSPDF) na nafasi yake kuchukuliwa na na Jenerali Santino Deng Wol.

    Rais hakutoa sababu ya hatua hiyo.

    Rais Kiir pia alimfuta kazi Jenerali Ruben Malek Riak kutoka nafasi yake kama naibu waziri wa ulinzi na kumteua Luteni Jenerali Chol Thon Balok katika nafasi hiyo .

    Katika mabadiliko madogo katika huduma za ujasusi, Rais Kiir pia alimbadilisha Jenerali Thomas Duoth Guet kama mkurugenzi mkuu wa mrengo wa ujasusi wa Huduma ya Usalama wa Kitaifa (NSS) na Jenerali Simon Yien Makuac.

    Rais alimpandisha cheo Akol Khor Kuc, mkuu wa mrengo wa usalama wa ndani wa NSS kwa cheo cha Luteni-mkuu wa kwanza, wakati akiendelea kuhudumu katika nafasi yake .

    Naibu waziri wa ulinzi na Jenerali Guet wameteuliwa kama mabalozi kwa Eritrea na Kuwait mtawaliwa.

  5. Mpenzi wake Rapa wa Afrika Kusini AKA afariki aripotiwa kujiua

    Polisi wa Afrika Kusini wanachunguza hali inayozingira kifo cha mwanamke mwenye umri wa miaka 22, aliyetambuliwa kama mchumba wa rapa maarufu AKA, baada ya kuanguka kutoka ghorofa ya 10 ya hoteli ya Cape Town Jumapili.

    Rapa maarufu wa Afrika Kusini AKA - ambaye jina lake halisi ni Kiernan Forbes - anasemekana hafarijiki kufuatia kifo cha mchumba wake Anele Tembe. Wawili hao walikuwa wakitembelea Cape Town wakati tukio hilo lilipofanyika.

    Maelezo kuhusu kifo chake yatakuwa sehemu ya uchunguzi wa polisi.

    Lakini ripoti katika vyombo vya habari vya nchini humo zinaonyesha kwamba Bi Tembe anaaminika kujiua.

    Shirika la umma la utangazaji, SABC, linaripoti kuwa mnamo Disemba polisi waliingilia kati wakati kijana huyo wa miaka 22 alipojaribu kuruka kutoka hoteli moja huko Durban. Anaaminika alikuwa na msongo wa mawazo vyombo vya habari vya huko vinasema.

    Familia za Forbes na Tembe hazijathibitisha madai haya. Katika taarifa ya pamoja walisema walishtushwa na kifo cha binti yao.

    Walimtaja Anele kama msichana wa kipekee na mwenye vipawa ambaye alikuwa na maisha mazuri ya mbeleni - na zimeuliza kupewa faragha kuomboleza msiba huo.

  6. Rais Samia akutana na rais wa zamani wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi

    Rais wa Tanzania Samia Sulu Hassan leo amekutana na kufanya mazungumzo na rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi ambaye amempongeza akisema ameanza vizuri majukumu yake ya kuliongoza taifa hilo.

    Mwinyi alisema lengo lake kufanya ziara hiyo lilikuwa kumjulia hali rais Samia na kumhakikishia msaada wowote atakaohitaji katika majukumu yake kama kingozi wa Tanzania.

    Mwinyi aliwarai Watanzania kumuunga mkono rais Samia na kupeuka tofauti ambazo zitalirudisha nyuma taifa.

  7. Jeshi la DR Congo lachukua udhibiti wa maeneo yaliokuwa chini ya waasi

    Jeshi la kitaifa limechukua udhibiti wa maeneo ambayo yalishambuliwa na kushikiliwa na muungano makundi ya waasi mashariki mwa jimbo la Kivu Kaskazini mwa DR Congo, msemaji wa jeshi anasema.

    Mapigano makali mwishoni mwa wiki kati ya jeshi dhidi ya APCLS - Nyatura pamoja na waasi wa FDLR kwa maeneo yaliyokombolewa katika eneo la Masisi ambalo waasi waliteka baada ya kuwafukuza wanajeshi wiki iliyopita.

    “Hali ni shwari, maeneo yote sasa yanadhibitiwa na jeshi la kitaifa. Tulishinda APCLS - Nyatura na FDLR ”, Msemaji wa jeshi Meja Ndjike Kaiko huko Kivu Kaskazini ameiambia BBC.

    Muheto, Gatovu, Mpati, Kirumbu ni miongoni mwa maeneo ya eneo la Masisi ambayo yalikamatwa na muungano wa vikundi vya waasi, na kusababisha maelfu ya wakazi wa eneo hilo kukimbia makazi yao.

    Alhamisi iliyopita, Shemsa Malengure wa Nyabiondo alikimbia mashambulio ya waasi kwenda mji wa Goma na watoto wake wanne, anasema hana uhakika iwapo ni salama kurudi nyumbani sasa.

    “Hakuna unachoweza kufanya ukiona wanajeshi wanakimbia. Tuliacha mali zetu hatujui ikiwa tutapata kitu ikiwa tutarudi. " Anaiambia BBC.

    Mnamo mwaka wa 2019, Rais Félix Tshisekedi alizindua 'operesheni kubwa za kijeshi' ili 'kutokomeza' vikosi vinavyosababisha maafa mashariki mwa DR Congo, lakini miaka miwili baadaye waasi wamebaki katika eneo hilo.

    Huko Goma na Beni, miji mikuu ya mkoa wa Kivu Kaskazini, kuna maandamano ya kila siku tangu wiki iliyopita ya wakazi wanaowataka walinda amani wa UN katika eneo hilo waondoke, kwa sababu ya kutofanikiwa kutekeleza misheni yao ya kudumisha utulivu ..

    Vikosi vya UN vimekuwa nchini DR Congo kwa zaidi ya miongo miwili sasa.

    • DRC: Majeshi yafanikiwa kuteka ngome ya waasi wa ADF
    • Je, wakati umewadia kwa DRC kuzungumza na waasi?
  8. Virusi vya Corona : Ireland yawataka wasafiri kutoka Kenya kuingia karantini kwanza

    Wasafiri wanaoelekea Ireland kutoka Kenya watalazimika kujitenga kwa wiki mbili baada ya kuwasili katika nchi hiyo ya bara Ulaya.

    Siku ya Jumamosi, Dublin iliongeza Kenya na nchi nyingine kadhaa kwenye toleo lake la orodha ya nchi zilizowekea vikwazo vya usafiri kwa ajili ya Covid-19, ambazo wasafiri wake lazima wangeweka mapema hoteli watakazotumia kama karantini.

    Maafisa walisema agizo hilo ambalo linaanza kutumika mnamo Aprili 15 linalenga kuzuia kuenea kwa virusi vya Corona.

    • Kenya, Ufilipino, Bangladesh zitawekewa marufuku ya kuingia Uingereza
    • Kenya yajibu marufuku ya Uingereza kwa kuwawekea raia wa nchi hiyo masharti

    Nchi nyingine tano ziliongezwa kwenye orodha huku kukiwa na wasiwasi juu ya aina mpya za Covid-19

    Nyingine ni pamoja na Ubelgiji, Ufaransa, Italia, Luxemburg, Marekani , Canada, Bangladesh, Pakistan, Uturuki, Armenia, Bermuda, Bosnia na Herzegovina, Curaçao, Maldives na Ukraine.

    Wasafiri kutoka Kenya watahitajika, kuanzia saa 4 asubuhi Alhamisi hii, kujiandikisha katika hoteli zilizotengwa za karantini kwa gharama zao wanapowasili Ireland.

    "Mipangilio hii inatumika kwa abiria yeyote ambaye amekuwa katika yoyote ya nchi hizi katika siku 14 zilizopita, hata ikiwa anapitia mojawapo ya nchi hizi na hata ikiwa amebaki barabarani," sehemu ya taarifa kutoka kwa tovuti ya ubalozi wa Ireland imesema.

  9. Chad yahesabu kura huku Deby akiwania muhula wa sita

    Kura zinahesabiwa nchini Chad kufuatia uchaguzi wa Jumapili ambapo rais aliyepo madarakani Idriss Deby anatarajiwa kwa kiasi kikubwa kushinda.

    Kuhesabiwa kwa kura kulianza mara baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa katika mji mkuu N’Djamena, limeripoti shirika la habari la Reuters.

    Raia wapatao milioni saba wa Chad walikuwa wanastahili kupiga kura katika uchaguzi huo.

    Bw Deby, ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 30, alikuwa anakabiliwa na wagombea sita dhaifu baada ya wagombea wakuu wa upinzani kususia au kuzuiwa kushiriki kuchaguzi huo.

    Mwandishi wa BBC Killian Ngala alisema sio watu wengi wanaoonekana mitaani kutokana na kwamba joto kali limewafanya watu wakae ndani ya nyumba zao.

    Amesema kuwa wapiga kura walielezea hofu tofauti, huku baadhi wakisema kuwa hawana uhakika kama uchaguzi utakua wa huru na haki, na wengine wakisema hawahitaji kupiga kura kwasababu matokeo huenda yalipangwa.

    Mwanamke mmoja aliiambia BBC kuwa alikuwa ni mwenye furaha kutekeleza jukumu lake la kiraia, na anatarajia rais atakayechaguliwa atatatua matatizo ya kimsingi kama kuhakikisha kuanakuwa na huduma bora za afya kwa watu.

    Matokeo ya awali wanatarajiwa kutangazwa tarehe 25 Aprili, na ya mwisho yatatolewa tarehe 15 Mei.

  10. Mauji ya Daunte Wright: Maandamano yazuka baada ya polisi kumuua mtu mweusi

    Vitoa machozi vimetumiwa na amri ya kutotoka nje kutolewa wakati wa maandamano ya hasira baada ya polisi kumpiga risasi mtu mweusi aliyesimamishwa na polisi wa trafiki katika jiji la Brooklyn kaskazini mwa Minneapolis nchini Marekani.

    Mwanamume huyo ametambuliwa na jamaa zake kama Daunte Wright mwenye umri wa miaka 20.

    Meya wa Brooklyn Centre alitoa amri ya kutotoka nje mjini kote hadi saa 06:00 (11:00 GMT), akiwaambia watu "muwe salama, endeni nyumbani".

    Taharuki huko Minneapolis iko juu wakati kesi ya afisa wa zamani anayedaiwa kumuua George Floyd ikiendelea.

    Gavana wa Minnesota Tim Walz alisema "alikuwa akifuatilia kwa karibu hali hiyo" na akiombea familia ya Bw Wright.

    Soma zaid:

    • George Floyd: Mfahamu Mmarekani mweusi aliyeuawa na kifo chake kusababisha maandamano Marekani
    • George Floyd: Je ni kipi kilichotokea dakika 30 za mwisho kabla ya kifo chake?
  11. Mwanajeshi awashitaki polisi kwa kuvunja sheria ya barabarani

    Mwanajeshi mweusi wa Marekani mwenye cheo cha Luteni amewasilisha mashitaka dhidi ya polisi wawili ambao walimshikia bunduki zao na kumpulizia maji ya pilipili wakati alipokuwa akisimamisha gari.

    Luteni Caron Nazario amevaa sare yake katika picha iliyochukuliwa na kamera ndogo ya polisi, iliyochukuliwa mwezi Disemba katika jimbo la Virginia.

    "Kusema ukweli ninaogopa kutoka nje ," anawaambia maafisa wawili wa polisi. " Ndio unapaswa kuogopa, anasema afisa.

    Polisi wanasema alisimamishwa kwa kushindwa kuonesha kibali cha kuendesha gari lakini vibali vya muda vinaonekana katika video hiyo.

    Katika tukio hilo, mwanajeshi huyo ambaye alifungwa pingu mikono yake wakati gari lilipokuwa likikaguliwa , aliuliza ni kwanini nguvu zinatumiwa dhidi yake na akajibiwa na afisa wa polisi: "kwasababu haoneshi ushirikiano." Baadaye aliachiliwa bila mashitaka.

    Mashitaka, yaliwasilishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Marekani ya Norfolk, Virginia, dhidi ya polisi hao wa idara ya Windsor, Joe Gutierrez and Daniel Crocker, wanaodaiwa kukiuka haki za kikatiba, ikiwa ni pamoja na kushambulia na kufanya msako kinyume cha sheria

    Hapakuwa na jibu la moja kwa moja kutoka kwa Idara ya polisi ya Windsor.

    Mashitaka haya yanakuja wakatikukiwa na ongezeko la uchunguzi juu ya madai ya ukatili wa posli dhidi ya walio wachache na haki za kijamii.

    Afisa wa zamani wa polisi Derek Chauvin kwa sasa anakabiliwa na kesi ya mauaji ya George Floyd.

    Picha za Bw Chauvin, ambaye ni mzungu, huku goti lake likiwa limekandamizwa kwenye shingo ya Mmarekani mweusi Bw Floyd ziliibua maandamano makubwa kote duniani dhidi ya ubaguzi wa rangi.

  12. Eritrea yawachilia Wakristo 36 waliofungwa kwa imani yao

    Maafisa nchini Eritrea wamewaachilia kwa dhamana wafungwa 36 ambao wamekuwa mahabusu kwasababu ya imani yao.

    Vyanzo vya habari hii vimeiambia BBC kuwa 14 kati ya wafungwa hao wamekuwa mahabusu kwa miaka minne iliyopita katika kisiwa cha Dahilik. Wengine 20 waliokamatwa mwishoni mwa mwezi uliopita wameachiliwa kwa dhamana.

    Wafungwa wote wanatoka katika madhehebu ya Kiinjilisti na Kipentekosti.

    Mwaka wa 2002 Eritrea ilianzisha sheria ambayo inazuia makanisa yote isipokua makanisa ya Orthodox, Katoliki na Kilutheli.

    Waislamu wa madhehebu ya Sunni wanatambuliwa rasmi.

    Serikali ya Eritrea imekuwa ikiwaachilia huru watu waliofungwa kwasababu za kidini.

    Mwezi Septemba mwaka 2020, serikali ya Eritrea liwaachilia mahabusu zaidi ya 20 ambao walikuwa wamefungwa kwa miaka mingi . Mwezi Disemba, maafisa pia waliwaachilia wafuasi 28 wa kikundi cha Mashahidi wa Jehovah baada ya kutumikia kifungo cha jela kwa muda mrefu.

    Wakristo wengi, bado wamebakia magerezani na wengine wamekuwa wakikamatwa mara kwa mara, kulingana na wanaharakati wa uhuru wa dini.

    Serikali ya Eritrea inawashutumu Wakristo wa madhebebu ya Kipentekoste na kiinjilisti kwa kutumiwa na serikali za kigeni.

    Eritrea, ambalo ni taifa lenye usiri, na la kijeshi kwa hali ya juu, imekuwa ikitawaliwa na Isaias Afwerki tangu ilipopata uhuru wake kutoka kwa Ethiopia mwaka 1993, bila uchaguzi au bunge na muswada wa katiba uliopo haujawahi kutekezwa.

    Soma zaidi:

  13. Somalia yapokea chanjo ya corona kutoka Uchina

    Somalia imepokea dozi 200,000 za chanjo ya Sinopharm Covid-19 kutoka Uchina.

    Waziri wa afya Fawziya Abikar alipokea dozi hizo kutoka kwa balozi wa Uchina nchini Somalia Qin Jian.

    Wizara ya afya ya nchi hiyo ilituma picha za tukio hilo kwenye mtandao wake wa Twitter:

    Somalia ilikuwa imepokea shehena ya kwanza ya dozi 300,000 za chanjo kupitia mpango wa Covax.

    Jumla ya watu 12,406 walithibitishwa kupatwa na maambukizi ya virusi vya corona ikiwa ni pamoja na vifo 618, kulingana na takwimu kutoka wizara ya afya nchini humo.

  14. Mamilioni wanakabiliwa na njaa Somalia huku kukiwa na hali mbaya ya hewa

    Shirika la kimataifa la misaada ya kibinaadamu linasema wimbi la makundi ya nzige, hali mbaya ya hewa na kiwango cha chini cha mvua vinamaanisha kuwa mamilioni ya watu nchini Somalia hawatakuwa na chakula cha kutosha.

    Shirika la Save the Children linasema, mimea na mazao ya mboga mboga yanatarajiwa kupungua kwa 80% katika msimu huu.

    Mapato yatokanayo na mauazo ya mifugo, ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Somalia, yanatarajiwa kushuka kwa hadi 55%.

    Shirikka hilo linasema kuwa wanawake wanahangaika kujaribu kupata mlo mmoja tu kwa siku kwa ajili ya watoto wao. Baadhi ya watoto hao wana utapiamlo tayari.

    Inakadiriwa kuwa mwaka huu, familia masikini nchini Somalia zitaweza kupata 15% ya chakula chake kutokana na mazao yao. Katika nyakati nyingine ngumu, mazao yao yamekuwa yakiwapatia karibu nusu ya chakula chao.

    Wasomali tayari wanakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na ghasia za muda mrefu za wanamgambo wa kiislamu, hali tete ya kisiasa na miaka 30 ya kutokuwa na serikali kuu yenye ufanisi.

  15. Chadema yataka kuonana na Samia

    Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Chadema kimeomba kuonana na rais wa nchi hiyo Samia Suluhu Hassan, kiongozi mkuu wa Chadema ameeleza.

    Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema amemuandikia Rais Samia barua kumuomba kuonana naye ili kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali utakaoliletea taifa furaha, haki na ustawi.

    Akizungumza na vyombo vya habari Jumapili Bw Mbowe alisema "Wote tumejifunza, serikali ikiharibikiwa, nchi yote inaingia simanzi. Hii haina maana sisi wa Chadema tumegeuka waimba mapambio wa Rais Mama Samia. Inatupa sisi changamoto ya kuongeza juhudi za kuboresha sera zetu na kuongeza ushindani wa hoja."

    Bw Mbowe amesema wanategemea kumweleza Mama Samia na kumkabidhi mapendekezo yao kadhaa ya kina ya namna bora ya kuanza upya katika azma ya "kujenga utengemano wa nchi" na akaongeza kuwa wanaamini atatambua nafasi ya vyama vya upinzani.

    "Hatupaswi kumtakia mabaya kwa sababu tu ni zao la CCM. Bali tunatakiwa kuongeza juhudi na maarifa kumkabili kwa ushindani wenye kujenga na siyo kubomoa. Tunamwombea afanye mema wakati wa utawala wake ili kupata ustawi wa taifa letu."

    Bw Mbowe amesema kuwa: "kauli za rais, Mama Samia Suluhu Hassan zinatuchanganya na anapaswa kulijua hili. Anapoongea nia yake ya kuenzi sera, mipango na tabia ya Magufuli, taifa linasinyaa na kuhuzunika."

  16. Natumai hujambo... karibu kwa matangazo yetu mbashara leo Jumatatu tarehe 12.04.2021