Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Profesa aliyetoa tahadhari ya Corona atakiwa kuomba radhi Tanzania

Katika taarifa ya baraza la chuo kikuu huria imesema kuwa makamu mkuu wa chuo kikuu huria Tanzania Prof. Elifas Bisanda anatakiwa kuomba radhi kwa wizara ya elimu kutokana na waraka wa tahadhari ya Corona aliyoitoa kwa wanafunzi na wafanyakazi wa chuo chake.

Moja kwa moja

Lizzy Masinga, Dinah Gahamanyi and Esther Namuhisa

  1. Mpaka hapa tumefika mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja katika kurasa ya BBC Swahili, tukutane tena hapo kesho. Shukrani

  2. Mtaalamu wa upasuaji aiondoa gundi iliyokuwa imeganda kwenye ngozi ya kichwa

    Daktari bingwa wa upasuaji wa kurekebisha maumbile,Michael Obeng, Mmarekani mwenye asili ya Ghana,amefanikiwa kuondoa gundi iliyokuwa imegandishwa kwenye ngozi ya kichwa cha mwanamke mmoja aliyeonesha kichwa chake kwenye video mtandaoni.

    Mwanamke huyo alijipaka gundi hiyo bila kujua akidhani ni mafuta ya kurembesha nywele zake, kwa mujibu wa video za TMZ.

    Dkt. Michael Obeng alichukua saa nne kuondoa gundi hiyo kutoka kwa kichwa cha Tessica Brown, tovuti hiyo imeandika.

    Daktari huyo bingwa aliyesomea chuo kikuu cha Havard, ambaye sasa hivi anaendesha shughuli zake katika eneo la Beverly Hills alijitolea kufanya upasuaji huo ambao ungegharimu dola 12,500 bila malipo baada ya kusikia masaibu yaliyompata Bi. Brown ambaye alishirikisha wengine yaliyompata kupitia video ya TikTok wiki iliyopita.

    Mwanamke huyo alikuwa ametumia gundi inayotumiwa kugandisha vigae, sakafu za mbao na mapambo ya nyumbani na kulazimika kukata nywele ambazo alikuwa amebandika kwasababu zilikuwa zinavuta ngozi yake sana.

    Baada ya kupata matibabu, Bi. Brown aliyejawa na hisia alionekana akipitisha vidole vyake kwenye nywele zake.

    Dkt. Obeng, ambaye ana historia ya kufanya kemia, ameelezea TMZ kwamba alitumia kemikali mbalimbali kulainisha kiungo cha msingi (polyurethane,) kwenye gundi hiyo aina ya Gorilla Glue.

    Alisema alifanya utafiti huo na kufanikiwa kutengeneza mchanganyiko wa kemikali kuondoa gundi hiyo iliyojumuisha aloe vera, mafuta ya mzaituni na nyinginezo.

    Baada ya kumaliza kutengeneza mchanganyiko huo, kwanza alijaribu katika nywele zilizokuwa zimegandishwa kwa aina hiyo ya gundi ili kuhakikisha kwamba itafanya kazi.

    “Ana bahati kwasababu hakupata majeraha makubwa katika ngozi yake ya kichwa. Aina hii ya gundi huwa sio mchezo,” alisema, na kuongeza kuwa gundi hiyo ilifanya nywele zake na kuzigandisha kama kijiti.

    Alitoa wito kwa watu kuwa makini zaidi na kusoma vichupa vya kemikali mbalimbali wanavyonunua kabla ya kuanza kutumia bidhaa hizo.

    Dkt. Obeng amebobea katika upasuaji wa kubadilisha maumbile na kulingana na tovuti hiyo, yeye ndio mwanzilishi wa shirika ambalo hufanya upasuaji wa bure katika mataifa yanayoendelea kukua na pia hutoa mafunzo kwa madaktari wa eneo.

    • Daktari wa upasuaji kumsaidia mwanamke aliyegandisha nywele zake kwa gundi
    • Aomba kuombewa baada ya kuweka nywele zake gundi kwa bahati mbaya
  3. Tarehe ya hukumu dhidi ya kesi inayomkabili Rais Museveni yatangazwa

    Jopo la majaji tisa wa Mahakama ya juu nchini Uganda wametangaza kuwa tarehe 18 Machi, 2021 ndiyo watatoa hukumu ya kesi iliyowasilishwa na Robert Kyagulanyi kupinga matokeo ya uchaguzi wa Rais yaliyompatia bwana Museveni ushindi.

    Majaji hao kwa mara ya kwanza wamekutana na pande zote mbili katika mahakama hiyo mjini Kampala na kutoa muongozo wa kuanza kusikiliza kesi kwa muda wa siku 45 zinazotakiwa na katiba ya Uganda.

    Jaji mkuu wa Uganda, Alfonse Owiny Dollo ndiye ameongoza jopo la majaji wanaosikiliza kesi hiyo ya Robert Kyagulanyi.

    Jaji mkuu amezitaka pande zote mbili kuzingatia muda waliopewa kwa kutoa ushaidi, kwani hukumu ya kesi imepangwa kutolewa Machi 18.

    Kyagulanyi kupitia kwa mawakili wake wanamshtaki Rais Museveni, Tume ya uchaguzi na mwanasheria mkuu, ambao wote walikuwepo mahakamani kutetea ushindi wa Rais Museveni aliopata wa asilimia 58%.

    Kuanzia leo upande wa mashitaka na washitakiwa watakuwa wanabadilishana nyaraka za kesi hiyo na mashaidi hadi Machi 5,ameeleza Asumani Basalirwa, wakili wa Bobi Wine.

    Hii ni mara ya nne kwa Rais Yoweri Museveni kushitakiwa na wapinzani wake baada ya kutangazwa mshindi, Dkt Kiiza Besigye alimshitaki mara mbili na Amama Mbabazi mwaka 2016 lakini Rais Museveni aliibuka mshindi.

  4. Mbunge aitaka serikali kuzungumzia ‘vifo vitokanvyo na ugonjwa wa kupumua’

    Mbunge wa jimbo la Mbulu nchini Tanzania ameelezea wasiwasi wake kuhusu vifo vinavyotokana na ugonjwa wa kupumua vinavyotokea kwa wingi katika jimbo lake, Gazeti la Mwananchi limeripoti.

    Katika kikao cha bunge mjini Dodoma, bwana Zacharia Isaay ameitaka Serikali ya Tanzania kueleza kina sababu inayopelekea watu kufa kwa ugonjwa unaofanana, ambao huwa wanaita 'pneumonia', matatizo ya kupumua.

    "Serikali iache kigugumizi jimboni kwangu watu wanakwisha Spika,"amesema Isaay.

    Mbunge huyo ameelezea wasiwasi wake katika msimu huu wa baridi jimboni labda hali inaweza kuwa mbaya zaidi.

    "Jana nilikwenda hospitali ya hapa Benjamin Mkapa (Dodoma) kwa ajili ya kufanya vipimo lakini wakaniambia mitungi ya gesi imejaa,watu ni wengi sasa nimesema kama watu watanichukia basi lakini nimesema," Mwananchi imemnukuu mbunge huyo.

    Aidha, Mbunge huyo ameomba Serikali kuangalia namna ya kuboresha dawa za miti shamba ambazo ameeleza kuwa zinasaidia kwa kiasi kikubwa lakini akabainisha kuwa zinapatikana kwa gharama kubwa.

  5. Helkopta ya jeshi yaanguka Uganda

    Helkopta ya Jeshi la Uganda- UPDF imeanguka mjini mjini Entebbe majira ya mchana.

    Kwa mujibu wa ripoti kuhusu ajali hiyo ambayo ilitokea karibu na ufukwe kwa ziwa victoria, zinasema kulikuwa a abiria wawili .

    Msemaji wa jeshi amesema, Wahanga wa ajali hiyo walikimbizwa mara moja hospitalini na huku chanzo cha ajali hiyo kikifanyiwa uchunguzi.

  6. Air Namibia yasitisha safari zake

    Namibia imeamua kusitisha safari zote za ndege ya taifa ya Air Namibia.

    Kampuni hiyo ya ndege imewataka wateja wote kuomba kurejeshewa fedha zao na kusitisha safari zao.

    Tangazo hilo limesababisha ajira za watu zaidi ya 600 kupotea , gazeti la taifa hio limeripoti.

    Maamuzi hayo yametoka kwa baraza la mawaziri la kutaka safari zisitishwe, taarifa ya gazeti hilo imeeleza.

    Wafanyakazi watapokea mshahara kwa kipindi cha miezi 12 ijayo ila hawatapata mafao, Shirika la habari la Namibia limeripoti.

    Ndege hiyo ilikuwa na misukosuko ya uendeshaji wake -wiki iliyopita wajumbe wa bodi walijiuzuru wakiishutumu serikali kuingilia kati masuala ya ndege hiyo.

    Kwa mujibu wa tovuti ya Aviation24.be - tovuti inayotoa taarifa kuhusu masuala ya anga-imesema Namibia Air ilikuwa na changamoto za kifedha na suala la tatizo la usalama, na kuibuka kwa janga la corona ndio kumeifanya sekta ya usafirishaji kuanguka kabisa.

  7. Msumbiji:Eneo la kuhifadhia maiti kuongezwa baada ya ongezeko la vifo vilivyotokana na corona

    Maafisa wa mji wa Msumbiji wa Chimoio wametangaza mipango ya kuongeza chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali kuu ya jimbo kutokana kuongezeka kwa idadi ya vifo vinavyotokana na Covid-19.

    João Ferreira, Meya wa jiji amethibitisha kuongezwa kwa eneo la chumba hicho.

    Mradi huo utajumuisha kuongezwa kwa jengo la kuhifadhia maiti na kuongeza uwezo wa jokofu za kuhifadhia maiti kwa gharama ya thamani ya dola 5,300 (£3,800) katika hospitali ya jimbo la Manica Chimoio.

    Chumba cha kuhifadhia maiti ambacho kinaendeshwa na halmashauri hivi karibuni kiliongezewa uwezo kuanzia miili mitano hadi 60.

    Jiji limekuwa na wastani wa vifo vitano kila siku.

  8. Wanasiasa walioshutumiwa kuhusika na ugaidi wagoma kula Ethiopia

    Kiongozi wa upinzani nchini Ethiopia Jawar Mohammed, sambamba na watu wengine 19, wamekuwa kwenye mgomo wa kutokula kwa zaidi ya siku 13, kwa mujibu wa mawakili wao.

    Kundi hilo lilishtakiwa kujihusisha na vitendo vya kigaidi kuhusiana na wimbi la vurugu za wenyewe kwa wenyewe baada ya kuuawa kwa mwanamuziki maarufu nchini humo, Hachalu Hundessa.

    Zaidi ya watu 150 walipoteza maisha wakati wa vurugu hizo baada ya mtumbuizaji huyo kutoka kabila la Oromo kupigwa risasi mjini Addis Ababa.

    Bw. Jawar na Bekele Gerba, Naibu Mwenyekiti wa chama cha Oromo Federalist Congress(OFC) , ni miongoni mwa waliokuwa kwenye mgomo wa kutokula katika gereza la Kallitti.

    Wanataka ''kuachiliwa kwa wafungwa wote wa kisiasa wa kabila la Oromo na kukoma kwa uonevu wa familia za wafungwa wa kisiasa'', mawakili waliandika kwenye ukurasa wa Facebook.

    Mmoja wa mawakili, Kedir Bulo, aliiambia BBC idhaa ya Afaan Oromoo kuwa wafungwa wannne walizirai siku chache zilizopita na baadhi walikimbizwa hospitalini kwa ajili ya matibabu zaidi.

    Mamlaka hazijasema chochote kuhusu mgomo wa kutokula.

    Familia zilizozungumza na BBC zimesema kuwa walikuwa na hofu kuhusu hali za wafungwa

    Siku ya Jumanne makundi ya kidini na viongozi wa kisiasa walijaribu kuwashawishi wafungwa kumaliza mgomo bila mafanikio.

  9. 'Vijana wa chini ya miaka 18 marufuku kufuga rasta'

    Mkuu wa Wilaya ya Mjini huko visiwani Zanzibar, Rashid Msaraka ametangaza kuanza operesheni ya kuwanyoa nywele vijana wenye umri chini ya miaka 18, waliofuga rasta au kunyoa mtindo wa 'panki.'

    Amesema kama wanazitaka wakafugie sehemu nyingine na endapo wazazi wao wameshindwa kuwakata hizo nywele, atawakata yeye.

    ''Vijana wote wenye umri chini ya miaka 18 kama huyu..kama wazee wao wameshindwa kuwakata hizi nywele tutawakata sisi'' alitahadharisha kiongozi huyo.

    Picha ya video imesambaa katika mitandao ya kijamii ikionesha msaidizi wa kiongozi huyo akimkata nywele kijana aliyekuwa amezisokota nywele zake.

    Kitendo hicho kimeibua mjadala kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, watu wakihoji ni sheria ipi iliyomuongoza kiongozi huyo kutoa agizo la kumkata nywele kijana huyo.

  10. Profesa aliyetoa tahadhari ya Corona atakiwa kuomba radhi Tanzania

      • Author, Munira Hussein
      • Nafasi, BBC Africa

    Katika taarifa ya baraza la chuo kikuu huria imesema kuwa makamu mkuu wa chuo kikuu huria Tanzania Prof. Elifas Bisanda anatakiwa kuomba radhi kwa wizara ya elimu kutokana na waraka wa tahadhari ya Corona aliyoitoa kwa wanafunzi na wafanyakazi wa chuo chake.

    “Baraza la Chuo Kikuu Huria, limekaa kikao cha dharura na kuagiza Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Elifas Tozo Bisanda aombe radhi kwa Wizara ya Elimu, Chuo Kikuu Huria na Umma kwa waraka wa tahadhari ya Corona alioutoa Februari 8, 2021.” Inasema taarifa hiyo ya baraza la chuo

    Awali katika waraka wake, Prof Bisanda aliwataka wanafunzi na wafanyakazi wa chuo hiko, kujilinda na maambukizi ya virusi vya Corona ikiwa ni pamoja na kuepuka misongamano na kuvaa barakoa

    Aliongeza kuwa masomo na vikao vifanyike kwa njia ya mtandao.

    Muda mchache baada ya waraka huo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, maana Wizara ya Elimu ilibatilisha waraka kutokana na kukiuka utaratibu wa wizara ya afya wa muongozo kwa vyuo na taasisi ya elimu ya juu.

    Mwezi uliopita Kanisa Katoliki nchini Tanzania lilitoa tahadhari juu ya wimbi jipya la maambukizi ya corona na kuwataka wananchi kuchukua hatua zote za kujikinga.

    Tahadhari hiyo ilitolewa kupitia waraka ulioandikwa na Rais wa Baraza la Maaskofu wa Katoliki Tanzania (TEC) Askofu Gervas Nyaisonga.

    Hata hivyo Wizara ya afya nchini humo bado haijathibitisha taarifa za uwepo wa wagonjwa au vifo vinavyo sababishwa na wimbi jipya la virusi vya corona.

    Mara ya mwisho kutolewa kwa taarifa za mwenendo wa maambukizi ya virusi vya corona ilikua mwezi Aprili mwaka jana.

  11. Hujambo na tunakukaribisha tena kwa matangazo yetu ya mubashara leo tarehe 11.02.2021