Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Ubalozi wa Marekani Tanzania watoa tahadhari ya maambukizi ya corona

Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania umetoa tahadhari ya ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona.

Moja kwa moja

Lizzy Masinga, Dinah Gahamanyi and Esther Namuhisa

  1. Ubalozi wa Marekani Tanzania watoa tahadhari ya maambukizi ya corona

      • Author, Munira Hussein
      • Nafasi, BBC Africa

    Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania umetoa tahadhari ya ongezeko la maambukizi ya ugonjwa wa corona.

    Katika taarifa yake iliyotumwa kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, ubalozi huo, umesema kuwa kumekua na taarifa za ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona tangu mwezi Januari.

    ‘’…hatua za kuondosha na kuzuia maambukizi ya Covid-19 bado zimeeendelea kuwa za kiwango cha chini, serikali ya Tanzania haijatoa takwimu zozote kuhusu visa vya maambukizi au vifo vilivyotokana na Covid-19 toka mwezi Aprili 2020’’ inasema sehemu ya taarifa hiyo.

    Ubalozi huo pia unasema hospitali na vituo vya afya nchini Tanzania vinaweza kuzidiwa kwa haraka na idadi ya wagonjwa.

    ‘’Uwezo mdogo wa hospitali nchini kote Tanzania unaweza kusababisha wagonjwa walio katika hali ya dharura kuchelewa kupatiwa huduma, jambo linaloweza kuhatarisha maisha.’’

    Taasisi mbalimbali zimeendelea kutoa tahadhari ya maambukizi ya virusi vya corona.

    Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Tanzania (SUA) ilitoa taarifa hapo jana kwa wanafunzi na wafanyakazi wake kujilinda dhidi ya maambukizi ya corona.

    Nacho Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kilitoa waraka wa kuchukua tahadhari ya kujilinda na maambukizi ya corona.

    Hata hivyo waraka huo ulibatilishwa na wizara ya elimu kwa kukiuka utaratibu uliotolewa na wizara ya afya.

    Mwezi uliopita Kanisa Katoliki nchini Tanzania lilitoa tahadhari juu ya wimbi jipya la maambukizi ya corona na kuwataka wananchi kuchukua hatua zote za kujikinga.

    Tahadhari hiyo ilitolewa kupitia waraka ulioandikwa na Rais wa Baraza la Maaskofu wa Katoliki Tanzania (TEC) Askofu Gervas Nyaisonga.

    Hata hivyo Wizara ya afya nchini humo bado haijathibitisha taarifa za uwepo wa wagonjwa au vifo vinavyo sababishwa na wimbi jipya la virusi vya corona.

    Mara ya mwisho kutolewa kwa taarifa za mwenendo wa maambukizi ya virusi vya corona ilikua mwezi Aprili mwaka jana.

  2. Uganda yaondoa vizuizi vya intaneti na mitandao ya kijamii

    Serikali ya Uganda imetangaza kuondoa vizuizi vyote ilivyokuwa imeviweka katika intaneti na mitandao ya kijamii.

    "Tuaomba radhi kwa usumbufu wowote uliojitokeza, lakini ilikuwa ni kwa ajili ya usalama wa taifa letu," Peter Ogwang, Waziri wa mawasiliano, aliandika kwenye tweeter.

    Aliongeza: "Tuwe wateja wa kujenga na sio kubomoa , tuwe wateja wazuri wa mitandao ya kijamii."

    Huduma ya mitandao ya kijamii ilizuiwa usiku wa kuamkia tarehe 14 Januari, siku ya uchaguzi mkuu.

    Rais Yoweri Museveni alishutumu kampeni za mitandao ya kijamii kuwa na ubaguzi.

    Hatua hiyo ilikuja baada ya Facebook kusema kuwa inazifungia zaidi ya akaunti 200 zinazohusiana na kampeni za chama tawala.

    Kampuni ya mitandao ya kijamii ilidai kuwa akaunti hizo zilikuwa zinasambaza taarifa zisizo sahihi kudhibiti mijadala kabla ya siku ya kupiga kura.

    Facebook ilisema akaunti hizo zilikuwa za Uganda, na zilikuwa zinatuma taarifa gushi kwa wananchi wake na hata kutuma taarifa hizo mara kadhaa ili kuzipa taarifa hizo umaarufu zaidi.

    Mkuu wa taarifa za vitisho Facebook, David Agranovich, alisema uchunguzi wao ulibaini kuwa unahusisha akaunti feki zilizohusisha moja kwa moja wizara ya mawasiliano na teknolojia.

    Facebook pia iliondoa akaunti 139 za Instagram.

    Akaunti hizo zilikuwa zilikuwa zinamuunga mkono Rais Museveni na chama chake cha National Resistance Movement.

    Mpinzani wake mkuu ambaye ni mwanamuziki aliyegeuka kuwa mwanasiasa Robert Kyagulanyi anayefahamika kama Bobi Wine, alikuwa na miaka minne tu wakati wakati Bw. Museveni aingie madarakani mwaka 1986.

    Bwana Museveni ameingia muhula wa sita wa utawala wake baada ya kuchuana vikali na mpinzani wake Bobi Wine, ambaye anadai matokeo yalikuwa ya uongo.

  3. Kikongwe mwenye miaka 116 apona Corona

    Mwanamke mzee zaidi barani Ulaya ambaye ni mtawa mfaransa ameponda Covid-19, siku chache kabla ya siku kuu ya kuzaliwa kwake ambayo atatimiza miaka 117.

    Mtawa huyo alikutwa na maambukizi ya virusi vya corona Januari 16 lakini hakuonesha dalili zozote. Alisema hata hakugundua kuwa ana ugonjwa huo. Alijitenga na wakazi wengine ambao walikuwa wakiishi katika nyumba ya malezi huko Toulon, kusini mwa France, lakini sasa ameelezwa kuwa amepona kabisa.

    Sista Andre, ambaye ni mlemavu wa macho na hutumia kiti cha kusukuma anasubiri kusheherekea siku yake ya kuzaliwa siku ya Alhamisi, akiwa amewaalika watu wachache zaidi tofauti na miaka iliyopita.

    "Amekuwa na bahati sana," David Tavella, msemaji wa nyumba ya malezi ameeleza.

  4. Familia moja yapoteza ndugu wanne mfululizo

    Nchini Tanzania , Familia moja ya mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Profesa Delphina Mamiro imepata pigo ndani ya mwezi mmoja kwa kupoteza watu wanne mfululizo ndani ya familia moja, Gazeti la Mwananchi limeripoti.

    Profesa Delphina, mume wake na wazazi wake wote , mama na baba yake wamefariki pia kwa kupishana siku tatu tatu.

    Profesa Delphina alianza kujisikia vibaya mwanzoni mwa mwezi huu na kufariki dunia akipatiwa matibabu hospitali na siku chache baadaye mumewe alifariki dunia.

    Wazazi wake Delphina walifariki Januari 13 na 16,mkoani Kilimanjaro ,Moshi na hivyo Profesa huyo na mume wake walitoka Morogoro na kwenda kuzika.

    Lakini baada ya kurudi , wote wanandoa hao waliugua na kufariki dunia.

    Vifo vyao ni miongoni mwa vifo vilivyoibua hisia mbalimbali nchini Tanzania, wakati ambapo zimekuepo taarifa nyngi kuhusu watu kupoteza ndugu na jamaa zao siku za hivi karibuni.

  5. Rayvanny azindua albamu ya kwanza tangu aanze tasnia ya muziki

      • Author, Roncliffe Odit
      • Nafasi, BBC Nairobi

    Muimbaji wa Tanzania, Raymond Shaban Mwakyusa, almaarufu Rayvanny ameachia video yake ya kwanza kutoka kwa albam yake mpya, Sounds From Africa.

    Video hiyo inayoitwa 'Kiuno' ni wimbo nambari 18 katika albamu hiyo yenye nyimbo 23.

    Sounds From Africa ndio albamu ya kwanza ya Rayvanny wa lebo ya WCB Wasafi.

    Albamu hiyo hadi sasa imepata ufanisi mkubwa kwa kusikilizwa zaidi ya mara milioni 105 kwenye majukwaa ya kidijitali, wiki moja tu tangu kutolewa.

    Akizungumza alipozindua albamu hiyo, Rayvanny aliwashukuru mashabiki wake na usimamizi wa WCB Wasafi kwa kufanikisha juhudi zake za kimuziki.

    "Albamu yangu ya kwanza katika kazi yangu ya muziki, asante Mungu kwa hili #SoundsFromAfrica," alisema Rayvanny kwenye Twitter.

    Muimbaji wa Marekani Enisa ni miongoni mwa wale walioshirikishwa kwenye albamu hiyo, kwenye wimbo wa Number One Remix.

    Wengine walioshirikishwa kwenye albamu hiyi ni Diamond Platnumz, Mbosso, Joe Boy, Innoss’B, Saida Karoli, Vannesa Mdee na Jah Prayzah.

    Albamu hiyo inapatikana kwenye majukwaa yote ya kidijitali.

  6. Mbunge afukuzwa kwa kukataa kuvaa tai akiita 'kitanzi cha mkoloni'

    Kiongozi wa Chama cha Maori ameondolewa kutoka kwenye bunge la New Zealand kwa kutovaa tai.

    Wabunge wa kiume wanaweza tu kuuliza maswali bungeni humo ikiwa wamevaa tai.

    Spika Trevor Mallard alimzuia mara mbili Rawiri Waititi kuuliza maswali. "Sio kuhusu tai, ni kuhusu utambuzi wa kitamaduni," Bwana Waititi alisema wakati anatoka kwenye chumba hicho, vyombo vya habari vya huko viliripoti.

    Ametaja tai "kitanzi cha mkoloni" na badala yake amevaa kidani cha jiwe.

    Baada ya kuzuiwa kwa mara ya pili, Bw Waititi aliendelea na swali lake hadi Bw Mallard alipomuamuru aondoke kwenye ukumbi huo.

    Bw Waititi alisema ametendewa "isivyofaa", na kuongeza kuwa alikuwa amevaa "mavazi biashara ya Maori".

    Kiongozi mwenza wa Chama cha Maori, Debbie Ngarewa-Packer, ambaye mwenyewe alikuwa amevaa tai, alimtetea mwenzake lakini hakufaulu.

  7. Rais wa Somalia aitisha mkutano kutatua mgogoro

    Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Farmajo ameitisha mkutano na viongozi wa serikali ya shirikisho wiki ijayo ili kutatua mkwamo wa jinsi ya kuendelea na uchaguzi.

    Muhula wa Rais Farmajo ulimalizika Jumatatu baada ya mazungumzo kuhusu uchaguzi kuvunjika mnamo tarehe 5 Februari.

    Vikundi vya upinzani vimesema havitambui tena mamlaka ya Bwana Farmajo na walitaka kuundwa kwa ushirika wa mpito.

    Ofisi ya rais iliandika katika ukurasa wa twitter kuhusu mkutano uliopangwa kufanyika wiki ijayo huko Garowe, jimbo la Puntland.

    Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumanne liliwahimiza viongozi wa Somalia "kufikia makubaliano ya kufanyika kwa uchaguzi.

    Limekaribisha kutangazwa kwa mazungumzo zaidi tarehe 15 Februari.

    Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat Jumatatu alikuwa amemtaka Rais Farmajo na viongozi wa serikali ya shirikisho "kufikia makubaliano juu ya maswala yaliyosalia ili kuruhusu kufanyika kwa uchaguzi wa bunge na urais bila kuchelewa sana".

  8. Serikali Tanzania ‘yabatilisha’ waraka wa Corona wa Chuo Kikuu Huria

      • Author, Munira Hussein
      • Nafasi, BBC Africa

    Wizara ya Elimu, sayansi na teknolojia imetaka chuo kikuu huria kuendelea na shughuli zake Kama kawaida.

    Tamko hili limekuja baada ya utaratibu na ushauri uliotolewa na makamu mkuu wa chuo hiko Prof. Elifas Bisanda kutaka mikutano na masomo yafanyike kwa njia ya mtandao ikiwa ni kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

    Taarifa hiyo imeongeza kuwa maoni yaliyotolewa na makamu mkuu wa chuo ni batili.

    “Maelekezo yaliyotolewa na Prof. Bisanda ambayo ni maoni yake binafsi hayajazingatia muongozo wa udhibiti wa maambukizi ya ugonjwa wa Corona katika shule, vyuo na taasisi za elimu nchini wa wizara ya afya wa terehe 27 mei 2020” inasema taarifa hiyo ya wizara ya Elimu.

    Katika taarifa yake ya awali katika Waraka umewataka wanafunzi na wafanyakazi

    kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na kuwa tishio la maambukizi "linashamiri".

    "Kwa upande wa wanafunzi tunasisitiza wakae nyumbani na kusoma kwa njia ya mtandao, hatutaruhusu wanafunzi na wageni kuingia kwenye kampasi zetu bila sababu maalumu’’ inasema taarifa hiyo.

    Kwa upande wa wafanyakazi wao wataendesha mikutano yao kwa njia ya mtandao.”

    Mwezi uliopita Kanisa Katoliki nchini Tanzania lilitoa tahadhari juu ya wimbi jipya la maambukizi ya corona na kuwataka wananchi kuchukua hatua zote za kujikinga.

    Tahadhari hiyo ilitolewa kupitia waraka ulioandikwa na Rais wa Baraza la Maaskofu wa Katoliki Tanzania (TEC) Askofu Gervas Nyaisonga.

    Hata hivyo Wizara ya afya nchini humo bado haijathibitisha taarifa za uwepo wa wagonjwa au vifo vinavyo sababishwa na wimbi jipya la virusi vya corona.

    Mara ya mwisho kutolewa kwa taarifa za mwenendo wa maambukizi ya virusi vya corona ilikua mwezi Aprili mwaka jana.

    Unaweza pia kutazama:

    • Virusi vya corona: Waziri wa Afya Dorothy Gwajima atengeneza na kunywa tiba asili ya Tanzania
  9. Hujambo na Karibu tena kwa matangazo yetu mubashara leo Jumatano tarehe 10.02.2020