Virusi vya Corona: Saudia yapiga marufuku raia wa kigeni kuizulu

Chanzo cha picha, AFP
Vyombo vya habari nchini Saudi Arabia vinaripoti kuwa nchi hiyo imeweka marufuku dhidi ya raia wasio wa nchi hiyo kuingia nchini humo, wakiwemo mabalozi, wahudumu wa afya na familia zao.
Hatua hiyo itaziathiri nchi 20, huku Saudi Arabia ikihangaika kupambana na janga la corona.
Taarifa hiyo imesema nchi ambazo raia wake wamewekewa marufuku hiyo ni pamoja :
Argentina na Milki za kiarabu, Ujerumani, Marekani, Indonesia, Ireland, Italia, Pakistan, Brazil, Ureno, Uingereza, Uturuki, Afrika Kusini, Sweden, Uswiss,Ufaransa, Lebanon, Misri, India na Japan.
Marufuku hiyo itaanza kutekelezwa kuanzia saa tatu usiku (kwa saa za Saudi Arabia ) Jumatano, tarehe 3 Februari .
"Aidha , marufuku hiyo inawahusu raia wanaopita katika mataifa hayo 20 ," yameripoti magazeti ya Saudi Arabia.









