Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mawaziri wawili wa Malawi wafariki dunia kutokana na corona
Mawaziri wawili wa Malawi wamefariki dunia ndani ya saa mbili baada ya kuugua Covid 19
Moja kwa moja
Dinah Gahamanyi
Tanzania yapiga mnada vitalu 30 katika hifadhi ya wanyama
Serikali ya Tanzania imetangaza kupiga mnada maeneo 30 ya kitalii ya uwindaji yaliyopo ndani ya hifadhi ya wanyama pori na maeneo mengine.
Mamlaka ya wanyama pori nchini Tanzania (TAWA) inakaribisha maombi kwa wale wenye vigezo vya kuweza kununua maeneo yatakayofanyiwa mnada kwa njia ya kielektroniki.
Tawa imeweka vigezo ambavyo makampuni yanapaswa kuzingatia , ikiwa ni pamoja na kujisajili kuwinda nchini humo pamoja na kuwa na mkurugenzi mmoja mwenye uzoefu wa miaka mitano kuhusu biashara ya wanyama pori na hifadhi ya wanyama pori nchini humo.
“Makampuni ya uwindaji yataweza kupata vitalu vitano kila mmoja katika makundi tofauti. Mnada huo unatarajiwa kufanyika Februari 08, mwaka 2021 na utafanyika kwa muda wa siku saba” mamlaka imeeleza.
Baadhi ya ya vitalu vitakavyouzwa vipo katika hifadhi ya Selous,mbuga ambayo imetajwa na shirika la umoja wa mataifa la Unesco kuwa ni eneo la urithi wa dunia.
Utalii ni nguzo muhimu ya uchumi wa Tanzania.
Serikali iliweka maeneo 26 ya uwindaji ,mtandaoni kwa ajili ya mnada mwaka 2019 ili kuhakikisha kkuwa rushwa inadhibitiwa na kunakuwa na uwazi.
Iliripotiwa kuwa si vitalu vingi viliweza kuuzwa mwaka jana.
Uchaguzi Uganda 2021:Vyombo vya usalama kutuma vikosi vyake nchi nzima
Wakati kampeni zikielekea ukingoni hii leo, Vyombo vya usalama nchini Uganda vimesema kuwa vitatuma vikosi vyake katika wilaya zote 39 nchini humo ili kuhakikisha kuwa kuna usalama katika maeneo yote ya nchi hiyo.
Tangazo hilo limekuja ikiwa ni siku ya mwisho ya kampeni za uchaguzi unaotarajiwa kufanyika siku ya Alhamisi.
Miezi miwili ya kampeni nchini humo imegubikwa na ghasia na kukamatwa kwa viongozi wa upinzani pamoja na wafuasi wao.
Polisi wamesema madumu ya mafuta , magari yanayobeba mlipuko na magari mengine ya mizigo hayataruhusiwa maeneo ya mji mkuu siku ya kupiga kura.
Wanahofia kuwa vitu kama hivyo vinaweza kutumiwa na waandamanaji kama silaha.
Watu hawataruhusiwa kuegesha magari yao barabarani mjini Kampala.
Wiki iliyopita, Mkuu wa polisi wa Uganda Martin Ochola alitoa angalizo kwa yeyote atakayefanya vurugu wakati wa uchaguzi atajuta siku aliyozaliwa.
Mwezi Novemba, ghasia zilitokea baada ya mgombea urais Bobi Wine kukamatwa wakati wa kampeni zake.
Wanajeshi hao watakuepo kwa ajili ya kuhakikisha usalama unakuepo ila imekosolewa kuwa ni jambo litakalowapa hofu wapiga kura.
Wakenya wakasirishwa na uteuzi wa Naomi Campbell kuwa balozi wa utalii
Wakenya kupitia mtandao wa Twitter wameikosoa wizara ya utalii kwa kumteua mwanamitindo wa Uingereza Naomi Campbell, badala ya kumteua mkenya, kama balozi wa Kenya wa utalii.
Waziri wa utalii Najib Balala katika taarifa yake amesema ilikuwa ni taarifa ya kufurahisha katika sekta hiyo.
Bi Campbell alisifu serikali ya Kenya kwa kuimarisha miundombinu katika eneo la pwani ikiwa ni pamoja na kuimarisha uwanja wa ndege wa Malindi kuwa wa hadhi ya kimataifa na kuongeza kuwa hatua hiyo itaimarisha utalii katika eneo hilo.
Lakini baadhi ya Wakenya wanahisi cheo cha balozi wa utalii kinapaswa kutolewa kwa Mkenya aliyeleta mafanikio kimataifa kama mchezaji filamu Lupita Nyong'o au mchekeshaji Elsa Majimbo.
Wakenya hawa walikuwa na haya ya kusema:
"Ni kwanini hatukumteua Lupita Nyong'o wetu na kumnadi mtu ," Victor Amalemba alitweet.
"Ni kwanini Ajuma Nasenyana hakupaewa nafasi hiyo na ni Mkenya, kwanini Lupita hakupata ofa hiyo na ni Mkenya, Kwanini Debra Sanaipei hakupata nafasi hiyo na niMkenya... kigezo gani kilitumiwa katika uchaguzi? Mtu asiye Mkenya?" Syombua Kibue alitweet.
Malawi yawapoteza mawaziri wawili kutokana na corona
Malawi imepata pigo kubwa baada ya mawaziri wake wawili kufariki dunia kutokana na Covid 19.
Waziri wa habari wa Malawi, Gospel Kazako amethibitisha kuwa mawaziri hao ambao ni Waziri wa serikali za mitaa, Lingson Belekanyama na Waziri wa uchukuzi Sidik Mia wamefariki ndani ya masaa mawili tofauti.
Mwishoni mwa juma, rais wa nchi hiyo Lazarus Chakwera alitoa hotuba maalumu kwa njia ya radio kwa taifa akitoa wito wa kuheshimiwa kwa hatua zilizowekwa za kupambana na maambukizi ya Covid 19 kufuatia ongezeko kubwa katika vifo na maambukizi ya virusi hivyo. Bw Chakwera anatarajiwa kutoa hotuba nyingine kwa taifa baadae leo, kwa mujibu wa Kazako.
Mwanafunzi Msenegal mwenye kipaji atoweka Ufaransa
Uchunguzi umeanzishwa nchini Ufaransa baada ya kutoweka kwa mwanafunzi mwenye kipaji Msenegali ambaye alikuwa akisoma katika shule ya kifahari mjini Paris.
Mwanafunzi huyo Diary Sow hakurejea shuleni baada ya mapumziko ya Krismasi na kusababisha hofu Senegal na Ufaransa.
Akielezewa kama"mwanafunzi bora wa Senegal ", Bi Sow alishinda tuzo kazaa za kielimu na kuchapisha kitabu chake cha kwanza cha tamthilia mwaka jana.
Saw huyo mwenye umri wa miaka 20, hajaonekana tangu tarehe 4 Januari.
Raia wa Senegal wanaoishi katika mataifa ya kigeni wamekuwa wakimtafuta kupitia mitandao ya kijamii. Watu mashuhuri wa Ufaransa ikiwa ni pamoja na mcheza filamu Omar Sy, wameshirikisha umma ombi lao la kutafutwa kwa Bi Sow kupitia mitandao ya Instagram na Twitter.
Mwanamitindo Naomi Campbell atangazwa kuwa balozi wa Kenya wa Utalii
Mwanamitindo Naomi Campbell amekubali uteuzi wa kuwa balozi wa kimataifa wa Utalii Kenya.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na Wizara ya Utalii na Wanyamapori, makubaliano hayo yamefikiwa kati ya Campbell na waziri wa utalii na wanyamapori, Najib Balala.
“Tunafurahishwa na taarifa kuwa Naomi Campbell atakuwa balozi wa utalii na kusafiri kimataifa akitangaza Kenya” Waziri amesema.
Wakati wa mkutano huo, Naomi Campbell alisifu serikali ya Kenya kwa kuimarisha miundombinu katika eneo la pwani ikiwa ni pamoja na kuimarisha uwanja wa ndege wa Malindi kuwa wa hadhi ya kimataifa na kuongeza kuwa hatua hiyo itaimarisha utalii katika eneo hilo.
Mwanamitindo huyo maarufu duniani atasaidia kuitangaza Kenya kama eneo ambalo ni kivutio cha utalii duniani.
Bi Campbell amekuwa akiwa akitembelea mara kwa mara eneo la Malindi kuvinjari nyakati za mapumziko yake.
Wizara ya Utalii na Wanyamapori nchini Kenya ilishirikisha umma taarifa ya kuidhinishwa kwa Bi Campell kuwa balozi wa Kenya wa Utalii kwenye ukurasa wake wa twitter:
Waziri wa Afrika Kusini apatikana na corona
Waziri wa nchi katika ofisi ya rais Jackson Mthembu amekuwa waziri wa nne katika serikali ya Afrika Kusini kupatikana na virusi vya corona.
Bw Mthembu alipimwa virusi hivyo baada ya kuwa na dalili, ilisema ofisi ya rais.
Amewekwa katika karantini pamoja na kila mtu aliyekaribiana naye
Waziri Mthembu alitweet akisema ana maumivu ya tumbo :
Afrika Kusini ina aina mpya ya virusi vya corona inayosambaa kwa kasi kubwa.
Nchi hiyo ilirekodi wagonjwa wapya 15,046 na vifo vipya416, na kulifanya taifa hilo kufikia jumla ya wagonjwa wa corona1,246,643 na vifo 33,579.
Burundi yafunga mipaka yake baada ya kuongezeka kwa wagonjwa wa corona
Burundi imetangaza kufunga mipaka yake ya ardhi na majini kufuatia ongezeko kubwa la watu waliopatikana na virusi vya corona.
Watu100 wamepatwa na maambukizi mpaya ya virusi vya corona nchini Burundi, ikiwa ndio itadi kubwa ya maambukizi kuwahi kushuhudiwa tangu ugonjwa huo ulipoibuka mwezi machi 2019.
Kuanzia leo Jumanne hakuna mtu yeyote atakayeweza kuvuka kuingia au kutoka nchini Burundi isipokuwa kwa wasafiri wanaotumia usafiri wa ndege pekee.
Hata hivyo wasafiri watakaoingia kwa ndege nchini humo watalazimika kwenda moja kwa moja katika hoteli maalumu na kuishi huko kwa siku saba amkako watapimwa virusi vya corona.
Aidha serikali imetangaza kuanzisha shughuli ya upimaji wa virusi vya corona kwa wakazi wa mji mkuu Bujumbura kwa yeyote anayehisi kuwa ana dalili za Covid-19.
Tayari watu zadi ya 980 wamekwishapatwa na virusi vya corona nchini Burundi na watu wawili ndio waliokufa kwa virusi hivyo kulingana na takwimu za wizara ya afya ya Burundi.
Je Sultani wa mwisho wa Zanzibar yuko wapi?
Baada ya kuishi mafichoni hususan nchini Uingereza Jamshid bin Abdullah Al Said, aliyekuwa sultani wa Zanzibar , akiwa ndio Sultan wa mwisho wa masultani waliotawala miaka 91 kisiwani humo kutoka kwa familia ya al Busaid , alihamia katika ufalme wa Oman...Bonyeza hapa kusoma zaidi taarifa hii
Raila Odinga ataka urais uwe kwa zamu kwa misingi ya kuponya taifa
Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Kenya –ODM Raila Odinga ameunga mkono wito wa rais wa Kenya Uhuru Kenyatta wa kutaka rais ajaye atoke katika jamii tofauti ambayo haijawahi kuongoza.
Akizungumza na kikundi cha vijana Jumatatu Bw Raila alisema kuwa urais ni sula tata kwani Kenya ni taifa lenye makabila mengi.
“Kama mnavyofahamu Kenya ni jamii yenye makabila mengi, na kutokana na hili tunalichukuliwa kwa umakini kutokana na tofauti za kikabila ambazo tunazo katika nchi yetu,” alisema Raila.
Mwishoni mwa Juma Rais Uhuru Kenyatta aliibua mjadala hususa ni katika mitandao ya kijamii nchini Kenya pale aliposema ‘’Ni makabila mawili tu ambayo yameiongoza Kenya tangu uhuru wake.Huenda umefika wakati kwa makabila mengine ambayo hayajawahi kuongoza Kenya kuongoza’’.
Akiunga mkono Kauli ya Rais Kenyatta, Bw Raila alisema haoni madhara yoyote kama urais utakuwa ni wa zamu , hususan ni pale uteuzi unapofanywa na rais anayependelea watu kutoka makabila/ jamii nyingine.
Kiongozi huyo wa ODM anaamini kama urais utakuwa wa zamu taifa linaweza kupona.
Wanajeshi wa Uganda waripotiwa kuvamia makazi ya mgombea wa urais Bobi Wine
Mgombea wa Urais nchini Uganda Robert Kyagulanyi amelazimika kukatiza mahojiano yake na radio baada ya wanajeshi kuvamia nyumba yake mjini Kampala.
Vyombo vya habari nchini Uganda vinaripoti kuwa leo asubuhi wanajeshi walizingira nyumba yake , na kuwakamata walinzi wake wote na mtu yeyote waliyempata katika eneo la makazi ya mwanasiasa huyo wa upinzani.
Hata hivyo hakuna sababu iliyotolewa juu ya uvamizi huo.
Bw Kyagulanyi alikuwa kihojiwa katika kipindi cha radio cha kituo cha Kenya Kenya HOT 96 cha kila asubuhi aliposema kuwa anawaona maafisa wa kijeshi wakiwapiga walinzi wa usalama wake.
Sauti zilizikika kwa mbali kupitia redio wakati wa tukio hilo kabla ya Bobi Wine kukata simu ya mahojiano.
Mwandishi wa habari eff Koinange alitweet kiungangishi cha mahojiano:
Wakati haya yakijiri Rais Yoweri Museveni ambaye anawania muhula wa sita madarakani anatarajiwa kulihutubia taifa leo kupitia vyombo vya habari vya kitaifa. Waganda wanatarajia kufanya uchaguzi wa wabunge na rais siku ya Alhamisi.
Kampeni za uchaguzi nchini Uganda zimekuwa zikigubikwa na gasia zinazosababisha mauaji.
Hujambo na karibu kwa matangazo yetu mubashara leo tarehe 12.01.2021