Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Fahamu siri inayoendelea kumtajirisha bilionea mkubwa duniani

Jeff Bezos tajiri mkubwa duniani anayesimamia kampuni ya kimataifa ya Amazon inayofanya vizuri.

Moja kwa moja

Asha Juma

  1. Fahamu siri inayoendelea kumtajirisha bilionea nambari moja duniania duniani

    Jeff Bezos tajiri mkubwa duniani anayesimamia kampuni ya kimataifa ya Amazon inayofanya vizuri.

    Kampuni yake inakadiriwa kuwa na thamani ya takribani dola bilioni $171 sawa na (£137bn), na pia ameweza kutengeneza mabilioni ya pesa wakati wa janga la Covid-19 .

    Lakini je, anazingatia nini katika kuhakikisha anaendelea kufanikiwa?

    Fahamu siri inayomfanyatajiri mkubwa duniani kuendelea kutajirika

    1. kila tatizo linaweza kutatuliwa kwa kufikiria na uwepo wa ukweli.

    2. Kila wakati mteja ni mfalme.

    3. Fikiria anachotaka mteja na namna ya kutimiza hitaji lake.

    4. Kila siku chukulia kana kwamba ni siku ya kwanza ya biashara yako. Kuwa na hamu ya kutaka kuona unavumbua kitu cha kipekee hadi mafanikio yake.

    5. Kuwa na moyo wa kutaka kujaribu kitu hata kama kutakuwa na hatari ya kupoteza.

    6. Na hata usipofaulu, hautakuwa sawa na ambaye hajajaribu. Hivyobasi, pendelea kuwa mtu wa kudhubutu.

    7. Hutawahi kujuta kwa kujaribu kitu fulani.

    “Unapofikiria vitu ambavyo hujafanya ukiwa umetimiza miaka 80, mara nyingi ni vile ambavyo hukujaribu kabisa. Ni nadra sana kujuta kwasababu ya jambo ambalo ulijaribu kufanya lakini halikufanikiwa.”

    8. Zungumza unachodhani ni sahihi.

    9. Usiogope ushindani.

    10. Angalia malengo ya muda mrefu.

    Inasemekana kuwa tajiri huyu wa dunia Bezos, “yuko tayari kuchukua miaka 10 kufanya kitu kitakachomwezesha kupata peza miaka ijayo” na kusalia na lengo lake mradi linaonesha dalili ya kupiga hatua.

    Soma zaidi kuhusu tajiri mkubwa duniani

  2. Wenyeji watumia gari la zima moto kukabiliana na nyuki

    Wakaazi wa maeneo matatu nchini Cameroon watoroka makaazi yao baada ya kuvamiwa na nyuki.

    Watu watano wamepelekwa hospitali, wanne kati yao wakiwa watoto.

    Tukio hilo limefanya maafisa wa usalama kutoa wito kwa wenyeji kurejea nyumbani na kutulia wanapoendelea kukabiliwa.

    Gari la zima moto ndilo linalotumika kukabaliana na nyuki hao.

    Hadi kufikia sasa bado haijajulikana chimbuko la nyuki hao.

    Awali, wenyeji waliamua kutumia njia ya kitamaduni ya kuchoma moto makaratasi ili kufuza nyuki kwasababu moto na moshi ni adui ya nyuki.

    Hata hivyo, mbinu hiyo ilishindwa kufua dafu na badala yake wakaazi ndio waliolazimika kutoroka.

    Aidha, walio majumbani wameonya kutotoka nje kwasababu ya hatari ya kuvamiwa na nyuki hao.

  3. Mwalimu muuaji wa Al-Shabab auawa kwa risasi

    Mwalimu na wanaume wengine wawili wameuawa kwa kikosi cha ufyatuaji risasi Somali baada ya kuhukumiwa kwa kosa la kutekeleza mauaji kwa niaba ya kundi la wanamgambo wa al-Shabab.

    Vifo vyao ni agizo la mahakama ya jeshi katika mji wa Mogadishu.

    Mohamed Haji Ahmed alikuwa mwalimu wa lugha ya Kiingereza katika chuo kikuu cha Mogadishu.

    Pia alikuwa muuaji aliyetumwa na al-Shabab – na alitekeleza mauaji ya maafisa wa ngazi ya juu serikalini.

    Pia alielezewa kama "muuaji asiye na huruma" – na kushutumiwa kwa kuwa mkuu wa kikosi cha eneo cha mauaji kilichoendeshwa na kundi la al-Shabab mjini Mogadishu na eneo la Benaadir.

    Pamoja na wanaume wengine wawili, aliuawa kwa kupigwa risasi Jumapili asubuhi.

    Mwanaume huyo, 27, alipatikana na hatia ya mauaji ya Jenerali Gen Abdullahi Mohamed Sheikh mwaka 2017, naibu mkuu wa sheria Mohamed Abdirahman Mohamud mwaka 2019 na jenerali polisi Mohamud Haji Alow baadaye mwaka huo.

    Soma taarifa zaidi:

  4. Matokeo ya uchaguzi Marekani 2020: Biden achagua timu ya wanawake tu ya habari na mawasiliano Ikulu

    Raia wa Marekani Joe Biden amechagua kikosi cha timu ya waandishi wa habari waandamizi yenye wanawake tu katika kile ambacho kinasemekana kuweka historia nchini humo.

    Timu hiyo itaongozwa na Kate Bedingfield, aliyekuwa naibu mkurugenzi wa mawasiliano wakati wa kampeni yake.

    Jen Psaki, ambaye alikuwa mkurugenzi wa mawasiliano wa Rais Barack Obama Ikulu, atakuwa waziri wa habari.

    Bwana Biden ameahidi kuwa na utawala wake unaojumuisha kila mmoja Marekani.

    "Ninafuraha kuwatangazia leo, timu ya mawasiliano Ikulu inajumuisha wanawake tu," Bwana Biden amesema katika taarifa.

    "Timu hii ya wanawake waliohitimu wenye uzeofu, inajumuisha kila moja na imejitolea kwa pamoja kujenga tena nchi hii."

    Watakao msaidia makamu rais Kamala Harris katika masuala ya habari na mawasiliano watakuwa ni Symone Sanders na Ashley Etienne.

    Tofauti na nafasi zingine katika baraza la mawaziri, ofisi hii ya habari na mawasiliano haihitaji kuthibitishwa na bunge la Seneti.

    Bwana Biden ataapishwa kuchukuwa rasmi majukumu ya rais Januari 20.

  5. Vikosi vya Tigray Ethiopia 'vyadungua ndege ya kivita'

    Eneo la kaskazini mwa Ethiopia la Tigray limesema kuwa vikosi vyake vimedungua ndege ya kivita ya serikali ya Ethiopia na kuteka marubani wanne huku vita vikiingia wiki ya nne, kulingana na kituo cha runinga kinachomilikiwa na Tigray.

    "Ndege ya kivita, MiG, iliyokuwa imetumwa na Waziri mkuu Abiy na rais wa Eritrean Isaias kuua watu wa Tigray imedunguliwa na vikosi vya Tigray na kuanguka karibu na eneo la katikati ya Tigray la Abiy Adi huku rubani akitekwa," kituo hicho cha televisheni kimesema.

    Waziri wa Ethiopia wa masuala ya demokrasia Zadrig Abraha ameambia kipindi cha BBC cha Newsday kuwa taarifa za kudunguliwa kwa ndege ya jeshi la Ethiopia sio za kweli.

    Mawasiliano katika eneo la Tigray yamekatizwa huku vyombo vya habari vikitegemea taarifa rasmi kutoka kwa pande zote mbili zinazopigana vita.

    Novemba 28, serikali kuu ilitangaza kuwa vikosi vyake vimetwaa mji wa Mekele baada ya wiki kadhaa za mapigano.

    Malefu ya watu inaaminika kuwa wamefariki dunia katika mapigano hayo huku wakimbizi karibu 43,000 wakitorokea Sudan.

    Soma zaidi:

  6. Somalia yamuita nyumbani balozi wake na kumfukuza wa Kenya

    Serikali ya Somalia imesema kuwa imemuita nyumbani balozi wake nchini Kenya Mohamud Ahmed Nur Tarzan, na kuishutumu nchi hiyo kwa kuingilia siasa za nchi yake.

    Somalia pia imemtaka balozi wa Kenya nchini Somalia kufunga virago "kwa ajili ya majadiliano".

    Somalia imeishutumu Kenya kwa kushinikiza serikali ya Jubbaland kukataa makubaliano ya uchaguzi yaliofikiwa Septemba 17, katika uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika mwezi ujao.

    "Serikali ya Somalia ilichukua uamuzi huo kulinda eneo lake la utawala baada ya kujitokeza kuwa Kenya inaingilia kimaksudi masuala ya Somalia eneo la Jubbaland," Mohamed Ali Nur, Waziri wa mambo ya nje wa Somalia amesema katika taarifa iliyotolewa.

    "Serikali] ya Somalia imeonesha kusikitishwa kwake na serikali ya Kenya kwa kuingilia moja kwa moja masuala ya ndani ya siasa za Somalia hatua ambayo inaweza kuchangia ukosefu wa uthabiti, usalama na maendeleo kwa eneo zima,” taarifa hiyo imesema.

    Kenya inaunga mkono utawala wa Ahmed Mohamed Islam maarufu kama "Madobe" huko Jubbaland, kwasababu ya maslahi yake ya kiusalama na kieneo.

  7. Papa Bouba Diop afariki dunia

    Aliyekuwa kiungo wa kati wa Senegal, Fulhama na Portsmouth Papa Bouba Diop amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 42.

    Diop alijitokeza mara 129 katika Ligi ya Premier na pia aliwahi kuchezea Uingereza katika timu za West Ham United na Birmingham City.

    Alichezea Senegal mwaka 2002 katika Kombe la Dunia na kufunga bao lililowafanya kuibuka na ushindi katika mechi ya ufunguzi baada ya Senegal kuichabanga Ufaransa bao moja kwa nunge.

    "Ukishakuwa shujaa wa Kombe la Dunia mara moja, siku zote unakuwa shujaa wa Kombe la Dunia," Fifa imeandika ujumbe huo katika mtandao wa kijamii.

    Ujumbe uliotumwa katika mtandao wa Twitter na klabu ya Fulham umesema kuwa klabu hiyo "umeshutushwa" na taarifa za kifo chake na pia wametumia jina la utani la Diop: "Lala salama, Wardrobe."

    Senegal ilifika robo fainali katika kombe la dunia la mwaka 2002 huku Diop akifunga mara mbili zaidi katika mechi ya makundi iliyotoka sare ya 3-3 na Uruguay.

    Pia amewahi kushiriki katika mashindano ya Kombe la Afrika ikiwemo wakati Senegal ipokuwa ya pili mwaka 2002. Diop alistaafu soka mwaka 2013.

  8. Museveni ashutumu wanasiasa wa upinzani kupotosha vijana

    Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameshutumu waandamanaji na wanasiasa wa upinzani kwa kuwapotosha vijana kujiingiza katika vitendo vya uhalifu.

    Bwana Museveni amesema wazo la kuwa mheshimiwa Bobi Wine akikamatwa kutakuwa na ghasia lisirejee tena.

    ‘’Hakuna mwanasiasa ambaye ana mamlaka kuliko sheria’’, Museveni alisema.

    Aliongeza kuwa wanasiasa wanalipa magenge ya uhalifu ambao wametangaza baadhi ya sehemu za mji wa Kampala eti hazitawaliki na hata kuvamia maafisa wa polisi wanaoshika doria.

    Bwana Museveni ameshutumu watu waliorekodiwa wakivamia maafisa wa usalama na waliokuwa wamevaa mavazi ya rangi ya njano inayoashiria chama tawala.

    ‘’Hili, halitawahi kutokea tena, kwasababu waliotekeleza hayo wameona matokeo ya kucheza na moto’’, amesema rais Museveni.

    Bwana Museveni pia alisema kuwa ajenda za wanasiasa wa upinzani ni kupata uungwaji mkono kutoka nje ya nchi ambao nia yao ni kukosesha uthabiti nchi ya Uganda.

    Rais Museveni aliongeza kuwa makosa makubwa ni wagombea urais walikiuka hatua zilizowekwa za kukabiliana na virusi vya corona na kutojali utekelezaji wa sheria.

    Pia, alitoa risala zake za rambirambi kwa raia wa Uganda waliopoteza wapendwa wao wakati wa ghasia hizo na kuongeza kwamba serikali itawalipa fidia.

    Bobi Wine anatafuta kumuondoa madarakani Museveni ambaye ametawala nchi hiyo kwa miaka 34 - katika uchaguzi utakaofanyika Januari 2021.

    Pia unaweza kusoma zaidi:

  9. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja, hii leo ikiwa ni tarehe 30/11/2020.