Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Tarehe ya kesi ya 'nabii' tajiri Shepherd Bushiri na mkewe yatangazwa

Mahakama ya juu zaidi nchini Malawi imepanga kusikiliza kesi ya Nabii milionea Shephard Bushiri na mke wake Mary tarehe 1 Disemba.

Moja kwa moja

Dinah Gahamanyi

  1. Mpaka hapa tumefikia mwisho wa matangazo ya moja kwa moja.Shukrani!

  2. Mahakama yapanga tarehe ya kesi ya Nabii Bushiri

    Mahakama ya juu zaidi nchini Malawi imepanga kusikiliza kesi ya Nabii milionea Shephard Bushiri na mke wake Mary tarehe 1 Disemba.

    Katika kesi hiyo waendesha mashitaka watakuwa wakipinga kuachiliwa huru bila masharti kwa

    Bushiri na mke wake ambao walikwepa kesi ya dhamana nchini Afrika Kusini na kutorokea katika nchi yao ya asili-Malawi wakidai kwamba walikuwa wanatishiwa maisha yao.

    Wanakabiliwa na mashitaka ya utakatishaji wa pesa na ufisadi nchini Afrika Kusini.

    Kibali cha kuwakamata kilitolewa na serikali ya Afrika Kusini kupitia ushirika wa polisi ya kimataifa-Interpol na wakajisalimisha kwa polisi nchini Malawi ambao waliwakamata na kuwaweka mahabusu kwa usiku mmoja.

    Walipelekwa katika mahakama ya hakimu mkazi mjini Lilongwe ambako waliachiliwa huru kwa misingi kwamba kukamatwa kwao hakukufuata utaratibu sahihi.

    Mwendesha mashitaka wa serikali alikuwa ameiomba mahakama iwaruhusu polisi kuendelea kuwashikilia wawili hao katika mahabusu kwa siku 30 zaidi, ili kuipatia muda serikali ya Afrika Kusini wa kuwasilisha rasmi ombi la kuwapeleka Afrika Kusini kukabiliana na kesi yao.

    Waendesha mashitaka wa Malawi wamekata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama.

    Unaweza pia kusoma:

    • Nabii Shepherd Bushiri: Mke wa muhubiri 'tajiri' Nabii Mary ni nani, na taarifa zaidi kuwahusu
    • Kasri ya Mchungaji milionea Bushiri na mkewe Mary imeshikiliwa
  3. Ethiopia 'yaanza awamu ya mwisho' ya mashambulio ya Tigray

    Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema kuwa vikosi vya shirikisho vimeanza awamu ya mwisho ya harakati zake za kijeshi katika jimbo la kaskazini mwa Ethiopia la Tigray.

    Katika taarifa yake, alisema wata "wajali sana " raia 500,000 wanaoishi katika mji mkuu wa jimbo hilo, Mekelle, na kuwaepusha na madhara wakati wa operesheni hiyo.

    Lakini Bw Abiy aliwatahadharisha raia wakae majumbani mwao.

    Alisema kuwa maelfu ya vikosi vya Tigray na wanamgambo walijisalimisha katika kipindi cha saa 72 zilizopita- lakini maafisa waTigray bado hawajajibu kuhusiana na madai hayo.

    Imekuwa vigumukuthibitisha madai kutoka pande hizo mbili kwasababu ya kuzimwa kwa mawasiliano.

    Bw Abiy alikuwa amevipatia vikosi vya Tigray muda wa saa 72 viwe vimejisalimisha, muda ambao uliisha Jumatano.

    Alikataa uingiliaji wa mataifa ya kigeni katika masuala ya ndani ya Ethiopia na akasema hali ya Tigray itatatuliwa kulingana na sheria na kanuni za kimataifa.

    Umoja wa Mataifa uliitaka serikali ya Ethiopia kuwalinda raia dhidi ya mashambulio dhidi ya Mekelle.

    Soma zaidi huhusu yanayojiri Ethiopia katika taarifa ifuatayo:

    • Mzozo wa Ethiopia: Waziri mkuu aamuru mashambulio dhidi ya mji wa Mekele
  4. Mwanaume adaiwa ‘kufufuka’ baada ya kufa Kenya

    Mwanaume mmoja kutoka Kaunti ya Kericho nchini Kenya amewashangaza wengi na kuibua gumzo mitandaoni baada ya kudaiwa kufufuka akiwa katika chumba cha maiti saa chache baada ya kupelekwa kwenye chumba hicho.

    Kwa mujibu wa mjomba wake Denis Langat, mwanaume huyo ambaye anajulikana kama Peter Kiplangat alipelekwa hospitalini Jumanne asubuhi baada ya kupoteza fahamu akiwa nyumbani lakini akathibitishwa kufa alipofikishwa hospitalini.

    Kulingana na mjomba wake, Peter alishituka na kupiga mayowe baada ya mhudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti kupasua sehemu ya paja, mojawapo ya mchakato ambao hufanywa kama njia moja ya kuuhifadhi mwili unapowekwa kwenye chumba cha maiti.

    Hapo ndipo mhudumu huyo alipokimbia na kumuita daktari.

    Akizungumza na waandishi wa habari katika kaunti ya Kericho, daktari mkuu wa Kapkat, Gilbert cheruiyot, amesema kuwa Denis Langat alifikishwa hospitalini akiwa amepoteza ufahamu, lakini jamaa zake walipoona kuwa wauguzi wanachukua muda kuwashughulikia, wakampeleka katika chumba cha mauti.

    "Wakati mhudumu wa chumba cha kuhifadhia waliona kwamba bado mgonjwa yuko hai, waliwaita wahudumu wengine waje wamzindue.

    Kwa sasa ndugu wa Denis Langat wanadai haki Kwa kuishutumu hospitali kutowajibika.

  5. Upasuaji wa ubongo mgonjwa akiwa macho wafanyika kwa mara ya kwanza kenya

    Nchini Kenya umefanyika upasuaji wa kwanza wa ubongo huku mgonjwa akiwa macho.

    Upasuaji huo umefanyika katika Hospitali ya-Nairobi Hospital, mjini Nairobi Kenya ambapo mgonjwa huyo alikuwa macho na kuweza kuzungumza wakati wote wa upasuaji huo.

    Madaktari wa upasuaji wanategemea mchakato wa kipekee a upasuaji unaomfanya mgonjwa awe macho, ambao bado ni hatari, lakini unaweza kuleta matokeo bora na kupunguza hatari ya jeraha katika ubongo.

    Katika aina hii ya tiba, madaktari bingwa wa upasuaji wa fuvu la kichwa wanaweza pia kufuatilia hali ya mgonjwa wakati wa upasuaji, hii ikimaanisha kuwa wanaweza kuondoa uvimbe ambao kwa kawaida usingeweza kutolewa salama.

    Upasuaji huo wa kufungua fuvu la kichwa au 'brain craniotomy', kwa lugha ya kitaalamu unaangaliwa kama mafanikio makubwa katika sekta ya tiba kuweza kufanyika nchini Kenya.

  6. Waziri mkuu wa zamani wa Sudan afariki kwa virusi vya corona

    Waziri Mkuu wa zamani wa Sudan Sadiq al-Mahdi amefariki dunia kutokana na ugonjwa wa corona wiki tatu baada ya kulazwa hospitalini kwa katika Muungano wa nchi za kiarabu(UAE), kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na familia yake na kutoka chama chake cha Umma-National Umma Party.

    Alilazwa baada ya watu 21 wa familia ya al-Mahdi kupata maambukizi ya virusi vya corona mapema mwezi wa Novemba.

    Al-Mahdi ambaye amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 84- alikuwa Waziri Mkuu hadi 1989 wakati alipopinduliwa katika mapinduzi na Rais Omar al-Bashir.

  7. Mwanasiasa wa Uganda afungwa jela kwa kuwaita majaji 'wapumbavu'

    Mahakama ya juu nchini Uganda imemuhukumu kifungo cha jela mgombea wa zamani wa urais kwa kutumia lugha ya matusi dhidi ya majaji , ikiwa ni pamoja na kuwaita majaji "Wapumbavu wasio na uwezo wa kazi yao".

    Ivan Samuel Ssebadduka alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kwa kuidharau mahakama, kulingana na taarifa za vyombo vya habari nchini humo.

    Mwezi Sempemba Bw Ssebadduka alikuwa amepeleka ombi latika mahakama ya juu akitaka kusimamishwa kwa kigezo cha mgombea wa urais kukusanya kura za uteuzi.

    Pia alitaka kuahirishwa kwa sheria za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona zilizokuwa zimewekwa na wizara ya afya katika mikutano ya kampeni.

    Alitumia maneno hayo ya matusi alipokuwa akitetea ombi lake mbele ya majaji.

    Hakimu mkuu wa mahama kuu nchini Uganda Alfonse Owinyi-Dollo alinukuliwa akisema kuwa ukosoaji dhidi ya majaji unapaswa kuwa sahihi na wa haki na haupaswi kukiuka haki za watu wengine:

  8. Polisi wa Uganda waizingira hoteli ya Bobi Wine

    Police nchini Uganda wameizingira hoteli ambayo mgombea wa urais nchini humo Robert Kyagulanyi, al maarufu Bobi Wine, katika mji wa Hoima magharibi mwa Uganda ambako ndiko alipo na maafisa wake wa kampeni.

    Bobi ametuma ujumbe wake wa twitter akisema kuwa alilazimika kutumia njia ndefu kufika mjini humo baada ya wanajeshi kufunga barabara ambayo alitarajia kutumia.

    "Wametufuata kwenye hoteli yetu na kuizingira ," alitweet.

    Televisheni ya Uganda NTV alitweet ujumbe kuwa " lengo la operesheni hiyo bado halijajulikana ".

    Bobi Wine alituma picha za polisi wakiwa nje ya hoteli alimokuwa:

    Gazeti la Uganda Daily Monitor lilitweet kuwa Bobi Wine alikuwa amekataliwa kuingia katika mji huo ambako alikuwa amealikwa kama mgeni katika kipindi cha redio.

    Wagombea katika uchaguzi ujao wameambiwa wafanye kampeni zao kwa njia ya vyombo vya habari na kuepuka mikusanyiko mikubwa ya watu kwasababu ya virusi vya corona

    Wiki iliyopita Bobi Wine alikamatwa kwa kukiuka sheria za kuzuwia virusi vya corona.

  9. Mtanzania Gabriel Laizer awa bilionea baada ya kupata madini ya thamani kubwa

    Mchimbaji mdogo wa madini kutoka kata ya Mndalala wilayani Longido ameibuka bilionea baada ya kupata madini ya rubi yenye thamani ya shilingi bilioni 1.7 .

    Akieleza historia ya uchimbaji wa madini hayo bilionea, Gabrielb Laizer amesema ana miaka minne na nusu tu tangu alipoanza shughuli hiyo na hawajawahi kufanikisha kupata madini kama hayo wakati mwingine.

    ‘’Ninachotaka kusema ni kumshukuru rais wetu John Pombe Magufuli kwa jitihada zake na nia yake njema ya kuamini kuwa sisi Watanzania tunaweza kufanya kazi ambayo wazungu walikua wanafanya. Na kupitia imani hiyo tunadhihirisha leo kwa vitendo kwamba tunaweza kufanya kazi na lakini pia tunakua wazalendo, kuhakikisha kwamba kile ambacho kinapatikana kinafanyika katika hali ya uaminifu bila utoroshaji ili kuhakikisha kwamba mapato yote yatokanayo na madini haya yanakwenda kumnufaisha kila Mtanzania’’, amesema Gabriel Sendeu Laizer.

    Sendeu anakuwa Bilionea anayeingia kwenye rekodi Tanzania katika kipindi cha mwaka mmoja akitanguliwa na Saniniu Laizer ambaye alipata madini ya Tanzanite na kuibuka Bilionea.

  10. Hujambo na katibu tena kwa matangazo yetu mubashara leo tarehe 26.11.2020