Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Benki Kuu ya Tanzania yachukua usimamizi wa Benki ya China
Benki Kuu ya Tanzania imetangaza kuchukua usimamizi wa Benki ya Biashara China
Moja kwa moja
Asha Juma
Matokeo ya uchaguzi Marekani 2020: Timu ya Trump yataka kura za Wisconsin kuhesabiwa tena
Rais Donald Trump anataka kura za Wisconsin zihesabiwe tena ambako mpinzani wake Joe Biden anatabiriwa kushinda kwa kura 20,000.
Saa kadhaa kabla ya siku ya mwisho ya kuwasilisha malalamishi Jumatano kufika, timu ya kampeni ya Trump inataka kura za kaunti ya Milwaukee na Dane zihesabiwe tena.
Bwana Trump amekuwa akidai kwamba kulikuwa na wizi wa kura na kukataa kumkabidhi mwenzake rasmi madaraka.
Bwana Biden amesema hatua ya kuchelewa kukabidhi madaraka itaathiri zaidi kukabiliana na janga la virusi vya corona.
Timu ya kampeni ya Trump imewasilisha kesi kadhaa kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais katika majimbo muhimu ingawa maafisa wa uchaguzi wanasema hakuna ushahidi wowote unaoonesha uchaguzi ulikumbwa na udanganyifu.
Hata hivyo, licha ya ukosefu wa ushahidi, karibu nusu ya wapiga kura wa Republican wanaamini madai ya rais ya wizi wa kura ni ya kweli, kulingana na kura ya maoni ya shirika la habari la Reuters
Rais mteule Joe Biden wa chama cha Democrat inakadiriwa kuwa alishinda uchaguzi huo kwa zaidi ya kura milioni 5.6.
Upande wa kura za wajumbe zenye kuamua nani ndiyo anayeibuka na ushindi, Joe Biden amepata kura 306 huku Donald Trump akipata kura 232.
Msumbiji: Watu 500,000 watoroka makazi yao kwasababu ya wanamgambo wa Kiislamu
Wanamgambo wa Kiislamu Msumbiji wasababisha watu 500,000 kuhama makazi yao
Waziri Mkuu wa Msumbiji Carlos Agostinho do Rosario amesema watu zaidi ya 500,000 wamelazimika kuhama makazi yao kwasababu ya wanamgambo wa Kiislamu katika eneo lenye utajiri wa gesi kaskazini mwa mkoa wa Cabo Delgado.
Jumatano , waziri huyo ameliambia bunge kuwa raia wa Msumbiji waliotafuta hifadhi nchi jirani ni pamoja na wa maeneo ya Niassa, Nampula, Zambézia, Sofala na Inhambane.
Serikali ilikuwa imetenga kitengo chake cha kutoa msaada wa dharura kwa raia hao.
Benki Kuu ya Tanzania yachukua usimamizi wa Benki ya China
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Aboubakar Famau
- Nafasi, BBC News, Dar es Salaam
Benki Kuu ya Tanzania imetangaza kuchukua usimamizi wa Benki ya Biashara China ambayo ina tawi lake jijini Dar es Salaam nchini Tanzania kuanzia leo Novemba 19, 2020.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema hii leo jijini Dodoma, gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Florens Luoga amesema kutokana na mamlaka aliyopewa ya sheria za benki na taasisi za fedha, Benki Kuu imeamua kuchukua usimamizi wa Benki hiyo ya China baada ya kushindwa kukidhi masharti ya kuwa na akiba ya kutosha ili kuweza kuendesha shughuli za kibenki.
Benki hiyo hivi sasa itakuwa chini ya uangalizi wa Benki Kuu ya Tanzania kwa muda wa siku 90, huku bodi yake ya wakurugenzi pamoja na menejimenti ikisimamishwa na huduma zote kwa wateja kusitishwa.
Mzozo wa Ethiopia:Maelfu watoroka vita Tigray, UN
Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa limeiambia BBC kuwa maelfu ya raia wanaendelea kukimbilia nchini Sudan wakitoroka vurugu zinazoendelea kundirima kaskazini mwa Ethiopia eneo la Tigray.
Mwakilishi wa Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) nchini Sudan, Axel Bisschop, amesema wengi wao ni familia zinazotoroka ghasia na wanatembea kwa miguu kwasababu hali katika eneo la Tigray inaendelea kuwa ya hatari zaidi.
Hata hivyo Ethiopia imekanusha madai kuwa inalenga raia wasio na hatia wakati ambapo inaendelea na kampeni yake dhidi ya chama cha Tigray People's Liberation Front (TPLF).
Vikosi vya serikali vimesema vinaendelea kuingia katika mji wa Mekelle, ingawa imekuwa vigumu kuthibitisha taarifa hizo kwasababu ya kukatizwa kwa mawasiliano.
Hadi kufikia sasa, zaidi ya raia 30,000 wamevuka mpaka na kuingia nchini Sudan.
Siku ya choo duniani:Je waweza kutumia choo hiki cha vioo?
Moja ya maeneo maarufu nchini Japani umeongeza kivutio kisicho cha kawaida ambacho ni vyoo vya umma angavu.
Mbunifu wa vyoo hivyo ambaye pia ni mhandisi Shigeru Ban, amesema vyoo hivyo ambavyo unaweza kuona mwenzio anachofanya upande wa pili au akiwa ndani vimewekwa mji wa Shibuya wenye watu wengi.
Ingawa hilo linaonekana kama kuvuka mipaka ya utamaduni hivi, lengo ni kubadilisha mitazamo ya watu kuhusu vyoo vya umma.
Mbunifu Shigeru ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya Pritzker amesema katika taarifa "Vyoo angavu vimewekwa katika bustani mbili za Shibuya, ya - Yoyogi Fukamachi na Haru-no-Ogawa.
"Kuna mawili yanayotutia wasiwasi, wakati unaingia choo cha umma, hasa vilivyo maeneo ya bustani," amesema kwenye tovuti rasmi ya mradi huo, "Kwanza ni usafi, na pili ni ikiwa kuna mtu ndani au la."
Ubunifu wa Shigeru Ban unatoa ufumbuzi wa matatizo hayo mawili baada ya utengenezaji wake wa vyoo ambayo ukuta wake ni kioo - kwanza mtu anaweza kuona kinachoendelea ndani akiwa nje.
"Hili linamruhusu mtu kuangalia kama choo ni kisafi na iwapo kuna mtu anayekitumia," taarifa hiyo imesema. "Usiku, vyoo hivyo vinatoa mwanga wa kuvutia kama taa ya kandili."
Maelezo zaidi:
Baraza la mawaziri Zanzibar 2020: ACT hawajawasilisha jina la makamu wa rais
Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussen Mwinyi ametangaza baraza la mawaziri hii leo na kuainisha kuwa, wapinzani hawapo katika baraza hilo kwa kuwa hawajawakilisha majina yao baada ya kuwaandikia barua.
"Tuliwaandikia barua ili walete jina la kwanza la makamu wa rais kwa mujibu wa katiba kwa kuwa walipata zaidi ya asilimia 10 lakini hawajafanya hivyo mpaka sasa.
Rais Mwinyi alieleza kuwa kuna nafasi mbili ambazo zipo wazi na wanatoa muda kikatiba ili kusubiri endapo wataleta majina hayo, kwa kuwa hata wabunge wao hawajaapishwa.
Aidha alisisitiza kwamba hata wakati wa kampeni nia yake ilikuwa ni kuleta umoja Zanzibar na hicho ndio anataka kukifanya.
"Wakati wa kampeni nilisema, tunataka Wazanzibari kuwa pamoja".
Uchaguzi Uganda 2021:Watu saba wafariki dunia wakidai kuachiliwa huru kwa Bobi Wine
Idadi ya waaandamanaji waliofariki dunia wakati wa maaandamano ya Jumatano ya kupinga kukamatwa kwa Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, imeongezeka na kufikia saba, polisi imesema.
Msemaji amezungumza na BBC Alhamisi asubuhi na kusema kuwa zaidi ya waandamanaji 40 walijeruhiwa katika makabiliano na polisi.
Shirika la Msalaba Mwekundu Uganda linasema kuwa wafanyakazi wake waliwasaidia watu 11 waliokuwa na majeraha ya kupigwa risasi.
Wakati huohuo, upinzani umesitisha kampeni zake kushinikiza kuachiliwa huru kwa Bobi Wine.
Waliokuwa majenerali wa jeshi Mugisha Muntu na Henry Tumukunde pia wametaka polisi kusitisha unyanyasaji dhidi ya wagombea urais wa upinzani na raia.
Polisi imesitisha matukio kadhaa ya kampeni ya wagombea wa upinzani.
Bobi Wine alikamatwa katika mkutano wake wa kampeni mashariki mwa Uganda.
Polisi walimbeba Bobi Wine na kumuweka kwenye gari lao wakidai kuwa amevutia umati mkubwa wa watu zaidi ya 200, kuliko idadi iliyopendekezwa na Tume ya Uchaguzi kama njia moja ya kukabiliana na virusi vya corona.
Mawakili wa Bobi Wine wanasema bado mteja wao hajafikishwa mahakamani.
Soma zaidi:
Rais Cyril Ramaphosa anafuatilia kujua aliyemtorosha Nabii Bushiri milionea
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema kuwa kutoroka kwa Nabii wa Malawi na mke wake nchini humo ni jambo ambalo analifuatilia kwa karibu na ameahidi kuchukua hatua baada ya kupata taarifa za kina.
Nabii Shepherd Bushiri na mke wake Mary, wanakabiliwa na mashtaka ya ulaghai na utakatishaji wa fedha nchini Afrika Kusini.
Wawili hao walitoroka nchini Afrika Kusini wiki liyopita na kujiwasilisha kwa polisi nchini Malawi baada ya Afrika Kusini kutoa kibali cha kukamatwa kwao.
Kupitia televisheni ya eneo, Rais Ramaphosa amesema tukio la wawili hao kutoroka "halikutakiwa kutokea".
"Bila shaka tutachukua hatua," Rais alijibu alipoulizwa ikiwa serikali inapanga kufanya lolote.
Baadhi ya taarifa zinasema kuwa muhubiri huyo aliyejitangaza mtume pamoja na mke wake walitoroshwa nchi humo kwa njia haramu na genge la watu ambalo linahusika na uuzaji wa magari yaliyoibwa nchini Afrika Kusini na kupelekwa Malawi.
Pia kuna baadhi ya vyombo vya habari Afrika Kusini vilivyosema kuwa nabii huyo alitoroka kwa kutumia ndege ya rais.
Hata hivyo serikali zote mbili zimekanusha madai hayo.
Soma zaidi:
Marekani yashutumu vurugu zilizotokea Uganda baada ya kukamatwa kwa Bobi Wine
Marekani imeshutumu ghasia zilizojitokeza katika mji mkuu wa Kampala na miji mingine nchini Uganda kufuatia kukamatwa kwa mgombea wa urais Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine.
Ujumbe wa Marekani umesema kuwa "pande zote zipinge vita" na kuchukua hatua za kupunguza wasiwasi uliotanda nchini humo.
Bobi Wine alikamatwa wakati wa mkutano wa kampeni kwa madai ya kukiuka miongozo ya kukabiliana na virusi vya corona iliyowekwa na Tume ya uchanguzi.
Hata hivyo, muda mfupi baadaye wafuasi wake walianza maandamano wakidai aachiliwe huru.
Polisi wamesema watu watatu waliuawa huku wengine 34 wakijeruhiwa.
Uganda itafanya uchaguzi wa urais mnamo mwezi Januari 2021.
Pia unaweza kusoma:
Uchaguzi Uganda 2021:Wagombea urais wa upinzani Uganda wasitisha kampeni, huku watu watatu wakiwa wameuawa
Wagombea urais kutoka vyama vya upinzani nchini Uganda wamesema kuwa wanasitisha kampeni zao hadi pale mgombea mwenzao Robert Kyagulanyi maarufu Kama Bobi Wine atakapoachiwa huru.
Wagombea hao wamesema ni vigumu kwao kuendelea na kampeni huku mgombea mwingine akiwa anaendelea kunyanyaswa na polisi kwa madai yasiyo na msingi.
Bobi Wine alikamatwa jana Jumatano Mashariki mwa eneo la Luuka baada ya polisi kumshtumu kwa kosa la kusababisha mikusanyiko ya watu ikiwa ni uvunjaji wa miongozo ya kukabiliana na virusi vya corona iliowekwa na Tume ya Uchaguzi.
Na punde tu baada ya wafuasi wake kupata taarifa, walianza kuandamana wakidai aachiliwe huru.
Hata hivyo polisi imethibitisha kuwa watu watatu waliuawa wakati wa makabiliano kati yao na wafuasi wa Bobi Wine.
Taarifa ya polisi haikusema watu hao wamefariki vipi ingawa video na picha zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilikuwa zinaonesha watu waliotapakaa damu huku wengine wakioneshwa kutoweza kufanya lolote yaani wamepigwa risasi na kufariki dunia.
Aidha, taarifa ya polisi inasema watu 34 walijeruhiwa katika maandamano hayo.
Mgombea mwingine, Patrick Amuriat Oboi, pia amekamatwa.
Mikutano ya kampeni ya Bobi Wine imekuwa ikizuiwa na polisi katika matukio kadhaa.
Uganda itafanya uchaguzi wa urais Januari na hadi kufikia sasa polisi imekuwa ikihakikisha miongozi ya kukabiliana na janga la corona inatekelezwa.
Soma maelezo zaidi:
Hujambo na karibu katika matangazo ya moja kwa moja hii leo ikiwa ni tarehe 19/11/2020.