Maxence Melo:Mwanzilishi wa Jamii Forums akutwa na hatia, aachiwa kwa masharti

Mwasisi wa mtandao wa Jamii Forums nchini Tanzania, Maxence Melo amekutwa na hatia katika shtaka la kuzuia uchunguzi wa polisi hata hivyo ameachiwa kwa sharti la kutokutenda kosa kama hilo kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Moja kwa moja

Asha Juma

  1. Na hadi kufiki hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu ya moja kwa moja kwa hii leo. Panapo majaaliwa tukutane tena hapo kesho.

  2. Mwanamuziki Tshala Muana wa DR Congo ameachiliwa huru

    Mwanamuziki maarufu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Tshala Muana ameachiliwa huru.

    Awali, vyanzo vya kiintelijensia nchini humo vilithibitisha kuwa Tshala Muana amekamatwa.

    Inasemekana kuwa wimbo alioutoa hivi karibuni kwa jina, 'kukosa shukrani' ndio chanzo cha masaibu yake.

  3. China:Marufuku kutembea na mbwa hadharani

    Picha ya mwanamke akitembea na mbwa China

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kaunti moja nchini China huko Yunnan imelazimika kufikiria tena sera ya kupiga marufuku wakazi wa eneo hilo kutembea na mbwa katika maeneo ya umma kuanzia Novemba 20.

    Taarifa hiyo imesema, yeyote atakayekutwa anatembea na mbwa hadharani mara tatu, mbwa wake atachukuliwa na mamlaka na kuuawa.

    Maafisa wamesema hiyo ni hatua ya kulinda wakazi kwasababu kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya mbwa kuuma watu.

    Hata hivyo, sera hiyo imekasirisha watu katika mitandao ya kijamii huku maafisa wakisema huenda "wakafikiria tena" hatua hiyo.

    Taarifa hiyo inasema kuanzia Novemba 13, itakuwa ni lazima kwa wamiliki wote kusalia na mbwa wao nyumbani muda wote.

    Pia imeongeza kwamba sera hiyo inatoa muongozo mzuri wa kuishi na mbwa.

  4. Shirika la reli Kenya laagizwa kuwalipa fidia waliokuwa wafanyakazi wake miaka 25 baadaye

    Mahakama moja mjini Nairobi Kenya, imeagiza Shirika la Kenya Railways kulipa mamia ya mamilioni ya pesa kama malimbikizi ya mshahara kwa waliokuwa madereva wa treni wa shirika hilo wakati huo.

    Ingawa mahakama hiyo haikusema ni pesa ngapi shirika hilo inatakiwa kuwalipa, waliokuwa wafanyakazi wao takriban 197 walikuwa wanataka kulipwa fidia ya shilingi milioni 429 katika nyongeza ya mshahara wao kesi ambayo imekuwa ikiendelea kwa kipindi cha miaka 25.

    Jaji wa mahakama ya kushughulikia masuala ya wafanyakazi na ajira Maureen Onyango imeipa shirika hilo hadi Decemba 16, 2020, kulipa wafanyakazi hao pamoja na riba yao kuanzia Mei 2009 hadi mshahara wao utakapo malizika kulipwa.

    Kesi hiyo iliwasilishwa na chama cha wafanyakazi wa reli mwaka 1995.

  5. Twiga mweupe duniani awekewa kifaa cha kumfuatilia

    Twiga mweupe pekee duniani

    Chanzo cha picha, Hirola Conservancy

    Twiga mweupe duniani huko kaskazini mashariki mwa Kenya amewekewa kifaa cha kumfuatilia, wahifadhi mazingira wanasema.

    Twiga huyo alisalia peke yake baada ya wawindaji haramu kumuua twiga wa kike na mtoto wake wa rangi hiyo hiyo mnamo mwezi Machi katika kaunti ya Garissa nchini Kenya.

    Twiga mweupe pekee duniani

    Chanzo cha picha, Hirola Conservancy

    Kifaa hicho kimewekwa katika moja ya pembe zake ambacho kinatoa taarifa za eneo alipo kila baada ya saa moja.

    Hatua hiyo itawezesha wahudumu kufuatilia mienendo yake na kumlinda dhidi ya wawindaji haramu.

  6. Zaidi ya Wakenya milioni moja waliambukizwa corona, Utafiti

    Watu waliovaa barakoa

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Zaidi ya watu milioni moja nchini Kenya walikuwa wameambukizwa virusi vya corona kufikia mwezi Juni, utafiti umebainisha.

    Idadi ni kubwa ikilinganishwa na takwimu kutoka serikalini zilizotolewa wakati huo.

    Utafiti huu ulifanywa na wanasayansi kutoka taasisi ya utafiti wa matibabu, KEMRI.

    Wanasayansi walikagua sampuli za damu zilizokusanywa na shirika la taifa la kukusanya damu kati ya mwezi wa Aprili na Juni na kuonesha kuwa zaidi ya asilimia nne ya Wakenya walikuwa na kinga ya mwili au antibodies inayoonyesha watu hao walikuwa na virusi hivi na kupona.

    Wiki sita baada ya kisa cha kuanza cha corona kutangazwa nchini Kenya, watu zaidi ya elfu tatu walichangia kutoa damu.

    Damu hii ilikuwa itumike kusaidia watu waliohitaji kuongezwa damu wakati huu wa janga la covid-19.

    Mtu akitoa damu

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Watafiti wanasema hakuna aliyeripoti kuwa na dalili sawa na zile za corona.

    Wanasayansi kutoka taasisi ya KEMRI walikaugua damu hizo na kupata kuwa mtu mmoja kati ya Wakenya 25 walikuwa wameambukizwa virusi – walipona na wengi wao hawakujua hali zao.

    Utafiti huo unaonesha kuwa asilimia nane ya watu hawa walikuwa wanatoka katika maeneo ya Mombasa na Nairobi.

    Wataalam wa Afya katika taasisi hiyo wanasema kuwa utafiti huu unonesha Kenya ilifikia kilele chake cha kwanza cha maambukizi ya Covid-19 mapema zaidi kuliko ilivyofikiriwa hapo awali.

    Mataifa ya Msumbiji na Malawi ni miongoni mwa nchi za bara Afrika ambazo zimefanya utafiti wa aina hii.

    Kwa sasa, zaidi ya watu 65,000 wamepatikana kuwa na virusi vya corona huku wengine wapatao elfu moja mia mbili wakipoteza maisha yao nchini Kenya.

  7. Maxence Melo:Mwanzilishi wa Jamii Forums akutwa na hatia, aachiwa kwa masharti

    max

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mwasisi wa mtandao wa Jamii Forums nchini Tanzania, Maxence Melo amekutwa na hatia katika shtaka la kuzuia uchunguzi wa polisi hata hivyo ameachiwa kwa sharti la kutokutenda kosa kama hilo kwa kipindi cha mwaka mmoja.

    Bwana Melo pamoja na mwanzilishi mwenza wa mtandao wa Jamii Forums BwMike Mushi walifuguliwa kesi yenye mashtaka mawili mwaka 2016 katika Mahakama ya Kisutu. Kosa la kwanza likiwa ni kuendesha mtandao ambao haujasajiliwa kwa kikoa (domain) cha Tanzania (.tz) na shitaka la pili la kuzuia uchunguzi wa polisi kwa kutokutoa taarifa za waachama wawili wa mtandao huo waliodaiwa kuandika madai ya uhalifu kuhusu benki ya CRDB na Mamlaka ya Bandari nchini Tanzania.

    Kwa mujibu wa wakili wa wawili hao Bw Benedict Ishabakaki, Melo amekutwa na hatia ya shtaka la pili la kuzuia uchunguzi, huku Mike Mushi akikutwa hana hatia katika mashtaka yote mawili.

  8. Urusi inapanga kujenga kambi ya jeshi lake Sudan

    Urusi kuanzisha kambi ya jeshi Sudan katika pwani ya Bahari Nyekundi.

    Chanzo cha picha, AFP

    Rais wa Urusi Vladimir Putin ameidhinisha kuendelezwa kwa makubaliano na Sudan ya kuanzishwa kwa kambi ya jeshi katika pwani ya Bahari Nyekundi.

    Urusi inapanga kujenga kituo cha usafirishaji na ukarabati kwa jeshi lake la majini ambacho kitakuwa na wafanyakazi wasiozidi 300.

    Rasimu ya makubaliano ya kambi hiyo itakuwa viungani mwa kaskazini mwa Bandari ya Sudan.

    Wachambuzi wanasema, Urusi imeongeza shughuli zake Afrika katika miaka ya hivi karibuni hatua inayochukuliwa kama njia moja ya kupunguza ushawishi wa China na Marekani barani humo.

  9. Ethiopia iko tayari kupokea wakimbizi waliotoroka Tigray

    Wakimbizi wakivuka mto Setit mpaka wa Sudan na Ethiopia

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema kuwa nchi yake iko tayari kupokea na kuwashika mkono maelfu ya watu wanatoroka makazi yao kwasababu ya mapigano yanayoendelea kaskazini mwa nchi hiyo eneo la Tigray.

    Umoja wa Mataifa umesema kuwa karibu watu elfu 20 huenda wamevuka mpaka na kuingia nchi jirani ya Sudan katika kipindi cha siku 10 zilizopita.

    Habari za hivi karibuni zasema jeshi la Ethiopia limechukua udhibiti wa eneo la kimkakati la Alamata.

    Kikosi maalum cha Tigray wakati wa sherehe ya Mekelle Februari 19, 2020.

    Chanzo cha picha, AFP

    Upande mwingine, chama cha Tigray People’s Liberation Front - TPLF kimeshtumu serikali kwa kufanya mashambulio ya anga katika mji wa Mekelle.

    Hata hivyo imekuwa vigumu kuthibitisha madai yote hayo kwasababu umeme na mawasiliano yamekatwa katika eneo hilo.

    Ethiopia imekataa wito wa kufanyika kwa mazungumzo na kusisitiza kuwa hatua hiyo itaendeleza uvunjaji wa sheria licha ya kuwa maelfu ya raia wanatorokea Sudan.

    Waziri Mkuu Abiy ameahidi amani na kuunga mkono wale wanaorejea nchini humo lakini bado haifahamiki ikiwa hilo linaweza kufikiwa vipi wakati mapigano yanaendelea.

    Maelezo zaidi:

  10. Mwanamuziki wa DR Congo Tshala Muana akamatwa

    Huu ni mwaka 1993 Tshala Muana, na mwanamuziki huyu ameshinda kadhaa za kimataifa

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Vyanzo vya kiintelijensia vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vimethibitisha kuwa mwanamuziki maarufu nchini humo Tshala Muana amekamatwa.

    Hadi kufikia sasa familia ya msanii huyo bado haijatoa taarifa yoyote lakini vyanzo vya habari nchini humo vinasema kwamba alikamatwa hapo jana majira ya mchana.

    Hivi karibuni mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 62 ametoa wimbo kwa jina, 'kukosa shukrani' ambao inaaminika kuwa ndio chanzo cha masaibu yake.

    Mashairi ya wimbo huo yanaashiria mtu ambaye hakutajwa kwa jina alipewa mazingira mazuri yakumuwezesha maishani lakini amesahau kurejesha wema baada ya kuingia madarakani.

    Wengi wanaamini kuwa mwanamuziki huyo ambaye ni mshindi wa tuzo mbalimbali anamzungumzia rais Felix Tshisekedi -lakini Tshala Muana bado hajathibitisha hilo.

    Tshala Muana alikuwa karibu sana na familia ya aliyekuwa rais wa Congo Joseph Kabila.

  11. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja hii leo ikiwa ni tarehe 17/11/2020.