Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Rais Magufuli: Cheo cha Waziri Mkuu hakina ‘uhakika’

Rais wa Tanzania John Magufuli amemuapisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa awamu ya pili na kumtahadharisha kuwa nafasi yake haina uhakika wa kuwa nayo kwa miaka mitano.

Moja kwa moja

Asha Juma

  1. Na hadi kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu ya moja kwa moja kwa hii leo. Asante kwa kuwa nasi.

  2. Museveni afuta ujumbe wa Twitter unatoa wito wa mazungumzo Ethiopia

    Rais wa Uganda Yoweri Museveni amefuta ujumbe aliosema kuwa ni lazima kuwe na majadiliano juu ya mzozo wa kaskazini mwa Ethiopia "unaosababisha watu kupoteza maisha yao bila sababu na kuzorotesha uchumi".

    Ujumbe wake umewadia baada ya kukutana na aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Ethiopia Demeke Mekonnen nchini Uganda.

    Hata hivyo ujumbe huo sasa hivi umefutwa.

    Hadi kufikia sasa hakuna taarifa yoyote inayoelezea kwanini ujumbe huo umefutwa huku serikali ya Ethiopia ikikataa wito wa kufanyika kwa mazungumzo na chama cha Tigray People's Liberation Front (TPLF).

    Awali, serikali ya Ethiopia ilikanusha madai kuwa Bwana Museveni atakuwa mpatanishi kati ya serikali na chama cha TPLF.

    Bwana Museveni alisema mazungumzo yake na Bwana Demeke "yaliangazia zaidi amani na masuala ya kiusalama yanayoathiri Ethiopia kwa sasa".

    Pia unaweza kusoma:

  3. Njiwa Kim kutoka Ubelgiji auzwa kwa euro milioni 1.6

    Njiwa wa kike aliyepewa jina la Kim mwenye umri wa miaka miwili ameweka rekodi ya dunia kwa kuuzwa kwa bei ya juu zaidi.

    Awali, thamani ya njiwa Kim ilikuwa euro 200 pekee lakini baada ya mnada uliohusisha raia wawili wa China akauzwa kwa euro milioni 1.6.

    Kurt Van de Wouwer, familia iliyomlea njiwa huyo, ilishtuka baada ya kupata taarifa hizo, kulingana na Shirika la Habari la Reuters.

    Rekodi ya awali iliwekwa na njiwa wa kiume Armandoaliyeuzwa kwa euro milioni 1.25.

    Njiwa Armando aliyepewa jina la utani la "Lewis Hamilton" baada ya mashindano ya dunia ya Formula 1, alistaafu na tayari ameshazalisha njiwa wengine alipokuwa anauzwa mwaka 2019.

    Njiwa Kim aliwahi kushinda mashindano mengine mwaka 2018 ikiwa ni pamoja na mbio za masafa ya kati.

  4. Diamond Platinumz na Zuchu wang’ara katika Tuzo za AFRIMMA

      • Author, Roncliffe Odit
      • Nafasi, BBC Nairobi

    Msanii wa Bongo Flava na Rais wa kundi la WCB Wasafi Diamond Platinumz ndiye mshindi wa mwaka huu wa Tuzo za AFRIMMA.

    Diamond kutoka Tanzania ameshinda kitengo cha msanii bora wa Afrika Mashariki, na kumrambisha sakafu mtani wake wa jadi Alikiba pia kutoka Tanzania.

    Wengine ni pamoja na Eddy Kenzo wa Uganda, Mbosso na Rayvanny (wote wa kundi wa WCB Wasafi), Harmonize wa Tanzania pamoja na waKenya Khaligraph Jones na Otile Brown.

    Tuzo za AFRIMMA husherehekea muziki wenye asili ya Afrika, ikiwemo mitindo ya Bongo Flava, Afrobeats, Genge, Kwaito, Lingala na Soukous miongoni mwa mitindo mingine.

    Tuzo za mwaka huu zilitangazwa mubashara katika ukurasa wa YouTube wa AFRIMMA kutoka jijini Dallas, Marekani.

    Tuzo hizo zilishuhudia msanii wa karibuni zaidi kusainiwa na lebo ya WCB Wasafi, Zuchu, akitwaa Tuzo la Msanii Bora Mpya.

    Akizungumzia ushindi wake, Zuchu amewashukuru sana mashabiki wake, na kutoa shukran za kipekee kwa bosi wake Diamond Platinumz ambaye anasema amechangia pakubwa katika ufanisi wake.

    Hii tuzo ni yetu mimi na mashabiki zangu na wasichana wote wanaonitazama kama mfano hii ni tuzo yetu. MY FAMILY I love you so much mamangu wewe ndo icon na role model wangu AM BOWING DOWN TO YOU MY QUEEN. TO my management, thank you so much for investing in me, kuwekeza kwangu ikawe mfano wa kuendelea kusapoti wasichana muwaamini kwamba wanaweza sana #WCB4life. Diamond Platnumz the hero of all time, this award goes to you GOAT. NOBODY FIGHTS FOR ME LIKE YOU,’ aliandika Zuchu.

    Hata hivyo msanii wa Afrika Kusini Master KG wa wimbo Jerusalema alikuwa ndiye nyota wa tuzo za AFRIMMA mwaka huu baada ya kushinda tuzo 4 ikiwa ni pamoja na Msanii Bora wa Mwaka, Wimbo Bora wa Mwaka, Msanii Bora wa Kiume Afrika Kusini na Collabo Bora ya Mwaka.

  5. Rais Magufuli: Cheo cha Waziri Mkuu hakina ‘uhakika’

    Rais wa Tanzania John Magufuli hii leo amemuapisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa awamu ya pili na kumtahadharisha kuwa nafasi yake haina uhakika wa kuwa nayo kwa miaka mitano.

    Rais Magufuli amemsifia Majaliwa akisema ni mchapakazi na muadilifu na anastahili nafasi hiyo, japo si sahihi kwa watu kuhesabu kuwa atasalia kwa kipindi chote cha miaka mitano ijayo.

    “Baada tu ya kumchagua kuwa Waziri Mkuu naona kuna watu wanasherehekea na baadhi ya magazeti yanaandika kuwa atakuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10. Hilo si sahihi.”

    Rais Magufuli ameeleza kuwa ni Waziri Mkuu mmoja tu Fredrick Sumaye (1995-2005) ambaye amedumu katika wadhifa huo kwa miaka mitano na wengine wote walikaa kwa vipi fi vifupi zaidi.

    Majaliwa alihudumu kama Waziri Mkuu katika miaka mitano ilopita ya awamu ya kwanza ya Magufuli.

    ''Guarantee (uhakika) pekee alokuwa nao (Majaliwa) ni wa miaka mitano ilopita. Miaka mitano ijayo linaweza kutokea lolote...Huo ndio ukweli. Kitu pekee kitakachomfanya abaki hapo ni utendaji kazi wake...Majaliwa ni mtendaji mzuri na ndio maana sikupata shida kumchagua tena,'' ameelezea rais Magufuli.

    Kwa upande wake, baada ya kula kiapo katika ya Ikulu Chamwino, Waziri mkuu Majaliwa amesema:

    ''Namshukuru sana rais kwa kunipa nafasi tena, Mh. Rais utaunda Baraza la Mawaziri muda mfupi ujao jukumu langu ni kusimamia utendaji kazi wao, nitapita kila wizara na kuwataka waweke mpango kazi wa yale yaliyoanzishwa kwenye Ilani na kwenye hotuba yako''.

    Bwana Majaliwa ameonesha atakayoyapa kipaumbele ikiwemo kupanda kwa bei ya saruji na kuahidi kulitafutia ufumbuzi suala hilo.

    ''Tulipokuwa kwenye kampeni, kumeibuka kupanda kwa bei ya saruji bila sababu ya msingi, hatutarajii saruji kuwa na bei kubwa...sasa naanza na hili la saruji'', amesema Bwana Majaaliwa.

    Maelezo zaidi:

  6. Wanafunzi wote Kenya kurejea shuleni Januari

    Waziri wa Elimu nchini Kenya George Magoha ametangaza kuwa wanafunzi wote watarejea shuleni Januari 4.

    Kwasasa, ni wanafunzi wa mwaka wa mwisho pekee waliorejea shuleni huku katika baadhi ya taasisi mafunzo kwa wanafunzi wengine yamekuwa yakiendelea kwa njia ya mtandano.

    Kalenda ya shule ilivurugika kwasababu ya virusi vya corona.

    Mwanzoni mwa janga la virusi vya corona, wizara ya elimu ilifuta mwaka wote wa masomo wa 2020 lakini baadaye ikatangaza kuwa wanafunzi wa mwaka wa mwisho waruhusiwe kuanza tena masomo kwa njia ya ana kwa ana.

  7. BBC Africa Eye: Uchunguzi wa BBC umefichua mitandao ya kuuza watoto

    Uchunguzi wa mwaka mzima na BBC Africa Eye umefichua mitandao inayostawi nchini Kenya, ambayo inanyakua watoto kutoka kwa mama walio katika mazingira magumu na kuwauza kwa faida.

    Soma zaidi:

  8. Wafuasi wa Bobi Wine watawanywa kwa mabomu ya machozi Uganda

    Wafuasi wa mgombea urais ambaye pia ni mwanamuziki Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, wamerushiwa vitoza machozi na polisi Jumapili nchini Uganda, pamoja na kumkataza mgombea huyo kuingia kwenye eneo alilopanga kufanya kampeni.

    Wafuasi wa Bobi Wine walikuwa wamekusanyika katika mji wa Kumi, mashariki mwa nchi hiyo walipotawanywa.

    Msafara wake baadaye ukakatazwa kuingia katika eneo la Sironko na kulazimika kurejea mji wa Mbale ambapo wafuasi wake walifyatuliwa vitoza machozi.

    Bobi Wine aliweka picha za makabiliano kati ya polisi na wafuasi wake kwenye mtandao wa Twitter:

    Raia nchini Uganda watapiga kura Januari 14 kumchagua rais na wabunge.

    Rais Yoweri Museveni ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi miongo mitatu anatafuta kuchaguliwa tena.

    Pia miongozo ya wizara ya afya inapinga wanasiasa kukusanyika na makundi makubwa ya wafuasi yao, badala yake, kuhutubia umati wa watu usio zidi 70.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Mkutano wa dharura Kenya huku madaktari 10 wakifariki dunia kwa corona

    Waziri wa Afya nchini Kenya Mutahi kagwe amesema kuwa leo Jumatatu kutafanyika mkutano wa dharura kujadiliana ongezeko la maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 nchini humo sio tu kwa raia wa kawaida bali hata kwa wahudumu wa afya.

    Hatua hiyo inajiri huku Chama cha Madaktari nchini Kenya kikitoa ilani kwa serikali ya mgomo wa siku 21 baada ya wahudumu wa afya wapatao 10 kupoteza maisha katika kipindi cha siku nne zilizopita kwasababu ya virusi vya corona.

    Madaktari wanashutumu serikali kwa kuhatarisha maisha yao.

    Ijumaa wiki iliyopita madaktari wanne walifariki dunia siku hiyo ingawa bado haijajulikana kama walikuwa wamekutana na wagonjwa wenye maambukizi ya virusi vya corona.

    Kaimu katibu wa chama cha madaktari Mwachonda Chibanzi, amesema kuwa hawatasitisha mgomo huo hadi matakwa yao yatakapotimizwa.

    Maelezo zaidi:

  10. Afrika Kusini yataka muhubiri milionea aliyetorokea Malawi arejeshwe

    Serikali ya Afrika Kusini imesema kuwa imewasiliana na Malawi ili ikabidhiwe muhubiri mtata, Shepherd Bushiri, na mke wake Mary, baada ya wanandoa hao kuvunja masharti ya dhamana.

    Wawili hao wanakabiliwa na makosa ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha nchini Afrika Kusini.

    Bwana Bushiri, kiongozi wa Kanisa la Enlightenment Christian Gathering Church, ambaye pia anafahamika na wafuasi wake kama Major 1, alitangaza Jumamosi kwamba ametoroka Afrika Kusini baada ya kupokea vitisho vya kuuawa.

    Aidha, alikataa kuelezea wazi BBC namna alivyofanikiwa kutoroka lakini inakisiwa kuwa walipita mpakani kwa njia ya magendo kwa usaidizi wa genge linalohusika na uuzaji wa magari yalioibwa.

    Kutoroka kwake kumechochea mazungumzo ya kidiplomasia kati ya Afrika Kusini na Malawi.

    Serikali ya Afrika Kusini imewataja wanandoa hao kamawatoro ambao ni lazima wakabidhiwe nchi hiyo ili kukabiliana na mkono wa sheria.

    Rais wa Malawi Lazarus Chakwera ambaye alikuwa Afrika Kusini kwa ziara rasmi wiki iliyopita, alishtumiwa kwa kumsaidia Bwana Bushiri kutoroka – madai ambayo ameyakanusha.

    Pia serikali ya Afrika Kusini imethibitisha kuwa mhubiri huyo milionea nchini Malawi, hakutoroka kwa kutumia ndege ya rais.

    Maelezo zaidi:

  11. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja hii leo ikiwa ni tarehe 16/11/2020.