Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
UN yaitaka Msumbiji kuchunguza matukio ya mauaji
Umoja wa Mataifa umetaka mamlaka nchini Msumbiji kuchunguza ripoti kuwa wanamgambo wamewaua takribani watu 50
Moja kwa moja
Aliyeghushi video ya ndoa ya Rais Buhari ashtakiwa Nigeria
Mwanaume moja nchini Nigeria anashutumiwa kutengeneza video ya kughushi ya Rais Muhammadu Buhari akimuoa mmoja wa mawaziri wake wa kike na kuichapisha mtandaoni ameshtakiwa katika jimbo la Kaskazini la Kano.
Video ilimuonesha Rais Buhari na Waziri wa masuala ya kibinadamu Sadiya Umar Farouq.
Kabiru Mohammed alikamatwa na mamlaka za usalama mwezi Januari lakini alishtakiwa siku ya Jumanne.
Idara hiyo imesema mshukiwa huyo amekiri kuwa alitengeneza video hiyo.
Mahakama ilisema kuwa video hiyo imeharibu sifa za watu na kusababisha hali ya kukosa imani katika familia za watu.
Upande wa mashtaka umeiomba mahakama kumnyima dhamana Mohammed ili kuruhusu kukamilika kwa uchunguzi na kupata ushauri wa kisheria kutoka kwa wizara ya sheria jimboni Kano.
Lakini mahakama ilimpa dhamana baada ya wakili wake kusema kuwa shtaka lake linaweza kupatiwa dhamana.
Kesi hiyo itasikilizwa tena tarehe 5 mwezi Februari mwaka 2021.
Zimbabwe kuisaidia Msumbiji wakati uasi ukiongezeka
Rais Emmerson Mnangagwa amesema Zimbabwe iko tayari kusaidia nchi jirani Msumbiji wakati uasi ukiongezeka Cabo Delgado Kaskazini mwa Msumbiji.
Aliandika katika ukurasa wa twitter "usalama wa ukanda wetu ni muhimu kwa ulinzi wa watu wetu".
Kiongozi wa Msumbiji Filipe Nyusi alikutana na Mnangagwa mwezi Mei ili kuomba msaada wa kijeshi kutoka baraza la usalama cha Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika.
Mwezi Oktoba gazeti la Expresso da Manha liliripoti kuwa Marekani iliiomba Zimbabwe kuisaidia Msumbiji katika operesheni ya kupambana na wanamamgambo.Zimbabwe ilikubali kwa sharti la Marekani kuiondolea Zimbabwe vikwazo.
Moja kati ya mashambulizi ya hivi karibuni huko Cabo Delgado, wanamgambo waliwakata vichwa watu karibu 50 katika kipindi cha siku tatu kwenye uwanja wa mpira wa miguu katika kijiji cha Muatide.
Tovuti binafsi ya O Pais iliripoti siku ya Jumanne kuwa wanamgambo pia walijaribu kuvamia magereza matatu miongoni mwa magereza makubwa katika jimbo la Kaskazini.
Haijulikani mashambulizi hayo yalitekelezwa lini.
Mzozo ulioibuka mwaka 2017, umetishia kuzorotesha usalama katika ukanda wakati wanamgambo walipoanza kuingia mkoa wa Mtwara nchini Tanzania, eneo la mpaka na Msumbiji.
UN yaitaka Msumbiji kuchunguza mauaji
Umoja wa Mataifa umetaka mamlaka nchini Msumbiji kuchunguza ripoti kuwa wanamgambo wamewaua takribani watu 50 na kuwachinja wanawake na watoto katika mji wa Carbo del Gado Kaskazini mwa nchi hiyo.
Taarifa ya chombo hicho inasema kuwa Katibu Mkuu wa UN António Guterres “alishtushwa “ na ripoti hizo.
Katika shambulio la hivi karibuni, wanamgambo wa Kiislamuwaliubadili uwanja wa mpira wa miguu kuwa ‘’uwanja wa mauaji”, ambapo walikata vichwa na miili , ripoti zilieleza.
Matukio ya hivi karibuni ya kukata vichwa ni mfululizo wa mashambulizi yaliyotkelezwa na wanamgambo katika mji ulio na utajiri wa gesi Cabo Delgado tangu mwaka 2017.
Mpaka watu 2,000 wameuawa na karibu 430,000 wameachwa bila makazi katika eneo hilo lenye mzozo linalokaliwa na idadi kubwa ya Waislamu.
Wanamgambo hao wanahusishwa na kundi la Islamic State(IS), ambao wanaonekana kuweka mizizi Kusini mwa Afrika.
Kundi hilo limetumia umaskini na ukosefu wa ajira kama kichocheo kuajiri vijana katika mapigano yao ya kuanzisha utawala wa Kiislamu katika eneo hilo.
Wakazi wa eneo hilo wamelalamika kuwa wamepata faida kidogo sana kutokana na madini ya ruby na soko la gesi.
Shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International limewatuhumu wanajeshi wa Msumbiji kwa kufanya ukatili wakati wa kudhibiti vurugu hizo, lakini wizara ya ulinzi ilitupilia mbali ripoti hizo.
Riek Machar ashutumiwa kwa “kushindwa kuongoza”
Makamu wa Rais wa Sudan Kusini, Riek Machar, ameshutumiwa kwa "kushindwa kuongoza" na afisa wa juu wa chama chake cha Sudan People's Liberation Movement in Opposition (SPLM-IO).
Katibu Mkuu Peter Tingo , amewasilisha barua ya kazi siku ya Jumanne baada ya kutumikia nafasi hoyo kwa miaka minne.
Amemshutumu bwana Machar kwa kushindwa “kuonesha utawala bora” na kukiongoza chama bila mashauriano.
Ofisi ya Machar haijasema lolote kuhusu shutuma hizo.
“Umekiendesha chama bila uwazi, hasa katika masuala ya kufanya maamuzi. Hauheshimu muundo wa taasisi uliowekwa na katiba ya taasisi,” Bw. Tingo aliandika katika barua yake ya kuacha kazi.
Amesema kuwa kuacha kwake kazi hakutaathiri utekelezaji wa makubaliano ya amani yaliyotiwa saini na Bw.Machar na hasimu wake wa kisiasa Rais Salva Kiir mwezi Februari baada ya miaka kadhaa ya mzozo.
Maseneta kuvaa mavazi ya kitamaduni kwenye Bunge la Seneti
Spika wa bunge la Seneti nchini Kenya amewaruhusu maseneta kuvaa nguo za kitamaduni ndani ya bunge.
Maseneta, wa kiume na wa kike, awali waliruhusiwa kuingia kwenye bunge wakiwa wamevalia mavazi rasmi au mavazi ya watoa huduma, nguo za diniau nguo nyingine kwa idhini maalumu.
Spika Ken Lusaka, akiridhia kufanyika kwa mabadiliko hayo siku ya Jumanne, alisema katiba inaruhusuwatu kudumisha utamaduni wao.
Aliulizwa kwa nini seneta kutoka jamii ya Wamasai alikuwa amevaa shuka yenye shanga nyekundu wakati kikao cha bunge.
Ali Seneta wa Wajir Abdulahi Ali alisema kulegeza sheria hizo kutasababisha "mavazi ya kila aina" bungeni.
Lakini Spika Lusakaalisema haitakuwa haki kumtaka Seneta Ledama Ole Kina kuondoka bungeni kwa kuwa alikuwa na vazi la heshima.
Seneta Kina aliweka picha ya video kwenye mtandao wa twitter akionesha vazi lake.
Ethiopia imesema imewaua wapiganaji 550 wa Tigray
Shirika la utangazaji la Ethiopia limesema kuwa wanajeshi wa nchi hiyo wamewaua wapiganaji 550 wa Tigray (TPLF) wakati huu ambapo mzozo katika eneo hilo la Kaskazini ukishika kasi.
Madai hayo hayajathibitishwa na mashuhuda huru.
Hii imekuja wakati ripoti zikionesha kutokea kwa vifo vya mamia ya watu kwa pande zote mbili.
Siku ya Jumanne, mkuu wa wapiganaji wa TPLF, Debretsion Gebremichael aliishutumu serikali ya nchi jirani ya Eritrea kwa kuanzisha mashambulizi dhidi ya jimbo la Tigray.
Shutuma hizo zilikanwa na pande zote, serikali ya Eritrea na Jeshi la taifa la Ethiopia.
Msemaji wa kamati ya dharura ya serikali, Redwan Hussein, siku ya Jumanne alisema kuwa bado kuna uwezekano wa mazungumzo kati ya serikali na mamlaka za Tigray.
Lakini alisema “vifaa vilivyokamatwa na vikosi vilivyokamatwa na vikosi vilivyo vitiifu kwa TPLF lazima viharibiwe, watu wanaoshikiliwa na vikosi vya Tigray waachiliwe na wale walioanzisha mashambulizi wafikishwe mbele ya mikono ya sheria”.
Wakati huo huo polisi wa Ethiopia wamesema kuwa wanajeshi 17 - wakiwemo maafisa wakuu - wanaotuhumiwa kuwa sehemu ya njama wakati jeshi la kaskazini lilipodaiwa kushambuliwa wiki iliyopita wamekamatwa.
Maafisa wamesema kuwa waliharibu mawasiliano kati ya uongozi na jeshi lote la taifa.
Haijulikani kama watuhumiwa hao walijibu shutuma hizo.
Magufuli awapongeza Joe Biden na Kamala Harris
Rais wa Tanzania John Magufuli amempongeza Rais mteule Joe Biden na aliyekuwa mgombea mwenza Kamala Harris kwa ushindi walioupata katika uchaguzi mkuu wa Marekani.
Katika Ukurasa wake wa Twitter Rais Magufuli ameseme anawahakikishia wawili hao kuwa Tanzania itaendelea kutunza uhusiano uliopo kati ya nchi hizo mbili.
Vurugu za baada ya uchaguzi zashika kasi Ivory Coast
Kuna Ripoti za kutokea kwa vurugu za baada ya uchaguzi nchini Ivory Coast baada ya Rais Alassane Ouattara kuchaguliwa tena kwa muhula wa tatu.
Watu watatu wameuawa na wengine kujeruhiwa siku ya Jumanne katika eneo la ngome ya upinzani kwa mujibu wa mamlaka za eneo hilo wakinukuliwa na mashirika ya habari.
Mapigano yaliripotiwa maeneo ya mji wa M’Batto ulio Kusini –kati ambao umeonekana kuwa ngome ya upinzani kwa mgombea wa upinzani Pascal Affi N’Guessan, ambaye alikamatwa siku ya Ijumaa.
Bw. N’Guessan anakabiliwa na mashtaka ya ugaidi na uhaini baada ya kupinga ushindi wa Rais Ouattara.
Rais Ouattara amemualika mpinzani wake, Rais wa zamani Henri Konan Bédié kwa mazungumzo baada ya kutokea vurugu.
Bw.Bédié hajazungumza lolote kuhusu mualiko huo.
Raia wa Ethiopia wakimbilia Sudan kuepuka mapigano Tigray
Maafisa nchini Sudan wamesema takriban raia wa Ethiopia 6,000 wamewasili nchini humo, wakikimbia mapigano jimboni Tigray.
Mamlaka za Sudan zinajiandaa kupokea zaidi watu 200,000 watakaovuka mpaka siku za usoni.
Kambi ya wakimbizi kuhimili idadi kubwa ya watu inaandaliwa, huku taasisi za misaada zikitahadharisha kutokea kwa changamoto ya hali ya kibinadamu
Waziri Mkuu wa Ethiopia alizanzisha operesheni ya kijeshi huko Tigray dhidi ya viongozi wa eneo hilo ambao walioanzisha mzozo dhidi ya mamlaka ,za serikali.
Mamia wameuawa kwenye mapigano hayo.