Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Serengeti yashinda tena Tuzo ya Hifadhi bora Afrika 2020

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeshinda tuzo ya kuwa hifadhi bora katika Bara la Afrika kwa mwaka 2020.

Moja kwa moja

Lizzy Masinga

  1. Na hapa ndio mwisho wa matangazo mubashara, tukutane tena hapo kesho.Shukrani

  2. Serengeti yashinda tena Tuzo ya Hifadhi bora ya Afrika 2020

    Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeshinda tuzo ya kuwa hifadhi bora katika Bara la Afrika kwa mwaka 2020.

    Tuzo hizo zimetangazwa siku ya Jumatatu na Taasisi ya World Travel Awards (WTA) ya nchini Marekani kwa njia ya Mtandao.

    Hii ni mara ya pili kwa Hifadhi ya Taifa Serengeti kushinda katika kundi la hifadhi zinazoongoza kwa ubora zaidi barani Afrika baada ya kunyakua tuzo hiyo mwaka 2019.

    Serengeti imeibuka mshindi katika shindano lililoshindanisha hifadhi nyingine za Central Kalahari (Botswana); Etosha (Namibia); Kidepo Valley (Uganda) Kruger (Afrika Kusini) na Maasai Mara (Kenya).

    Serengeti inajivunia umaarufu kwa msafara wa nyumbu wahamao zaidi ya milioni mojana nusu, aina mbalimbali za wanyamapori wanaopatikana kwa wingi, mandhari nzuri ya kuvutia pamoja na shughuli mbalimbali zinazowavutia watalii wengi.

  3. Vibarua mpaka wa DRC na Rwanda walalamikia hali ngumu ya maisha

      • Author, Yves Bucyana
      • Nafasi, BBC Swahili

    Ni miezi nane sasa tangu mpaka wa Rusizi-Bukavu kufungwa, maelfu ya watu ambao walikuwa wanalazimika kuvuka kwenda Bukavu nchini DRC kutoka mji wa Rusizi nchini Rwanda, wanasema maisha yamekuwa magumu sana kwao.

    Mipaka ilifungwa tangu mwezi Machi, kwa sababu ya janga la corona.

    Hivi karibuni ,Rwanda na DRC walikubaliana kufungua mpaka kwa idadi ndogo ya watu walio na sababu maalum huku watu hao wakijigharamia katika vipimo vya Covid 19.

    Jambo ambalo halijaleta mabadiliko makubwa katika upande wa ajira ,kwa kuwa idadi ni ndogo bado.

    Wananchi wa eneo hilo wanasema hali ya kiuchumi na maisha yamebadilika mno hakuna aliyepata msaada wa chakula serikalini wakati wa sheria ya kutotoka nyumbani. "Maisha yalisimama kwa sababu mpaka huu ndio ulikuwa riziki yetu.’’

    "Badala yake, tuna madeni mengi,tumekuwa omba omba ...mara kilo ya sukari ,mara mchele ili kunusuru maisha ya watoto yaani tuko katika maisha magumu’’ Uwamahoro Olive anasema alikuwa akivuka mpaka kila siku kwenda Bukavu kufanya kazi ya kutengeneza bustani.

    ‘’Mimi kazi yangu ni ya kutengeneza bustani, nilifanya kazi hiyo mjini Bukavu kwa miaka 8 sasa. .ni kazi iliyokuwa inaingiza kila mwezi nilikuwa napata takriban dolla 80.Tangu mipaka kufungwa tunahangaika sana hata kupata chakula ni shida’’,alisema mkazi mwingine.

    Fundi mwingine wa ujenzi anayeishi katika mji wa Rusizi alisema: "Kule Congo kuna kazi nyingi za kufanywa, hata wakati mwingine wanakuita wenyewe kwa ajili ya kazi ,huwezi kuenda Congo na kurudi nyumbani mikono mitupu.’’ Rwanda imeishafungua viwanja vya ndege, lakini haijafahamika lini itakapofungua mipaka ya ardhini.

  4. Muigizaji wa Nigeria kushtakiwa mahakamani baada ya picha zake kuzua mjadala mtandaoni

    Mwanazuoni wa dini ya Kiislamu Kaskazini mwa Nigeria ametaka muigizaji Rahama Sadau ashtakiwe katika mahakama ya Kiislamu kwa madai ya kuchochea maoni ya kashfa juu ya Nabii Muhammad, baada ya kuweka picha zake akiwa amevalia mavazi ya yanayomuonesha mgongo wazi kwenye mitandao ya kijamii ambayo yalichukuliwa na watu wengine kuwa ya aibu.

    Muigizaji huyo aliomba radhi na kufuta picha hizo baada ya kusababisha ghadhabu kwa raia wengi hasa wa Kaskazini mwa Nigeria.

    Hatahivyo, hiyo haikutosha kumzuia mtaalamu huyu kutaka kesi yake isikilizwe kwenye mahakama ya Kiislamu, si kwa sababu ya picha zenyewe bali kwa sababu ya namna watu walivyozungumzia kitendo hicho.

    Watu waliomtetea Sadau kuhusu picha hizo pia walimkosoa Nabii.

    Aliyu Dahiru,ambaye anatafiti masuala ya kijinsia kaskazini mwa Nigeria, amesema upande wa mashtaka umejaribu "kujibu kupita kiasi" na kuongeza kuwa "hali ya kuwachukia wanawake kaskazini inasababisha uonevu wa mtandao".

    Sadau alisimamishwa kushiriki kwenye tasnia ya sinema eneo la kaskazini kwa kuhusika kwenye video ya muziki akionekana kumkumbatia msanii wa kiume.

  5. Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema ‘operesheni zitaendelea kama ilivyopangwa’

    Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema ‘’ Operesheni ya kusimamia sheria’’ katika jimbo la Kaskazini la Tigray ‘’inaendelea kama ilivyopangwa’’.

    Alisema katika ukurasa wake wa Twitter kuwa operesheni itakoma ‘’baada ya jeshi la Junta kudhibitiwa, utawala halali kurejeshwa katika eneo, pia waliokimbia kuhakikisha wanafikishwa kwenye vyombo vya kisheria’’.

    Bw. Abiy alitangaza operesheni ya kijeshi dhidi jimbo la Tigray baada ya kudai kuwa majeshi ya eneo hilo yalishambulia kituo cha kijeshi cha vikosi vya serikali kuu.

  6. Rais wa Ivory Coast amualika mpinzani wake kwa ajili ya mazungumzo

    Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara amemualika mpinzani wake, Rais wa zamani Henri Konan Bédié kwa ajili ya mazungumzo baada ya kutokea vurugu zilizosababishwa na ushindi wake wa kishindo kuelekea kuliongoza taifa hilo kwa muhula wa tatu.

    Viongozi wa upinzani walisusia kura za mwezi uliopita na kuapa kuunda serikali ya mpito ambayo itaandaa uchaguzi mpya.

    Siku ya Jumatatu mahakama ya kikatiba ilithibitisha ushindi wa Bw.Ouattara.

    Alipata 94.27% ya kura zilizopigwa. Hakuna rufaa dhidi ya uchaguzi wa rais unaowezekana sasa, kwa mujibu wa sheria ya nchi hiyo.

    Rais Outtara alimualika Bw. Bédié kwenye ‘’mkutano siku chache zijazo kwa ajili ya mazungumzo ya wazi na ya kweli kusaidia kurudisha uaminifu,’’ Shirika la habari la Ufaransa limeripoti.

    Viongozi kadhaa wa upinzani wanakabiliwa na mashtaka ya ugaidi na uchochezi baada ya kupinga kuchaguliwa tena kwa Rais Ouattara.

    Takribani watu 40 wameuawa kutokana na vurugu zinazohusiana na uchaguzi tangu mwezi Agosti.

  7. Mwanasheria nchini Nigeria ataka maandishi ya kiarabu kwenye fedha yaondolewe

    Mahakama mjini Lagos Nigeria inatarajia kusikiliza kesi iliyofunguliwa na mwanasheria dhidi ya Benki Kuu ya Nigeria akitaka kuondolewa kwa maandishi ya kiarabu kwenye fedha za nchi hiyo.

    Malcolm Omirhobo pia anataka jeshi la Nigeria kuondoa maandishi kutoka kwenye nembo ya jeshi yanayoashiria kuwa Nigeria ni nchi ya Kiislamu, kinyume na katiba ya nchi hiyo kuwa ni taifa lisilofungamana na dini yoyote.

    Mwanasheria huyo anataka maandishi hayo yawekwe kwa lugha ya Kiingereza au kwa lugha yoyote miongoni mwa lugha tatu zinazotumika nchini humo –Hausa, Yoruba au Igbo.

    Hatahivyo, Benki Kuu imekana kuwa maandishi hayo ni ishara ya Uislamu.

    Watu wengi nchini humo, hasa eneo la Kaskazini , huongea Kiarabu. Hata hivyo Kiingereza ni lugha kuu ya mawasiliano nchini humo.

  8. Job Ndugai achaguliwa kuwa Spika wa Bunge Tanzania

    Job Ndugai amechaguliwa kuwa spika wa Bunge la Tanzania hii leo kwa ushindi wa asilimia 99.7.

    Ndugai aliliongoza bunge hilo akiwa spika kwa kipindi cha miaka mitano, ambapo hii leo akmekitetea kiti chake kwa ajili ya kukitumikia kwa miaka mitano mingine.

    Awali Katibu wa Bunge, Stephen Kigaigaialisema kuwaamemuengua Bonaventura Peter Ndekenja wa chama cha NRA aliyemtumia barua pepe akieleza nia yake ya kutaka kuwa Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

    ''Yeye si mbunge hivyo chama chake kilipaswa kuwasilishajina lake Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) kuthibitisha kama ana vigezo vya kuwa mbunge'' kwa kutofanya hivyo ndugu Ngegenja amekosa sifa,'' alinukuliwa Kigaigai na gazeti la Mwananchi.

    Kutokana na hilo Job Ndugai alikuwamgombea pekee wa nafasi hiyo aliyepigiwa kura kwa ajili ya nafasi hiyo.

    Sasa Spika Ndugai ana jukumu la kuwaongoze wabunge wateule kula kiapo cha utii.

  9. Bunge la 12 laanza rasmi hii leo huko jijini Dodoma katikati mwa Tanzania

    Hii leo Spika wa bunge na naibu wake watachaguliwa rasmi na baadae kufuatia shughuli ya wabunge waliochaguliwa kula viapo vya utii.

    Hata hivyo kuna maswali mengi yanaulizwa iwapo bunge hili ambalo asilimia zaidi ya 80 ni kutoka chama tawala cha CCM litaweza kuisimamia vyema serikali katika shughuli zake.

  10. Uwanja wa Ndege wa Bujumbura wafunguliwa Burundi

    Kuanzia siku ya Jumapili, Uwanja wa ndege wa Bujumbura umefunguliwa kwa ajili ya ndege zinazofanya safari kimataifa baada ya kufungwa kwa miezi saba kutokana na janga la virusi vya corona.

    Burundi imekuwa nchi ya mwisho ya Afrika mashariki kufungua anga yake baada ya Tanzania mwezi May, Sudani Kusini mwezi Julai, Kenya na Rwanda mwezi Agosti na Uganda mwezi Septemba.

    Mamlaka ya anga imesema, abiria watakaoingia watahitajika kuwasilisha cheti kinachoonesha majibu ya vipimo vilivyofanywa saa 72 zilizopita yanayoonesha kutokuwa na maambukizi ya virusi, kufanyiwa vipimo na kukaa karantini kwa saa 72, kwa gharama zao.

    Melance Ndayisenga, mkazi wa jiji la Bujumbura, amefurahishwa na kufunguliwa kwa uwanja wa ndege lakini amesema sekta ya utalii imeporomoka kutokana na kufungwa kwa uwanja huo wa ndege.

    Burundi mpaka sasa imerekodi maambukizi kwa watu 421 na kifo cha mtu mmoja.

  11. Habari , Karibu kwa matangazo ya moja kwa moja hii leo