Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi Zanzibar: Kura ya awali yapigwa huku ghasia zikiripotiwa
Mabalozi wa Uingereza na Marekani nchini Tanzania wametumia mtandao wa Twitter kutoa rai juu ya kufanyika kwa uchaguzi wa amani visiwani Zanzibar.
Moja kwa moja
Esther Namuhisa and Asha Juma
Twitter:Tunashuhudia mtandao wetu kuminywa Tanzania
Mtandao wa Twitter umetoa taarifa kwa umma kuhusu kushuhudia kuminywa kwa mtandao huo nchini Tanzania wakati taifa hilo likielekea kwenye uchaguzi mkuu.
Twitter imesema kufungwa kwa intaneti ni jambo lenye madhara na kuvunja haki za binadamu.
Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo Maalim Seif aachiwa huru Zanzibar
Maalim Seif ameachiwa huru jioni hii baada ya kukamatwa na maafisa wa polisi mapema leo katika kituo cha kupigia kura cha Garagara hatua ambayo imeshutumiwa vikali na viongozi wa upinzani.
Kupitia mtandao wa Twitter, Chama cha ACT-Wazalendo kimeandika kuhusu kuachiwa kwake.
ACT Wazalendo wadai watu 9 wameuawa Zanzibar, polisi yakanusha kutokea mauaji
Imesalia siku moja kabla ya uchaguzi Tanzania
Mitandao ya kijamii yaminywa Tanzania
Watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Tanzania wamekuwa na wakati mgumu wa kutumia mtandao wa Twitter na WhatsApp ikiwa ni siku moja kabla ya uchaguzi.
Tangu majira ya asubuhi, watumiaji wa WhatsApp wameshindwa kupakua picha au video.
Watumiaji hao wanaweza kutuma au kupokea ujumbe mfupi wa maneno pekee kwa njia ya WhatsApp .
Twitter inaweza kupatikana kwa wale ambao wanatumia VPN.
Jitihada za BBC kupata maelezo kutoka mamlaka ya mawasiliano nchini humo (TCRA) hayakuzaa matunda.
Watumiaji wengi wanahusisha suala hili la zuio la intaneti na uchaguzi mkuu.
Uchaguzi wa awali umeanza Zanzibar, leo asubuhi kwa watumishi wa uchaguzi na maafisa wa usalama.
Ghasia zimeripotiwa kutokea katika kisiwa cha Zanzibar na chama cha upinzani mkuu kisiwani huko ACT-Wazalendo wanadai kuwa watu nane wameuawa.
Ingawa polisi wamekanusha madai hayo na kuthibitisha kuwa wamewakamata watu 42 pekee.
Picha na video za vurugu zimeonekana mtandaoni kabla ya zuio la mtandao huo kuanza.
Kesho Oktoba 28 , Tanzania bara na visiwani inatarajiwa kufanya uchaguzi mkuu wa marais, wabunge na madiwani.
Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo Maalim Seif akamatwa Zanzibar
Balozi wa Marekani, Uingereza watoa wito dhidi ya ghasia Zanzibar
Mabalozi wa Uingereza na Marekani nchini Tanzania wametumia mtandao wa Twitter kutoa rai juu ya kufanyika kwa uchaguzi wa amani visiwani Zanzibar.
Mabalozi hao, David Concar wa Uingereza na Donald J. Wright wa Marekani wamewataka wote wanaohusika kuhakikisha amani inatawala Zanzibar.
Umoja wa Afrika watoa wito wa uchaguzi wa amani Tanzania
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat ametoa wito wa uchaguzi wa amani, wenye kujumuisha kila mmoja na wa haki nchini Tanzania.
Mwenyekiti ametoa wito kwa washikadau wengine, vyama vya kisiasa na wafuasi wake kushiriki uchaguzi kwa amani na kujizuia kufanya vitendo vyovyote vya ghasia.
Aliendelea kusihi serikali kuhakikisha mazingira mazuri yanayowezesha raia kupiga kura zao kwa njia salama na ya amani.
Bwana Mahamat amekumbuka safari ya kupigiwa mfano ya Tanzania katika utekelezaji wa demokrasia na amani na kutoa wito uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020 kuwa fursa mpya ya kuimarisha demokrasia na amani nchini humo.
Umoja wa Afrika umepeleka wataalamu wa uchaguzi nchini Tanzania kuanzia Oktoba 22 hadi Novemba 3, 2020 unaoongozwa na mheshimiwa Goodluck Jonathan, aliyekuwa rais wa Nigeria.
Habari za hivi punde, Polisi Tanzania yakanusha mauaji ya watu Pemba
Inspekta Jenerali wa Polisi Tanzania Simon Sirro amekanusha taarifa kwamba polisi nchini Tanzania imewapiga risasi na kuwauwa watu 3 huko Pemba katika tukio la jana usiku.
Akizungumza na vyombo vya habari katika mji wa Dar es-Salaam asubuhi ya leo, Bwana Sirro amesema kwamba Jeshi la Polisi linawashikilia vijana 42 mpaka sasa visiwani Zanzibar, kutokana na vurugu za jana usiku zilizotokea Pemba.
Kwa upande wake, upinzani unadai hadi kufikia sasa watu watano wameuawa katika vurugu hizo huku wengine wakijeruhiwa baada ya polisi kutumia risasi kutawanya raia waliokuwa wamekusanyika.
Bwana Sirro alifafanua kuwa vijana waliokamatwa walikuwa wanawarushia polisi na baadhi ya maafisa wa uchaguzi mawe waliokuwa wanasambaza masanduku ya kupiga kura eneo hilo kabla ya uchaguzi wa mapema unaoendelea hii leo.
Aidha Bwana Sirro ameonya kuwa mtu au watu waliopanga kusalia kwenye vituo vya kupigia kura baada ya kupiga kura zao kwa madai kwamba wanalinda kura akisema hilo halikubaliki na haliwezi kuvumiliwa.
Umoja wa Mataifa watoa wito wa kuwepo kwa uchaguzi wa amani Tanzania
Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa Tanzania kuhakikisha uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 unafanyika kwa njia ya amani.
Katika taarifa siku ya Jumatatu iliyotolewa kwa niaba ya Bw. Antonio Gutteres inasema mchakato shirikishi wa uchaguzi na ushiriki mpana wa vyama vya siasa na wagombea wao, haswa wanawake, unabaki muhimu kwa kulinda maendeleo yaliyofanywa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha utulivu, demokrasia na maendeleo endelevu.
Katibu mkuu wa Umoja huo pia ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa na wafuasi wao kushiriki katika uchaguzi huo kwa amani na kujiepusha na visa vya vurugu.
Mamlaka pia imetakiwa kutoa mazingira salama ambayo yatawawezesha Watanzania kutekeleza haki yao ya kiraia na kisiasa.
Uchaguzi Tanzania 2020: Wapinzani wadai watu watano wameuawa Pemba
Chama cha Upinzani cha ACT-Wazalendo kinadai kuwa idadi ya waliouawa kisiwani Pemba kufuatia vurugu za uchaguzi jana usiku na leo asubuhi imefikiwa watu watano ingawa polisi imekanusha taarifa hizo.
Awali, Mkurugenzi wa Mkurugenzi wa mawasiliano wa ACT Salim Bimani aliiambia BBC kwamba watu watatu waliuawa kwa risasi kisiwani Pemba jana usiku.
Leo asubuhi chama hicho kupitia mtandao wa Twitter kimeeleza kuwa idadi ya walioawa ni watu wanne.
Hata hivyo, polisi kisiwani Pemba kupitia Kamishna Msaidizi Juma Saad Hamis imekanusha madai hayo ikisema kwamba ilitumia vitoa machozi pekee na si risasi za moto.
Ripoti hizo zinajiri wakati ambapo shughuli ya upigaji kura miongoni mwa maafisa maalum wanaohusika na usalama pamoja na usimamizi wa kura wakipiga kura hii leo.
Jinsi upigaji kura unavyoendelea Zanzibar
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Halima Nyanza
- Nafasi, BBC Swahili
Zoezi la upigaji kura ya mapema visiwani Zanzibar linaendelea kwa makundi maalumu tu ya wapiga kura.
Sikiliza maoni ya mmoja wa waliopiga kura.
Utaratibu wa kupiga kura ya mapema Zanzibar ulivyo?
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Halima Nyanza
- Nafasi, BBC Swahili
Zoezi la upigaji kura ya mapema huko Zanzibar limeanza saa moja asubuhi. Kwa hii leo wanaopiga kura ni wa chache kwa sababu ya utaratibu uliopangwa.
Mwanahabari wa BBC Halima Nyanza yuko katika kituo cha upigaji kura katika Skuli ya Vikokotoni karibu kabisa na soko la Darajani.
Kura hii ya mapema ni ya kwanza kabisa kufanyika huko visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, kura hii itawarahisishia watendaji ambapo wengi wao kesho Oktoba 28 watakuwa na majukumu ya kuhudumia wapiga kura ili kufanikisha tukio la kesho la upigaji kura.
Kutokana na kuwa mara nyingi huwa wanakosa nafasi ya kutekeleza haki yao ya kupiga kura ndio maana wakatengewa siku hii.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC Hamid Mahmod ametaja wale watakaohusika na kura hii ya mapema.
‘’Wapiga kura watakaohusika na upigaji kura mapema ni kama ifuatavyo,
Wasimamizi wa uchaguzi, pili wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupiga kura, askari polisi, wajumbe wa tume, watendaji wa tume, wapiga kura watakaohusika na ulinzi na usalama siku ya uchaguzi
Bwana Mahmod amesisitiza kuwa wananchi hawatakiwi kwenda katika vituo vya kupiga kura isipokuwa tu kwa wale ambao orodha yao imewekwa vituoni kwa ajili ya kupiga kura ya mapema.
Aidha kulingana na utaratibu uliopo ni kwamba sio vituo vyote vitakavyofunguliwa isipokuwa tu kwa vilivyoorodheshwa kama anavyofafanunua Mmwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC Hamid Mahmod
‘’Naomba ifahamike kuwa katika kila eneo la upigaji kura kutakuwa na kituo kimoja tu kitachopangwa kwa ajili ya kupiga kura ya mapema.
Kulingana na Bwana Mahmod vituo vingine vya kupiga kura vitafungwa na watendaji wa uchaguzi hawatakuwepo.
‘’Pia vituo hivyo havitakuwa na masanduku ya kupiga kura wala kura zenyewe.’’
Kura zitakuwa kwa idadi maalum kuwatosheleza wapiga kura waliopangwa kupiga kura mapema tu.
Habari za hivi punde, Vituo vya kupigia kura vyafunguliwa Zanzibar
Hatimaye baada ya miezi mitatu ya kampeni zoezi la upigaji kura visiwani Zanzibar linaanza asubuhi hii, zoezi litakaloanza na kura ya mapema kwa makundi maalumu tu ya wapiga kura.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC Hamid Mahmod amesema shughuli hii ya upigaji kura itaanza saa moja kamili asubuhi na kumalizika saa kumi jioni.
Upinzani mkubwa uko kwa wagombea urais kutoka chama tawala cha cha CCM, Hussen Mwinyi na Maalim seif Sharif Hamad wa chama cha ACT.
Polisi na wasimamizi wa vituo vya kupiga kura kushiriki uchaguzi leo
Kisiwa cha Zanzibar nchini Tanzania kitashiriki kwenye uchaguzi mkuu mara mbili, ifikiapo Jumanne tarehe 27 mwezi Oktoba na Oktoba 28.
Uchaguzi huo ambao ni wa kihistoria unafanyika kwa siku mbili ili kutoa fursa kwa makundi yaliokuwa yakipata changamoto za kupiga kura kushiriki
Kura hii ya awali kwa watumishi wenye majukumu maaalumu wakati wa uchaguzi kwa mujibu wa sheria, imekuwa ikileta sintofahamu.
Baadhi ya watendaji wakiwemo maafisa wa kusimamia zoezi zima la uchaguzi wanatarajiwa kupiga kura
Rais anayeondoka Mohammed Shein amemaliza mihula yake miwili.
Uchaguzi huo unahusisha wadhfa wa urais, wabunge na madiwani.
Natumai hamjambo hii leo ikiwa ni siku ya kihistoria kisiwani Zanzibar ambapo raia wanapewa fursa ya kumchagua kiongozi wao