Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Fatma karume afutwa uwakili

Kamati ya maadili ya mawakili Tanganyika leo hii imetoa uamuzi wa kutoa jina la Fatma Karume katika orodha ya mawakili kwa kumkuta na hatia ya kukiuka maadili ya uwakili.

Moja kwa moja

Esther Namuhisa

  1. Kufikia hapo tunakamilisha matangazo haya ya moja kwa moja. Tukutane tena Alhamisi 24/09/2020

  2. Aliyekuwa rais wa Liberia aanzisha programu ya wanawake viongozi

    Rais wa zamani wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf ameanzisha programu maalum ya uongozi ya wanawake barani Afrika.

    Mpango huo ulizinduliwa Machi 8 wakati wa maadhimisho ya sherehe ya wanawake kimataifa, lengo likiwa ni kutoa mafunzo ya uongozi wa kiwango cha juu katika umma.

    Bi. Sirleaf ameiambia BBC kuwa lengo ni kuongeza idadi ya wanawake katika uongozi.

    "Nia yangu ni kutaka sauti za wanawake zisikike na kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi ."

    Programu hiyo inapokea maombi ya watakaoanza mwakani, maombi yanaruhusiwa kutumwa mpaka Septemba 30 mwaka huu.

    Bi Sirleaf alisema ili idadi ya wanawake iweze kuongezeka katika uongozi ni muhimu kwa wanaume kushirikishwa na kuoneshwa ni nini wanawake wanaweza kufanya kama viongozi.

    "Tunataka kubadili mtazamo wa wanaume "bi.Sirleaf alisisitiza.

  3. Wanafunzi wauawa katika mlipuko wa lori la mafuta Nigeria

    Watu wapatao 25 wamefariki nchini Nigeria baada ya tenki la mafuta ya petroli kulipuka mjini Lokoja.

    Polisi wamesema kuwa dereva wa lori alishindwa kulidhibiti gari na kukosa uelekeo.

    Baadhi ya wahanga ni wanafunzi wa shule ya msingi.

    Mashaidi wamesema ajali ilitokea mapema Jumatano katika eneo lenye magari mengi mjini.

    Lori hilo la mafuta lililokosa uelekeo na kugonga magari mengine na kulipuka karibu na eneo la Kogi.

    Msemaji wa polisi mjini Lokoja bwana Willy Aya ameiambia BBC kuwa baadhi ya watu waliungua na hawawezi kutabulika, wakiwemo wanafunzi wa shule.

    Ajali za mlipuko wa malori ya mafuta nchini Nigeria zimekuwa nyingi.

    Mwezi Juni, watu wanne waliuawa mjini Lagos baada ya mlipuko wa magari manne.

    Wiki iliyopita tenki lingine la mafuta ya petroli lilipuka.

  4. Fatma karume afutwa uwakili

      • Author, Humphery Mgonja
      • Nafasi, BBC Field Producer

    Kamati ya maadili ya mawakili Tanganyika leo hii imetoa uamuzi wa kutoa jina la Fatma Karume katika orodha ya mawakili kwa kumkuta na hatia ya kukiuka maadili ya uwakili.

    Kupitia kurasa yake ya tweeter Fatma Karume ameweka bayana kuwa hatokata rufaa kupinga maamuzi hayo.

    Mwaka mmoja uliopita wakili huyo alisimamishwa kufanya kazi za uwakili kwa upande wa Tanzania bara.

    Maamuzi hayo yalitolewa na Jaji Feleshi kwenye kesi iliyofunguliwa na Ado Shaibu akipinga uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali(AG).

    Mahakama Kuu iliamuru Fatma apelekwe kamati ya maadili kwa madai ya kushambulia ofisi ya Mwanasheria Mkuu.

    Sababu yake ilitajwa kuwa kile alichokizungumza katika kesi iliofunguliwa na katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano katika chama cha Wazalendo Ado Shaibu kupinga uteuzi wa Mwanasheria mkuu wa serikali Dkt Adelarus Kilangi aliyeteuliwa na rais John Pombe Magufuli mnamo February Mosi 2018.

    Wiki hii Fatma karume aliachishwa kazi kastika kampuni ya uwakili ya IMMA alipokuwa akifanya kazi kwa kile kilichotajwa kuwa amekuwa mwanaharakati harakati.

  5. Bunge laamua hatma ya uchaguzi Ethiopia

    Bunge la Ethiopia limepitisha azimio la kuruhusu taifa hilo kuhairisha uchaguzi mkuu na kutaka ufanyike ndani ya mwaka mmoja.

    Mwaka mpya wa Ethiopia unaanza Septemba 11, hivyo uchaguzi utafanyika kabla ya mwezi Septemba mwaka huu.

    Bunge limepitisha azimio hilo katika kikao maalum kilichofanyika Jumanne.

    Mbunge mmoja alipiga kura kupinga azimio hilo wakati nane waliridhia, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Ethiopia.

    Taifa hilo limehairisha uchaguzi kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.

    Ikiwa ukanda wa kaskazini wa Tigray ukiendelea na uchaguzi basi utatambulika kuwa batili, waziri mkuu Abiy Ahmed alieleza.

    Chama cha Tigray People’s Liberation Front (TPLF) kilishinda kwa kura za 98% katika uchaguzi wa kikanda.

    Kiongozi wake, Debretsion Gebremichael,alitaja uchaguzi huo kuwa wa kihistoria.

  6. Wakenya sasa ruksa kushiriki mazishi ya waliokufa na corona

    Kuanzia sasa raia wa Kenya wataweza kushiriki shughuli za mazishi ya wapendwa wao waliofariki kutokana na virusi vya corona baada ya serikali kulegeza masharti tofauti na awali ambapo walipiga marufuku.

    Awali ndugu wa karibu wa mtu aliyekufa kwa corona hakuruhusiwa kufanya chochote zaidi ya kuangalia kwa mbali wakati maafisa wa afya waliojihami kwa mavazi maalum wakifanya shughuli za mazishi.

    Maafisa wa afya wamesema kuwa miili ya marehemu waliokufa kutokana na maambukizi ya virusi vya corona haiwezi kuambukiza virusi hivyo.

    Shirika la afya duniani (WHO) na kituo cha kudhibiti magonjwa Afrika CDC hawajasema bado kama maiti haiweza kuambukiza Covid-19, lakini wamebadilisha utaratibu na kuruhusu familia kuaga wapendwa wao.

    Nchini Kenya', maofisa wa afya watakuepo katika mazishi ili kutoa muongozo na kuhakikisha usalama unazingatiwa.

    "Tutaruhusu shughuli zote za mazishi za kidini na kitamaduni kufuatwa kulingana na tamaduni za marehemu,"

    Serikali imekiri kuwa zuio waliloliweka mwezi uliopita lilikuwa gumu kufuatwa.

  7. Kiongozi wa upinzani Zimbabwe akatazwa kutumia mitandao ya kijamii

    Mwanasiasa wa upinzani nchini Zimbabwe,Job Sikhala ameachiwa kwa dhamana baada ya kuwekwa mbaroni mwezi uliopita akihusishwa na maandamano dhidi ya serikali.

    Bwana Sikhala alikamatwa tarehe 21 Agosti, na kushtakiwa kwa kosa la uchochezi na uhamasishaji wa vurugu.

    Alikamatwa na polisi kufuatia maandamano yaliyotokea tarehe 31,Julai.

    Bwana Sikhala ameachiwa huru Jumanne baada ya kutoa dhamana ya $590 na kupewa amri ya kutoweka ujumbe wowote mtandaoni na kwenye makundi ya WhatsApp.

    Chama chake cha 'Movement for Democratic Change' kiliandika kwenye kurasa ya tweeter.

  8. Viongozi wa Afrika wapongezwa kupambana na Covid-19

    Mkuu wa kituo cha kudhibiti magonjwa Afrika (CDC) amewasifu viongozi wa Afrika kwa kuunga mkono jitihada za pamoja za kushughulikia janga la virusi vya corona.

    John Nkengasong ameiambia BBC kuwa mkakati wa afya ya umma barani Afrika , ukiwemo wa ongezeko la upimaji, kuwafikia wale waliohusiana na walipata corona pamoja na uvaaji wa barakoa umeweza kushusha kiwango cha maambukizi ya virusi vya corona.

    Shirika la afya duniani (WHO) awali lilisema kuwa mlipuko wa Covid-19 barani Afrika unaweza kuwa makubwa zaidi.

    Jumatatu , takwimu mpya zimeonesha kuwa virusi vipya vya corona vimeshuka barani Afrika kwa asilimia kumi na mbili -12%.

    Dkt Nkengasong alisema:Takwimu zinawakilisha jitihada za kiafya za umma na viongozi wa bara zima kwa ujumla katika kulinda afya.

    Virusi hivi katika jumuiya yetu vilihitaji umoja wetu katika kupambana dhidi ya janga hilo na hicho ndicho tulichofanya.

    Alisema bara hili lilikabiliana na ugonjwa kama Ebola ambao umeweza kusaidia kuweza kujua namna ya kukabiliana na janga la virusi vya corona.

    Amesema hatua ambazo zimechukuliwa na nchi tofauti zimeweza kusaidia kukabiliana na janga hili kwa urahisi.

  9. 'Sherehe za kimila ruksa Uganda' licha ya Covid 19

      • Author, Isaac Mumema
      • Nafasi, BBC Swahili

    Serikali ya Uganda imeiruhusu jamii ya Bamasaba Mashariki mwa nchi hiyo kuendelea na utamaduni wao wa jadi wa kuwapasha tohara vijana ambao hufanyika katika kipindi hiki kila baada ya miaka miwili.

    Tamasha au sherehe zinazohusiana na utamaduni huo zitazingatia kanuni za kudhibiti janga la COVID-19.

    "Kwa kufuata masharti ya watalaamu wa afya, wamekubaliana na viongozi wa kitamaduni kufanya zoezi la Embalu, lakini wasisherekee kwa kupiga ngoma ya kadodi, kwa sababau ngomo hiyo ndiyo inaleta mkusanyiko mkubwa wa watu..Jeshi la polisi lifanye uangalizi wa zoezi hilo la Embalu" rais Museveni ameeleza.

    Rais Museveni amewaruhusu Bamasaba katika hotuba yake aliyoitoa mwishoni mwa juma siku ya jumapili,

    "Utamaduni huu ni muhimu sana kwa Bamasaba mara mvulana akifikisha umri wa kuanzia miaka 15," Mzee Wamoto Wambete amesema.

    Sherehe za Embalu hufanyika mara mbili kwa mwaka, kutokana na janga la COVID19 huenda hazitafanyika za mara ya pili za kufunga mwaka anaelezea tena Mzee Wamoto:

    Utamaduni wa Embalu ya Bamasaba unawakusanya pia ndugu zao waliko Kenya Babukusu kushirki katika sherehe hizo , ambapo tayari sekita ya utalii nchini Uganda imeziweka katika vivutio vya watalii nchini.

  10. Maandamano dhidi ya serikali yawajerui wengi Cameroon

    Raia mmoja ameuawa na wengine kujeruhiwa nchini Cameroon katika maandamano ya kuipinga serikali yaliofanyika maeneo mbalimbali nchini humo siku ya Jumanne, kwa mujibu wa wakili wa chama cha upinzani.

    Wakili huyo, bwana Robert Amsterdam, ameweka kwenye kurasa ya tweeter video ya mwandamanaji akiwa amelala na hapumui.

    Aliandika: "Tumepokea ripoti kuwa muandamanaji mmoja alipigwa risasi na kuuawa na polisi katika mji wa Douala na wengine wengi walikuwa wamejeruhiwa na kukamatwa."

    Serikali ilitoa onyo dhidi ya maandamano hayo yaliyohamasishwa na kiongozi wa upinzani Maurice Kamto.

    Waandamanaji walitaka mgogoro wa 'Anglophone' ufikie tamati na mabadiliko yawekwe kwenye utaratibu wa uchaguzi.

    Bwana Kamto amesema kuwa kama masuala mawili aliyopendekeza hayatafanyiwa kazi , basi maandamano yataendelea mpaka rais Paul Biya atakapolazimka kutoka madarakani.

    Bwana Biya amekuwa madarakani tangu mwaka 1982. Alichaguliwa tena mwaka 2018 katika uchaguzi ambao bwana Kamto aidai kuwa ameshinda.

  11. Karibu katika matangazo mubashara