Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Sauti ya Museveni iliathirika kwa barakoa aliyoivaa Tanzania
Rais wa Uganda,Yoweri Museveni amepata ahueni baada ya sauti yake kupotea kutokana na barakoa aliyoivaa kipindi alipozuru Tanzania, wiki moja iliyopita.
Moja kwa moja
Esther Namuhisa
Sauti ya Museveni iliathirika kwa barakoa aliyoivaa Tanzania
Rais wa Uganda,Yoweri Museveni amepata ahueni baada ya sauti yake kupotea kutokana na barakoa aliyoivaa kipindi alipozuru Tanzania, wiki moja iliyopita.
Bwana Museveni alisema barakoa inalinda watu dhidi ya virusi vya corona hivyo ilimbidi avae barakoa wakati wa safari yake nchini Tanzania "niliporejea sauti yangu ilikuwa imeathirika".
Hakutoa ufafanuzi kuhusu changamoto aliyoipata lakini Jumamosi alisitisha safari yake ya kwenda mjini Jinja mashariki mwa Uganda. Hivyo alimtuma makamu wa rais Edward Ssekandi kumuwakilisha.
Hata hivyo mwenyeji wake rais wa Tanzania, John Magufuli hakuwa amevaa barakoa wakati rais Museveni alipomtembelea nchini mwake.
Ingawa rais Magufuli alifanya wageni kucheka baada ya kumnukuu rais Museveni alipomuuliza kama anaweza kuvaa barakoa naye akamjibu anaweza kuja hata akiwa amevaa blanketi.
Viongozi hao wawili walikutana kutia saini makubaliano kuhusu ujenzi wa bomba la mafuta.
Zaidi ya vifo 300 vya tembo vimesababishwa na sumu Botswana
Mwaka huu, zaidi ya vifo 300 vya tembo nchini Botswana vimesababishwa na sumu katika maji, lakini bado kuna maswali mengi ambayo hayana majibu, maofisa wa wanyama pori wamenukuliwa na wakala wa habari Reuters.
Vifo hivyo vinavyotokea katika mkondo wa maji wa Okavango vimewashtua wahifadhi na kuwafanya wachunguze kisa cha vifo hivyo, ikiwa hakuna dalili za wanyama wengine kufa wakati huohuo.
Reuters imemnukuu Mmadi Reuben, afisa mifugo kutoka idara ya wanyama pori na hifadhi za taifa, amesema vipimo vya mwisho vimeonesha kuwa chanzo cha vifo hivyo ni bakteria wanaofahamika kama 'cyanobacterial neurotoxins'.
"Bakteria hao huwa wanapatikana katika maji. Ingawa bado kuna maswali mengi ambayo hayajapata majibu kama vile kwa nini ni tembo tu ndio wanakufa na kwanini katika eneo moja tu.Utafiti unaendelea kufanyika kutoka kwa wataalamu kadhaa," aliongeza.
Wakati mkurugenzi wa idara ya wanyama pori na hifadhi ya taifa bwana, Cyril Taolo, alisema idadi ya vifo vya tembo imeongezeka kutoka 281 ambayo iliripotiwa Julai mpaka kufikia 330, Reuters imeripoti.
Namna mpya ya utafutaji ajira Tanzania
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Humphery Mgonja
- Nafasi, BBC Field Producer
Katika kutatua changamoto ya ajira nchini Tanzania, wahitimu waliosoma vyuo mbalimbali nje ya nchi wamekutanishwa pamoja huku makampuni, taasisi binafsi na taasisi za serikali zinazohitaji wataalamu waliobobea kwenye nyanja za kiuchumi teknolojia, afya na utawala walialikwa ili kuelezea ujuzi wao kwa lengo la kufungua milango ya kuajiriwa.
Wazo hilo limeanzishwa na kuratibiwa na taasisi inayohusika kutaftia wanafunzi ufadhili wa masomo nje ya nchi Global education link.
Abdulmalik Mollel mkurugenzi wa taasisi ya mtandao wa elimu anasema ‘’ imekuwa siku ya kipekee maana waajiri wataweza kuona wataalamu wanaowafaa na kuwachagua wenyewe kwa hiyo tukio hili linawapa fursa kuwakutanisha waajiri na wanaotafuta ajira sisi tumetumika kama daraja la kufanikisha hili’’
Kwa upande wa wahitimu hao wanaona jukwaa hilo ni fursa muhimu kuonesha uwezo wao ili waajiri kuepuka kukimbilia kuajiri wageni na kuacha wazawa ambao wamebobea katika fani mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Zaidi ya wahitimu elfu tatu walihudhuria pamoja na taasisi zinazotoa ajira zaidi ya kumi ,huku tukio hilo likienda sambamba na mahafali ya wahitimu waliomaliza masomo yao nje ya nchi na kushindwa kufanya sherehe katika nchi hizo sababu ya mlipuko wa virusi vya korona ‘’
Makanisa yanaweza kufungwa tena Sudani Kusini
Askofu wa kanisa katoliki mjini Juba nchini Sudani Kusini, Stephen Ameyu Martin, ametoa angalizo kuwa kanisa katoliki linaweza kufunga tena makanisa yake nchini humo kutokana na ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona.
Huduma za ibada za Kanisa katoliki nchini humo zilifunguliwa Jumapili baada ya kufungwa kwa kipindi cha miezi sita ,huku kukiwa na hatua kali za udhibiti wa afya.
Rais Salva Kiir na viongozi wengine wa ngazi za juu ni miongoni mwa waumini waliohudhuria misa Jumapili, katika mji mkuu wa Juba.
Askofu alisema walikuwa wanasubiri ruhusa kutoka Vatican kabla ya kurejesha huduma za misa.
“Kama mlipuko utaongezeka basi watafunga tena makanisa kwa sababu lengo letu la kuja kusali ni kuwa na maisha marefu.Lakini kama tunasali na tunapata maambukizi zaidi - tutakuwa hatutunzi maisha yetu, ni kama tunatoa bure maisha yetu katika mlipuko,” aliwaambia waamini.
Misikiti na makanisa ya madhehebu mengine yalifunguliwa wiki mbili baada ya serikali kulegeza masharti dhidi ya corona.
Walimu watakiwa kurejea shuleni Kenya
Walimu wa shule za msingi na sekondari nchini Kenya wametakiwa kuripoti katika shule wanazofundishia kuanzia Septemba 28, Jumatatu ili kujiandaa na kufunguliwa kwa shule.
Mtandao wa Citizen umeandika, mwenyekiti wa tume ya elimu,bi. Sara Ruto kutoka Taasisi ya maendeleo ya mitaala Kenya(KICD) amependekeza shule kufunguliwa katikati ya mwezi Oktoba.
Hatahivyo, waziri wa elimu bwana George Magoha amesema siku rasmi ya kufunguliwa shule itatangazwa baada ya kamati kufanya mazugumzo.
“Si mimi ninayetoa tarehe ya kufungua shule, nitakaa meza moja na kamati na kujadili siku ya kufungua shule" alieleza Prof. Magoha.
Aidha wanafunzi ambao wanafanya mitihani ya mwisho mtawaona wakiwasili shuleni kwanza na wanafunzi wengine watarejea shule ndani ya wiki chache.
Darasa la saba, darasa la nane, kidato cha tatu na nne wanatarajiwa kuanza kwenda shule kwanza.
Vital Kamerhe anatarajiwa kusikiliza kesi yake leo hii
Mshirika mkuu wa serikali ya rais Felix Tshisekedi nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Vital Kamerhe anatarajiwa kufika mahakamani leo hii baada ya kushindwa kuhudhuria Ijumaa kutokana na sababu za kiafya.
Bwana Kameme alihukumiwa kifungo cha miaka 20 kwa kosa la ufisadi na wizi wa takriban dola milioni 50 za Marekani.
Aidha Kamerhe hatoruhusiwa kuwania wadhfa wowote kwa miaka 10 baada ya kuhudumia hukumu yake na hata kushikilia wadhfa wowote wa serikali.
Kamerhe ndiye aliyesababisha Tshisekedi leo hii awe Rais wa DRC.
Kupitia Muungano walioufanya wa CACH, wawili hao walifanikiwa kumshinda Martin Fayulu aliyekuwa akipewa nafasi kubwa ya kuwa mbadala wa Rais Joseph Kabila, aliyemaliza muda wake wa kikatiba kuongoza DRC.
Upinzani Ivory Coast wampinga rais kuwania muhula wa tatu
Wapinzani wakuu wa uchaguzi wa urais nchini Ivory Coast wamewataka raia kuandamana ili kumzuia rais Alassane Ouattara kuwania muhula wa tatu wa nafasi ya urais, katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao.
Henri Konan Bédié –rais wa zamani wa taifa hilo –alitangaza kuwa vyama vya upinzani viliungana ili kulinda Amani.
Takribani watu 10 wameuawa tangu ghasia zianze mwezi uliopita baada ya bwana Ouattara kutangaza kuwania tena nafasi ya urais baada ya mrithi aliyechaguliwa kufariki ghafla.
Uchaguzi huo unaonekana kuwa mtihani mkubwa wa kulinda amani ya mataifa ya Afrika Magharibi , tangu mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliosababishwa na uchaguzi, miaka 10 iliyopita.
Sudan yataka kuondolewa katika orodha ya wafadhili wa ugaidi
Sudan imetuma ujumbe wa kiwango cha juu kwenda Falme za Kiarabu ili kufanya mazungumzo na maofisa wa Marekani, wakati nchi hiyo ikijaribu kutaka kuondolewa katika orodha ya mataifa yanayoufadhili ugaidi.
Ujumbe wa Sudan unaongozwa na kiongozi wa taifa hilo Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.
Mwaka 1993, Marekani iliiongeza Sudan katika mataifa yanayowaunga mkono wanamgambo wa kiislamu (IS) pamoja na Osama Bin Laden – ambaye aliishi nchini humo kwa miaka mitano.
Sehemu ya mazungumzo hayo, Marekani imeitaka Sudan kulipa zaidi ya dola milioni 300 (£232m) kama fidia kwa familia ambazo ni wahanga wa shambulio hilo.
Serikali ya Marekani inataka kujaribu kuishawishi Sudan kuwa na uhusiano mzuri na Israel.
Uganda kufungua milango kwa watalii
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ametangaza kulegeza masharti ya kudhibiti Ugonjwa wa corona kwa kufungua mipaka ya kimataifa na kuruhusu utalii kurejea.
Aidha raia wa Uganda wanaorejea kutoka nje ya nchi watalazimika kujitenga nyumbani kwa muda wa siku 14.
Rais Museveni akihutubia kupitia matangazo ya televisheni siku ya Jumapili, amesema wageni wanaowasili nchini humo wanalazimika kufanya vipimo vya corona, saa 72 kabla ya kuwasili.
Nyumba za ibada zimefunguliwa lakini idadi ya waumini imetakiwa kutozidi watu 70.
Hata hivyo wanafunzi wanaomaliza shule ya msingi, sekondari na taasisi za ufundi na biashara watafungua shule katikati ya mwezi Oktoba mwaka huu.
Museveni amesema madarasa mengine yatafunguliwa Januari mwakani.
Vilevile makatazo ya kuzuia usafiri wa umma na binafsi yameondolewa.
Michezo ya nje imeruhusiwa kurejea, lakini haitakuwa na mashabiki.
Wachezaji walikuwa katika msimu wa kujitenga na wanapaswa kuwa wamepimwa saa 72 kabla ya michuano katika kila wiki mbili.
Makatazo mengine kama zuio la mikusanyiko ya umma na kutembea usiku kuanzia saa tatu hadi 12 asubuhi litaendelea.
Rais Museveni amelegeza masharti ya kudhibiti ugonjwa wa covid 19 licha ya maambukizi ya ugonjwa huo kuongezeka na kufikia 6,287, huku vifo vikifikia 63.
Karibu katika matangazo mubashara