Chombo kingine cha habari chafungiwa Tanzania
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekifungia kituo cha utangazaji cha Wasafi FM kwa muda wa siku saba kuanzia Septemba 12 hadi Septemba 18 mwaka huu.
Moja kwa moja
Ambia Hirsi
Chombo kingine cha habari chafungiwa Tanzania

Chanzo cha picha, Tweeter/Wasafi
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekifungia kituo cha utangazaji cha Wasafi FM kwa muda wa siku saba kuanzia Septemba 12 hadi Septemba 18 mwaka huu.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya kituo hicho kukiuka kanuni za Mawasiliano ya kielektroniki na posta katika utangazaji wa radio na televisheni za mwaka 2018 ambazo zinamtaka mtangazaji kutangaza maudhui ya staha.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba amesema kuwa ukiukwaji huo wa kanuni uliofanyika katika vipindi vya The Switch na Mashamsham, utasababisha kituo hicho kusitisha huduma za utangazaji kwa muda wa siku saba na kuomba msamaha kwa siku ya leo.
Aidha adhabu hiyo si kwamba itakuwa aina hiyo kwa wote, bali inaweza kubadilika.
Mwanzoni mwa mwezi huu, chombo kingine cha habari Clouds media kilifungiwa kwa kukiuka kanuni ndogo za uchaguzi.
Makazi ya msemaji wa serikali ya Uganda yashambuliwa
Polisi nchini Uganda wanalifanyia uchunguzi shambulio lililotokea nyumbani kwa msemaji wa serikali ,nje kidogo ya mji mkuu wa Kampala.
Msemaji huyo, Ofwono Opondo,aliandika katika kurasa yake ya mtandao wa Tweeter usiku wa Alhamisi kuwa amepoteza mawasiliano na familia yake ambayo ilikuwa inashambuliwa nyumbani.
Bwana Opondo aliviambia vyombo vya habari nchini humo kuwa watu wengi walivamia nyumbani kwake na kuifungia familia yake katika chumba kimoja wakati wakiiba vyumba vingine.
Naibu msemaji wa Polisi , Polly Namaye amethibitisha tukio hilo na kusema kuwa familia ipo salama ingawa bado wapo katika mshtuko.
Polisi bado wanafuatilia washukiwa wa tukio hilo.
Yanga yazindua jezi mpya
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Humphery Mgonja
- Nafasi, BBC Field Producer

Chanzo cha picha, Yanga
Klabu ya soka ya Yanga ya Tanzania leo hii imezindua jezi zake itakazotumia katika msimu wa 2020/ 2021.
Yanga wamezindua jezi hizo watakazotumia katika msimu huu ikiwa tayari msimu wa ligi kuu Tanzania bara umekwisha anza kwa mzunguko mmoja kuchezwa.
Katika mchezo wa kwanza wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Yanga ama wapenzi wa soka wakiita timu ya wananchi walitumia jezi ya msimu uliopita kutokana na jezi hizi zilizozinduliwa kutokuwepo.

Chanzo cha picha, Yanga
Wadhamini wa klabu hiyo kampuni ya GSM walieleza sababu ya kuchelewa kuzinduliwa kwa jezi hizo ni sababu ya usafiri kutokana na janga la Corona hivyo ndio maana jezi hizo zilichelewa kuwasili nchini Tanzania.
Yanga itashuka dimbani siku ya jumapili kucheza na Mbeya City katika mchezo wa mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania bara.
Kenya kushiriki katika jaribio la chanjo ya Oxford

Chanzo cha picha, Reuters
Kenya itashiriki hatua za mwisho za jaribio ya kitabibu la chanjo ya virusi vya corona ambayo inatengenezwa na AstraZeneca na chuo kikuu cha Oxford.
Taifa hilo litakuwa la pili kutoka barani Afrika kushiriki katika jaribio ambalo lilisitishwa siku ya Jumatano, baada ya mshiriki mmoja kutoka Uingereza kupata madhara.
Tayari zaidi ya washiriki 1,000 kutoka Afrika Kusini wamehusishwa katika jaribio hilo kutoka Afrika Kusini.
Wafanyakazi wa afya wapatao 400 watashiriki katika jaribio ambalo litafanyika nchini Kenya katika pwani ya Mombasa na Kilifi.
Miji hiyo miwili ndio ilichaguliwa na serikali.
Chanjo inayotengenezwa na AstraZeneca-chuo kikuu cha Oxford ni miongoni mwa majaribio tisa mengine ambayo yamefanyika katika sehemu kubwa ya dunia.
Washiriki watapewa chanjo mara mbili katika wiki nne.
Na wataruhusiwa kuendelea na shughuli zao za kawaida. Kupata virusi hakutawafanya kutoka katika jaribio.
Jaribio litaangalia usalama wa chanjo, uwezo wa uzalishaji wa kinga na ufanisi wake.
Matokeo ya awali yatatolewa mnamo mwezi Novemba.
Msumbiji yapinga madai ya Amnesty International kuwa inawatesa wafungwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Amnesty inalaumu wanajeshi wa Msumbiji kwa ukiukwaji wa haki za binadamu Jeshi la Msumbiji limekanusha tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu iliyotolewa dhidi yake na shirika la kutetea haki la Amnesty International kufuatia juhudi zake za kukabiliana na wanamgambo wa kiislamu katika mkoa wa Cabo Delgado kaskazini mwa nchi hiyo.
Mapema wiki hii Amnesty International iliwalaumu wanajeshi wa Msumbiji kwa kuekeleza mauaji, na kuwatesa wafungwa wanaoazuiliwa katika kile kinadai kuwa mauaji ya kiholela na kusafirisha idadi kubwa ya maiti na kuzizika katika makaburi ya pamoja.
Shirika hilo linatumia ushahidi ambao linasema ni kanda ya video na picha ambazo "limethibitisha" kutoka eneo hilo zikionesha uhalifu unaotekelezwa dhidi ya wafungwa wanaozuiliwa na maafisa hao.
Lakini msemaji wa wizara ya ulinzi ya Msumbiji, Omar Saranga, anasema Amnesty haikuzingatia picha hizo huenda zimetolewa na waasi ili kudhalilisha jeshi.
Pia amelishutumu Amnesty International kwa "kukaa kimya dhidi ya unyama ambao umekuwa ukitekelezwa katika mkoa wa Cabo Delgado tangu 2017".
WHO na Afrika CDC yazindua mtandao wa maabara ya Covid-19

Chanzo cha picha, AFP
Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kituo cha kuzuia na kudhibiti magonjwa Afrika (CDC) wamezindua mtandao mpya wa maabara ambao utaimarisha mpangilio wa uchunguzi wa virusi vya corona barani Afrika.
Mpango huo unachunguza uwezekano wa kuzaana kwa virusi vya corona ili kujiandaa vyema kutoa huduma katika sekta ya afya ya umma.
Wataalamu kutoka WHO na kituo cha CDC Afrika wanaamini hatua hiyo itasaidia nchi kuelewa tofauti kati ya chembe chembe ya virusi vya SARS na vile vya Cov-2, ili kuimarisha uwezo wa nchi kujitayarisha kwa matibabu au uwezekano wa kupata chanjo.
Maabara 12 maalum zitajumuishwa kwenye mtandao huo barani Afrika.
Hatua hiyo inakuja baada ya CDC Afrika kusema kuwa ripoti za awali zilikuwa zinaonesha kuwa viwango vya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 vinashuka katika hali ambayo imepunguza idadi ya watu wanaoambukizwa virusi na wale wanaofariki kutokana na virusi hivyo ikilinganishwa na maeneo mengine dunani.
WHO hata hivyo imeonya hatua ya kusherehekea mapema matokeo hayo kwasababu baadhi ya nchi za Afrika haziwafanyii vipimo raia wao ikilinganishw ana maeneo mengine duniani.
Morocco yavunja mtandao wa kupanga njama za IS
Polisi nchini Morocco wanasema kuwa wamevunja mtandao wa wanamgambo wa kundi la Islamic State ambao ulikuwa unapanga kufanya mashambulio ya mabomu.
Watu watano wamekamatwa katika misako tofauti iliyofanywa katika miji ya Tangiers na Rabat.
Mishipi ya kufungia vilipuzi na vifaa vingine vilipatikana katika misako hiyo.
Washukiwa wanasemekana walikuwa wanapanga kufanya mashambulio yaliolenga kuvuruga ustawi wa nchi.
Hakuna maelezo yaliyotolewa kuhusu ni wapi walilenga kutekeleza mashambulio hayo.
Mabaki ya samaki maarufu wa Zambia 'yatoweka'

Chanzo cha picha, Edgar Lungu/Facebook
Mabaki ya 'Mafishi' – samaki maarufu wa Zambia ambaye kifo chake kimeombolezwa tangu Jumatatu – yametoweka mahali iliyokuwa imehifadhiwa.
Samaki huyo aliishi kwenye kidimbwi cha Chuo Kikuu cha Copperbelt (CBU) kwa zaidi ya mwongo mmoja na wanafunzi walimchukulia kama chanzo cha bahati.
Aliombolezwa na viongozi wakuu serikalini akiwemo rais Edgar Lungu na baadhi ya mawaziri wake.
Naibu Chansela wa CBU Naison Ngoma, amethibitisha kutoweka kwa mabaki ya mafishi na kuongeza kuwa uchunguzi umeanzishwa kubaini kilichotokea, kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la Zambia Daily Mail.
“Nalifahamishwa kwamba samaki huyo alianza kutoa harufu mbaya kwenye jokovu Iakini nilipoulizia yuko wapi niliambiwa ametoweka’’alinukuliwa kusema.
Prof Ngoma anasema huenda samaki huyo ameliwa au kutupwa.
Ameongezea kuwa hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya wale waliohusika na kutoweka kwa samaki huyo.
Karibu katika matangazo mubashara

