Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Magufuli asifu Kiswahili kuwa miongoni mwa mafanikio yake SADC
Rais wa Tanzanania John Magufuli amkabidhi uenyekiti wa SADC rais wa Msumbiji Felipe Nyusi.
Moja kwa moja
Seneta aachiwa huru baada ya mandamano
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Faith Sudi
- Nafasi, BBC Swahili, Turkana
Wakaazi wa mji wa Bomet nchini Kenya wameandamana kulalamikia kukamatwa kwa seneta wao Dkt. Christopher Langat.
Seneta huyo ni mmoja wa maseneta watatu ambao wamekamatwa kutokana na kile maseneta wengine wanadai ni kuwazuia kupiga kura ya ugavi wa hela ambayo inajulikana kama "one man one shilling one vote".
Waliokamatwa ni pamoja na seneta wa kaunti ya Kakamega bwana Cleophas Malala na seneta wa Samburu Dkt. Steve Lelegwe.
Hata hivyo suala la iwapo kikao kiahirishwe hadi watatu hao wapatikane liligomba mwamba baada matokeo ya kura kutoka sawa.
Seneta 29 wakiunga mkono na 29 kupinga.
Hata hivyo seneta huyo wa Bomet ameachiliwa Kulingana na ujumbe ambayo wakili wake Nelson Havi amechapisha kwenye amtandao wake.
Leo Katika Dira ya Dunia...
Idadi ya vifo yaongezeka katika shambulio la kigaidi Somalia
Takribani watu 17 wanaaminika kuuawa kufuatia shambulio la kigaidi lililotoa katika hoteli iliyoko ufukweni mwa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Shambulio hilo lilikomeshwa na kikosi maalumu cha jeshi .
Watu kadhaa wamejeruhiwa katika ghasia hizo ambazo rais wa Somalia Mohammed Farmajo, amewalaumu wanamgambo wa kundi la al-Shabab.
Watu takribani 200 wameokolewa katika hoteli hiyo.
Awali msemaji wa serikali alisema watu 11 wamefariki pamoja na wanamgambo watano.
Polisi imesema watu waliouawa ni pamoja na maafisa wawili wa serikali, walinzi watatu wa hoteli, raia wanne na wengine hawakuweza kutambuliwa.
Hoteli ya Elite ipo katika eneo ambalo lina ulinzi mkali mjini Mogadishu na maarufu kwa kuwa na wageni wanasiasa, wafanyabiashara, waandishi na wanaharakati.
Maseneta wakamatwa siku ya kupigia kura bajeti
Maseneta watatu nchini Kenya “wamekamatwa” siku ya kuipigia kura bajeti inayoainisha Kaunti za taifa hilo.
Matokeo ya kura hizo yamehairishwa kwa mara ya nane sasa kwa kushindwa kufikiwa makubaliano ya mfumo wa kusambaza dola bilioni 2.9 katika kaunti zote 47.
Kiongozi wa zamani wa Upande wa Serikali katika Seneti Bwana Kipchumba Murkomen amewaambia maseneta Jumatatu, kuwa seneta Cleophas Malala pamoja na seneta Christopher Langat walikamatwa wakiwa majumbani kwao, mjini Nairobi, wakati Ltumbesi Lelegwe alikamatwa akiwa anaelekea bungeni.
Polisi hawajibu lolote bado kuhusu madai hayo.
Leo hii wabunge wametaka hatua hiyo ya upigaji kura kwa bajeti ya Kaunti kuhairishwa na badala yake kujadala kuhusu madai ya kukamatwa kwa wenzao watatu.
Magufuli asifu Kiswahili kuwa miongoni mwa mafanikio yake SADC
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Aboubakar Famau
- Nafasi, BBC Africa, Dar es Salaam
Rais wa Tanzania John Magufuli ambaye pia ni mwenyekiti aliyemaliza muda wake wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa nchi za Afrika SADC ameisifu Jumuiya ya kimataifa kwa kulegeza vikwazo vya kiuchumi vilivyowekewa nchi ya Zimbabwe mwaka 2000.
Magufuli ameyasema hayo hii leo katika mkutano wa 40 wa Jumuiya hiyo ambao umefanyika kwa njia ya video huku yeye akiwa katika ikulu ya Chamwino huko katika makao makuu ya Tanzania Dodoma.
"Baadhi ya mafanikio yameanza kupatikana, mathalan, Umoja wa Ulaya umeanza kuona umuhimu wa kutatua mgogoro wa kibinadamu nchini humo kwa kutoa misaada ya kuonyesha utayari wa kusaidia utaalamu kwenye sekta za maendeleo," amesema rais Magufuli.
Magufuli amesema pia baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chake cha uenyekiti ni pamoja na Kiswahili kufanywa kuwa lugha ya nne rasmi katika Jumuiya hiyo.
Mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya SADC umefanyika katika mazingira tofauti na ilivyo miaka yote. Kutokana na janga la Covid19, wakuu hao hawakuweza kukutana sehemu moja, hivyo umeendeshwa kupitia njia ya mtandao.
Mwenyekiti mpya wa Jumuiya hiyo kwa sasa ni rais wa Msumbiji bwana Filipe Nyusi.
Makanisa yafunguliwa DRC baada ya miezi mitano
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Mbelechi Msochi
- Nafasi, BBC Swahili
Huduma za ibada katika makanisa ya nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), zimerejea baada ya takribani miezi mitano iliyopita.
Makanisa hayo yalifungwa kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.
Jumapili hii, mamia ya Wakristo nchini humo wamejumuika kwa pamoja katika sala wakiwa na shangwe kubwa.
Makanisa yakiwa na vifaa vya kunawia mikono na vipima joto huku kila mkristo akivalia barakoa.
Huku polisi wakiwa na mavazi ya kiraia wakiwepo katika makanisani kuhakikisha kuwa muongozo wa kujikinga dhidi ya corona unafuatwa.
Aidha ibada hizo zimewagawa waumini kuingia kwa awamu katika ibada ili kupunguza msongamano.
Lakini hatua hii imekuja wakati ambao baadhi ya waangalizi wakihofia kuongezeka zaidi kwa visa vya maambukizi ya corona.
Hata hivyo kwa sasa DRC, imefungua mipaka yake na usafiri wa ndege na gari unaruhusiwa kutoka jimbo moja kwenda jimbo lingine.
Rwanda yafunga masoko makuu baada ya ongezeko la virusi vya corona
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Yves Bucyana
- Nafasi, BBC Swahili
Rwanda imefunga masoko makuu ya jijini Kigali kwa muda wa siku 7 kutokana na ongezeko kubwa la maambukizi ya virusi vya corona.
Masoko yaliyofungwa ni pamoja na soko kuu la Nyarugenge mjini Kati na soko la Nyabugogo maarufu kwa walanguzi.
Wizara ya afya imetangaza kwamba itaanzisha zoezi la kufanya vipimo vya watu kwenye masoko yanayoendelea na shughuli zake kwa muda wa wiki mbili kabla ya kuchukua mikakati zaidi.
Kulingana na wizara ya afya ya Rwanda watu 151 walipatikana na virusi vya corona kufuatia sampuli zilizochukuliwa mnamo siku mbili zilizopita,wengi wao walipatikana katika masoko hayo.
Rwanda imekwisharekodi visa 2,453 vya Covid19.watu 1,648 walipona,wengine 797 bado wanapata matibabu na 8 walikufa.
Kwa upande mwingine wizara ya mambo ya ndani imesema kwamba baadhi ya masoko yatahamishiwa nje ya jiji la Kigali kwenye sehemu zilizo wazi ili kupunguza msongamano kwenye masoko.
Zimbabwe yakataa lawama za maaskofu wa kanisa katoliki
Serikali ya Zimbabwe imekataa kupokea barua ya lawama ambayo imeandikwa na maaskofu wa kanisa katoliki, ikugusia masuala ya rushwa, umaskini na unyanyasaji wa haki za binadamu.
"Hakuna janga la kisiasa wala jambo lingine lolote", katibu wa masuala ya habari Bwana Nick Mangwana ameeleza.
Aidha amelishutumu Barazala maaskofu Wakatoliki nchini humo kuanzisha makundi ambayo yanaweza kusababisha ghasia.
Maaskofu walilitaka taifa lifanye maamuzi ya haraka ya kukabiliana na changamoto za kiuchumi na siasa.
"Hali mbaya iliyopo Zimbabwe, imesababisha uchumi kuanguka, kuongezeka kwa umasikini na ukiukaji wa haki za binadamu," wameandika Maaskofu saba kutoka miji mbalimbali ya Zimbabwe.
"Rushwa imefikia kiwango cha hatari mno," waliongeza.
Raia wa Zimbabwe wamekuwa wakiandamana wakiishutumu serikali kwa rushwa na kudhoofisha uchumi kwa zaidi ya asilimia 70%.
Rais Emmerson Mnangagwa anawalaumu wapinzani wa kisiasa kwa kushirikiana na wageni kujaribu kulididimiza taifa hilo.
Hivi karibuni serikali ya Zimbabwe imepokea lawama nyingi kutokana na maandamano na kusababisha watu kadhaa kushambuliwa na kukamatwa.
Watu 12 wauawa na wanamgambo mashariki mwa Kongo
Watu kumi na wawili wameuawa ndani ya siku tatu na wanamgambo mjini Beni, mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, maafisa nchini humo wameliamba shirika la habari la AFP.
Kundi la wanamgambo la ADF walishambulia vikosi vya jeshi la serikali katika kijiji cha Mwenda usiku wa Jumamosi, na kuwaua watu wanane, kiongozi wa kijiji Donat Kibwana alinukuliwa akisema na vyombo vya habari.
Wakulima wanne waliuawa wakiwa shambani katika kijiji cha jirani cha Mbau, siku ya Jumamosi, shirika AFP lilimnukuu kiongozi wa Beni, Bwana Richard Kivanzanga akisema.
Askari wawili wa Kongo walijeruhiwa katika ghasia hizo na kundi la ADF katika kijiji cha Kpolowu siku ya Jumamosi, kwa mujibu wa msemaji wa jeshi katika eneo la Beni, Antony Mualushayi.
ADF, ni kundi la harakati za wanamgambo wa kiislamu ambalo zilianzia nchini Uganda mwaka 1990, ambao wanalaumiwa kwa mauaji ya raia zaidi ya 1,000 katika mkoa wa Beni kaskazini mwa jimbo la Kivu tangu mwaka 2014.
Wahanga wa shambulio la Sudani Kusini wazikwa katika makaburi ya pamoja
Watu thelathini na watatu waliouawa wakati wa shambulio lililotokea kanisani nchini Sudani Kusini wamezikwa katika makaburi kadhaa ya pamoja.
Askofu wa kanisa la Anglikana la Episcopal, Moses Anur Ayom alisema kanisa la Mtakatifu Luka lililopo katika mji mkuu wa jimbo la Bor lilishambuliwa wiki kadhaa zilizopita na kundi la vijana.
Msimamizi mkuu wa kanisa hilo, Padre Daniel Garang Ayuen, aliuliwa vibaya katika shambulio hilo.
Haijatangazwa wazi ni kwanini imechukua wiki mbili kwa taarifa za shambulio hayo kuripotiwa.
Jamii za Murle, Dinka na Nuer zimekuwa zikishutumiwa kwa kujihusisha kwa muda mrefu katika mashambulio ya aina hiyo
Kijiji chote cha Makol Chuei kwa sasa hakina watu.
“Watu wasio na hatia walishambuliwa katika eneo la kanisa," Askofu Anur aliiambia BBC katika mji mkuu wa Juba, siku ya Jumapili.
Karibu katika matangazo mubashara Jumatatu 17.08.2020