Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tetemeko la ardhi Tanzania: 'Kiti changu kiliyumba upande upande Nairobi’
Waziri wa masuala ya kigeni nchini Rwanda ametilia shaka azma ya majirani zake Burundi kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.
Moja kwa moja
Habari za hivi punde, Israel yakubaliana na UAE kuimarisha uhusiano kati yao
Israel na UAE wamekubaliana kuimarisha uhusiano wao , rais wa Marekani Donald Trump ametangaza.
Taarifa ya pamoja iliotolewa na Trump, waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na mwanamfalme wa Abu Dhabi Mohammed bin Zayed imesema kwamba inatumai kwamba makubaliano hayo ya kihistoria yataleta amani katika eneo la mashariki ya kati.
Kutokana na hilo, waliongezea, Israel itasimamisha mipango yake ya kuyanyakua maeneo zaidi ya ukanda wa Gaza.
Hadi kufikia sasa Israel ilikuwa haina uhusiano wa kidiplomasia na mataifa ya kiarabu yalio katika Ghuba.
Hatahivyo wasiwasi uliopo kuhusu ushawishi wa Iran umesababisha mawasiliano kati yao.
Mesut Ozil: Hakuna mtu atakayenilazimisha kuondoka Arsenal
Kiungo wa kati wa klabu ya Arsenal Mesut Ozil anasema kwamba atasalia katika klabu hiyo hadi siku ya mwisho ya kandarasi yakemwezi Juni 2021.
Mchezaji huyo wa zamani wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 31, hajashirikishwa kuichezea timu yake tangu ligi ya Premia kurudi mwezi Juni, huku mkufunzi wa Arsenal akidai ni kutokana na sababu za mchezo huo.
Lakini Ozil alikana ripoti kwamba klabu hiyo ilikuwa tayari kumlipa mshahara wake wa mwisho wa £350,000 kwa wiki.
‘’Mambo yamekuwa magumu lakini naipenda Arsenal’’ , aliamba jarida la michezo la Athletic.
‘’Nitaamua ni lini nitaenda , na sio watu wengine’’,.Ozil aliyejiunga na Arsenalkwa dau la £42.4m kutoka Real Madrid 2013, hakuchezeshwa wakati wa mkufunzi Unai Emery lakini akarudishwa uwanjani na kaimu mkufunzi Freddie Ljungberg.
Rwanda yatilia shaka hatua ya Burundi kuimarisha uhusiano kati yao
Waziri wa masuala ya kigeni nchini Rwanda ametilia shaka azma ya majirani zake Burundi kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.
Hatua hiyo inajiri baada ya matamshi ya wiki iliopita ya rais mpya wa Burundi Evariste Ndayishimiye ambaye aliishutumu Rwanda kwa kuwazuia zaidi ya wakimbizi 72,000 wa Burundi.
Waziri wa masuala ya kigeni nchini Rwanda Vincent Biruta siku ya Jumatano alikana madai hayo.
Wakimbizi hao wanadaiwa kutoroka Rwanda 2015 wakati wa mgogoro wa Burundi wa kisiasa kufuatia tangazo la aliyekua rais wa taifa hilo Pierre Nkurunziza kwamba atawania muhula wa tatu ..
Kurudishwa nyumbani kwa wakimbizi hao ndiko ambako kumezua mgogoro kati yao.
Bwana Biruta aliwaambia waandishi wa habari katika mji mkuu wa Kigali kwamba , Rwanda inataka uhusiano mzuri na majirani zakehususan Burundi, lakini akatilia shaka hatua ya taifa hilo kuimarisha uhusiano wao.
Kwa taarifa zaidi bonyeza: Wakimbizi wa Burundi walio Rwanda kuanza kurudi nyumbani tarehe 27 Agosti
Tetemeko la ardhi Tanzania: 'Kiti changu kiliyumba upande upande Nairobi’
Raia wa Tanzania na wenzao wa Kenya wamekuwa wakichapisha jumbe za twitter kuhusu walichoshuhudia wakati tetemeko la ardhi lenye nguvu za 6.0 katika vipimo vya Ritcher lilipopiga mji wa kibiashara nchini Tanzania Dar es Salaam.
Mawimbi ya tetemeko hilo yalisikika katika maeneo ya pwani ya Kenya na mji mkuu wa Nairobi siku ya Jumatano jioni.
Hakuna uharibifu ulioripotiwa.
Watu walituma jumbe za waliyopitia katika mitandao ya kijamii.
Fahamu unachotakiwa kufanya wakati wa tetemeko la ardhi
Mambo ya kufanya wakati wa tetemeko la ardhi
Shuka chini kisha ingia kwenye sehemu iliyofunikwa mfano chini ya meza, kisha shikilia ili isihame na eneo ulipo.
Kama huna meza basi kaa eneo la ukuta ambalo halina dirisha , kama hakuna vyote basi weka mikono yako kichwani uzibe kichwa chako. Subiri hapo hapo hadi tetemeko litakapokwisha.
- Kama upo kwenye jengo imara, baki hapo hapo
- Kama upo ndani ya jengo lililochakaa basi tafuta njia salama ya kutoka nje
- Usitumie lifti kutoka kwenye jengo.
- Tumia ngazi kufika nje ya jengo
Kwa habari zaidi ingia katika tovuti ya bbcswahili
Mustakabali wa wakimbizi wa Burundi waliko Rwanda kujadiliwa
Shirika la umoja wa mataifa la wakimbizi (UNHCR) nchini Rwanda limetangaza kuwa na mkutano wa kwanza wa kujadili suala la wakimbizi wa Burundi walioko Rwanda.
Mkutano huo umepangwa kufanyika leo baina ya pande tatu;Rwanda,Burundi na shirika hilo.
Mkutano huo unaofanyika kwa njia ya Video umekuja baada ya maombi ya baadhi ya wakimbizi wa Burundi kutaka kurejea nchini mwao na pia shutuma za serikali ya Burundi kwamba wakimbizi walishikwa mateka nchini Rwanda.
Wakati huo huo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Rwanda Vicent Biruta ameilaumu Burundi kukosa utashi wa kisiasa katika kurejesha uhusiano kati ya nchi mbili.
Tetemeko la ardhi Tanzania limetokea wapi?
Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa kipimo cha 5.9 Jumatano usiku limetikisa baadhi ya maeneo ya Tanzania hususani ukanda wa pwani na kishindo chake Kufika mpaka katika baadhi ya maeneo ya nchi jirani ya Kenya.
Kwa mujibu wa taasisi ya uchunguzi wa jiolojia ya Marekani, 'US Geological Survey (USGS)', kitovu cha tetemeko hilo ilikuwa katika eneo lililopo kilomita 66 mashariki mwa mji mdogo wa Vikindu, Mkoani Pwani.
Eneo hilo ni nje kidogo ya jiji kuu la biashara la Tanzania, Dar es Salaam.
Tetemeko hilo lilipiga katika kina cha kilomita 15.5 (maili 9.6).
Hakuna uharibifu wowote ulioripotiwa baada ya tetemeko hilo.
Kishindo kilisikika katika pwani ya Kenya Mombasa na baadhi ya maeneo ya Nairobi.
Tetemeko hilo imekuja siku chache baada ya wakazi wanaoishi pembezoni mwa ziwa Baringo nchini Kenya kuripotiwa kuwa na tetemeko baada ya kiwango cha maji kujaa kwa sababu ya mvua zinazoendelea.
Tetemeko hilo liliripotiwa na wanaoishi huko kilomita 7 kutoka ziwani na inadaiwa kuwa tetemeko lilitokea kila usiku kwa wiki mbili zilizopita.
Msumbiji yapambana kukomboa bandari yake 'iliyotekwa na IS'
Jeshi la Msumbiji limesema kuwa mapigano yanaendelea katika bandari ya Mocimboa da Praia, baada ya kuripotiwa kuwa wanamgambo wa kiislamu wamewazidi nguvu siku ya Jumatano.
Jeshi limesema bado jitiahada zinaendelea ili kuweka mji huo salama, kwa sababu magaidi hao wanawatumia wenyeji kujilinda.
Kumekuwa na siku kadhaa za mapigano katika bandari ambayo ina utajiri wa gesi kaskazini mwa Msumbiji.
Wanamgambo wanaohusishwa na kundi la 'Islamic State' - wamefanya uvamizi katika baadhi ya miji na kusababisha mamia ya maelfu ya wakazi kupoteza makazi yao.
Kwa taarifa zaidi ingia bonyeza link ifuatayo : Msumbiji yapigania kukomboa bandari iliyotekwa na IS
‘Hakuna tishio la Tsunami Tanzania’
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema hakuna tishio la kutokea kwa mawimbi makubwa ya tsunami nchini humo kufuatia tetemeko la ardhi la Jumatano usiku.
Tetemeko la ukubwa wa kipimo cha 5.9 lilitokea saa mbili usiku baharini katika eneo lililopo kusini mashariki mwa Mkoa wa Pwani.
Kishindo cha tetemeko hilo kimeripotiwa katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam, Zanzibar na Mombasa, Kenya. Hata hivyo, hakuna madhara makubwa ya miundombinu ama kwa maisha ya binadamu yaliyoripotiwa kufuatia tukio hilo.
Kutokana na tetemeko hilo kutokea baharini, kumekuwa na hofu kuwa linaweza kusababisha mawimbi makubwa ya tsunami.
“...Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imefanya uchambuzi wa taarifa za tetemeko hilo katika kituo chake cha Tahadhari ya Tsunami ili kuona iwapo kuna uwezekano wowote wa tetemeko hilo kusababisha mawimbi ya Tsunami baharini. Matokeo ya uchambuzi huo yanaonesha kuwa hakuna tishio la Tsunami kutokana na tetemeko hilo,” imeeleza taarifa ya TMA.
Kwa mujibu wa TMA tetemeko hilo halikuwa nguvu kubwa na hakuna maporomoko ya ardhi yaliyojitokeza baharini ambayo yangeweza kuzalisha tsunami.
“Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inawashauri watumiaji wa eneo la bahari ikiwa ni pamoja wananchi wanaoishi katika maeneo yaliyokaribu na bahari ya Hindi kutokuwa na hofu na kuendelea na shughuli kwa kuzingatia taarifa ya hali ya hewa Baharini kama ilivyotolewa awali na Mamlaka.”
Karibu katika matangazo mubashara Alhamisi 13.08.2020