Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Jeshi la Tanzania lawataka wananchi kuondoka katika misitu ya mpaka wa Msumbiji

Jeshi la Tanzania limewataka raia wanaoishi katika maeneo ya pori karibu na mpaka wa Msumbuji kuhama eneo hilo wakati wakijiandaa kupambana dhidi ya wanamgambo.

Moja kwa moja

Esther Namuhisa

  1. Huo ndio mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja kwa leo tutaonana tena hapo kesho.

  2. Leo Katika Dira ya Dunia ....

  3. Je uhusiano wa Rwanda na Burundi utarejea?

      • Author, Samba Cyuzuzo
      • Nafasi, BBC Great Lakes

    Mamlaka ya Rwanda inasema kuwa ina wasiwasi kama Burundi itarejesha uhusiano na nchi yake baada ya rais mpya wa Burundi kusema “kamwe hawatakuwa na uhusiano na nchi ambazo hazina msimamo wa kile wanachosema”.

    Rais Evariste Ndayishimiye ameishutumu Rwanda kwa kuwateka nyara wakimbizi wa Burundi wapatao 72,000 , ambao walikimbilia Rwanda wakati wa migogoro ya kisiasa mwaka 2015.

    Katika mkutano na waandishi wa habari, Waziri wa mambo ya nje nchini Rwanda, Vincent Biruta,ameonyesha kutokukubaliana na madai ya rais wa Burundi.

    “Rwanda ni taifa la tatu ambalo lina wakimbizi wengi wa Burundi hivyo hatuwezi kuwaweka mateka kwa sababu hata wakimbizi wa nchi nyingine waliondoka.” alisema bwana Biruta.

    Bwana Biruta aliongeza kuwa Rwanda inataka uhusiano mzuri na majirani zake haswa Burundi, lakini hotuba ya rais wa Burundi inawapa wasiwasi.

    Tangu mwaka 2015 , uhusiano wa Rwanda na rais wa zamani wa Burundi Pierre Nkurunziza, haukuwa mzuri na hivyo kuathiri familia na shughuli za mpakani.

  4. Jenerali wa zamani awania urais dhidi ya bosi wake wa zamani Museveni

    Leo hii,Jenerali Henry Tumukunde ambaye alikuwa msaidizi wa siku nyingi wa rais Yoweri Museveni wa Uganda, amezindua harakati zake za kuwania kiti cha urais.

    Baada ya bwana Tumukunde kuzindua kundi la watakaomsaidia katika kampeni zake kama mgombea huru.

    Jenerali huyo ameeleza kuwa hana imani tena na suala la kuungana na wanasiasa wengine bali anataka kujenga jukwaa lake la upinzani.

    Wakati wa uzinduzi huo alizindua wimbo wake wa kampeni unaoitwa Kisoboka.

  5. Wakenya wanaoishi Beirut waandamana ubalozini

    Raia wa Kenya wanaoishi katika mji wa Beirut, Lebanon wameandamana nje ya ofisi za ubalozi wa Kenya nchini humo wakitaka kurudi nyumbani.

    Video na picha kadhaa zinazoonyesha maandamano ya Wakenya nje ya ofisi za ubalozi, zimesambaa mtandaoni.

    Wakenya hao ambao wengi ni wanawake, wanaaminika kuwa ni wafanyakazi wa majumbani ambao wamepoteza ajira zao baada ya mlipuko.

    Video ambayo imewekwa mtandaoni na kituo cha habari nchini Kenya, NTV wanasikika wakisema wanataka kurudi nyumbani.

    Balozi wa Kenya, Kuwait bi Halima Mohamud, ambaye anahusika na raia wa Kenya wanaoishi Lebanon, alinukuliwa na tovuti ya 'Nairobi News' akisema Wakenya waliokwama huko watarejeshwa nyumbani.

    "Tunawasiliana na raia hao wa Kenya wajiandikishe wakati wakijaribu kushughulikia suala lao .

    Tangu ndege za Kenya zianze kufanya kazi tayari raia 30 wa Kenya wamerejeshwa kwa kupewa nyaraka sahihi za kusafiria, alinukuliwa katika tovuti hiyo.

  6. Jeshi la Tanzania lawataka wananchi kuondoka katika misitu ya mpaka wa Msumbiji

    Jeshi la Tanzania limewataka raia wanaoishi katika maeneo ya pori karibu na mpaka wa Msumbuji kuhama eneo hilo wakati wakijiandaa kupambana dhidi ya wanamgambo, kwa mujibu wa gazeti la kila siku nchini Tanzania,The Citizen.

    Mkuu wa operesheni hiyo alisema jeshi litaanza kuwatafuta wahalifu katika pori la Ruvuma ,na baadae Mtwara na Lindi.

    Mwezi Mei, Tanzania ilipeleka majeshi yake katika mikoa hiyo ya mpakani baada ya kuibuka kwa shambulio la lililotekelezwa na wapiganaji wa kiislamu kaskazini mwa Msumbiji.

    Wapiganaji hao tayari wamevamia miji kadhaa na kuua mamia ya watu na maelfu kuhama makazi yao.

    • Kenya 'kujihusisha na chanjo ya Urusi'

      Maofisa wa afya nchini Kenya wamesema kuwa watajihusisha na chanjo ya virusi vya Corona iliyotengenezwa nchini Urusi, kituo cha redio cha nchini humo, Capital FM kimeripoti.

      Hatua hii imekuja baada ya taifa hilo kuwa la kwanza duniani kutangaza chanjo dhidi ya maambukizi ya corona.

      Lakini wataalamu wameibua hofu yao kuhusu kasi iliyotumika katika kazi hiyo, huku wakidahani kuwa inawezekana watafiti walitumia njia ya mkato.

      “Tutashirikiana na Urusi ili kuhakikisha kuwa chanjo hiyo ni salama kabla hatujaanza kuitumia,” Katibu mku wa afya Mercy Mwangangi amenukuliwa akiviambia vyombo vya habari.

      Alisema serikali ya Kenya itafuata utaratibu kupitia wizara ya mambo ya nje.

      Kwa sasa Kenya imethibitisha kuwa na maambukizi 27,425 ya virusi vya corona.

    • Uchumi wa Uingereza wadorora kwa kiwango kikubwa zaidi baada ya miaka 11

      Uchumi wa Uingereza umekumbwa na pigo kubwa zaidi kurekodiwa kati ya mwezi Aprili na Juni wakati ambapo kulikuwa na marufuku ya kutoka nje ili kuzuia maambukizi ya corona.

      Kipindi hicho kimelifanya taifa hilo kushuka kiuchumi rasmi.

      Uchumi umeshuka kwa 20.4% ukilinganisha na miezi mitatu ya mwanzo ya mwaka huu.

      Maduka yamelazimika kufungwa wakati viwanda na vifaa vya ujenzi pia vikiwa havina soko.

      Hali hii imeisukuma Uingereza kwa mara kwanza kushuka kiuchumi tangu mwaka 2009.

      Ofisi ya takwimu ya taifa (ONS) zimesema uchumi unaweza kurudi katika hali yake mwezi Juni kwa kuwa serikali imeanza kupunguza masharti na mizunguko kuanza.

      Ndani ya mwezi hadi mwezi, uchumi umekuwa kwa asilimia 8.7 kwa mwezi Juni, baada ya ongezeko la asilimia 1.8 mwezi Mei.

      Lakini mkuu wa Tume ya takwimu ya taifa, bwana Jonathan Athow alisema, licha ya pato jumla la taifa kushuka mwezi Juni, bado ipo nyuma kwa kiwango cha sita mwezi Februari kabla ya virusi vya corona havijajapamba moto.

    • Watu 81 wauawa katika zoezi la kukabidhi silaha Sudan Kusini

      Mamlaka ya Sudan Kusini imesema kuwa takribani watu 81 wamekiwemo raia 26 wameuawa katika mapigano kati ya raia wenye silaha na wanajeshi, wakati wa zoezi la kurejesha silaha. Msemaji wa jeshi amesema askari 30 ndio wamefariki na wengine wamejeruiwa.

      Vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kuwa watu wapatao 130 wameuawa.

      Serikali ilikuwa inafanya zoezi la kuchukua silaha ambazo zinamilikiwa na raia baada ya rais Salva Kiir kutangaza mwezi Julai kuwa zoezi hilo lifanyike ili kusaidia kumaliza vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa kuziondoa silaha mikononi mwa raia.

      Inadhaniwa kuwa kuna mamilioni ya bunduki zinazomilikiwa na raia.

      Lakini baadhi ya raia ambao ni jamii ya wafugaji , wanataka serikali kuwahakikisha usalama wao kabla hawajakabidhi bunduki zao.

    • Dwayne 'The Rock' Johnson ndiye muigizaji wa kiume anayeongoza kwa kipato

      Muigizaji wa filamu nchini Marekani Dwayne Johnson, maarufu ''The Rock'' ametajwa kuwa muigizaji wa kiume anayelipwa kiasi kikubwa zaidi cha fedha kwa mwaka wa pili sasa, kwa mujibu wa jarida la Forbes.

      Mwanamieleka huyo wa zamani ameriptiwa kupokea kiasi cha dola milioni 87.5 (£67m) kati ya Juni Mosi, 2019 na Juni Mosi, 2020, ikijumlisha na malipo ya filamu ya kwenye Netflix ya ‘RedNotice’ ambayo ni dola milioni 23.5.

      Muigizaji huyo pia ana kampuni ya kutengeneza nguo, iitwayo ‘Project Rock’.

      Waigizaji 10 wanaolipwa kiwango cha juu mwaka huu jumla wamepata dola milioni 545.5 –zaidi ya robo inayopatikana kutoka kwenye Netflix, Forbes imesema.

      Nyota wa filamu ya Red Notice, Johnson pamoja na muigizaji mwenzake Ryan Reynolds walikuwa waigizaji wa pili kupata kiwango cha juu zaidi ya malipo ya dola milioni 71.5.

      Miongoni mwa mikataba ya filamu zake ilikuwa dola milioni 20,pamoja na filamu ya 'Red Notice', na dola milioni 20 kwa filamu nyingine ambayo haijulikani katika filamu za Netflix.

      Watatu alikuwa muigizaji na muandaaji ,Mark Wahlberg, ambaye alipata dola milioni 58, wakati Ben Afflecka akawa wanne na nafasi ya tano akachukua Vin Diesel.

      Muigizaji wa India, Akshay Kumar ndio msanii pekee kutoka Bollywood aliyekuepo katika 10 bora. Yeye alikuwa wa sita kwa kiwango cha dola milioni 48.5, ambacho jarida la Forbes lilisema kimetoka katika mikataba yake ya bidhaa nyingine.

      Katika orodha hiyo alikepo mbunifu wa Hamilton,Lin-Manuel Miranda, actors Will Smith na Adam Sandler, na nyota wa filamu ya veteran Jackie Chan.

      Hata hivyo orodha ya muigizaji wa kike anayelipwa kiwango cha juu zaidi bado hakijatolewa.

      Mwaka jana alikuwa Scarlett Johansson ambaye aliongoza kwa kipato cha juu cha dola milioni 56 – pungufu ya kiwango hata cha aliyepata muigizaji wa kiume aliyechukua nafasi ya saba.

    • Ndege zisizo na rubani kuokoa maisha ya wagonjwa wa saratani Rwanda

        • Author, Yves Bucyana
        • Nafasi, BBC Swahili

      Sheria ya kutotoka nje ili kudhibiti maambukizi ya Covid19 nchini Rwanda, iliruhusu mpango mpya kwa wagonjwa wa saratani kupata dawa za kuwasaidia kwa kutumia ndege zisizo na marubani maarufu kama drones.

      Ndege hizo za kampuni ya Marekani ya Zipline zilianza kufanya kazi nchini Rwanda mwaka 2016 zikisaidia kupeleka damu na dawa katika maeneo ya vijiji vilivyotengwa na maeneo mengine.

      Lakini sasa zimeanza kuwahudumia wagonjwa wa saratani ambao maisha yao yangekuwa hatarini bila kumuona daktari.

      ‘’Wakati wa sheria ya kutotoka nje tuliona kwamba ilikuwa ngumu kwa wagonjwa kusafiri kwenda hospitalini kwa ajili ya kupata dawa za kansa kwa sababu lazima watibiwe na wataalamu’’Daktari Bigirimana Jean Bosco aliiambia BBC

      Ndege za kampuni ya Zipline hufanya safari zaidi ya 20 kwa siku kusambaza dawa katika vijiji vya masharikiya Rwanda ambako ni vigumu kwa safari za gari.

      ‘’Ndege ikifika katika hospitali au zahanati hudondosha kifurushi cha dawa kwa njia ya kielectroniki kisha inarudi yenyewe katika kituo chake cha kupakia dawa nyingine.Hii ndiyo njia salama ambayo pia inapunguza urefu wa safari.drone hutumia dakika 45 kwa safari ya masaa 6 ya kutumia gari ‘’Blaise Musabe ni mfanyakazi wa kampuni hiyo amefafanua.

      Kwa upande wao wagonjwa mpango huu umeonekana kuwa neema kwao.

      ‘’Drone ilitusaidia sana kutufikishia dawa hapa nyumbani, tulipopokea sheria ya kutotoka nje kutokana na covid19 nilianza kuingiwa na wasiwasi kwamba maisha yangu yatakuwa hatarini. Awali nilikuwa natumia kama dola 30 kulipia nauli ,hapo sijataja uchovu wa safari pamoja na kuacha biashara zangu,nafurahi sana mpango huu unatusaidia’’Marie Louise Kagoyire,ni mgonjwa wa kansa ya damu.

      Tangu mwezi Aprili, wagonjwa zaidi 270 wa kansa tayari wamesaidiwa kwa kufikishiwa dawa na drone .

    • Namibia yakataa fidia ya mauaji ya kimbari iliyotolewa na Ujerumani

      Rais wa Namibia Hage Geingob amekataa kupokea fidia iliyotolewa na Ujerumani kwa ajili ya mauaji ya kimbari wakati wa ukoloni.

      Jeshi la Ujerumani liliuwa mamia ya maelfu ya watu wa jamii ya Herero na jamii ya Nama kati ya mwaka 1904 na mwaka 1908, wakati wa ghasia za kupinga ukoloni.

      Inadaiwa pia kuwa asilimia sabini na tano (75%) ya idadi ya watu wa Herero na nusu ya idadi watu wa Nama waliuawa.

      Nchi hizo mbili zilianza majadiliano juu ya fidia ya kimbari tangu mwaka 2015 na tayari wamekuwa na mazungumzo mara nane hadi sasa.Rais Geingob alikuwa anatoa muktasari wa majadiliano hayo kati ya timu ya majadiliano ya Namibia na wawakilishi kutoka Zed Ngavirue.

      "Fidia iliyotolewa sasa na serikali ya Ujerumani bado haijakubaliwa na serikali ya Namibian," taarifa kutoka kwa Rais ilieleza . Aidha hakukuwa na maelezo zaidi yaliyotolewa kufafanua uamuzi huo.

      "Ujerumani imekubali kuomba radhi lakini imekataa kufikia maafikiano kati yao ya kuuguza majeraha waliyoyaacha”, taarifa hiyo iliongeza.

      Ukurasa wa Twitter wa ofisi ya rais wa Namibia uliweka picha ya rais Geingob na Ngavirue .

    • Karibu katika matangazo yetu mubashara leo Jumatano 12.08.2020